Mwanya kwa Wanyama kutesa akiwajibikia Spurs wajitokeza
Na MWANDISHI WETU
VICTOR Wanyama huenda akanufaika kutokana na marufuku ya wachezaji Harry Winks na Moussa Sissoko kupangwa na Jose Mourinho katika kikosi kitakachopepetana na Norwich katika Ligi Kuu, leo Jumamosi.
Kiungo huyu alicheza dakika moja dhidi ya waajiri wake wa zamani Southampton (Septemba 28) na dakika 23 dhidi ya Leicester (Septemba 21) chini ya kocha aliyetimuliwa Mauricio Pochettino. Hajakuwa hata kwenye benchi katika mechi 12 za ligi zilizopita.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya hajapata kuchezea Mourinho hata sekunde moja ligini, ingawa kocha huyo Mreno alimuonjesha dakika tisa dhidi ya miamba wa Ujerumani Bayern Munich kwenye Klabu Bingwa Ulaya mnamo Desemba 11 uwanjani Allianza Arena. Wanyama alijaza nafasi ya Eric Dier katika mechi hiyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akihusishwa na uhamisho katika kipindi kifupi kijacho. Hata hivyo, huenda akachezea Spurs kabla ya kuyoyomea kwingineko baada ya Winks na Sissoko kulishwa kadi za njano dhidi ya Brighton & Hove Albion mnamo Alhamisi. Taarifa zinasema wawili hao watakosa mechi dhidi ya Norwich kwa sababu watakuwa wakitumia marufuku ya mechi moja baada ya kufikisha kadi tano za njano msimu huu.
Kiungo Tanguy Ndombele alikosa mechi dhidi ya Brighton akihofia kujeruhiwa tena naye Dele Alli aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Brighton alionyesha kusumbuliwa na kinena mwisho wa mechi hiyo.
Kulazimika
Vyombo nchini Uingereza vinasema kuwa Mourinho sasa atalazimika kuchagua viungo atakaochezesha kutoka kwa orodha ya Dier, Oliver Skipp, Christian Eriksen, Wanyama na Giovani Lo Celso.
Aidha, Wanyama amepata pigo katika juhudi za kujiunga na Hertha Berlin baada ya tetesi kuibuka jana kuwa Wajerumani hao wanafanya mazungumzo na kiungo wa Arsenal, Granit Xhaka.
Fununu zilikuwa zimesema kuwa Wanyama anamezewa mate na Hertha Berlin pamoja na Celtic ya Scotland, West Ham (Uingereza) na klabu kadhaa nchini China.