Nishabikie Liverpool au Spurs? Sonko ajipata kwa njia panda
Na PETER MBURU
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ni mmoja wa Wakenya wengi wanaoshindwa timu watakayoshabikia katika mechi ya fainali za ya UEFA, baada ya timu za Tottenham na Liverpool kufuzu, zote zikiwa na wachezaji wa kutoka Kenya.
Baada ya Tottenham kucharaza Ajax mabao 3-2 usiku wa Jumatano na Liverpool kunyorosha Barcelona mabao 4-0 Jumanne, timu hizo zilifuzu kwenye fainali ya Jumamosi ya Juni 1, jijini Madrid.
Tottenham iko na Mkenya Victor Wanyama, nayo Liverpool Divock Origi, ambao wanawapa Wakenya wakati mgumu kuamua. Swali ni je, watashabikia timu ipi?
Mashabiki wa soka sasa wamebandika mechi hiyo #AKenyanAffair kutokana na uwepo wa Wakenya wawili katika timu zote, wengine wakiitajakuwa ‘Mashemeji Derby’.
“Kama ilivyotabiriwa, ni suala la Kenya katika fainali za UEFA inayoandaliwa Juni 1, 2019 kati ya Klabu ya Liverpool na Klabu ya Tottenham katika uwana wa Estadio Metropolitano, Madrid, Uhispania. Lakini sasa nimechanganyikiwa kati ya #VictorWanyama na #DivockOrigi nitakuwa upande wa nani,” Sonko akashangaa Alhamisi.
Wakenya wengine wameamua kuzitakia timu zote bahati, na atakayecheza mchezo mwema ashinde.