• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Warembo wa tattoo wadai ni vigumu kupata mume

Warembo wa tattoo wadai ni vigumu kupata mume

NA RICHARD MAOSI

WAREMBO wenye chale au michoro ya tattoo ambazo hazifutiki, sasa wanalia kwamba wanatengwa na wanaume ambao huwatema kama kiazi moto.

Taifa Leo ilipozuru hafla moja ya kifahari jijini Nairobi, baadhi ya warembo hao walifunguka kwamba ni vigumu kwao kupata wanaume wa mahusiano ya kudumu.

Wanadai wanaume wamekuwa wakiwakimbia na kuwaogopa bila sababu.

“Siamini kwamba licha ya urembo huu wangu sijapata dume la kunipenda eti kwa sababu tu nimejichora tattoo,” akafunguka mwanadada aliyejitambulisha tu kwamba anaitwa Amina.

Akaongeza: “Sisi ni binadamu kama hao wengine hivyo tusibaguliwe jinsi hiyo.”

Anasema mabanati wengi– yeye akiwa mmoja wao–wanateseka na hata kukabiliwa na msongo wa mawazo kwa kile wanachokidai kuwa wanaume wengi wanapendelea “mrembo kienyeji”.

Amina anasema alijichora tattoo alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu kimojawapo nchini kiwa ni baada ya kupata msukumo kutoka kwa marafiki zake.

Anadai kuwa tattoo ni urembo kama urembo mwingine kama vile kusuka nywele huku akikiri kwamba “kweli zinapokuwa nyingi mwilini huanza kukera.”

Kwa upande wake binafsi, anajutia maamuzi yake kwa sababu alijichora tattoo ambazo haziwezi kufutika.

“Ninatamani kuwa kwa uhusiano na mwanamume mmoja tu wa kunipenda kwa udhati wa moyo wake wote lakini inakuwa vigumu kwa sababu wale ambao wameniingiza boksi huniacha siku chache tu kabla ya mahusiano yetu kupiga hatua zaidi,” akafunguka.

Naye mrembo mwingine *Diana ambaye hufanya kazi ya kuwachora wanaume na akina dada tattoo katika eneo la Nairobi West, anasema tattoo ni urembo tu wa kawaida.

“Ningependa kuwashauri wanaume kuangazia tabia za akina dada badala ya kuwabagua kwa msingi wa kujichora mwilini,” akasema *Diana.

Kwenye mtandao wa kijamii Bw Alfred Sang aliandika akisema aliachana na mchumba wake yapata miezi mitatu iliyopita baada ya kugundua alikuwa amejichora tattoo katika mapaja.

Naye Bw Collins Ilaji anasema afadhali kuwa na mchumba ambaye anatumia mihadarati kuliko wa kujichora tattoo.

Kwa upande wake Bw Felix Mwangangi, anaunga mkono uchoraji wa tattoo “kwa sababu huimarisha mwonekano wa mtu na vilevile huwa zimebeba jumbe mbalimbali za kuhifadhi kumbukumbu.”

Mbali na warembo waliochorwa tattoo, wengine waliofichua kuwa mambo hayajakuwa rahisi kwao ni waliotoboa sehemu ya nyama baina ya mianzi miwili ya pua ambapo huwa wanaingiza kipini cha umbo la mviringo.

  • Tags

You can share this post!

Balala aachiliwa kwa dhamana

Malawi yakataa mahindi kutoka Kenya

T L