Michezo

SURA TISHO: Liverpool yaicharaza Everton 1-0 dimba la FA

January 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MERSYSIDE, Uingereza

LICHA ya mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na kocha Jurgen Klopp, kikosi cha Liverpool kilionyesha kiwango cha juu cha mchezo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Everton na kufuzu kwa raundi ya nne ya dimba la FA Cup.

Bao hilo muhimu lilifungwa na kinda Curtis Jones katika mechi hiyo ya raundi ya tatu iliyochezewa Anfield, Jumapili usiku.

Klopp alifanyia mabadiliko tisa kikosi kilichoichapa Sheffield, Alhamisi katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Makinda walioanza kwa mara ya kwanzi ni Takumi Minamino, Nathaniel Phillps na Yasser Larouci ambaye aliingia katika kipindi cha pili.

Mfungaji ambaye ana umri wa miaka 18 alipachika wavuni bao hilo wavuni dakika ya 71 kutokana na kombora la umbali wa mita 15 ambalo lilimchanganya kipa wa kimataifa Jordan Pickford.

Everton waliishinda Liverpool kwa mara ya mwisho mnamo Septemba 1999.

Klopp alisema, “Nilishuhudia soka safi kutoka kwa wachezaji wasiokuwa na uzoevu, waliokuwa wakicheza kwa mara ya kwanza katika kiwango hicho, mbele ya mashabiki wengi, dhidi ya timu kubwa. Nilifurahia mno jinsi walivyojiamini na kusakata soka safi.”

“Yeyote anayetamani kuwa mchezaji wa Liverpool sharti aelewe desturi za timu hii. Hatuwezi kuwa bora kila wakati duniani, lakini tuna uwezo wa kupigana hadi dakika ya mwisho. Tutaendelea kudumisha historia ya klabu hii.”

Kocha huyo aliamua kuwapumzisha mastaa kadhaa wakiwemo Sadio Mane, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Virgil Dijk, lakini mkongwe James Milner alianza kabla ya kuumia na kutolewa nje baadaye.

Kwa upande mwingine, kocha Carlo Ancelotti wa Everton aliingiza uwanjani kikosi kikuu ambacho kilizua upinzani mkali, licha ya kupoteza nafasi kadhaa karibu na eneo la hatari.

Juhudi za Dominic Calvert-Lewin, Mason Holgate na Richardison kufunga mabao zilizimwa na kipa matata Adrian wa Liverpool.

“Tulipoteza kwa sababu tulishindwa kucheza vizuri katika kipindi cha pili. Tulipoteza nguvu, tulikosa imani, hatukuelewana vyema kuanzia nyuma kuelekea mbele.”

“Tutazungmza na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kutuwezersha kjuimarisha kikosi kizima,” aliongeza.

Uwepo wa Divock Origi uliiongezea nguvu katika safu ya ushambuliaji, huku safu ya kiungo ikimilikiwa na makinda.

Ngome ilikuwa chini ya kinda Phillps ambaye alirejea majuzi kutoka Stuttgart alikokuwa kwa mkopo. Jones ambaye alizaliwa miaka miwili baada ya Everton kushinda Liverpool kwa mara ya mwisho alionyesha kiwango cha juu katika mechi hiyo.

Hata Yasser Larouci aliyeingia katika nafasi ya Milner alishangaza wengi kutokana na ujasiri wake.