UEFA: Salah, Mane na Firmino vs Neymar, Mbappe na Cavani
Na CECIL ODONGO
MECHI za kuwania klabu bingwa barani Uropa msimu wa 2018/19 hatimaye zinarejea kuanzia Jumanne ya Agosti 17 na Jumatano ya Agosti 18 katika viwanja mbalimbali baada ya Real Madrid kutia kibindoni ubingwa wa mwaka 2017.
Hata hivyo mechi kubwa Jumanne itakuwa ya Kundi C kati ya Liverpool na PSG ugani Anfield kuanzia saa nne usiku baada ya kikosi cha Inter Milan ya Italia kutesa dhidi ya Tottenham Hot Spur ya Uingereza katika mechi ya kundi A saa mbili kasoro dakika tano.
Wachezaji nyota Mohamed Salah, Roberto Firmino, Sadio Mané wa Liverpool watakabiliana vikali na wenzao Neymar, Kylian Mbappé na Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain katika mechi inayotarajiwa kuvutia utazamaji wa mamilioni ya mashabiki wa soka nchini na duniani.
Mibabe wa soka ya Ufaransa Monaco ndio watafungua pazia ya msimu huu watakapokabana koo na mabingwa wa ligi ya Uropa msimu jana(2017/2018) Atletico Madrid nyumbani katika mechi ya mapema itakayomshuhudia starika wa Colombia Radamel Falcao akipiga dhidi ya waajiri wake wa zamani.
Rekodi ya vijana wa Diego Simeone dhidi ya wapinzani kutoka Ufaransa ni duni mno. Kati ya michuano tano iliyowakutanisha awali wameweza kuibuka na ushindi mara moja tu. Mechi hiyo itaanza saa mbili kasoro dakika tano usiku.
Barcelona ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali katika ligi ya Laliga msimu huu wataikaribisha PSV kutoka Uholanzi katika mechi ya kundi B. ‘The Catalans’ wanaojivunia huduma za Mastaa Lionnel Messi na Luiz Suarez bado wana machungu ya kubanduliwa katika awamu ya robo fainali na AS Roma ya Italia msimu wa 2017/18.
Mechi nyingine zitakazosakatwa Jumanne kuanzia saa nne ni Schalke vs Porto, Red Star Belgrade vs Napoli, Club Brugge vs Borussia Dortmund na Galatasaray vs Lokomotiv Moscow.