Real Madrid kuamua hatima ya Bale mwishoni mwa msimu
Na MASHIRIKA
KOCHA Zinedine Zidane wa Real Madrid amesema kwamba mustakabali wa nyota matata mzawa wa Wales, Gareth Bale anayehusishwa pakubwa na Man-United utaamuliwa mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa Zidane, kudumishwa au kufurushwa kwa Bale uwanjani Santiago Bernabeu kutategemea ukubwa wa mchango wake katika michuano 10 ijayo ya waajiri wake.
Licha ya kuwasaidia Real kutia kapuni jumla ya mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Bale mwenye umri wa miaka 29 bado amekosa kuwa kipenzi cha mashabiki wengi ugani Bernabeu, Uhispania.
Japo majeraha yamekuwa kiini cha kusuasua kwa Bale katika ngazi za klabu na timu ya taifa, Zidane anahisi kwamba nyota huyo angali na ushawishi mkubwa katika kikosi cha Real licha ya madai kwamba hahusiani vyema na masogora wenzake.
Man-United wamekuwa wakihusishwa na Bale tangu 2013 alipobanduka Tottenham Hotspur nchini Uingereza na kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Real.
Mbali na Man-United, kikosi kingine kinachowania maarifa na ubunifu wa Bale ni waliokuwa waajiri wake Tottenham ambao wako radhi kuweka mezani kima cha Sh7 bilioni ili kumsajili upya.
Bale aliagana na Tottenham yapata miaka mitano na nusu iliyopita katika uhamisho uliorasimishwa kwa Sh11 bilioni.
Iwapo wataambulia pakavu katika juhudi zao za kumshawishi Bale kujiunga nao, Man-United ambao pia wanahusishwa na Philippe Coutinho wa Barcelona, wamepania kusaka samjili ya kiungo Toni Kroos, 29, ambaye pia ni mchezaji wa Real.
Hata hivyo, kutua kwa Bale au Kroos ugani Old Trafford ni biashara itakayokuwa zao la makubaliano kwamba Paul Pogba wa Man-United anayoyomea Uhispania kuwawajibikia Real ambao pia wanazihemea huduma za Eden Hazard, Kylian Mbappe na Christian Eriksen wa Chelsea, PSG na Tottenham mtawalia.
Nafasi ya tatu
Real kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 59 baada ya kuwapepeta limbukeni Huesca 3-2 mnamo Jumapili.
Isco aliwafungulia Real ukurasa wa mabao kabla ya Ceballos na Karim Benzema kuwaongoza waajiri wao kutoka nyuma na kufuma wavuni mabao yaliyowapa alama tatu.
Atletico Madrid waliowakomoa Alaves 4-0 mnamo Jumamosi wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 59 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Barcelona ambao waliwakwaruza Espanyol 2-0.