Makala

Mwalimu Dida alifungwa jela kwa kukosana na mkewe wa nne raia wa Amerika


MWALIMU Mohamed Abduba Dida aliwasili Illinois  Januari, 2019 ili kuendeleza masomo yake akiwa na nia ya kurejea Kenya mwishoni mwa safari yake ya masomo.

Akiwa Illinois, mtu ambaye aliyegombea urais mara mbili na kushindwa  alifanya harusi yake ya nne.

Dida alikuwa tayari ameoa wanawake watatu nchini Kenya, lakini moja ya ndoa zake iliishia kwa talaka.

Watu  wa familia yake, wakiwemo wake wake wengine wawili, hawakujali uamuzi wa mwalimu huyo wa zamani kuoa.

Kupitia ndoa aliyofanya Amerika, mtoto alizaliwa, wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto wengine kumi na wawili wanaoishi nchini Kenya.

Mambo yalibadilika sana mnamo Julai, 2021 wakati Dida na mkewe walihusika katika mzozo ambao ulimfanya afungwe jela miaka saba.

Mnamo Jumanne, familia ya Dida ilisema katika mahojiano kuwa licha ya masaibu yake, mke huyo wa Amerika bado ni sehemu ya familia yao kwani hajawasilisha kesi ya talaka.

Mke wa pili wa Dida, Amina Halake, mama Habiba na kifungua mimba  wake  Luqman waliwaongoza wanafamilia kueleza kuwa wanajitahidi kupata wakili ili kumsaidia katika rufaa yake.

“Mwalimu Dida hakuwakilishwa mahakamani kwa sababu alifikiria kuwa ni mgogoro mdogo wa nyumbani ambao ungetatuliwa kwa mazungumzo. Alijiwakilisha na ninafahamu kuwa amewasilisha rufaa na ananiambia rufaa hiyo ina nafasi kubwa ya kufaulu,” Amina alisema.

“Kama familia, tunajaribu kutafuta njia ya kumtembelea na kutafuta wakili  kuweza kumsaidia. Tunaomba serikali kuingilia kati kwa kuwa kuna yale ambayo hatuwezi kufanya,” aliongeza.

Nambari ya simu ambayo familia ya Dida ilitupatia, na ambayo wanasema ni ya mwanamke huyo wa Amerika, haikujibiwa.

Arafa tulizotuma kwa nambari ya simu tukitaka kuthibitisha mmiliki wake aliyesajiliwa na kuomba mahojiano hazijajibiwa pia.

Amina anashikilia kuwa baada ya mzozo huo, mke mpya wa Dida alifanikiwa kupata agizo  kumzuia ili asiwe karibu naye au kuingia nyumbani kwao.

Aliongeza kuwa Dida alisisitiza kuingia kwenye nyumba hiyo, na pia katika msikiti anaohudhuria mwanamke huyo, jambo ambalo lilizaa masaibu yake.

Amina alisema kuwa aliwasiliana na mke wa Dida wa Amerika mara kadhaa ili mzozo huo utatuliwe kwa mazungumzo au Shariah, lakini hakufanikiwa.

Familia ya Dida inasisitiza kuwa kilichomsukuma jela ni mzozo wa nyumbani ambao ulipaswa kutatuliwa kwa mazungumzo au kwa mujibu wa  Shariah.

Amina aliongeza kuwa alifahamu kuhusu kufungwa kwa Dida kupitia mke wake wa Amerika, baada ya kushindwa kumpata kwa simu kwa siku kadhaa.

“Mwalimu Dida alikuwa akiwasiliana nasi mara kwa mara na  alisema kulikuwa na shida kati yake na mkewe. Ghafla, tuliacha kupata  simu kutoka kwake. Mwalimu Dida ni mtu wa familia, ana majukumu na alisimamia majukumu yake kwa bidii sana. Lakini mnamo 2022 tulipokosa simu zake kwa zaidi ya siku 10, tuliingiwa na wasiwasi kwa sababu alikuwa ameripoti mapema kwamba mambo hayakuwa mazuri sana kati yake na mke wake mpya,” Amina alisema.

“Nilipopoteza mawasiliano kabisa, niliwasiliana na mama Leila na ndipo aliponithibitishia kuwa alikuwa salama, alikuwa jela.”

Dida anatarajiwa kutoka gerezani Aprili 3, 2029. Rufaa  ambayo mgombea urais huyo wa zamani amewasilisha kutaka uhuru wa kufuata dini yake linaonyesha kuwa Big Muddy ni gereza la tatu kuzuilia Dida.

Kati ya Aprili na Oktoba 2022, alifungiwa katika gereza la Moline Mashariki kabla ya kuhamishwa hadi gereza la Kusini Magharibi.

Hatimaye alipelekwa katika gereza la Big Muddy mnamo Januari, 2023.

Familia inadai kuwa Dida amekuwa mgonjwa, na amenyimwa huduma za matibabu.

Habiba, ambaye sasa ana umri wa miaka 81, alisema anatumai serikali ya Kenya inaweza kuingilia kati ili Dida apate usaidizi unaohitajika kwa kwani anaugua kisukari.

“Naomba serikali yangu iingilie suala hili, na serikali ya Amerika ijue yeye (Dida) ni mgonjwa. Ana kisukari na shinikizo la damu. Amenyimwa nafasi za kupata dawa,” alisema.

Familia hiyo ilisema licha ya hali hiyo, Dida bado anafanya jitihada za kuwasiliana na familia yake alipopewa fursa ya kupata simu na askari wa gereza la Big Muddy.

“Kila anapopata fursa ya kutupigia simu, hufanya hivyo. Anatupigia kama mara mbili kwa mwezi. Alilalamika kwamba hakuwa akihisi vizuri katika mazungumzo ya mwisho naye. Alikuwa mgonjwa na hata alinyimwa haki ya kwenda hospitali hadi akalazimika kuzungumza na wakili fulani ili apewe (ruhusa) ya kupata matibabu,” Amina alisema.