Habari za Kaunti

Mwongozo wa wakazi kuchimba madini mbugani Tsavo waandaliwa

March 26th, 2024 3 min read

NA LUCY MKANYIKA

WIZARA ya Madini na Uchumi wa Baharini imeanzisha mchakato wa kuwakubalia wakazi wa Taita Taveta kuchimba madini ndani ya mbuga ya kitaifa ya Tsavo, baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa jamii ya eneo hilo ambayo ilihisi kutengwa.

Wenyeji wamekuwa wakilalamika kwamba hawafaidiki kutokana na rasilimali za madini zilizoko ndani ya hifadhi hiyo.

Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini Salim Mvurya, mwenzake wa Utalii na Wanyamapori Alfred Mutua, na viongozi wa Taita Taveta wakiongozwa na Gavana Andrew Mwadime, walihudhuria mkutano wa kunakili maoni ya wadau mnamo Jumatatu katika kaunti ya Taita Taveta ili kuunda mfumo ambao utaruhusu wakazi kuchimba mbugani humo.

Mbuga hiyo inachukua takriban asilimia 62 ya ardhi ya kaunti hiyo na wenyeji wamekuwa wakilalamika kuwa hawaoni manufaa yake.

Mpango huo unajiri baada ya viongozi, wakazi na wenyeji wa eneo hilo kumlilia Rais William Ruto mwaka 2023, wakitoa wito serikali ya Kenya Kwanza kushughulikia uonevu wa kihistoria na kupewa idhini ya uchimbaji madini ndani ya Tsavo.

Mfumo utakaopendekezwa unalenga kujumuisha masilahi ya jamii za eneo hilo na vilevile kuhifadhi mazingira na wanyamapori.

Tayari Idara ya Madini imeunda jopo la wadau mbalimbali ambalo linajumuisha wataalamu ambao wataunda mfumo huo ndani ya miezi miwili.

Jopo hilo linajumuisha maafisa kutoka Wizara ya Madini, ile ya Utalii na Wanyamapori, Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nema), Shirika la Huduma za Misitu (KFS), maafisa wa utawala na wanajamii wa kaunti hiyo.

Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori ya 2013 inaruhusu uchimbaji madini katika mbuga za kitaifa, huku idhini ikitolewa na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS).

Mbuga ya Tsavo inajulikana kwa madini kama vile vito vya thamani vikiwemo ruby na Tsavorite, ambavyo vinaweza kunufaisha pakubwa wenyeji katika kujenga uchumi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho katika hoteli ya Panlis, Mwatate, waziri Mvurya alikiri kuwa kuna kampuni chache ambazo zilipewa idhini za uchimbaji madini mbugani Tsavo.

“Ikiwa kuna vikwazo vya uchimbaji madini mbugani, basi watu wetu hawatanufaika kutokana na rasilimali zao. Mfumo huu utahakikisha kwamba rasilimali hii inanufaisha Kenya kwa upana lakini pia jamii za eneo hili,” alisema.

Kwa upande wake, waziri Mutua alisema kuwa mpango wa kuijumuisha jamii ya eneo hilo kuchimba katika hifadhi hiyo unanuia kukuza uchumi wa nchi na mapato ya wenyeji.

Alisema wakati umefika kwa wakazi wa Taita Taveta kunufaika kutokana na rasilimali zao.

“Ni muhimu kwamba jamii inufaike, badala ya kunufaisha mabwenyenye wachache wenye ushawishi. Ikiwa madini yanapatikana hapa basi ni haki kwa wenyeji pia kunufaika kutoka kwa rasilimali hiyo,” alisema Dkt Mutua.

Katibu wa Madini Elijah Mwangi ambaye aliongoza kongamano hilo, alisema rasimu ya mfumo huo itakamilika ndani ya miezi miwili kabla ya kushirikisha umma.

“Mfumo huo utakuwa tayari hivi karibuni,” alisema Bw Mwangi.

Hata hivyo, gavana Mwadime alisisitiza kwamba wenyeji wanastahili kupata sehemu kubwa ya uchimbaji madini, ikizingatiwa kuwa hifadhi iko ndani ya kaunti yao.

“Wakati wa kutoa idhini idadi kubwa ya wachimba madini inapaswa kutoka kwa jamii ya eneo hili. Uchunguzi wa kina kwa wachimba madini wanaoomba idhini unapaswa kufanywa kabla ya kuidhinishwa,” alisema Bw Mwadime.

Idara ya Madini ya serikali ya kaunti imependekeza upimaji wa kijiolojia ili kutambua maeneo ya wachimba madini, ugawaji wa maeneo kwa vikundi vilivyoandaliwa, na uanzishwaji wa kamati ya idhini inayojumuisha wadau wote.

Mapendekezo hayo yaliyosomwa na Afisa Mkuu wa Idara ya Madini Jimmy Mtawa yalipendekeza maeneo ya wachimba migodi yawekwe wazi na kutangazwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali ili kuzuia mizozo na KWS.

Aidha, yalishauri ukarabati wa maeneo ya uchimbaji madini ili kuzuia uharibifu wa mazingira na na vilevile mkataba wa kukodisha wachimbaji uwe angalau miaka 15.

Viongozi wengine wakiwemo Seneta Jones Mwaruma, Mwakilishi wa Wanawake Lydia Haika na wabunge Abdi Chome (Voi), Peter Shake (Mwatate), Danson Mwashako (Wundanyi) na John Bwire (Taveta) walihudhuria.

Walisema ni lazima serikali ihakikishe kuwa mfumo huo unawanufaisha wenyeji kikamilifu kwani sehemu kubwa ya kaunti hiyo iko ndani ya hifadhi hiyo.

“Tumekuwa tukikumbana na migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyamapori. Tunahitaji mfumo wa uchimbaji madini haswa kwa wachimbaji wadogo. Pia wanapaswa kupewa usalama kwani wanachimba katika mbuga,” alisema seneta Mwaruma.