Habari Mseto

Mvumbuzi wa ‘Kata Simu, Tupo Site’ akata kamba… Je, ulimjua?

March 21st, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

TANZANIA inaomboleza kifo cha mcheshi Umar Iahbedi Issa almaarufu ‘Mzee Mjegeje’ aliyefariki mnamo Jumatano.

Ripoti zilieleza kuwa marehemu, anayesifika kwa video yake ya kicheshi “Kata simu tupo site”, alifariki nyakati za asubuhi katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Kulingana na meneja wake, Real Jimmy, marehemu alikuwa akipokea matibabu katika hospitali hiyo, ijapokuwa hakueleza maradhi aliyokuwa akikumbwa nayo.

Mzee Mjegeje, aliyefahamika pia kama ‘Raisi wa Bagamoyo’, anatoka katika mji wa Bagamoyo, ukanda wa Pwani mwa taifa hilo.

Aliibukia kuwa maarufu kupitia video “Kata simu tupo site” ambayo iliwachangamsha watu wengi, hasa nchini Kenya mwaka 2022.

Kwenye video hiyo, Mzee Mjegeje anasisitiza kwamba lazima angetaka simu ya mtu aliyekuwa akimpigia, kwani alikuwa katika eneo la ujenzi kwa kusema, “Kata simu, kata simu, tupo site. Hatutaki usumbufu, unaelewa?”

Kauli hiyo iliibukia kuwa maarufu, huku ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na hata kutumiwa na wanamuziki kwenye nyimbo zao.

Marehemu alikuwa ameshirikiana na watu kadhaa maarufu katika tasnia ya sanaa nchini Tanzania, akiwemo mwanamuziki Harmonize.

Pia, alikuwa ameeleza nia yake kushirikiana na mwanamuziki Diamond Platnumz.

Amemwacha mke na mtoto mmoja.