TULIZIDIWA: Spurs yala kipigo kikali Uefa
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KOCHA Mauricio Pochettino amekiri kwamba vijana wake wa Tottenham Hotspur walionekana kukata tamaa mwishoni mwa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kucharazwa 7-2 na Bayern Munich ya Ujerumani, Jumanne usiku.
Hii ni ishara tosha iliyoonyesha jinsi timu yake inavyokabiliwa na kibarua kigumu baada ya kuanza vibaya kampeni za msimu huu.
Spurs walianza kufunga bao na kuongoza kipindi cha kwanza kwa 1-0, kabla ya mambo kuharibika katika kipindi cha pili ambapo Serge Gnabry alifunga mabao manne. Mabingwa hao wa Bundesliga waliongeza mabao mengine matatu katika muda mfupi.
Pochettino aliwaweka wachezaji wake katika chumba cha kubadilishia nguo kwa muda mrefu kabla ya kutokea na kuwaambia kwamba itabidi wakubali matokeo hayo ya kushangaza na kujirekebisha kwa ajili ya mechi za usoni.
“Tulichanganyikiwa mara tu walipotufunga mabao matatu, kwani wachezaji walionekana kuwa wachovu,” Pochettino alisema.
“Hatimaye tulijaribu kupigana vikali lakini hatukufaulu,” aliongeza.
“Niliwaelezeni wiki kadhaa zilizopita kwamba utakuwa msimu mgumu kwetu. Baada ya kushindwa na Liverpool kwenye fainali ya Klabu Bingwa, tumeanza upya na kuna mengi ya kufanyika kabla turejee katika kiwango kizuri. Tunahitaji kujipanga upya kwa mipango ya muda mfupi na mipango ya muda mrefu.”
“Tumeshindwa hapa kihalali na lazima tukubali. Kilichobakia sasa ni kuendelea kucheza kama timu na kurejea kwa kishindo baada ya kichapo hiki,” aliongeza Pochettino.
“Tulifanya makosa ambayo yaliwawezesha kufunga mabao mengi. Tumeudhika kwa sababu ni vibaya kwa timu kama yetu kufungwa mabao mengi hivyo.
“Lakini, wakati mwingine ni muhimu kuelewa kuwa mambo kama haya hutokea mpirani. Awali msimu uliopita, tulicheza vizuri dhidi ya Manchester City na Ajax na tukafuzu kwa fainali. Lazima nasi tuelewe kwamba kushindwa ni kawaida.”
Kufikia sasa, Spurs wameshinda mechi tatu pekee kati ya 10 katika mashindano tofauti msimu huu, na wako mkiani mwa Kundi B sawa Olympiakos, na huenda wakakosa kutinga hatua ya 16 iwapo watashindwa na Red Star Belgrade katika mechi ifuatayo.
“Hakika ni vigumu kuongea mengi kwa sasa,” Pochettino alisema. “Sikuwalaumu wachezaji hata. Sasa ni wakati wa kuwapa nafasi watulie kwanza. Nitazungumza nao baadaye. Hatutajirekebisha kwa kufokeana; kila mtu ameudhika.
“Uwanjani, nilifurahia dakika za kwanza 30 za kipindi cha kwanza, lakini ghafla bin vuu mambo yalibadilika katika kipndi cha pili na tukashindwa vibaya. Hakuna yeyote uwanjani pale aliyetarajia matokeo kama haya mwishowe. Ni matokeo ya kushangaza mno kwa mashabiki na hata wachezaji.”