Michezo

Wakenya wafukuza donge nono Diamond League, wakwepa Jumuiya ya Madola

February 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI wengi nyota wa Kenya hawajasisimuliwa na mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika nchini Australia mnamo Aprili 4-15, 2018.

Badala yake wameamua kutafuta donge nono kwenye Riadha za Diamond League.

Baadhi ya watimkaji shupavu walioamua kulenga macho yao kwa Riadha za Diamond League zitakazofanyika kutoka Mei 4 hadi Agosti 31, 2018 ni bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 800, David Rudisha.

Mshikilizi huyu wa rekodi ya dunia ya mbio hizo za mizunguko miwili alishinda medali ya fedha miaka minne iliyopita Kenya ilipomaliza juu ya jedwali la riadha kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola kwa dhahabu 10, fedha 10 na shaba tatu.

Bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 1,500 mwaka 2008 Asbel Kiprop, mfalme wa Nusu-Marathon duniani Geoffrey Kamworor na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya mbio za kilomita 21 Peres Jepchirchir hawatashiriki mashindano hayo nchini Australia.

Kiprop ameamua kuelekeza nguvu zake katika maandalizi ya Riadha za Diamond League, ambazo mshindi hutunukiwa Sh5, 062,500.

Bingwa wa New York City Marathon Kamworor atatetea taji lake la Nusu-Marathon duniani mnamo Machi 24, siku chache tu kabla ya mashindano ya Jumuiya ya Madola kuanza.

Jepchirchir, ambaye alishinda Nusu-Marathon duniani mwaka 2016 jijini Cardiff, Wales, yuko katika likizo ya uzazi.  Kamworor na Jepchirchir walijishindia karibu Sh3, 039,060 kila mmoja jijini Cardiff.

Malkia wa mbio za mita 1,500, Chepng’etich, ambaye alinyakua mataji ya Jumuiya ya Madola (2014), Olimpiki (2016) na Dunia (2017), pia yuko katika likizo ya uzazi.

Bingwa wa mbio za mita 800 wa Jumuiya ya Madola mwaka 2006, Janeth Jepkosgei, 34, ni mmoja wa wakimbiaji 170 walioalikwa kushiriki mchujo wa kuunda timu ya kuenda Australia.

Mchujo huo utafanyika katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi hapo Februari 17, 2018. Wanariadha 60 watapata tiketi ya kupeperusha bendera ya Kenya mjini Gold Coast, Australia.