Habari Mseto

Mama alilia msaada baada ya kumeza sindano kwa bahati mbaya

Na GEORGE MUNENE August 14th, 2024 2 min read

MWANAMKE mmoja anaomba usaidizi baada ya kumeza sindano kwa bahati mbaya akinyonyesha mtoto katika kijiji cha Mugambaciura, Kaunti ya Kirinyaga.

Bi Everline Karekia anapitia uchungu mwingi huku sindano ikiwa imekwama mwilini wiki nne baada ya tukio hilo.

“Nina uchungu mwingi na siwezi kula vizuri,” Karekia mwenye umri wa miaka 31 aliambia Taifa Leo Jumatano.

Mama huyo wa watoto wawili alisema alikuwa akishona nguo mtoto wake alipoanza kulia, akitaka kunyonyeshwa.

Aliacha kazi yake, akaweka sindano mdomoni na kuanza kumnyonyesha mtoto wake wa miezi minane.

Hata hivyo, alimeza sindano hiyo kwa bahati mbaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Embu lakini alifanyiwa uchunguzi pekee.

“Katika hospitali ya Embu tulilipa Sh800 kugharamia eksirei lakini hakuna juhudi zozote zilizofanywa kuondoa sindano kwenye koo la mke wangu,” Bw Kelvin Maina, mumewe Everline akasema.

Bi Karekia pia alitafuta matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya lakini sindano hiyo haikuweza kutolewa mara moja.

Bw Maina alisema hali ni mbaya na kuomba serikali kuingilia kati.

“Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi huenda nikampoteza mke wangu ambaye amekuwa akiteseka kwa zaidi ya mwezi mmoja,” Bw Maina akasema.

Alidai kuwa mkewe hangeweza kuhudumiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya ambayo ilipandishwa hadhi hivi majuzi hadi kituo cha matibabu cha kiwango cha tano.

“Tulipoenda Kerugoya tuliambiwa ukaguzi wa endoscopy ambayo ilitakiwa kufanywa kabla ya upasuaji wa kutoa sindano haujafanywa na tukatumwa kwenda hospitali ya kibinafsi ya eneo hilo ambapo tulitakiwa kulipa Sh10,000 ambazo hatukuwa nazo,” Bw Maina akasema.

Endoscopy ni utaratibu wa kimatibabu unaofanywa kuchunguza miundo ndani ya mwili kwa karibu na mirija ambayo imewekwa kamera iliyoingizwa kupitia koo au njia ya haja kubwa.

Bw Maina alisema mkewe alilazimika kurudi nyumbani akiwa na sindano kooni.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Afya wa Kaunti ya Kirinyaga, Dkt George Karoki alisema suala hilo linashughulikiwa na hospitali hiyo.

“Tulimhudumia mwanamke huyo na uchunguzi wa mionzi haukuonyesha kuwa kuna sindano kwenye koo. Kwa hivyo, tuliamua kumfanyia uchunguzi ili kubaini ukweli wa jambo hilo lakini hatukuwa na mashine ya endoscopy. Ilibidi kutumia ambulensi kumchukua mgonjwa kutoka nyumbani kwake na kumpeleka hospitali ya kibinafsi kwa ajili ya upasuaji huo. Tunashirikiana na hospitali za kibinafsi kuhusu masuala ya afya na ni kawaida kufanya hivyo,” Dkt Karoki akasema.

Wenyeji katika kijiji cha Mugambaciura walisema hakuna usaidizi wowote kutoka kwa viongozi wa kisiasa uliopeanwa huku wakiongeza kwamba familia ya mwathiriwa inahitaji pesa zaidi kugharamia matibabu yake kwani ni familia maskini.

Vilevile, waliongeza kwamba mwathiriwa hutumia muda mwingi wake kulala kutokana na uchungu mwingi anaohisi.

Tafsiri: SAMMY KIMATU