UEFA Valentino Dei: KTN Home kuonyesha Liverpool ikivaana na Porto
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI matata wa Liverpool na straika wa timu ya taifa ya Brazil, Roberto Firmino wamesema kwamba uthabiti unaojivuniwa na miamba hao wa soka ya Uingereza katika safu yao ya uvamizi ni moja kati ya mambo yatakayowachochea kuyazima makali ya FC Porto usiku wa Jumatano nchini Ureno.
Vikosi hivyo viwili vitashuka dimbani kuvaana katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Estadio do Dragao saa 22.45.
Kipute hicho kitapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya KTN Home kwa ushirikiano na kampuni ya Mediapro kutoka Uhispania.
Kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp, kikubwa zaidi kitakachowatambisha vijana wake ni kiu ya kuendeleza ubabe walioudhirisha katika mechi za makundi ambapo Liverpool waliibuka kidedea baada ya kuwapiga kumbo Sevilla, Maribor na Spartak Moscow.
Mabao 23
Katika kampeni hizo, masogora hao wa Klopp walitikisa nyavu za wapinzani mara 23 huku Firmino akipachika wavuni jumla ya mabao sita.
Nyota mzawa wa Misri, Mohamed Salah ambaye anatazamiwa Jumatano kuongoza idara ya ushambuliaji ya Liverpool alitia kapuni mabao matano sawa na kiungo Phillipe Coutinho aliyejiunga na Barcelona mnamo Janauri 2018.
Liverpool wanajibwaga katika mchuano huo wakitawaliwa na motisha ya kuwakomoa Southampton 2-0 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza wikendi iliyomshuhudia Salah akijizolea bao lake la 29 hadi kufikia sasa katika michuano yote aliyowapigia waajiri wake hao.
Virgil van Dijk
Mchuano huo utakuwa jukwaa mwafaka vilevile kwa beki ghali zaidi duniani, Virgil van Dijk kudhihirisha ukubwa wa uwezo alionao katika soka ya bara Ulaya huku Porto wakipania kuzitegemea pakubwa huduma za mafowadi Vincent Aboubakar na Moussa Marega.
Hadi kufikia sasa, Aboubakar amewafungia Porto jumla ya mabao 26 kutokana na michuano 32 iliyopita huku Marega akizititiga nyavu za wapinzani wao mara 16 katika mechi 20 zilizopita.