Michezo

Uingereza yajiandaa kung’oa kisiki Uhispania na kupiga sherehe Euro 2024

Na MASHIRIKA July 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, Uingereza

WAINGEREZA wanajiandaa kwa sherehe kubwa wikendi hii wakipanga kujaza baa na maeneo yaliyo na runinga kubwa kutazama timu yao ya taifa ikifukuzia taji la kwanza tangu mwaka 1966 itakapovaana na Uhispania katika fainali ya Kombe la Ulaya (Euro) 2024.

Fainali hiyo itasakatwa ugani Olympiastadion, Ujerumani hapo kesho saa nne usiku, huku mamilioni ya mashabiki kutoka Uingereza wakitarajiwa kukuja pamoja kushabikia timu yao almaarufu Three Lions ikitafuta kushinda Euro kwa mara ya kwanza kabisa.

Vijana wa kocha Gareth Southgate walipoteza 3-2 katika fainali ya makala yaliyopita kwa njia ya penalti dhidi ya Italia ugani Wembley.

Hapo kesho, runinga kubwa kabisa itakuwa katika ukumbi wa The O2 jijini London ulio na uwezo wa kusitiri mashabiki 15,000. Meya wa London Sadiq Khan ameandaa sherehe ya ukumbini The O2.

Mashabiki pia watakuwa katika bustani na baa zitakazokuwa zikionyesha fainali hiyo, huku wanabiashara wakitarajiwa kuvuna vilivyo.

Tayari mashabiki wengi wameomba serikali iwape likizo Jumatatu kusherehekea iwapo Three Lions itafanikiwa kung’ata mabingwa wa Euro wa mwaka 1964, 2008 na 2012, Uhispania.

Maduka kadhaa makubwa yametangaza kuwa yatafungwa mapema ili kuwapa wafanyakazi fursa ya kutazama fainali hiyo bila kuwakata mshahara. Bei ya bia inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 250 navyo vyakula kadhaa kwa karibu asilimia 150.

Ripoti nchini Uingereza zinasema kuwa mashabiki wengi wanapanga kupigia mabosi wao simu kuwafahamisha kuwa wanaugua ili wasiingie kazini Jumatatu iwapo Uingereza itatwaa taji.

Kwa mujibu wa kampuni ya BrightHR, wafanyakazi 1.5 milioni wanatarajiwa kutafuta likizo Jumatatu. Maombi ya kuenda likizo ya kila mwaka pia yameongezeka kwa asilimi 121.

Kampuni hiyo imebashiri kuwa wafanyakazi wengine 1.5 milioni watapiga simu kusema kuwa wao ni wagonjwa.

Mamia ya maelfu ya mashabiki wanaaminika watafika kazini kuchelewa, huku milioni 10 wakitarajiwa kufanya kazi nyumbani.

Uhudhuriaji

Bright HR, ambayo hufuatilia mahudhurio ya wafanyakazi katika kampuni 50,000 nchini Uingereza, ilisema kuwa visa vya wafanyakazi kutoa sababu kuwa ni wagonjwa vilipanda hadi asilimia 232 siku moja baada ya fainali ya Euro 2020.

Baadhi ya shule pia zimeeleza wanafunzi wao kuwa wanaweza kutazama fainali Jumapili na kufika shuleni kuchelewa kwa saa mbili Jumatatu.

Mwanamfalme William, ambaye ni rais wa Shirikisho la Soka nchini Uingereza, anatarajiwa kuhudhuria fainali ugani Olympiastadion.

Waziri Mkuu Keir Starmer, ambaye alikuwa uwanjani wakati Three Lions walitoka chini bao moja na kupiga Uholanzi 2-1, amethibitisha kwamba atashuhudia pia fainali ya kesho.

Sherehe zinatarajiwa kunoga Jumatatu iwapo Uingereza itaduwaza Uhispania. Kuna mipango ya timu hiyo kulakiwa kishujaa jijini London na pia kuzuru Kasri la Buckingham.