• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:47 AM
Sharp Boys walenga kuwasha moto ligi ya KYSD 

Sharp Boys walenga kuwasha moto ligi ya KYSD 

Na JOHN KIMWERE 

TIMU ya Sharp Boys ni miongoni mwa vikosi 18 vinavyopigania ubingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 12 muhula huu. Mechi hizo zinatazamiwa kushuhudia ushindani mkali kutoka kwa vikosi sita vinavyoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza.

Orodha ya timu hizo mpya inajumuisha Biira Sports Academy kutoka Mbotela, Full Time Rangers kutoka City Cotton, Blue Bentos kutoka Umoja, Kaiyaba Youth Sports Association kutoka Kaiyaba, Young Lions pia kutoka Kaloleni na Arizen Soccer Academy kutoka Mukuru kwa Reuben.

Kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo amesema “Tumeandaa kikosi chetu  huku tukilenga kushusha ushindani mkali ili kufanya vizuri kwenye kampeni za raundi kinyume na ilivyokuwa msimu uliyopita.”

Kocha huyo anasema ushindi wa vijana wake dhidi ya mabingwa watetezi, Kinyago United kwenye mechi ya utangulizi ulionyesha jinsi wameandaa kikosi hicho.

Kadhalika anadokeza kuwa mechi za ligi ya KYSD zimesaidia wachezaji wengi kupalilia vipaji vyao na kufaulu kupata nafasi kuchezea vipute vya juu ambavyo huandaliwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wakiwemo William Okwasumi (Sofapaka Youth), Vincent Odhiambo na Keith Imbali wote Gor Mahia Youth.

Kyalo anasema kando na Kinyago United pia Young Elephant ni kati ya vikosi ambavyo tayari vimeonyesha vimepania kutoa ushindani mkali kwenye kampeni za msimu huu.  Ili kuweka matumaini yao hai kocha huyo anadokeza wanataka kumaliza kileleni katika jedwali kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

TATU BORA

Katika mpango mzima kocha huyo anasema wamepania kupigana kwa udi na uvumba kuhakikisha wanamaliza miongoni mwa vikosi tatu bora kwenye kampeni za muhula huu.

Nahodha wa kikosi hicho, Dennis Ndisii anasema “Ingawa ndani ya wiki mbili zilizopita tumetoka nguvu sawa mara mbili tuna imani tuna uwezo tosha kuvuruga wapinzani wetu kwenye kampeni za muhula huu.”

Nahodha huyo anawaambia wachezaji wenzake kuwa kamwe wasikubali kulaza damu dimbani maana wakiteleza tu watakuta mwana sio wao.

Naye kocha wa Kinyago, Anthony Maina anasema chipukizi wake wapo tayari kukabili ushindani wowote watakaokutanishwa nao katika ngarambe ya msimu huu.

”Kiukweli tunafahamu timu zote zimepania kupambana mwanzo mwisho ili kuhakikisha tumepokonywa taji hilo ambalo tumelishinda mara 13,” Maina alisema na kutoa wito kwa kikosi chake kutokubali kupoteza kombe hilo.

You can share this post!

Kayaba Youth waapa kubeba taji la KYSD

Joho apata pigo huku wengi wakimuomboleza Hatimy