Habari za Kitaifa

Mwanafunzi aliyedhulumiwa na Mpalestina nchini Algeria alia kunyimwa haki

Na FRANCIS MUREITHI August 26th, 2024 2 min read

MWANAFUNZI Mkenya, anayesomea nchini Algeria amehukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani licha ya tuhuma za kudungwa kisu na mwenzake mwenzake akauguza majeraha mabaya.

Duru zinaarifu, Mkenya huyo alidungwa kwa kisu na Mpalestina akiwa katika chumba cha malazi na inashangaza kuona kesi iligeuzwa akawekelewa makosa.

Ian Koima Kiprotich, 24, anayesomea Shahada ya Uzamili ya Usanifu katika Chuo Kikuu cha Constantine 3, alihukumiwa mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024 na mahakama ya Algeria katika kesi ambayo hakuwakilishwa na wakili yeyote.

Hata hivyo, wanafunzi wa Kenya nchini Algeria, wamelaani hukumu hiyo wakisema Kiprotich alinyimwa haki, na wanataka ukweli ufanyike kwa mwenzao.

Kulingana na mwanafunzi mmoja Mkenya ambaye aliomba tulibane jina lake, wawili hao waligombana na Kiprotich alidungwa kisu mara tano.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Centre-Universitaire de Constantine akiwa katika hali mbaya na kulazwa kwa siku tatu chini ya uangalizi maalum.

Lakini aliporuhusiwa kutoka hospitalini, Kiprotich alishtuka kukamatwa na kushtakiwa kwa “kumshambulia” mwanafunzi wa Kipalestina na kuitusi familia yake.

“Alidungwa kisu mara kadhaa shingoni, pajani na tumboni na mwanafunzi Mpalestina na mara akaanguka chini huku akivuja damu nyingi na kupoteza fahamu,” alisema mwanafunzi huyo Mkenya.

Wanafunzi hao walisema wanafunzi watatu kutoka Malawi, Uganda na Tanzania walioshuhudia zogo hilo, walifika kumuokoa na kumkimbiza hospitalini.

“Nashukuru Mungu kwamba maisha ya mwenzetu yaliokolewa na wanafunzi hawa watatu. Alikuwa akivuja damu nyingi kama ilivyothibitishwa na damu iliyotapakaa chumbani mwake,” mwanafunzi huyo Mkenya aliongeza.

Kiprotich hakuweza kumudu wakili wa kibinafsi na aliomba wakili wa umma, lakini juhudi zake za kumpata ziliambulia patupu.

Cha kushangaza ni kwamba, aliyemshtaki alipewa wakili wa umma mara moja kumwakilisha mahakamani, huku Kiprotich akipewa mkalimani shughuli za mahakama zilipokuwa zikiendeshwa kwa Kiarabu.

Mkalimani ni mtafsiri wa lugha.

“Kiprotich alinyimwa haki. Alikuwa na mashahidi watatu tayari kutoa ushahidi. Alinyimwa kesi ya haki kwa sababu hakuwa na muda wa kutosha na uwakilishi wa kisheria kuandaa utetezi wake,” alidokeza mwanafunzi huyo.

Aliongeza, “Mashahidi walikuwa tayari kutoa ushahidi kwamba Kiprotich alikuwa chumbani mwake wakati wa shambulio hilo. Lakini walitishiwa na mshambuliaji.”

Mwanafunzi mwingine wa Kenya, ambaye hakutaka jina lake litajwe pia, alisema shambulio hilo halikuchochewa.

“Kiprotich alikuwa chumbani mwake. Haikuwa vita. Kiprotich amenyimwa haki. Aliyemshtaki ana historia ya utovu wa nidhamu”.

Mwanafunzi mwingine alidai kuwa wakati fulani wa kesi hiyo, vita vya Israel dhidi ya Gaza vilitajwa, huku wakili anayemwakilisha mwanafunzi huyo wa Kipalestina akisema kuwa Algeria inapaswa kutetea Wapalestina wanaoteseka katika vita vya Gaza.

Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi