Habari za Kitaifa

NYS: Waliofungiwa nje kwa sababu ya tattoo waelezea majuto yao

February 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya vijana waliofika katika vituo vya usajili wa makurutu wa kujiunga na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) walipigwa na butwaa baada ya kutemwa nje kwa kuwa na michoro ya chale almaarufu ‘tattoo’.

Taifa Leo iliwahoji baadhi yao, wakijutia uamuzi waliosema ulitokana na msukumo wa ujana licha ya kukanywa na walimu na wazazi dhidi ya kuchorwa tattoo hizo.

“Mimi nilikuwa nimekanywa na mamangu dhidi ya kuenda kuchorwa tattoo mwilini. Niliiga wanasoka fulani katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Walimu walinikemea na ni vile tu ilibainika haingefutika ndipo nikakubaliwa kuendelea na masomo,” akasema mmoja wa vijana hao.

Lakini ulikuwa wakati wa kung’amua ya wahenga kuhusu majuto wakati alifika katika uwanja wa Thika kujaribu bahati ya kusajiliwa na ndipo akatemwa nje, kosa likiwa ‘tattoo’.

“Hakuna vile tutasajili mtu ambaye ana michoro mwilini. Hatujui hizo ni ishara za usajili wa wapi. Hatujui maana ya ushirika huo na hatutaki kujikanganya. Tunataka mtu ambaye amedumisha nidhamu ya ngozi yake jinsi alivyoumbwa,” akasema mshirikishi wa harakati hizo eneo hilo, Bw Christopher Mwaura.

Mchoro wa tattoo kwa mwili wa kijana aliyefika katika uwanja wa Thika kujaribu bahati yake kujiunga na NYS. PICHA | MWANGI MUIRURI

Cha kutamausha ni kwamba, hata vijana hao walioathirika wakipewa nafasi ya kufuta tattoo hizo, alama hizo zitabaki tu pale pale kama michoro isiyo na rangi hivyo basi kuwaweka nje tena.

Soma Pia: Warembo wa tattoo wadai ni vigumu kupata mume

Serikali inanuia kutumia usajili huo kupata makurutu katika vitengo vingine vya udumishaji wa usalama nchini.

Rais William Ruto tayari amesema kwamba asilimia 80 ya polisi na jeshi watakuwa wakisajiliwa kutoka kwa NYS.

[email protected]