• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
MNADANI: PSG wako tayari kumtupa Neymar sokoni

MNADANI: PSG wako tayari kumtupa Neymar sokoni

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamefichua azma ya kumpiga mnada nyota Neymar Jr iwapo watampata mnunuzi aliye radhi kujinasia huduma za mvamizi huyo mzaliwa wa Brazil katika kipindi hiki cha uhamisho wa wachezaji.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe la nchini Ufaransa, maamuzi ya kuuzwa kwa Neymar yanachochewa na hatua ya Rais Nasser Al’Khelaifi wa kikosi hicho kuondoa baadhi ya masogora wanaojihisi kwamba ni lazima waheshimike zaidi kikosini.

“Itawalazimu wachezaji kuwajibika zaidi badala ya kudai heshima kutokana na wingi wa mashabiki walionao mitandaoni. Sidhani kwamba PSG kwa sasa itakuwa na nafasi kwa mchezaji yeyote wa aina hiyo. Wale wanaotaka kufanya mambo wapendavyo na hata kukosa mazoezi watakavyo kwa kuwa wanahisi wana ufuasi mkubwa, wapo radhi kubanduka,” akasema Al-Khelaifi katika taarifa yake.

Tangu aagane na Barcelona na kutua PSG kwa kima cha Sh26 bilioni mnamo 2017, Neymar hajafikia kabisa matarajio ya waajiri wake ambao walipania kutia kapuni ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Panda-shuka za maisha ambazo Neymar amekabiliana nazo kambini mwa PSG ni miongoni mwa masuala ambayo yaliwahi kumfanya ahusishwe na uwezekano wa kutua kambini mwa Real Madrid.

Neymar Jr wa klabu ya PSG ya Ufaransa. Picha/ AFP

Ingawa hivyo, Neymar amefichua kwamba hana nia ya kujiunga na Real, ila badala yake, angehiari kurejea upya uwanjani Camp Nou kuvalia jezi za wapambe wa soka ya Uhispania, Barcelona.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa sasa anauguza jeraha la kifundo cha mguu baada ya kuumia mwanzoni mwa wiki jana akichezea Brazil dhidi ya Qatar katika mchuano wa Copa America.

Isitoshe, anakabiliwa na sakata ya kumdhulumu kimapenzi mwanafunzi mmoja wa chuo nchini Brazil, baada ya mwanamke huyo aliyewahi kukutana naye jijini Paris kujitokeza hadharani na kupasua mbarika. Zaidi ya hayo, wepesi wa kupata majeraha mabaya ambayo yamekuwa yakimweka mkekani mara kwa mara ni suala jingine ambalo limechangia kudidimiza ushawishi wa Neymar kambini mwa PSG.

Jeraha la goti alilopata mnamo Febaruari mwaka huu ni kiini cha kubanduliwa mapema kwa PSG kwenye kampeni za UEFA baada ya kuzidiwa maarifa na Manchester United waliotoka nyuma kwa mabao 2-0 n kuwapepeta katika mechi ya marudiano uwanjani Parc des Princes.

Jeraha

Katika msimu wa 2018-19, Neymar alipangwa katika kikosi cha kwanza cha PSG mara 16 pekee kwenye mechi za Ligue 1, na kwa sasa jeraha jingine la kifundo cha mguu limemweka nje ya kampeni za Brazil ambao ni wenyeji wa fainali za Copa America mwaka huu.

Awali, Neymar alikuwa amepigwa marufuku ya mechi tatu na vinara wa Ligue 1 kwa kosa la kumpiga shabiki baada ya PSG kuzidiwa maarifa na Rennes kwenye fainali ya kuwania ubingwa wa taji la Coupe de France.

Zaidi ya hayo, Neymar amevurugana mara kwa mara na baadhi ya wachezaji wenzake kambini mwa PSG. Amewahi kuzozania nafasi ya kuchanja penalti na mvamizi Edinson Cavani kabla ya kukabiliana peupe na fowadi mwenzake, Kylian Mbappe ambaye kwa sasa anahusishwa na uwezekano wa kutua uwanjani Santiago Bernabeu kuvalia jezi za Real.

Kwa mujibu wa shirika la CIES Football Observatory, thamani ya Neymar kwa sasa inakadiriwa kufikia Sh19 bilioni tangu ahamie PSG ambao kwa sasa wanaziwania huduma za kipa David De Gea wa Manchester United na beki Matthijs De Ligt ambaye pia ni nahodha wa Ajax Amsterdam nchini Uholanzi.

You can share this post!

Seneti kuandaa vikao vyake Kitui mnamo Septemba

Rangers roho juu ikikabili Stima ikitumai kuingia KPL

adminleo