Michezo

Newcastle United kufungulia mifereji ya fedha kumsajili Gareth Bale

May 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NEWCASTLE United wapo tayari kuweka mezani kiasi cha Sh8 bilioni ili kujinasia huduma za fowadi matata wa Real Madrid na timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale mwishoni mwa msimu huu.

Kufaulu kwa mipango yao hiyo kutamshuhudia Bale ambaye uhusiano wake na kocha Zinedine Zidane umevurugika uwanjani Santiago Bernabeu akirejea katika Ligi Kuu ya Uingereza, miaka saba tangu aagane na Tottenham Hotspur.

Kwa mujibu wa gazeti la FourFourTwo nchini Uingereza, kati ya vikosi vitatu ambavyo kwa sasa vinafukuzia saini ya Bale, ni Newcastle ndio ambao wameelekea kushangaza zaidi mashabiki.

Mbali na Newcastle, klabu nyinginezo zinazomhemea Bale ni Inter Miami ya kocha David Beckham na Spurs ambao wako radhi kumrejesha nyota huyo jijini London kwa kiasi cha Sh7 bilioni kwa matarajio kwamba atastaafu ulingoni akivalia jezi zao.

Hadi kufikia mwanzoni mwa Aprili, ingalikuwa muhali sana kwa kikosi cha kiwango cha Tottenham kuwania saini ya mchezaji wa haiba na laiki ya Bale.

Ingawa hivyo, matarajio ya kutwaliwa kwa kikosi hicho na mabwanyenye wa Saudi Arabia ambao wako tayari kutoa zaidi ya Sh42 bilioni ili kuimiliki Newcastle yatawapa klabu hiyo uthabiti wa kifedha utakaowawezesha kusajili masogora wazoefu wenye tajriba pevu na pana katika ulingo wa soka.

Kutwaliwa kwa Newcastle ambao kwa sasa wapo chini ya umiliki wa Mike Ashley, kunatazamiwa kufanyika katika kipindi cha majuma machache yajayo.

Kupungua kwa mapato ya Real msimu huu kutokana na janga la corona kunatarajiwa pia kuwaweka miamba hao wa soka ya Uhispania katika ulazima wa kuwatia baadhi ya wanasoka wao mnadani mwishoni mwa muhula huu.

Mbali na Bale ambaye mauzo yake yanatazamiwa kuwezesha Real kujinyakulia huduma za Harry Kane wa Tottenham, sogora mwingine ambaye huenda akabanduka uwanjani Bernabeu ni James Rodriguez ambaye ni raia wa Colombia.

Bale aliondoka Tottenham mnamo Septemba 2013 na amewashindia Real mataji yote ya haiba kubwa katika ulimwengu wa soka katika kipindi cha miaka saba iliyopita nchini Uhispania.

Bale mwenye umri wa miaka 30 alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning ya China mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Hata hivyo, Real walizuia uhamisho wake katika dakika za mwisho kwa sababu walitaka Suning walipie ada yote ya kumsajili na pia walikuwa bado wakimhitaji baada ya winga Marco Asensio kupata jeraha.