PATASHIKA: Liverpool yaendea mtihani mgumu wa Bayern Munich
Na MASHIRIKA
MUNICH, UJERUMANI
BAADA ya kuambulia sare tasa katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ugani Anfield, Liverpool wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa wenyeji Bayern Munich timu hizo zitakaporudiana leo usiku ugani Allianz Arena.
Mlinzi tegemeo, Van Dijk amesema ni lazima kila mtu ajitahidi kikosini, la si hivyo, kazi itakuwa ngumu kwao kubatilisha matokeo ugenini.
“Nafasi ya kufuzu ingalipo na nina hakika kila mtu amejiandaa vyema. Wakati huu tunalenga ushindi, licha ya matokeo mabaya yaliyotuandama katika mechi za karibuni za Ligi Kuu ya EPL,” alisema.
“Walicheza vizuri tulipokutana Anfield. Safu yao ya ulinzi ni nzuri, na itabidi tupigane vikali kuanzia mwanzo ili tufaulu. Hapa, itabidi tucheze kwa bidii kuliko tulivyocheza katika mechi mbili za hapo awali ugenini,” aliongeza.
Liverpool hawakuandikisha matokeo mazuri katika mechi za mchujo, lakini walifanikiwa kufuzu kwa hatua ya mwondoano.
Lakini Dijk alisisitiza kuwa timu yake ina uwezo wa kusajili ushindi na kusonga mbele, hata baada ya kushindwa kupata bao katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Anfield.
“Kutofungana katika mkondo wa kwanza ni nafuu kwa kile upande, lakini tunaelewa kuwa tukifunga bao, watahitaji kufunga mabao. Hivyo ndivyo itakavyokuwa. Tumejipanga kushinda hii mechi na kusonga mbele. Huenda wakatulemea kwa njia moja kutokana na kikosi chao imara. Lakini pia kumbuka hata sisi tuko tayari kuwakabili vilivyo,” alisema beki huyo mzaliwa wa Mholanzi.
“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu tuliagana bila kufungana. Kila mtu anajiamini kufuatia ushindi wetu wa mwishoni mwa wiki jana dhidi ya Burnley,” aliongeza.
Kikosi cha kocha Jurgen Klopp kitamtegemea Roberto Firmino ambaye amerejea kwa kishindo baada ya kupata nafuu kutokana na jeraha la kisigino.
Dhidi ya Burnley, Liverpool walipoteza nafasi nyingi, na hata ilibidi watoke chini kabla ya kuandikisha ushindi wa 4-2, ambao ulipatikana kutokana na mabao ya Firmino na Sadio Mane.
Kinachomsumbua Klopp ni kwamba mshambuliaji wake tegemeo, Mohamed Salah amecheza mechi sita bila kufunga bao, ingawa alicheza kwa kiwango cha juu dhidi ya Burnley.
Mabao tisa
Kufikia sasa, Mane amefunga mabao tisa, huku akijivunia kiwango kizuri. Sergio Aguero wa Manchester City anampitia mabao mawili, wakati Salah, Harry Kane na Pierre-Emerick Aubameyang wakishindia bao moja kila mmoja.
Ukiondoa mikwaju ya penalti, hakuna aliye na idadi kubwa kuliko staa huyo wa kimataifa wa Senegal msimu huu.
Firmino anaielewa vyema Bayern tangu alipokuwa nchini Ujerumani akiichezea Hoffenheim. Katika mechi za mchujo wa kufuzu, Liverpool ilipoteza mechi tatu za ugenini, huku bao la pekee kwenye mechi hizo likipatikana kupitia kwa James Milner walipocheza na PSG.
Ukiongeza fainali ya msimu uliopita, Liverpool imepoteza mechi tano za Klabu Bingwa ugenini, huku wakifungwa mabao 12, lakini kuimarika kwa kiwango cha Firmino huenda kukaleta mabadiliko kikosini.