Sofapaka wampa kigogo Elly Asieche utepe wa unahodha
Na CHRIS ADUNGO
KUONDOKA kwa beki na nahodha George Maelo kambini mwa Sofapaka kumechochea kikosi hicho kilichotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009 kumpokeza kiungo Elly Asieche utepe wa ukapteni.
Asieche ambaye ni miongoni mwa wachezaji ambao wamehudumu kambini mwa Sofapaka kwa kipindi kirefu zaidi, amekuwa msaidizi wa Maelo.
Wachezaji wengine wanne ambao wamekatiza rasmi uhusiano wao na Sofapaka ni Waganda Nicholas Sebwato na Brian Kajuba, Ronald Okoth ambaye amestaafu soka na kiungo wa zamani wa Gor Mahia na Tusker, Lulumba Okeyo.
Rais Elly Kalekwa amesema kwamba mapengo yaliyoachwa na Sebwato na Kajuba yatajazwa na wanasoka wawili wazawa wa Rwanda.
“Kuna mabeki matata kutoka ugenini wakaojiunga nasi bila ada yoyote. Tumeafikiana na mawakala wao, wao wenyewe na familia zao. Ilivyo, dalili zote zinaashiria kuwa watajiunga nasi kufikia mwisho wa wiki hii,” akasema Kalekwa.
“Asieche ndiye nahodha wetu mpya. Anajaza nafasi ya Maelo ambaye ameagana nasi kwa pamoja na wanasoka wengine wanne. Usimamizi kwa sasa unajishughulisha sokoni ili kujaza nafasi walizoziacha wazi,” akaongeza katika kauli iliyoungwa na meneja wa timu ya Sofapaka, Hillary Echesa.
Sofapaka wamethibitisha kwamba juhudi zao za kumsajili beki wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed zimegonga ukuta baada ya nyota huyo wa Harambee Stars anayewaniwa na Yanga SC nchini Tanzania, kutaka Sofapaka kuweka mezani Sh6 milioni kwa ajili ya saini yake.
Musa alikuwa pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Sofapaka mnamo Aprili 2018 baada ya kuagana na FK Tirana ya Albania. Mkataba wake na mabingwa mara 12 wa Ligi Kuu ya Zambia, Nkana FC ulitamatika Juni 2020.
Wakati uo huo, fowadi veterani wa Sofapaka, Kepha Aswani anasema analenga kustaafu soka baada ya miaka mitatu ijayo na kubwa zaidi katika matamanio yake ya sasa ni kutwaa taji la mfungaji bora katika msimu wa 2020-21. Aswani alikuwa sehemu ya kikosi cha Mathare United kilichonyanya ubingwa wa Ligi Kuu ya humu nchini mnamo 2008.