NSL ngumu msimu ukifika katikati
MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi ya Supa (NSL) zinaendelea kushuhudia ushindani mkali msimu ukiwa umefika katikati.
Hii ni kwa sababu timu sita ambazo zipo kileleni zimetenganishwa na alama saba pekee. Nairobi United inaongoza msimamo wa jedwali kwa alama 37, alama moja mbele ya APS Bomet, timu zote zikiwa zimesakata mechi 18.
Kibera Black Stars, Fortune Sacco, MOFA na Darajani Gogo zinafuata kwa alama 33, 32, 30 na 30 mtawalia. Timu mbili za kwanza kwenye NSL hufuzu kuingia Ligi Kuu (KPL) moja kwa moja mwishoni mwa msimu huku ile inayomaliza nambari ya tatu ikishiriki mchujo dhidi ya nambari 17 kwenye KPL.
APS Bomet na Darajani Gogo zimepoteza mechi tatu pekee msimu, idadi ambayo ni ya chini zaidi ikilinganishwa na timu nyingine. Luanda Villa ambayo ipo nambari 11 kwa alama 22 ndiyo imeyafunga mabao mengi, ikiwa imecheka na nyavu za wapinzani mara 30.
Wikendi, MOFA inayomilikiwa na straika wa Harambee Stars Michael Olunga na Darajani Gogo zililemewa kupunguza uongozi wa Nairobi United baada ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya Mombasa Stars na Fortune Sacco mtawalia.
Nambari tisa Kisumu All Stars ambayo ina alama 23 na ilikuwa na wanasoka 10 uwanjani, ilipoteza 2-1 dhidi ya Naivas kwenye uga wa Kenyatta, Machakos. Timu hiyo wiki jana ilipoteza ufadhili wa Kaunti ya Kisumu na sasa inawategemea wahisani kuwajibikia mechi zake.
Mkiani mwa NSL Assad inaendelea kuvuta mkia kwa alama tisa kisha Dimba Patriots kwa alama 11 timu zote zikiwa zimecheza mechi 17. Muhoroni Youth pia itabidi ijikaze kukwepa shoka kwa sababu ni nambari 17 kwa alama 12 baada ya mitanange 16.