Habari za Kitaifa

Mshtuko miili sita ikitolewa ndani ya timbo la kina kirefu mtaani Pipeline


WAKAZI katika eneo la Pipeline, Kaunti ya Nairobi, Ijumaa walikumbwa na mshtuko baada ya miili sita kupatikana ikiwa imetupwa kwenye timbo moja lililoachwa kutumiwa eneo hilo.

Miili hiyo, baadhi ikiwa imeanza kuoza na kuharibika vibaya, ilipatikana ikiwa ndani ya magunia na mifuko ya plastiki.

Maafisa wa polisi walishirikiana na wakazi waliojitolea kutoa miili hiyo huku mamia ya watu waliokusanyika kushuhudia tukio hilo wakihofia kuwepo miili zaidi iliyotupwa katika timbo hilo lenye kina kirefu.

Wakazi wamelalamikia kuzorota kwa usalama ikiwemo ongezeko la visa vya watu kujitia kitanzi eneo hilo.

Aidha, wamelaumu polisi kwa utepetevu na kukosa kuchukua hatua kwa wakati ufaao, hali iliyosababisha majuzi raia kuchukua hatua mikononi mwao na kuwateketeza washukiwa watatu wa wizi.

Uvumbuzi huo ulionekana kuchemsha ghadhabu ya Wakenya waliokuwa wametulia hasa baada ya Rais William Ruto kuvunja Baraza lake la Mawaziri Alhamisi na kuwafuta kazi mawaziri wote.

Inahofiwa kuwa miili hiyo ni ya watu waliouawa na polisi wakati wa maandamano katika eneo la Githurai na Rongai, Nairobi, kabla ya kutupwa eneo hilo.

Visa vya watu kutekwa nyara na kupatikana baadaye wakiwa wameuawa kikatili vimeongezeka mno katika siku za hivi karibuni kufuatia maandamano kote nchini yaliyoendeshwa na vijana almaarufu Gen Z kupinga Mswada wa Fedha 2024.