Michezo

Ogam, Shumah papa kwa hapa Kiatu cha Dhahabu KPL

Na CECIL ODONGO April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSHAMBULIZI wa Kakamega Homeboyz Moses Shumah sasa yupo sako kwa bako na straika Ryan Ogam wa Tusker kwenye mapambano ya Kiatu cha Dhahabu baada ya kufunga katika mechi ya Ligi Kuu(KPL) dhidi ya AFC Leopards Jumamosi.

Shumah, 23 alifunga bao la kusawazisha kupitia mpira wa kichwa dakika ya 45 katika ushindi wa 2-1 ambao Homeboyz ilipata dhidi ya Leopards katika uga wa Dandora jijini Nairobi.

Leopards ilikuwa imechukua uongozi katika mchuano huo dakika ya 11 kupitia bao la Victor Omune. Fowadi huyo aliutia mpira kwenye nyavu baada ya Lewis Bandi na C0llins Shichenje kupokezana pasi kisha kummegea mpira ambao aliujaza uwanjani huku mnyakaji Ibrahim ‘Babu’ Wanzala akitazama tu.

Hata hivyo, Shumah aliurejesha Homeboyz mchezoni kisha Henry Omollo ambaye alichukua nafasi yake dakika ya 75 akafunga bao la ushindi katika dakika ya 83.

Shumah sasa ana magoli 15 sawa na Ryan Ogam ambaye alifunga mara ya mwisho KPL mnamo Januari 15 wakati ambapo Tusker iliipiga Bandari 2-1 uwanjani Mbaraki. Iwapo Ogam ataendelea kuandamwa na ukame wa magoli basi Shumah atakuwa pazuri kutwaa tuzo hiyo iwapo ataendelea na rekodi yake ya kufunga mabao.

“Nitahakikisha kuwa Shumah anatwaa Kiatu cha Dhahabu kwa sababu talanta na uwezo anao. Ni kati ya wachezaji ambao wakiwa kwenye fomu bora, basi watasaidia Kenya kutamba hata kwenye CHAN  inayokuja mnamo Julai,” akasema Kocha wa Kakamega Homeboyz Francis Baraza

Ushindi wa Jumamosi uliipaisha Homeboyz hadi nafasi ya tano kwa alama 38 baada ya mechi 26 nao Leopards wameshuka hadi nambari sita kwa alama 37.