Habari za Kitaifa

Nyoro asukuma TSC iajiri walimu wa JSS, asema serikali imetoa pesa

Na CHARLES WASONGA September 8th, 2024 1 min read

MJADALA kuhusu hatima ya walimu vibarua wanaofundisha katika Shule ya Sekondari za Msingi (JSS) inaendelea kushamiri Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa Ndindi Nyoro akitaka tarehe watakayoajiriwa rasmi iwekwe wazi.

Akiongea Jumamosi, Septemba 7, 2024 Mbunge huyo wa Kiharu ameitaka Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kutoa tarehe hiyo kwa sababu serikali imetoa Sh18.7 bilioni za kuajiri walimu hao 46,000 kwa mkataba wa Akihutubu katika eneo bunge la Aldai wakati wa  maombi kwa watahimiwa kwa kidato cha nne, Bw Nyoro ameionya TSC dhidi ya kubadilisha kila mara tarehe ya kuajiri walimu hao.

“TSC itoe taarifa kuhusu tarehe ambapo walimu wa JSS watapewa ajira ya kudumu na wajue na wajiandae,” akasema.

Bw Nyoro amesema hayo majuma mawili baada ya TSC kuagiza walimu hao wa JSS wajaza fomu za kuongeza kandarasi yao kwa miezi minne zaidi kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka huu.

Kandarasi yao ya sasa ilitarajiwa kukamilika mnamo Julai 30, 2024

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Afisa Mkuu Mtendaji Nancy Macharia, ni baada ya miezi hiyo minne ambapo tume hiyo itaajiri walimu hao kwa kandarasi ya kudumu.

Ingawa suala la kuajiriwa kwa walimu hao ni majawapo ya sababu zilizochangia vyama vya walimu kuitisha mgomo, havikusema lolote kulihusu baada ya kusitisha migomo hiyo.

Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kilisitisha mgomo wake Agosti 25, 2024 na kile cha kutetea walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri (Kuppet)  kikaondoa mgomo wa wanachama wake Septemba 2, 2024 baada ya walimu kususia kazi kwa wiki moja.