Michezo

“Uchawi” wa kocha wa Harambee Stars warejeshea mashabiki uwanjani

Na CECIL ODONGO March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa Harambee Stars Benni McCarthy amefanikiwa kurejesha matumaini ya wanasoka kwenye mchezo huo katika mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Gambia na Gabon.

Katika mechi hizo za Kundi F, Kenya ilitoka nyuma na kuagana sare ya 3-3 na Gambia Alhamisi iliyopita huku wakichapwa 2-1 kwenye mechi dhidi ya Gabon Jumapili (Machi 23, 2025).

Mchuano wa Jumapili uligaragazwa katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo na ukahudhuriwa na halaiki ya mashabiki akiwemo Rais William Ruto, Kinara wa Upinzani Raila Odinga, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi miongoni mwa wanasiasa wengine mashuhuri.

Akiongea baada ya mechi hiyo, McCarthy alifurahia jinsi ambavyo uwanja wa Nyayo ulifurika na akaweka wazi mpango alioanao kujenga timu imara ya taifa.

“Wakenya wanapenda mpira na hilo limedhihirika jinsi tumeshabikiwa nyumbani. Sasa ni kazi ya kujenga timu hii kwa kipute cha CHAN na pia mashindano yajayo,” akasema McCarthy.

“Kibarua ninacho cha kuangalia wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani, kutambua talanta na kuziba baadhi ya mianya ambayo ipo katika kikosi cha taifa. Vijana walicheza vyema dhidi ya Gabon na ni jukumu langu kujenga kikosi imara, na kila anayetosha kuwa timu, atakuwepo,” akaongeza.

Kando na kurejesha mashabiki uwanjani, kocha huyo raia wa Afrika Kusini mara hii alipata kweli kuhusu wachezaji wa kigeni na wale kutoka ligi za nchi waliojiunga na timu ya taifa

William Lenkumpae, Jonah Ayunga, Michael Olunga na Timothy Ouma ni wachezaji kutoka ligi za nje ambao waling’aa kwa Stars.

Katika wachezaji wa ligi za nyumbani, Mohamed Bajaber alifunga bao la hadhi dhidi ya Gambia naye Rooney Onyango alicheza vizuri sana katika mechi ya Gambia pia.

Licha ya kupoteza dhidi ya Gabon, Kenya ilionyesha mchezo wa juu na McCarthy alikiri kuwa timu inahitaji marekebisho machache na wachezaji kujituma jinsi walivyofanya kuanza kupokea matokeo mazuri uwanjani.