Makala

Mji wa Kainuk ulivyosalia mahame licha ya usalama wa hali ya juu

April 27th, 2024 2 min read

SAMMY LUTTA NA LABAAN SHABAAN

LICHA ya hali ya usalama kuanza kurejea mjini Kainuk – mpakani mwa Turkana na West Pokot – wasafiri hawatii nanga hapo kufurahia chakula na malazi.

Kiwango cha utovu wa usalama kilishuka sababu ya kukitwa kwa kambi za vitengo mbalimbali vya vikosi vya usalama.

Magari ya ulinzi kutoka idara ya polisi na ile ya kijeshi yametapakaa maeneo hayo lakini magari ya abiria yameadimika mjini humo.

Hoteli zilizo sambamba kando ya barabara hazina uhakika kwamba zitapata wateja wa kutosha kuzuru humo.

Awali mikahawa hii iliwasaidia wasafiri wengi kupata mapochopocho na vinywaji mbali na kupumzika.

Baada ya usalama kudorora, magari mengi yalikosa kusimama hapo kama awali.

Kwa sasa, aghalabu wasafiri hutua eneo la Marich Pass, Pokot Magharibi na Lokichar, Turkana ambapo wanasongamana hotelini na maegeshoni mwa magari.

Mkazi wa Lodwar Bi Catherine Kokoi anaamini ukishinda sana Kainuk utajialikia balaa ya kushambuliwa.

“Kuna mtazamo kuwa kabla ya shambulizi, kuna wapelelezi ambao huwapa habari majangili msituni kuhusu magari ambayo yanaingia ama kutoka Kainuk bila kulindwa na kikosi cha usalama,” alifichua Bi Kokoi.

Barabara inayopita mji wa Kainuk, Turkana. Picha|Maktaba

Anaeleza madereva huendesha magari kwa mwendo wa kasi wakipita Kainuk. Na hii huwapa wapiga mbiu wakati mgumu kujua kama gari lina ulinzi.

Wakulima hushambuliwa na majahili licha ya kuendeleza shughuli zao kando ya Mto Malmalite ulio karibu na mji wa Kainuk.

Baada ya Bi Jane Akal kufiwa na mumewe mikononi mwa wezi wa mifugo 2019, alikumbatia kilimo kuwa njia ya kujikimu kiuchumi.

Anakumbuka kuwa magari awali yalisimama Kainuk na kumpa wateja wa mboga, chakula na vinywaji – hali si hivyo tena.

“Mashambulizi mfululizo yaliathiri shughuli zetu za kawaida zikihusisha kilimo, uchomaji makaa na utemaji kuni kibiashara. Tulitarajia mpango wa udumishaji usalama ungesaidia kurejesha wateja lakini sasa wamehamia miji mibadala,” alisikitika.

Mkazi mwingine wa Kainuk Bi Margaret Arot anataja kuwa usalama umeimarishwa tangu Februari 2023 maafisa wa polisi na majeshi walipotumwa huko.

Hii ilijiri siku nne baada ya maafisa wanne wa polisi kuuliwa, magari kuteketezwa na majahili waliojeruhi watu saba katika barabara ya Kitale – Lodwar.

“Mwanzoni tulikuwa na hofu hata ya kutembea kwa mita 200 kutoka nyumbani. Kuongezwa kwa vikosi vya jeshi kuwapiga jeki polisi wa vitengo mbalimbali vya polisi kulisaidia kukabili mashambulizi,” alikiri Bi Arot.

Kulingana naye, sasa wanaendeleza kilimo kando ya Mto Turkwel kwa usalama.

Pia watoto wao huenda shuleni na kurejea salama nyumbani.

Ila analalamika kuwa kama hawatapata wateja kutoka kwa wasafiri, mji huo wenye barabara nzuri hautaamka tena.