Police, Tusker, Gor kibarua kigumu msimu wa 2024/25 ukikaribia ukingoni
MECHI nne mwisho ndizo zitaamua mshindi wa taji la Ligi Kuu (KPL), ishara zote zikionyesha kuwa bingwa wa msimu ataamuliwa siku ya mwisho ya Mei.
Viongozi Kenya Police (alama 58), Tusker (alama 55) na Gor Mahia (alama 53) zote zipo pazuri kutwaa ushindi wa KPL mwishoni mwa msimu.
Ingawa hivyo, Gor bado imebaki na mechi tano baada ya Debi ya Mashemeji dhidi ya AFC Leopards kuahirishwa kutokana na ukosefu wa uwanja.
Iwapo Kenya Police na Gor zitashinda mechi zao zilizosalia zote, basi mchuano wa mwisho kati yao mnamo Mei 31 ndiyo itaamua mshindi wa KPL.
Kenya Police itacheza na Kakamega Homeboyz mnamo Jumatano ugenini kisha FC Talanta na Shabana kabla ya kuvaana na Gor katika mtanange wa mwisho.
Mechi hizi zinaonekana kuwa ngumu zaidi kwa timu hiyo ikilinganishwa na Tusker na Gor.
Tusker nao wamebaki na FC Talanta ambao watacheza nao katikati mwa wiki kisha Sofapaka, Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz katika mchuano wao wa mwisho.
Kando na AFC Leopards, Gor Jumatano hii itasakata dhidi ya wavuta mkia Nairobi City Stars kisha ugenini dhidi ya Murangá Seal, Ulinzi Stars ndipo wamalize msimu dhidi ya Tusker.
Japo Shabana ambao wana alama 49 pia wana nafasi finyu ya kutwaa ubingwa, pamoja na Kakamega Homeboyz (alama 48). Timu hizo zitaamua iwapo Kenya Police na Tusker zitamaliza ubabe wa Gor wa kushinda ubingwa wa KPL.
Mkiani mwa KPL, timu zote kutoka nambari 10 hadi nambari 18 bado zinaweza kushushwa ngazi na hilo linategemea matokeo ambayo timu hizo zitaanza kuonyesha kwenye mechi za katikati mwa wiki.