Habari

Ochieng' aahidi kuchapa kazi zaidi Ugenya

April 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BW David Ochieng’ ambaye ameshinda kiti cha ubunge cha Ugenya katika uchaguzi mdogo ulioandaliwa Ijumaa ameahidi kukamilisha miradi kadhaa ya maendeleo aliyoanzisha awali katika eneo hilo pindi atakapoapishwa rasmi.

Akihutubu baada ya kutawazwa mshindi na Afisa Msimamizi wa Uchaguzi katika eneobunge hilo Vincent Saitabau, Bw Ochieng’ ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa eneo hilo kati ya 2012 hadi 2017, aliwashukuru wapiga kura kwa ushindi huo.

“Ushindi huu unaonyesha imani ya wakazi wa Ugenya kwa utendakazi wangu. Na ninaahidi hapa kwamba nitajizatiti kukamilisha miradi yote ambayo tulianza pamoja na hata kuanzisha mingine,” akasema huku akishangiliwa kwa vifijo na nderemo.

“Na kama nilivyofanya hapo awali, nitasalia kuwa mwaminifu kwa wakazi wa eneobunge la Ugenya na kuwafanyia kazi kwa nguvu zangu zote,” akaongeza.

Bw Ochieng’ alitaja Chuo cha Mafunzo cha Ualimu (TTC) cha Ugenya ambacho alisema atahakikisha kuwa mabweni zaidi yamejengwa ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wengi.

“Nafahamu kuwa mabweni yaliyoko sasa katika Ugenya TTC hayotoshi. Nitatumia pesa za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF) kufadhili ujenzi wa mabweni zaidi kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaoongezeka kila uchao,” akasema.

Katika hatamu yake, Bw Ochieng’ pia alianzisha tawi la Chuo Cha Mafunzo ya Matibabu Nchini (MTC) katika eneo la Urenga, Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Msitu (Agrofestry College) na Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi (TVET) katika eneo la Sega, lililoko wadi ya Ugenya Kaskazini.

Ochieng’ ambaye ni wakili alipata kura 18,730 katika uchaguzi huo mdogo na kumbwaga mgombea wa ODM Chris Karan ambaye alizoa kura 14, 567.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya ushindi wa Bw Karan katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, kufutiliwa mbali na mahakama. Hii ni kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Ochieng’ akidai udanganyifu mkubwa ulitokea katika shughuli hiyo.

Ingawa Bw Karan alifanyiwa kampeni za kufana na vigogo wa ODM wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo, Bw Ochieng’ aliendesha kampeni ya nyumba hadi nyumba ambayo hatimaye imezaa matunda.

Umaarufu

Kushindwa kwa Bw Karan, ambaye ni mfanyabiashara mjini Mombasa, kunachambuliwa kuwa pigo kwa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga na ambacho kina umaarufu mkubwa katika eneo hilo.

Isitoshe, ushindi wa Ochieng’ ni pigo kubwa kwa Bw Orengo ambaye anatoka eneobunge hilo na aliyepania kutumia ushindi wa Karan kama ngazi ya kuwania Ugavana wa Siaya mwaka 2022.

Bw Odinga alichelea kuendesha kampeni katika eneo hilo kwa sababu ya kile ambacho makao makuu ya ODM yalisema kuwa shughuli zake nyingi katika wadhifa wake mpya wa Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Mbinu.

Hata hivyo, alipohudhuria hafla ya mazishi katika eneo hilo Machi, Bw Odinga aliwaomba wakazi wasimwaibishe kwa kuwaunga mkono wagombea wengine katika uchaguzi huo mdogo.

Idadi ya wapigakura walioshiriki katika uchaguzi huo ilikuwa ya kupendeza, ikiwakilisha asilimia 58 ya jumla ya wapigakura wote waliosajiliwa.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Hussein Marijan alisema kujitokeza kwa watu wengi kulionyesha umuhimu ambao wakazi waliweka kwa shughuli hiyo.