Mwendwa afichua FKF inadaiwa Sh100m na makocha wa zamani wa Harambee Stars
Na Geoffrey Anene
Madeni ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwa makocha wa zamani wa Harambee Stars yanatisha hali yake ya kifedha.
Rais wa FKF, Nick Mwendwa amefichua Jumanne jijini Nairobi kwamba shirikisho lake linadaiwa zaidi ya Sh100 milioni kutokana na kesi 12 zilizowasilishwa dhidi yake mahakamani.
Kocha Mbelgiji Adel Amrouche, ambaye aliongoza Stars kati ya Februari mwaka 2003 na Agosti 4 mwaka 2014 alipotemwa baada ya Kenya kukosa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2015, anadai FKF Sh60,390,000 (dola 600, 000 za Marekani). Mzawa huyu wa Algeria alikuwa amesaini kandarasi ya miaka mitano na FKF.
Mapema mwaka 2018, alishinda kesi ya kupigwa kalamu kabla ya kandarasi yake kutamatika mahakamani. Korti iliamua alipwe mamilioni hayo, ambayo FKF bado inapambana kuona yamepunguzwa.
FKF ilielekea katika mahakama ya kuamua kesi za michezo (CAS) kutafuta haki baada ya kulalamika kwamba kesi ya Amrouche dhidi ya FKF ilisikizwa na jaji mmoja.
Mrithi wa Amrouche, Bobby Wiliamson anadai FKF Sh55 milioni. Raia huyu wa Scotland alijiunga na timu ya taifa ya Kenya mnamo Agosti mwisho mwaka 2014 kama kocha mkuu akitokea klabu ya Gor Mahia.
Baada ya msururu wa matokeo duni, Williamson alifurushwa na FKF mapema mwaka 2016. Alishtaki FKF mnamo Mei 2016 akitaka fidia kwa sababu ya kutimuliwa kabla ya kandarasi yake kukamilika.
FKF pia inaandamwa na kesi ya kukwepa kulipia ushuru ya zaidi ya Sh40 milioni, ingawa Mwendwa amesema shirikisho hili litaendelea kuzungumza na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) kuhusu tukio hilo lilofanyika kati ya mwaka 2011 na 2012 wakati hakuwa ameingia ofisini. Mwendwa alichaguliwa kuongoza FKF mwezi Februari mwaka 2016.