• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:31 PM
Oliech akosoa hatua ya Mwendwa kupokeza Gor Mahia ubingwa

Oliech akosoa hatua ya Mwendwa kupokeza Gor Mahia ubingwa

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA mshambuliaji nyota wa timu ya taifa Harambee Stars Dennis ‘The Menace’ Oliech amemkashifu vikali Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Nick Mwendwa kwa kutwaa majukumu ya kampuni inayosimamia Ligi Kuu (KPL) na kutawaza Gor Mahia kuwa ndio mabingwa wa taji la msimu huu.

Mwendwa kupitia akaunti yake ya Twitter, alitangaza wiki jana kuwa mechi za msimu huu hazitarejelewa na kutaja K’Ogalo kama mabingwa wapya huku Chemelil Sugar na SoNy Sugar zikiteremshwa ngazi hadi Ligi ya Betika (BSL) msimu ujao.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL Jack Oguda, ametoa wito kwa timu kupuuza tangazo la Mwendwa kwa kuwa hatima ya ligi itaamuliwa baada ya Mei 15 wakati kafyu ya siku 21 iliyowekwa na serikali itatamatika.

Ligi Kuu iliahirishwa kwa muda usiojulikana mnamo Machi, zikiwa zimesalia mechi 10 msimuukamilike, kutokana na janga la virusi vya corona.

Oliech alimkashifu Mwendwa, akisema ni mapema mno kutangaza bingwa wa Ligi Kuu na pia hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa sababu hilo ni jukumu la KPL.

“Hali ya baadaye ya ligi ipo hatarini iwapo watu walioko ofisini wataitumia kupiga siasa. Mwendwa anatafuta umaarufu wa kisiasa ilhali anajua vizuri kwamba shirikisho halijakuwa likiwasaidia wachezaji ambao wamelemewa na ugumu wa maisha,” akasema Oliech.

Mwanadimba huyo alishangaa ni mfumo gani FKF ilitumia kuafikia wazo kwamba jedwali la katikati ya msimu litumike kubaini bingwa mpya ilhali klabu zote hazikuwa zimecheza mechi sawa wakati huo.

“Kulingana nami, Tusker wangepokezwa ubingwa kwa sababu FKF ilitumia msimamo wa jedwali la KPL la katikati ya msimu. Tusker walikuwa wakiongoza baada ya kujibwaga uwanjani mara 16 wakati Gor ilikuwa imecheza mechi 13. Mechi tatu za Gor Mahia zilichezwa baadaye mkumbo wa pili wa ligi ukiwa umeanza ndiyo maana ni vigumu kufahamu wakati ambapo msimu ulikuwa katikati,” akaongeza.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mathare United ambaye alifungia Harambee Stars mabao 34 enzi zake, alisisitiza kwamba mataifa mengi Afrika hayajafutilia mbali ligi zao na haelewi kwa nini FKF iliharakisha na kutamatisha msimu huu.

“Ni ubaguzi mkubwa kufutilia mbali ligi na kuteremsha ngazi Chemelil zikiwa zimesalia mechi 10 ilhali walikuwa na nafasi ya kukwepa shoka. Ni jambo la kusikitisha,” akaongeza.

Jagina huyo aliunga mkono klabu ambazo zimeapa kufika mbele ya Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Michezo (SDT) kutafuta haki kuhusu suala hilo.

You can share this post!

Polisi kutenga vituo vipya vya karantini kwa wanaokiuka...

Polisi wachunguza chanzo cha kifo cha Tecra Muigai

adminleo