• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
NDOTO YA LIVERPOOL: Klopp asema amejipanga

NDOTO YA LIVERPOOL: Klopp asema amejipanga

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, Uingereza

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool anaamini vijana wake wana kila mbinu ya kutwaa ubingwa wa gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu watakapokutana na Tottenham Hotspur jijini Madrid, Uhispania, Jumamosi.

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 51 amesema kikosi cha sasa ni bora kuliko cha msimu uliopita ambacho kilishindwa kwa mabao 3-1 na Real Madrid katika fainali jinini Kiev, Ukraine.

Klopp amesema Liverpool imejiandaa vyema kutwaa ubingwa huu bara kwa mara ya sita, na kuvunja nuksi ya kushindwa mara sita fainalini.

Kocha huyo amesisitiza kwamba timu ya sasa ni tofauti kabisa na kikosi kilichoshindwa na Real Madrid, msimu uliopita.

“Liverpool itatosheka tu itakaponyanyua kombe la kwanza chini yangu tangu nitue uwanjani Anfield. Kwa hakika nimejiandaa kumaliza kiu hii hapo Jumamosi, kutokana na uwezo mkubwa wa kikosi nilicho nacho kwa sasa,” alisema.

“Maishani mwangu sijawahi kuwa na kikosi imara kama hiki katika fainali. Nina timu ambayo iko tayari kabisa kutwaa ubingwa kwa vyovyote vile. Wachezaji wanajiamini na wanasubiri kwa hamu pambano la Jumamosi,” aliongeza.

“Tumesahau yaliyotokea msimu uliopita, kwa sababu hatukutarajia kucharazwa hivyo, lakini tumerejea tena, wakati huu tukiwa na matumaini makubwa. Wakati huo tukiwa uwanja wa ndege wa Kiev kuelekea nyumbani, kila mtu alikuwa na huzuni nyingi, lakini tulikutana na kuamua mwanzo mpya. Sasa sisi tu hapa tena, ni mshangao kwa wengi waliotupuuza,” alisema.

“Nadhani timu yoyote inayoshindwa fainalini, huwa haitarajii. Nilikaa na kubuni mpango mpya wa kuunda kikosi imara kabla ya msimu kuanza. Kunazia siku ya kwanza ya msimu huu, tulishirikiana bega kwa bega kikosini. Timu hii, hata kidogo, haiwezi kufananishwa na timu ya msimu uliopita. Msimu uliopita, haja yetu ilikuwa tu kwenda Kiev, lakini msimu huu tunalenga ubingwa.”

Klopp alithibitisha kwamba kiungo Naby Keita ataikosa fainali ya Jumamosi kutokana na jeraja la mguuni alilopata wakicheza na Barcelona pamoja na Roberto Firmino anayesumbuliwa na jeraha la misuli.

Ni kitu cha kujivunia

Kadhalika kocha huyo alisema ushindi wa taji la Klabu Bingwa utakuwa wa kujivunia katika maisha yake ya soka.

“Ninakumbuka nilipoisaidia Mainz kufuzu kwa ligi kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo 2004. Lakini iwapo nitaisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa UEFA, utakuwa ushindi mkubwa zaidi maishani mwangu.”

Georginio Wijnaldum, ambaye mabao yake mawili yaliisaidia Liverpool katika ushindi wake dhidi ya Barcelona katika hatau ta nusu-fainali, duru ya pili, ana imani watapata ushindi dhidi ya Tottenham katika fainali ya Jumamosi ambayo wengi wanadhania itakuwa ngumu.

“Spurs ina kikosi kizuri na tunatarajia upinzani mkali kwa dakika zote 90,” alisema Wijnaldum.

Tulimaliza mbele yao ligini, lakini kumbuka fainali ni fainali. Kwa sasa siwezi kujidai tutashinda, kwani timu zote ni sawa.”

“Chochote chaweza kutokea, lakini kwa sasa tunaendelea kujiandaa kwa siku hiyo. Hatuna presha yoyote kuhusu fainali. Ni fursa nyingine kwetu baada ya kuteleza msimu uliopita,” aliongeza Wilnaldum ambaye walicheza pamoja na Moaussa Sissoko (wa Tottenham) katika timu ya Newcastle United.

You can share this post!

NGUGI: Wamchao Mungu wana majukumu zaidi ya kuhubiri

IEBC yasubiriwa kuidhinisha sahihi za Thirdway Alliance...

adminleo