Michezo

Presha kwa Akonnor Gor ikivaana na Homeboyz Alhamisi

Na CECIL ODONGO December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MECHI ya Jumatano kati ya Gor Mahia na Kakamega Homeboyz ya Ligi Kuu (KPL) uwanja wa MISC Kasarani huenda ikaamua mustakabali wa Kocha wa Gor Mahia Charles Akonnor ambaye anaendelea kuandamwa na shinikizo za mashabiki.

Gor haijaonja ushindi katika mechi tatu mfululizo na iwapo itapigwa na Kakamega Homeboyz, basi Akonnor raia wa Ghana atajipata pabaya kesho.
Gor imeporomoka hadi nafasi ya tatu kwa alama 20 baada ya mechi 11, alama moja nyuma ya viongozi Kenya Police na Tusker ambayo imecheza mechi 12.
Gor ilipoteza 4-1 dhidi ya APS Bomet, ikapigwa 1-0 na AFC Leopards kwenye Debi ya Mashemeji kabla ya kuandikisha sare ya 1-1 na Bandari wikendi iliyopita
Kakamega Homeboyz pia imejikusanyia alama 20 lakini inadunishwa na mabao ingawa imecheza mechi 12 pia.
Msimu uliopita, Gor ilipiga Kakamega Homeboyz 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya timu hizo kuagana sare tasa kwenye mkondo wa pili.
Iwapo Gor itadondosha alama tena mnamo Jumatano basi huenda mashabiki wakamchoka Akonnor kabisa, baadhi tayari wakitaka ang’atuke.
Hii leo Posta itapambana na Bandari katika uwanja wa MISC Kasarani Annex huku KCB ikizipiga dhidi ya APS Bomet katika uwanja wa Kasarani.
Bandari bado haina kocha baada ya benchi yake ya kiufundi kufurushwa wiki iliyopita huku ushindi kwa Posta Rangers ukiwapaisha hadi kileleni mwa KPL kabla ya timu nyingine kucheza.
Posta Rangers ina alama 20 baada ya kuwa uwanjani kwa mechi 13 nao Bandari wapo nambari 13 kwa alama 13 baada ya mechi 12.
Mechi tatu zilizopita kati ya Posta Rangers na Bandari ziliishia sare.