Tatu za KPL kuaga kipute cha MozzartBet Jumamosi na Jumapili
TIMU tatu za Ligi Kuu (KPL) lazima zitaaga kipute cha Kombe la Mozzartbet huku raundi ya 16 ikichezwa Jumamosi na Jumapili, washindi wakitarajiwa kutinga awamu ya robo-fainali.
Klabu 10 za KPL zilifuzu raundi ya 16 na kutakuwa na mechi tatu ambazo zitakutanisha timu za ligi hiyo.
Kipute kikubwa kitakuwa kati ya Shabana na Kakamega Homeboyz kwenye uga wa Jomo Kenyatta, Kaunti ya Kisumu mnamo Jumapili.
Mabingwa wa zamani Gor Mahia nao watasafiri Mombasa kuvaana na Bandari katika uga wa Mbaraki kesho ambapo mshambulizi matata Benson Omala anatarajiwa atapangwa baada ya kujiunga rasmi na timu.
Mechi nyingine kati ya timu za KPL ni Bidco United dhidi ya Ulinzi Stars kwenye uga wa Kenyatta, Machakos mnamo Jumapili kuanzia saa saba mchana.
AFC Leopards ilikata rufaa kuhusu uamuzi wa Mara Sugar kupewa ushindi baada ya mechi ya raundi ya 32 kati yao katika uga wa Jomo Kenyatta kuzingirwa na fujo.
Uamuzi huo ulitolewa na jopo la kutatua mizozo baina ya timu kwenye shirikisho la soka nchini mnamo Machi 19 lakini haukuridhisha Ingwe na wakakata rufaa.
Katika mechi hiyo, mashabiki wa Ingwe waliingia uwanjani dakika ya 89 kulalamikia hatua ya refa kubatilisha uamuzi wa hapo awali wa kuwapa penalti.
Kwa hivyo, Mara Sugar na Ingwe hazitachezea wikendi hii zikisubiri uamuzi wa rufaa hiyo ambapo atakayefanikiwa atazichapa na Compel FC inayoshiriki ligi ya divisheni ya pili na ina makao yake Webuye.
Kando na Compel, timu nyingine zisizokuwa za KPL ambazo zimebakia katika Mozzartbet Cup ni Denmark, Kapenguria United na Kibera Soccer.
Denmark itachuana na Kariobangi Sharks ugani Mbaraki Jumamosi huku Kapenguria United na Kibera Soccer zikiwa na miadi na Kenya Police na Murangá Seal mtawalia siku ya Jumapili.
Mshindi wa Mozzartbet Cup atatunukiwa Sh2 milioni pamoja na kuwahi tikiti ya kushiriki Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF) 2024/25 msimu ujao.