Michezo

WINDO LA BAYERN: Wilfried Zaha avutia wakubwa Allianz Arena

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MUNICH, UJERUMANI

BAYERN Munich wako tayari kuweka mezani kima cha Sh11 bilioni zinazodaiwa na Crystal Palace kwa minajili ya huduma za fowadi matata wa Ivory Coast, Wilfried Zaha, 26.

Zaha aliwataka Palace kumwachilia mwanzoni mwa Julai ili atue uwanjani Emirates kuwajibikia Arsenal.

Hata hivyo, Sh5 bilioni ambazo Arsenal wapo radhi kuweka mezani ili kumsajili nyota huyu wa zamani wa Manchester United ni chini ya nusu ya fedha zinazotakiwa na vinara wa Palace.

Kusuasua kwa Arsenal kuboresha ofa yao kwa nia ya kumshawishi Zaha kujiunga nao ni jambo ambalo kwa sasa limemchochea kocha Niko Kovac wa Bayern kutuma maskauti wake nchini Uingereza kwa nia ya kuanzisha mazungumzo na Palace kuhusu uwezekano wa kujinasia maarifa ya sogora huyu.

Bayern wanalenga kusajili chipukizi wengi zaidi muhula huu hasa baada ya kuagana na maveterani Arjen Robben, Franck Ribbery na Thomas Muller.

Hatua ya Bayern kuwania maarifa ya Zaha inachochewa na kuambulia patupu kwa jitihada zao za kujinasia huduma za kiungo Leroy Sane wa Manchester City.

Awali, Bayern walikuwa pia wakihusishwa na uwezekano mkubwa wa kujinasia maarifa ya mvamizi Callum Hudson-Odoi kutoka Chelsea baada ya juhudi za kumshawishi Gareth Bale wa Real Madrid kujiunga nao kuambulia pakavu.

Hata hivyo, kocha Kovac amesisitiza kwamba Bale angali na fursa ya kutua ugani Allianz Arena iwapo atazitupilia mbali ofa anazoelekezewa sasa na PSG na Beijing Guoan kutoka Ufaransa na China mtawalia.

Zaidi ya Bayern, kikosi kingine kinachowania zaidi maarifa ya Zaha ni Everton ambao wamefichua nia ya kuweka mezani kima cha Sh9 bilioni ili kujinasia huduma za sogora huyu.

Palace almaarufu ‘The Eagles’ wanajitahidi sana kumkwamilia Zaha ambaye alikamilisha kampeni za msimu jana akiwa na mabao 10 kapuni mwake. Aidha, alichangia mabao mengine matano yaliyofumwa wavuni na waajiri wake hao.

Kuvunja moyo

Katika mojawapo ya njia za kuwavunja moyo Arsenal na Everton, Palace wamefichua kwamba thamani ya sogora huyu kwa sasa imefikia kiasi cha Sh11 bilioni.

Everton wapo radhi kuweka mezani kiasi hicho cha fedha hasa ikizingatiwa kwamba wana zaidi ya Sh3 bilioni walizozipata kutokana na mauzo ya kiungo Ademola Lookman aliyejiunga na RB Leipzig ya Ujerumani.

Kulingana na Farhad Moshiri ambaye ni mmiliki wa Everton, kikosi chake kipo radhi kufungulia mifereji ya pesa muhula huu na kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji.

Mapema mwaka huu, Zaha alifichua ukubwa wa kiu ya kujiunga na kikosi kitakachopiga soka ya UEFA msimu ujao. Hata hivyo, Judicael Zaha, 26, amesisitiza kwamba kaka yake huyo anapania sana kuvalia jezi za Arsenal kwa kuwa amekuwa shabiki sugu wa kikosi hicho tangu utotoni. Zaha ambaye angali na mkataba wa miaka minne kati yake na Palace, kwa sasa hupokezwa mshahara wa hadi Sh18 milioni kwa wiki ugani Selhurst Park.