Habari za KitaifaMakala

Hasara za moto shuleni zinaweza kuepukika mikakati ya usalama ikizingatiwa

Na CHARLES WASONGA September 7th, 2024 2 min read

MNAMO Septemba 6, 2024 asubuhi, taifa lilikumbwa na majonzi kufuatia mkasa ambapo wanafunzi 18 wa Shule ya Hillside Endarasha Academy, iliyoko Kieni, Nyeri, walikufa baada ya moto kuteketeza bweni lao mwendo wa saa tisa za usiku. Wanafunzi 16 waliteketea kiasi cha kutoweza kutambuliwa na wawili wakafa wakipokea matibabu.

Wanafunzi 27 walipata majeraha mabaya ya moto hadi 70 wakiwa hawajulikani waliko hadi tulipokuwa tukiandaa makala haya.

Lakini ikumbukwe kuwa tangu miaka ya 1990s, shule kadhaa zimewahi kukumbwa na mikasa kama hii na wanafunzi kuangamia.

Shule hizo ni pamoja na; Shule ya Upili ya St Kizito, iliyo Tigania, Meru, Shule ya Upili ya Wasichana ya Bombolulu iliyoko karibu na mji wa Mazeras, kaunti ya Kwale, Shule ya Upili ya Nyeri, Shule ya Upili ya Kyanguli, iliyoko Machakos, Shule ya Upili ya Wavulana ya Endarasha, Nyeri, Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Eldoret, Shule ya Msingi ya Mabweni ya Asumbi, Homa Bay, miongoni mwa zingine.

Mkasa mbaya zaidi

Hata hivyo, mkasa wa Shule ya Upili ya Kianguli ambapo wavulana 67 waliangamia ndio ulikuwa mbaya zaidi katika historia ya Kenya.

Moto huo ulisemekana kuanzishwa na wanafunzi wawili wenye umri wa miaka 16 walioripotiwa kukerwa na usimamizi wa shule hiyo.

Ni kutokana na mikasa kama hiyo ambapo serikali, kupitia Wizara ya Elimu ilichapisha Mwongozo wa Usalama Shuleni mnamo mwaka wa 2008.

Chapisho hilo kwa jina “Safety Standards Manual For Schools in Kenya 2008” linasheheni mikakati inayopasa kutekelezwa kulinda usalama wa wanafunzi shuleni kwa kuzuia aina mbalimbali ya mikasa, ikiwemo ya moto.

Kwanza, kulingana na chapisho hilo kila shule inapasa kuwa na Kamati ya Usalama yenye wajibu wa kufuatilia usalama wa wanafunzi madarasani, kwenye mabweni na katika maeneo mengine endapo kutatokea hatari yoyote.

Aidha, linasema kuwa madarasa na mabweni yanafaa kujengwa kwa namna itakayowazesha wanafunzi kujiokoa au kuolewa kunapotokea hatari yoyote.

Milango rahisi kufunguka

Kwa mfano, milango ya mabweni yajengwe kwa namna inayoweza kufunguliwa haraka kwenda nje. Madirisha nayo yawe ni ya kufunguka kuelekea nje na yasiwe na vyuma (grills).

Nafasi kati ya vitanda isipungue upana wa mita 1.2 ili kutoa nafasi ya wanafunzi kupita.

Aidha, nafasi ya kupitia katikati mwa mabweni, sharti iwe na upana wa angalau mita mbili kupitika kwa urahisi hali ya hatari inapotokea.

Mwongozo huo pia unapiga marufuku mwenendo wa wanafunzi wawili kulazimishwa kutumia kitanda kimoja na hivyo bweni moja kujaa wanafunzi kupita kiasi kinachoruhusiwa.

Mabweni yote shuleni pia yanapasa kuwekewa vifaa vya kuzima moto na maeneo ya kutorokea nyakati za hatari.

Milango ya mabweni inapasa kusalia imefungwa nyakati ambapo wanafunzi hawapo, wakiwa madarasani au katika shughuli za michezo.

Mwongozo huo pia unawahitaji walimu kufanya ukaguzi katika mabweni kila mara kabla ya wanafunzi kulala kuhakikisha kuwa masharti yote ya usalama yamezingatiwa.

Rekodi kuhusu idadi ya wanafunzi walioko ndani ya mabweni kila siku inafaa kuhifadhiwa na walinzi kushika doria kila mara kukagua hali ya usalama.

Wageni, wakiwemo wazazi hawafai kuruhusiwa kuingia ndani ya mabweni bila idhini maalum kutoka kwa mwalimu mhusika.

Lakini baada ya kutokea kwa mkasa wa moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy, wadau katika sekta ya elimu wakiwemo viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya walimu, walilalamika kuwa usimamizi wa mabweni umefeli kutekeleza masharti hayo ya usalama shuleni.

“Hii inatokana na kuzembea kwa Wizara ya Elimu, haswa Idara ya kuhakikisha ubora unazingatiwa katika shughuli zote shule,” akasema Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) Omboko Milemba.