Habari za Kitaifa

Mpasuko KUPPET kuhusu kusitishwa kwa mgomo wa walimu

Na VITALIS KIMUTAI September 4th, 2024 2 min read

MIGAWANYIKO imeibuka katika Chama cha Kutetea Maslahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) baada ya Bodi yake Kuu ya Kitaifa (NEB) kufutilia mbali mgomo wao Jumatatu, Septemba 3, 2024 bila kushauriana na asasi yenye usemi mkubwa zaidi katika chama hicho.

Hii imepelekea maafisa wake kutoka kaunti zote 47 kupinga hatua hiyo wakihisi kutohusishwa wakati wa kufikiwa kwa uamuzi huo.

Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) la KUPPET ndilo lenye usemi mkubwa zaidi na linashirikisha makatibu kutoka matawi yote 47 na wanachama 10 wa NEB.

NGC ndio yenye mamlaka ya kuanzia mchakato wa mgomo au kuufutilia mbali.

Mnamo Jumapili, Septemba 1, 2024 wanachama wa NGC walikutana katika mkahawa wa Sportsview, Kasarani, Nairobi na kuamua kwamba mgomo uendelee katika wiki yake ya pili kuanzia Jumatatu, Septemba 2, 2024.

Baraza hilo halijabatilisha uamuzi wake, ambao bado unapasa kuzingatiwa na wanachama wote wa KUPPET.

Taifa Dijitali ilifahamishwa kuwa NGC waliamua kuwa mabadiliko yoyote kuhusu hali ya mgomo ujadiliwe katika mkutano utakaoitishwa na Katibu Mkuu Akello Misori na kufanywa katika majukwaa ya mitandao.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu, Septemba 2 utaratibu huo haukufuatwa wakati ambapo NEB ilifutilia mbali mgomo. Hii ni kufuatia mkutano wa saa nyingi uliofanywa na wanachama wa NEB na maafisa wakuu wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) wakiongozwa na Afisa Mkuu, Nancy Macharia.

Uamuzi wa kufutiliwa mbali kwa mgomo huo, ambao ulikuwa umeingia wiki yake ya pili, ulimkasirisha Katibu wa KUPPET anayesimamia Shule za Upili, Edward Obwocha na akaondoka katika mkutano huo kwa hasira.

“Wanachama wote wa NGC walikubaliana Jumatatu kwamba wanachama wa NEB wangeshauriana na wadau wote, akiwemo Rais William Ruto, kuhusu hali ya mgomo. Lakini uamuzi wa mwisho wa kufutilia mgomo ungetolewa na wanachama wa baraza la NGC. Msimamo huo haukuheshimiwa,” akasema mwanachama mmoja wa NGC aliyeomba tubane jina lake mnamo Jumanne, Septemba 3, 2024.

Bw Obwocha aliambia Taifa Dijitali, kwenye mahojiano, kwamba KUPPET ilitoka “mkono mtupu” katika mkutano wake na TSC kwa sababu utaratibu uliowekwa haukufuatwa kufutilia mbali mgomo.

“Hatukutia saini utaratibu wa kurejea kazini ilivyodaiwa. Badala yake, Katibu Mkuu alitia saini taarifa kwa vyombo vya habari, akidai ni stakabadhi hiyo ya kisheria. Hakukuwa na stakabadhi inayoelezea utaratibu wa kurejea kazini,” Bw Obwocha akasema.

Akaongeza: “Niliondoka mkutano huo kwa sababu TSC ilikataa kutupa stakabadhi hiyo ili iwasilishwe kortini. Kwa miaka mingi, TSC haijakuwa ikiongozwa na nia njema inapofanya chochote kile haswa kinachohusiana na masilahi ya walimu. Kwa hivyo, hakuna kitakachobadilika.”

Imetafsiriwa na Charles Wasonga