Jela miaka 10 kwa kuvuruga mfumo wa Kenya Power

Na BERNARDINE MUTANU

MAHAKAMA moja jijini Mombasa Jumatano iliwahukumu wanaume wawili miaka 10 jela au dhamana ya Sh5 milioni kwa kuharibu mfumo wa Kenya Power eneo la Shimanzi, Mombasa.

Wawili hao Joseph Omuse na Faiz Kazungu, walikubali makosa ya uharibifu huo walipofika mbele ya Hakimu Mkuu Mombasa.

“Wahukumiwa walipatikana na vifaa vya stima Ijumaa wiki jana Agosti 17,” alisema meneja wa usalama wa Kenya Power Geoffrey Kigen.

Kwingineko, Kenya Power ilikamata watu watatu, Moses Khaemba, Dennis Mimo, na Antony Juma katika eneo la Seya, lokesheni ndogo ya Kwanza, Kaunti ya Trans Nzoia kwa kuharibu milingoti ya stima.

Kikosi cha usalama kilipata vyuma vya kupanda milingoti, mshipi wa usalama, msumeno wa nyororo na mlingoti wa mbao.

Onyo kali kwa wanabodaboda Lamu

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imewataka wahudmu wa boda boda kisiwani Lamu kuheshimu sheria inayowazuia kuhudumu ndani ya mji wa Shella.

Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, anasema sheria hiyo imejumuishwa na ile iliyowekwa hivi majuzi ya kuwataka kutohudumu ndani ya mji wa kale wa Lamu.

Jumatatu waendeshaji pikipiki zaidi ya 100 waliandamana na kuziba barabara ya Lamu kuelekea Shella katika eneo la Duduvilla kupinga kile walichodai kuwa ni unyanyasaji na ukandamizaji wa baadhi ya wakuu wa usalama wa kaunti ya Lamu.

Wahudumu hao wa boda boda waliwakashifu wakuu hao wa usalama kwa kuwazuia kuhudumu kwenye mji wa Shella na kutaja hatua hiyo kuwa yenye lengo la kusambaratisha biashara yao.

Katika mahojiano na Taifa Leo Ijumaa aidha, Bw Mwasambu alishikilia kuwa Shella ni miongoni mwa miji ya Lamu ambayo hupokea wageni wengi hasa watalii kila mwaka ambao huvutiwa na ukale wa mji huo.

Alisema mbali na kuhifadhi ukale na historia ya mji wa Lamu, idara yake imeandaa mikakati kabambe ya kuhakikisha miji mingine ya kihistoria kote Lamu inahifadhiwa.

Aliwataka wahudumu hao wa boda boda kuheshimu sheria hiyo la sivyo wakamatwe na kushtakiwa.

“Wasiseme sheria hiyo imewekwa katika mji wa kale wa Lamu pekee. Hapana. Sheria hiyo inafanya kazi hata Shella. Hakuna pikipiki zitakazoruhusiwa kuendeshwa ndani ya mji wa Shella. Huo ni mji unaopokea wageni wengi wanaovutiwa na historia na ukale wake. Wahudumu wa boda boda wanaruhusiwa tu kuendesha pikipiki zao nje ya mji huo na wala si ndani ya mji,” akasema Bw Mwasambu.

Kufuatia sheria hiyo, wahudumu wa pikipiki watahitajika kuendesha pikipiki zao kwenye barabara za nje ya Shella hadi nje ya Lamu, nje ya Lamu hadi mitaa ya Kashmir, Bombay, Kandahar, Mararani, Wiyoni na sehemu zingine zilizoko viungani mwa miji hiyo miwili mikuu.

Mnamo Agosti 2015, serikali ya kaunti ya Lamu iliafikia kupiga marufuku uendeshaji wa pikipiki, magari na baiskeli ndani ya kisiwa cha Lamu kama njia mojawapo ya kuhifadhi ukale na historia ya mji huo.

Usafiri ulioruhusiwa ulikuwa ule wa miguu na punda pekee.

Aidha kati ya 2017 na 2018, wahudumu wa pikipiki walianza kurudi na kutekeleza shughuli zao ndani ya kisiwa cha Lamu.

Kufikia sasa zaidi ya pikipiki 150 zinaendeshwa ndani ya kisiwa cha Lamu, hatua ambayo ni kinyume cha sheria zinazoambatana na ukale wa mji huo.

Mnamo 2001, mji wa kale wa Lamu uliorodheshwa na Shirika la Kisayansi, Elimu na Utamaduni ulimwenguni (UNESCO) kama eneo mojawapo linalotambulika zaidi kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake, yaani-UNESCO World Heritage Site.

UFISADI: Rais wa zamani wa Korea Kusini kuozea jela

PETER MBURU NA MASHIRIKA

Aliyekuwa Rais wa Korea Kusini kabla ya kung’olewa mamlakani Park Geun-hye Ijumaa alitupwa gerezani miaka 25 na mahakama ya rufaa nchi hiyo, kwa kupokea hongo kutoka kampuni ya Samsung alipokuwa uongozini.

Bi Park mwenye umri wa miaka 66 alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 24 na mahakama ya chini mbeleni kwa ufisadi, uongozi mbaya na makosa mengine ya jinai na akaamriwa kulipa pesa taslimu 18bilioni za nchi hiyo kama faini.

Lakini Ijumaa mahakama hiyo ya rufaa ikiketi eneo la Seoul ilimwongezea mwaka mmoja ndani na faini hadi 20bilioni won, ikisema hasara iliyosababishwa ilikuwa kubwa kuliko ilivyoamua mahakama ya chini.

Bi Park amekuwa akizuiliwa tangu mwaka uliopita na hakufika mahakamani wakati wa kusomewa hukumu Ijumaa.

Kitumbua cha uongozi wake kiliingia mchanga 2016 wakati maelfu ya waandamanaji walimiminika eneo la kati mwa Seoul wakitaka aondoke ofisini kwa miezi. Disemba mwaka huo, bunge la nchi hiyo lilimbandua kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi.

Machi 2017, Bi Park alikuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kusini kuwahi kubanduliwa na bunge, wakati mahakama ya kikatiba ilishikilia uamuzi wa bunge hilo.

Wakati wa kumhukumu mnamo Aprili, mahakama ya chini ilisema Bi Park pamoja na mwandani wake wa miaka mingi Coi Soon-sil walipokea bilioni 23 won kama hongo kutoka kwa biashara tatu kubwa, ikihusisha karibu bilioni 7.3 kutoka kampuni ya Samsung.

Agosti mwaka uliopita, mkuu wa Samsung nchi hiyo Bw Lee Jae-yong alihukumiwa miaka mitano gerezani kwa kuwahonga Bi Park na Bi Choi lakini akatoka jela Februari baada ya mahakama ya rufaa kukata nusu ya kifungo chake kisha kukitupa ikisema kiwango cha hongo alichotoa kilikuwa kidogo.

Vilevile Ijumaa, rafikiye Bi Park Bi Choi alitupwa jela miaka 20.

Kifungo hicho cha miaka 25 sicho pekee ambacho Bi Park anakumbana nacho, kwani mwezi uliopita alihukumiwa jumla ya miaka minane kwa makosa mawili ya kuvunja sheria za uchaguzi na matumizi mabaya ya pesa za serikali.

Wasanii 21,000 wavuna Sh200m kwa Safaricom

Na BERNARDINE MUTANU

Wanamuziki na wasanii wamefaidika kutokana na Sh200 milioni kutokana na Safaricom baada ya mauzo ya nyimbo zao kupitia kwa mpango wa Skiza.

Mkuu wa uhusiano mwema Safaricom Steve Chege alisema wasanii kufikia 21,000 waliojisajili Skiza Tunes wananufaika na mauzo hayo.

Kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza kiwango hicho cha fedha kila mwezi, alisema Bw Chege.

Aliongeza kuwa jukwaa hilo limewasaidia wasanii kupata pesa kutokana na mapato yao kwa kuuza nyimbo kwa wateja wa kupiga simu.

Kulingana na afisa huyo, Safaricom itazidi kuhamasiha wanamuziki nchini, “Safaricom imejitolea kuwekeza zaidi katika sekta ya muziki. Tulichukua hatua kuwawezesha wasanii kujipa pato,” alisema.

Safaricom mwaka jana ilitangaza ongezeko la asilimia 36 ya mapato kwa wasanii kutokana na mauzo ya muziki wao kwenye jukwaa la SKIZA.

Gor kunufaika na Sh12m kwa mauzo ya Walusimbi

NA CECIL ODONGO

MABINGWA mara 16 wa ligi ya KPL Gor Mahia, watavuna Sh12 milioni kutokanana na mauzo wa aliyekuwa mlinzi wao raia wa Uganda Godfrey Walusimbi kwa mibabe wa soka ya Afrika Kusin, Kaizer Chiefs.

Gor walisalimu amri katika juhudi zao za kumtaka Walusimbi  asalie klabuni na sasa watapokezwa kitita hicho kikubwa na washiriki hao wa ligi ya Absa baada ya pande zote mbili kuhitimisha makubaliano kuhusu uhamisho wa sogora huyo.

“Hakuna utata wowote kati yetu na Gor Mahia tena kuhusiana na hatua yetu ya kusaini beki wa Godfrey Walusimbi. Tumekuwa na majadiliano mapana yaliyohusisha wahusika wote na kuafikiana kuhusu dili tutakayowatangazia hivi kabla ya mwisho wa mwezi Agosti,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Kaizer Chiefs Bobby Motaung.

Walusimbi sasa atawagaragazia Chiefs baada ya kupokezwa cheti kinachoidhinisha uhamisho wake kabla ya mwisho wa mwezi wa Agosti huku fedha za uhamisho wake zikikabidhiwa mabingwa hao watetezi wa KPL  katika kipindi hicho.

Wabunge wafika kortini kumliwaza mwenzao aliyeshtakiwa kwa ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI

WABUNGE watatu Alhamisi walifika katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi ya Milimani kumliwaza Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuyu aliyeshtakiwa kwa ufisadi.

Waliofika mahakamani kumtembelea Bw Gakuyu ni pamoja na Mbunge wa Starehe Bw Charles Kanyi Njagua almaafuru Jaguar, Mbunge wa Embakasi ya Kati Bw James Mwangi na Mbunge wa Kamkunji Bw Yusuf Hassan.

Wabunge hao watatu walifika mahakamani mwendo wa saa nane mchana. Walimweleza Bw Gakuyu kwamba watamuunga mkono kwa hali na mali.

Bw Gakuyu na washukiwa wengine 11 walikana mashtaka 27 ya kufuja pesa za hazina ya kustawisha eneo bunge (CDF). Walidaiwa walipokea kinyume cha sheria Sh39 milioni.

Bw Gakuya aliachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa tasilimu. Washtakiwa wengine waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1.5 milioni na wengine wakapewa dhamana ya Sh750,000.

Akana kumeza mamilioni ya Dubai Bank

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa wizi wa Sh159 milioni kutoka kwa benki ya Dubai aliyeamriwa Jumatano azuiliwe rumande hadi Alhamisi korti iamuru ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la sasa yuko huru kwa dhamana ya Sh200,000.

Hakimu mkuu Bw Francis Andayi alimwachilia  Bw Justus Lindambizi Tito kwa dhamana baada ya kuthibitisha kuwa kuna washukiwa wengine waliofikishwa mahakama awali na kuachiliwa kwa dhamana ya laki mbili.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mnamo Ijumaa wiki iliyopita mfanyabiashata wa Mombasa Bw Zein Abubakar Said alishtakiwa kwa wizi huo na kufanya njama za kuilaghai benki hiyo.

Wakili Kirathe Wandugi anayemwakilisha Bw Tito alisema kuwa kuna kesi nyingine tatu zitakazounganishwa na hii dhidi ya  Bw Tito na Bw Said .

#MashemejiDerby: Ingwe yalenga kuigwara Gor bila kucha za Odera

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards itakosa mfumaji wake hodari Ezekiel Odera itakapokuwa ugenini dhidi ya mahasimu wa tangu jadi Gor Mahia kwenye Ligi Kuu uwanjani Kasarani hapo Agosti 25, 2018.

Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 30 anatumikia marufuku ya mechi mbili, dhidi ya Gor Mahia (Agosti 25) na Wazito (Agosti 29), kutokana na kadi tano za njano na moja nyekundu.

Odera, ambaye alifungia Ingwe mabao mawili katika mechi mbili zilizopita ikipepeta Nakumatt 4-2 Agosti 12 na goli moja iliponyuka Thika United 2-0 Agosti 18, ameona lango mara 11 kwenye ligi hii ya klabu 18 msimu huu.

Yuko mabao manne nyuma ya Elvis Rupia na magoli mawili nyuma raia wa Rwanda, Jacques Tuyisenge.

Ingwe huenda ikakosa huduma za Moses Mburu, Salim Abdalla, Robinson Kamura, Jafari Owiti na Dennis Sikhayi. Wachezaji hawa wanauguza majeraha mbalimbali.

Kiungo mvamizi Whyvonne Isuza ni mmoja wa wachezaji ambao kocha kutoka Argentina, Rodolfo Zapata atategemea kutafuta matokeo mazuri dhidi ya Gor, ambayo itahifadhi taji ikishinda gozi hili maarufu kama ‘Mashemeji Derby’.

Maadui hawa wamekutana mara 83 ligini. Leopards imeshinda Gor mara 27, ikapoteza 25, huku mechi 31 zikitamatika sare. Ingwe itakuwa mawindoni kutafuta ushindi wake wa kwanza dhidi ya Gor katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili. Mara ya mwisho Ingwe ililemea Gor ni 1-0 Machi 6 mwaka 2016.

Timu hizi zilikutana ligini msimu huu mnamo Julai 22 Gor ikiibuka mshindi 2-1 kupitia mabao ya Tuyisenge na George ‘Blackberry’ Odhiambo. Isuza alifungia Ingwe bao la kufutia machozi.

Gor inaongoza kwa alama 68 kutokana na mechi 27 nayo Leopards inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 48.

Ratiba:

Agosti 25, 2018

Nakumatt na Posta Rangers (11.00am, Camp Toyoyo), Chemelil Sugar na Ulinzi Stars (3.00pm, Chemelil), Kakamega Homeboyz na Wazito (3.00pm, Bukhungu), Sofapaka na Kaiobangi Sharks (3.00pm, Narok), SoNy Sugar na Tusker (3.00pm, Awendo), Gor Mahia na AFC Leopards (4.00pm, Kasarani);

Agosti 26, 2018

Bandari na Nzoia Sugar (3.00pm, Mombasa), Thika United na Vihiga United (3.00pm, Thika), Zoo na Mathare United (3.00pm, Kericho)

Aliyeahidi kulipa vijana aliohadaa kuwapeleka Afghanistan aambia korti hana hanani

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE aliyepatwa na mshtuko kundi la vijana zaidi ya 20 waliposimama kortini na kusema amewatapeli maelfu ya pesa akiwandanganya atawapeleka nchini Afghanistan kufanya kazi huko Alhamisi alieleza mahakama hana pesa za kuwalipa.

Bi Ednah Kendi Kiruki alikuwa ameomba korti mnamo Jumatano apewe muda kufanya mashauri na walalamishi kwa lengo la kuwalipa.

Lakini Alhamisi alipofikishwa kortini tena alimweleza hakimu , “nimeshindwa kupata pesa hizi ninazodaiwa.”

Hakimu aliamuru mshtakiwa arudishwe rumande kusubiri kusikizwa kwa kwa kesi dhidi yake.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu ama awasilishe dhamana ya shilingi laki tatu.

Mbunge matatani kupokea Sh39 milioni za CDF

Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Mwangi Gakuya (kulia laini ya umma) akiwa kortini Alhamisi. Picha/ EVANS HABIL

NA RICHARD MUNGUTI 

MBUNGE wa Embakasi kaskazini Bw James Mwangi Gakuya alishtakiwa pamoja na ndugu yake kwa kupokea zaidi ya Sh39milioni za hazina ya kustawisha eneo hilo la uwakilishi bungeni (CDF) kupitia miradi ya ujenzi wa barabara.

Bw Gakuya aliyetiwa nguvuni akiwa katika hafla ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Mzee Jomo Kenyatta  alishtakiwa pamoja na  washukiwa wengine 11 mbele ya hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo.

Mahakama ilimwachilia Mbunge huyo kwa dhamana ya Sh2milioni ama akishindwa kuilipa awasilishe mdhamini wa Sh5milioni.

Bw Gakuya , ndugu yake Patrick Waruingi Gakuya, Leah Waithera Guchu, Cleophas Omariba Oyaro, Richard Mwangi Chuchu,  Florence Ambura Njeri, Agnes Njeri Muthoni,Julius Maina Njoka,  Teresia Muthoni Macharia mmiliki wa kampuni ya Hunyu Bush Clearing and Bush Nuurseries, Stacey  ,Salome Nduta, kampuni za Mabaks Enterprises yao Mabw Gakuya na Tresmu Investments.

Washtakiwa walikanusha  mashtaka 27 dhidi yao kisha wakili Dunstan Omari akaomba waachiliwe kwa dhamana akisema “ hawatavuruga kesi kwa njia yoyote ile.”

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na viongozi wa mashtaka waliosema kuwa , “ washtakiwa wako na ushawishi mkubwa na watawatisha mashahidi walioorodheshwa kutoa ushahidi dhidi yao.”

Mbunge huyo alikabiliwa na mashtaka kwamba alitumia mamlaka yake na kampuni aliyokuwa anamiliki pamoja na nduguye kujipatia zaidi ya Sh39milioni kupitia ujenzi wa barabara kadhaa katika eneo hilo analowakilisha bungeni.

Mbunge huyo ,nduguye Waruingi  pamoja na kampuni yao Mabaks Limited walikbiliwa na shtaka la  kupokea kwa njia ya undanganyifu Sh19,691,772 kutoka kwa akaunti ya CDF ya Embakasi kaskazini.

Bw Oyaro alikabiliwa na mashtaka ya kukataa kuthibiti pesa za umma kwa kuruhusu pesa za umma zilipwe makampuni ambayo mbunge huyo alikuwa anahusika na umiliki wake.

Na wakati huo huo Bw Kombo aliwataka Waruinge na Stacey Wambui Njoki wafike kortini kujibu mashtaka kwa vile hawakuweza kufika.

Bw Kombo alielezwa washtakiwa hao hawakujua kuwa wanatakiwa kufika kortini kujibu mashtaka.

AMANI CAR: Wanamgambo watoa masharti 97 kwa AU

MASHIRIKA NA PETER MBURU

VIKOSI vya wanamgambo wa kivita Jamhuri ya Kati mwa Afrika (CAR) vimetoa matakwa 97 kwa Umoja wa Afrika (AU), wakati huu inapofanya juhudi za kuleta amani nchi hiyo ili vikubali kufika meza ya maelewano, zimesema ripoti kutoka AFP.

Kulingana na stakabadhi zinazomilikiwa na AU, matakwa 97 yameorodheshwa na vikosi hivyo, ili kukubali kuweka amani, yakiwemo kuundwa kwa serikali ya muungano.

Vikosi hivyo aidha vinataka msamaha rasmi kwa makosa vilivyotenda na kufanywa mabadiliko katika jeshi la nchi hiyo, ili kukubali kuweka amani.

Muungano wa AU umekuwa ukiongoza juhudi za kurejesha amani nchi hiyo, japo hakujakuwa na hatua ulizopiga.

Nchi hiyo iliingia kwenye vita tangu 2013 baada ya kubanduliwa kwa Rais Francois Bozize (aliyeungwa mkono na wakristo) na kikundi cha muungano wa waislamu kiitwacho Seleka.

Baada ya hapo, wakristo ambao ni asilimia 80 ya taifa hilo waliunda vikundi vya kujiteta na kuviita ‘anti-balaka’.

Nchi ya Ufaransa iliingilia kati kujaribu kulazmu Seleka kuondoka uongozini, kabla ya kupokeza juhudi za kurejesha amani humo muungano wa Umoja wa Mataifa (UN).

Hata hivyo, serikali kuu imekuwa hafifu zaidi, huku ikisalia na udhibiti wa eneo la Bangui pekee, huku vita siku nenda siku rudi vikisababisha vifo vya maelfu wa raia.

Kulingana na afisa aliye eneo la Bangui, wawakilishi wa vikosi hivyo wanatarajiwa kufanya mkutano na timu ya AU katika mji wa Bouar Jumatau kwa nia ya kuoanisha matakwa yao kabla ya kuwasilisha orodha ya mwisho kwa mamlaka.

Lakini serikali hadi sasa imekataa matakwa ya vikosi hivyo.

Russia pia imekuwa sehemu ya kutafuta amani nchi hiyo na inasemekana inaandaa mkutano wa kutafuta suluhu Jumamosi katika jiji kuu la Sudan, Khartoum, kupitia maafisa wa kidiplomasia kutoka Moscow ambao wamekuwa nchi hiyo.

Hata hivyo, msemaji wa CAR Ange-Maxime Kazangui Jumatatu alipinga kuwa serikali yake imehusika katika mazungumzo hayo, akishikilia kuwa wanaunga mkono juhudi za AU.

Kumekuwa na majaribio kadhaa ya kutatua mizozo CAR tangu kuanza kwa vitaa hivyo na maelewano saba ya amani yamewahi kuafikiwa, japo yote hayakuzaa matunda.

BOBI WINE: Shinikizo kwa Museveni aachilie huru msanii zazidi

Na ANTHONY OMUYA

RAIA wa Uganda wanaoishi Kenya waliandaa maandamano ya amani Agosti 23, 2018  jijini Nairobi kutaka serikali ya Uganda kukoma kumtesa mbunge na mwamamuziki Bobi Wine.

Waandamanaji walianza maandamano kutoka eneo la Freedom Corner kwenye bustani ya Uhuru Park. Zaidi ya watu mia nne waLishiriki kwenye maandamano hayo.

Wakiwa maandamanoni katika barabara ya Kenyatta,  walisema msanii huyo, mwanasiasa maarufu kwa sasa anayefahamika kwa jina halisi  Robert Kyagulanyi, ni mwenye ujasiri mkuu.

Walieleza kwa masikitiko kuwa mataifa mengi hayajachukua hatua za kidiplomasia dhidi ya  rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wa na kumtaja kuwa dikteta ambaye hastahili kuongoza taifa lolote lenye demokrasia na huru ulimwenguni.

Wandamanaji hao, wakiwemo wanaharakati wa  Kenya, wanamuziki na wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Kenya na Uganda walishutumu vikali hatua ya serikali ya Uganda na kutaja hatua ya kumshtaki na kumfikisha mahakamani  kama ukiukaji wa  haki za kibinadamu na kuvunja sheria za Umoja wa Kimataifa.

Walitumia vipaza sauti, mabango na nyimbo za msanii huyo za kisiasa  na kutaja kwamba wanapigania uhuru wa nchi ya Uganda, ambayo wanadai imo gizani kwa uongozi wa kiimla.

“Hakuna uhuru Uganda, wakati wa dikteta Museveni kuondoka uongozini umewadia. Yeye na familia yake. Mateke anayorusha ni ya punda. Haya ni mateke ya mwisho,” akasema Joseph Subuga ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Aidha wanataka mataifa  yaliyostawi na Umoja wa Kimataifa kuingilia kati na kuiwekea Uganda vikwazo.

“Tunataka Museveni atambue kuwa kamwe yeye  hawezi kuishi bila vikwazo kutoka Umoja wa Kimataifa. Awe tayari kupokea vikwazo kutoka kwa mataifa yaliyostawi. Uganda sio nchi yake bali ya wananchi wengi. Lazima atii sheria,” akafoka mmoja wa waandamanaji, Janet Kisila.

Mwanamuziki huyo na wengine 30  walitiwa nguvuni na wengine wenzake  30  katika mji wa Arua wiki iliyopita kwa madai ya kumiliki silaha. Mashtaka mapya dhidi ya mwanamuziki huyo ni kujaribu kuua bila kukusudia.

UGANDA: Onyo kwa viongozi dhalimu mapinduzi yaja!

Na WANDERI KAMAU

KATIKA historia, mapinduzi ya kiraia yamechangia pakubwa kung’atuliwa ya viongozi wa kiimla wanaokwamilia mamlakani.

Mapinduzi hayo hutokea wakati wananchi wanapochoshwa na udhalimu wa viongozi hao, ambapo huungana kwa kusahau tofauti zao za kikabila, kidini, kisiasa na kitamaduni.

Nchini Kenya, kuungana kwa wananchi kupitia muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2002, ndiko kulipelekea kushindwa kwa utawala wa Kanu.

Rais Mstaafu Daniel Moi, hakuwa na lingine ila kukubali uamuzi wa Wakenya, japo shingo upande.

Vivyo hivyo, mwelekeo huo ndio unaonekana kutokea nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni anakabiliwa na wimbi kali linalotishia kuyumbisha utawala wake wa kiimla.

Wimbi hilo linaloongozwa na mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine nalinaonekana kusambaa kote kote nchini humo.

Hii ni baada ya vikosi vya usalama kumkamata mwanasiasa huyo na wabunge kadhaa wa upinzani, kwa kisingizio cha “kutishia usalama wa kitaifa.”

Hadi sasa, hali ya taharuki ingali tete, huku baadhi ya nchi za kigeni kama Uingereza, zikitoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri Uganda.

Cha kushangaza ni kwamba, Bw Museveni anaonekana kujitia hamnazo kuhusu wimbi hilo, analodai kuwa la “warusha mawe.”

Undani wa maasi dhidi ya Museveni ni kuwa unaongozwa na wabunge vijana, ambao wamechoshwa na utawala wake wa zaidi ya miaka 30.

Kile kiongozi huyu anaonekana kutofahamu ni kuwa mawimbi haya husambaa kama moto wa nyikani, ambapo mwishoni, huwa wanageukwa hata na washirika wao wa karibu.

Mifano dhahiri ya viongozi waliowahi kung’atuliwa mamlakani na mapinduzi ya kiraia ni aliyekuwa rais wa Haiti, Papa Dok, Ferdinard Marcos (Ufilipino), Hosni Mubarak (Misri), Zine Idine Ben Ali (Tunisia), Muammar Gadaffi (Libya) kati ya wengine.

Ingawa baadhi ya mapinduzi hayo yaliendeshwa na nchi za kigeni kama Amerika, ukweli ni kuwa uingiliaji mataifa hayo huwa ni kuwasaidia raia kujikomboa dhidi ya utumwa wa kisiasa.

Uhalisia uliopo ni kuwa katika enzi hii ya mitandao ya kijamii, ni hadaa kubwa kwa kiongozi yeyote kujidanganya kwamba anaweza kuzima mawasiliano ya raia kuhusu mikakati watakayochukua ili kujikomboa.

Mapinduzi hayo ni onyo kwa viongozi wote Afrika kuwa enzi ya udhalimu wa kisiasa zimepitwa na wakati.

akamau@ke.nationmedia.com

TAHARIRI: Kampeni za 2022 hazimfaidi yeyote

NA MHARIRI

Ni jambo la kusitikisha na vile vile kushangaza kwamba, mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, viongozi mbalimbali wa kisiasa wamezindua kampeni wakilenga viti tofauti katika uchaguzi wa 2022.

Huku kwa kweli ni kudunisha na kudhalilisha raia wa nchi hii waliomiminika katika vituo vya kupigia kura na kuwachagua viongozi hao mwaka uliopita.

Viongozi hao walitoa msururu wa ahadi wakati wa kampeni za uchaguzi. Waliahidi kujenga barabara mpya, kusambaza maji safi vijijini, kusambaza nguvu za umeme katika kila pembe ya nchi na muhimu zaidi, kuhakikisha raia wa nchi hii wanapokea matibabu kwa gharama ya chini.

Ingawa tumo kwenye viwango tofauti vya ufanisi katika utekelezaji wa miradi hiyo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinapasa kuondolewa ili Wakenya wafurahie maisha kama wenzao kwingineko duniani.

Kampeni za kisiasa kwa kawaida huibua msisimko na hupandisha joto la kisiasa. Migawanyiko mikubwa hutokea huku majirani wakitofautiana kwa misingi ya misimamo yao ya kisiasa. Mbona viongozi wetu wakamie kuvuruga utulivu tunaofurahia baada ya kipindi kirefu cha kampeni mwaka jana?

Ni ubinafsi mkubwa kwa viongozi wanaoshikilia dau la nchi hii kuanza kampeni kwa zoezi litakalofanyika miaka minne ijayo bila kuwahudumia wananchi kwa sasa.

Isitoshe, baadhi ya viongozi kwa ujeuri mkubwa wanadai kulipwa madeni ya kisiasa miaka minne kabla ya uchaguzi mwingine kuandaliwa. Kwanza, tungependa kutaja hapa kwamba, hakuna deni katika siasa.

Wanasiasa wetu kama ilivyo kwingineko, huunda miungano ya kisiasa kwa lengo la kutwaa mamlaka. Hivyo basi, ni kinaya kwamba wale wanaodai madeni fulani ya kisiasa ndio wamo usukani mwa ngalawa kwa sasa. Ni tamaa iliyoje kwa kiongozi kupuuza vinono vilivyoandaliwa mezani na kuanza kudondokwa na mate kwa kuwazia vilivyo umbali wa miaka minne?

Ombi letu kwa wanasiasa ni kutumia nguvu, uwezo wao na raslimali zilizopo kuhakikisha wanaboresha hali ya maisha ya raia wa Kenya ambao wengi wao hawana namna ya kujipatia mkate wao wa kila siku.

Ni kudunisha raia wenzao kwa wanasiasa hao kuzunguka katika kila pembe ya nchi kujipigia debe kuhusu ufanisi tuliopata kama nchi ilhali kuna ushahidi tosha wa familia nyingi zinazoshinda mchana kutwa bila kutia chochote kinywani.

Wapiga kura wa sasa wana ufahamu mkubwa wa kisiasa na tunaamini wakati mwafaka ukifika, watawaadhibu kwa kuwatema wanasiasa kama hao ambao wanawatumia kama ngazi kujikweza kwa manufaa yao binafsi.

IPSOS: Wakenya wamsifu Kalonzo kama asiye na doa la ufisadi

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, hana doa la ufisadi ikilinganishwa na viongozi wengine wa kisiasa, kwa mujibu wa utafiti.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Ipsos ilionyesha asilimia moja pekee ya Wakenya ndio wanaamini Bw Musyoka ni mfisadi.

Vile vile, Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walitajwa na asilimia tano pekee ya Wakenya kujihusisha na ufisadi.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Julai 25 na Agosti 2 ulinuia kubaini wanavyodhani ama kujua kuhusu ufisadi nchini na matokeo yake yalitolewa jana.

Akitoa matokeo hayo katika makao makuu ya Ipsos, Lavington Jijini Nairobi Jumatano, mtafiti mkuu wa kampuni hiyo Prof Tom Wolf aidha alisema Wakenya wengi hawaamini kuwa wakubwa kwenye serikali na wafanyabiashara wenye umaarufu watahukumiwa.

“Ni asilimia 17 pekee ya Wakenya ambao wanaamini kuwa kuna uwezekano kwa wale wanaochukuliwa kuwa ‘samaki wakubwa’ kuhukumiwa, huku asilimia 73 wakiamini hilo haliwezekani,” akasema Prof Wolf.

Kulingana na utafiti huo vilevile, bado asilimia 35 ya Wakenya haiamini kuwa Rais Uhuru Kenyatta amejitolea kikamilifu kupigana na ufisadi, asilimia 27 yao wakiwa wafuasi wa chama chake cha Jubilee. Ni asilimia 21 pekee wanaoamini kwa uhakika kuwa Rais Kenyatta atafaulu kupunguza ufisadi nchini, huku 31 wakidhani tu ila bila kuwa na uhakika kuwa atafaulu.

Asilimia 17 ya waliohojiwa walisema haonyeshi dalili ila kuna uwezekano, huku asilimia 24 wakiwa na hakika kuwa hatafaulu.

Wengi wa waliohojiwa walitaja suala la kujihusisha na uongozi wa kisiasa na vitisho kutoka kwa watu wenye umaarufu, kama kikwazo kikuu cha vita dhidi ya ufisadi nchini.

“Jambo la kushangaza ni kuwa asilimia nne ya Wakenya wanadhani kuwa hakuna chochote kitakachofanywa chaweza kumaliza ufisadi Kenya,” akasema mtafiti huyo.

Lakini asilimia 31 walipendekeza adhabu kali zaidi kwa wanaopatikana na hatia, 23 wakimtaka Rais kuwapiga kalamu wale wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi nao asilimia 17 wakipendekeza uhamasisho zaidi kwa umma.

Nitarudi Kenya Septemba 4, mpende msipende – Miguna

Na BENSON MATHEKA

WAKILI mbishi Dkt Miguna Miguna aliyefurusha nchini mara mbili baada ya kuongoza hafla ya kumuapisha Raila Odinga kuwa “rais wa wananchi”, amesema kwamba atarejea nchini baada ya Septemba 4, 2018.

Kupitia ujumbe wa Twitter Alhamisi, Dkt Miguna anayeishi Canada, alitangaza kuwa hakuna kitakachomzuia kurejea Kenya licha ya serikali kumpokonya paspoti yake ya Kenya na kuiharibu.

“Nitarudi baada ya Septemba 4, shime,” aliandika kwenye Twitter.

Hili litakuwa jaribio la tatu la wakili huyo kurudi Kenya tangu Februari alipotimuliwa Kenya mara ya kwanza.

Mnamo Machi 16, Dkt Miguna alitangaza kuwa angerejea Kenya lakini hakufanya hivyo.

Alifurushwa Kenya Februari 6 siku sita baada ya kumuapisha Bw Odinga katika bustani ya Uhuru Park. Serikali ilidai kuwa alipoteza uraia wake wa Kenya na kwamba alikuwa nchini kinyume cha sheria.

Wakili huyo amekuwa akishikilia kuwa hajawahi kukana uraia wake wa Kenya, nchi aliyozaliwa na kwamba serikali ilikiuka agizo la mahakama kwamba arejeshewe paspoti yake na kuruhusiwa kuingia nchini.

Waziri wa usalama Fred Matiang’i alisema Miguna ambaye ana uraia wa Canada anapaswa kuomba upya uraia wake ili apate paspoti ya Kenya na kuruhisiwa kuingia Kenya.

Kulingana na serikali, Bw Miguna alipata paspoti iliyotwaliwa kinyume cha sheria.

Wakili Miguna amekataa kujaza fomu kuomba uraia wa Kenya akisema mtu hawezi kupoteza uraia wake wa kuzaliwa.

Amekuwa akikosoa muafaka kati ya Rais Kenyatta na Rais Kenyatta anaotaja kama usioweza kutatua shida zinazowatatiza Wakenya.

Kupitia jumbe za Twitter, Miguna amekuwa akidai kwamba Bw Odinga aliwasaliti wafuasi wake kwa kukubali kushirikiana na serikali.

Bw Odinga amenukuliwa akisema kwamba wakili huyo ni mtu asiyeweza kusaidiwa kwa sababu ya msimamo wake mkali.

Kwenye ujumbe wa kutangaza kurejea nchini mwezi ujao, Miguna alimlaumu Raila na Rais Kenyatta kwa masaibu yake.

“Mliharibu paspoti yangu ya Kenya na nyumba yangu, mkanikamata na kunitesa kabla ya kunifurusha, mnaweza kuandika haya kwa wino usiofutika: Nitarejea baada ya Septemba 4,” alisema.

Aliyeanika picha kujitapa anavyonajisi watoto anyakwa

NA KALUME KAZUNGU

MWANAMUME wa makamo ambaye alidai kuwanajisi wasichana wadogo na kisha kusambaza habari hizo kwa mitandao ya kijamii hivi majuzi hatimaye amekamatwa.

Mwanamume huyo aliyetambuliwa kwa jina William Mwanzombo,23, alikamatwa na polisi katika eneo la Mpeketoni, Kaunti ya Lamu jana.

Akithibitisha kukamatwa kwake, Afisa Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi wa kaunti ya Lamu, Paul Leting, alisema mwamanume huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mpeketoni kwa uchunguzi zaidi.

Bw Leting aidha alisema wameafikiana kumsafirisha mwanamume huyo hadi jijini Nairobi kwa mahojiano zaidi.

Alisema polisi wanashuku huenda mwanamume huyo anashirikiana na wengine ili kuendeleza ukatili miongoni mwa jamii na kusambaza maovu yao kwenye mitandao ya kijamii.

“Tumemkamata jamaa huyo mjini Mpeketoni. Tunamhoji na tumeafikiana kumsafirisha hadi Nairobi kwa uchunguzi zaidi. Huenda yuko na wenzake wanaoshirikiana ili kutekeleza maovu na kusambaza jumbe kwenye mitandao ya kijamii,” akasema Bw Leting.

Aidha aliwataka watumiaji wa mitandao ya kijamii na wananchi wa kaunti ya Lamu na Kenya kwa jumla kuwa macho na kuwaripoti kwa polisi wale wanaosambaza maovu mitandaoni hasa baada ya kuyatenda ili iwe rahisi kwao kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia aliwaonya wale wanaoendeleza unajisi miongoni mwa watoto kwamba siku zao zimehesabiwa.

Jamaa huyo ambaye anaaminika kutoka kaunti ya Kilifi, anadaiwa kuweka picha za watoto wasichana ambao alikuwa anajidai kushiriki nao ngono.

Mmoja wa wasichana hao alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili ilhali mwingine akiwa motto mdogo wa kati ya miaka mitano hadi sita.

Maafisa wa KEBS kukaguliwa upya

Na BERNARDINE MUTANU

Maafisa wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) watakaguliwa upya kulingana na Waziri wa Viwanda Peter Munya.

Waziri huyo Jumatano alisema kulikuwa na mipango ya kutekeleza marekebisho KEBS na kuongeza idadi ya wafanyikazi na kuwachunguza upya maafisa wa sasa.

Bw Munya alitoa agizo kwa bodi kubuni mikakati ya kuchunguza upya maafisa hao, katika zoezi litakaloanza mara moja.

“Tuna mpango wa kuongeza kiwango cha wafanyikazi, lakini tunataka kwanza kutathmini kiwango cha maadili kwa tunaowaajiri,” alisema Bw Munya.

Kulingana na waziri huyo, maafisa wa KEBS na maafisa wengine wa utekelezaji ni sehemu ya changamoto ilioko katika vita dhidi ya bidhaa ghushi na za magendo.

Maafisa wakuu wa KEBS akiwemo meneja mkurugenzi Charles Ongwae Juni walishtakiwa kwa uagizaji wa mbolea ya ubora wa chini na uenezaji wa stempu feki za KEBS.

Bei ya sukari kushuka

Na BERNARDINE MUTANU

Bei ya sukari inatarajiwa kushuka baada ya serikali kuachilia magunia milioni 1.37 ya bidhaa hiyo.

Sukari hiyo ilizuiliwa bandarini kwa kushukiwa kuwa mbaya kwa watumiaji. Mbunge wa Viwanda Peter Munya Jumatano alisema sukari hiyo ilichunguzwa na kupatikana kuwa salama kwa watumiaji.

Wiki iliyopita, wabunge walikataa ripoti ya uchunguzi iliyoonyesha baadhi ya maafisa wa serikali walihusika katika uagizaji wa sukari hiyo kutoka nje ya nchi.

Sukari hiyo imeachiliwa kwa waagizaji wake na inatarajiwa kuongeza kiwango cha sukari nchini, na kupunguza bei ya bidhaa hiyo.

Bei ya sukari nchini imepanda kwa kati ya Sh10 na Sh20 kwa sababu ya upungufu.

“Kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi, serikali itaachilia sukari iliyopatikana kuwa salama,” alisema waziri huyo.

Sukari hiyo itasindikizwa na polisi kutoka bandarini hadi katika viwanda za kuitengenezea ili iuzwe nchini.

Ruto na Waiguru wachemka kutajwa kuwa wafisadi zaidi

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto na Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru wamekemea vikali matokeo ya kura ya maoni ya Ipsos Synovate ambayo yaliwaorodhesha kama maafisa wa umma wafisadi zaidi nchini.

Matokeo ya kura hiyo ya maoni yaliashiria kuwa Bw Ruto na Bi Waiguru ndio wanashikilia nambari moja na mbili mtawalia kwa ufisadi, kulingana na maoni ya wakenya.

Kati ya wakenya 2,016 waliohojiwa  kote nchini, zaidi ya 660 walisema kuwa wanadhani Bw Ruto ndiye mfisadi zaidi nchini, huku angalau 624 wakisema Bi Waiguru ndiye wa pili kwa madoa ya ufisadi.

Lakini viongozi hao wawili hawakuchukulia suala hilo kwa wepesi, Bi Waiguru akitishia kuishtaki kampuni ya Ipsos kwa kumchafulia jina, nao wandani wa naibu wa rais wakipuuzilia matokeo hayo kuwa ya kumharibia juhudi zake za kuwa rais ifikapo 2022.

“Ipsos inatumiwa na wanasiasa kunichafulia jina kwa kuwa wanahofia kuhusu 2022. Wameona kuna maendeleo Kaunti ya Kirinyaga na wamekasirika,” Bi Waiguru akasema Jumatano, baada ya matokeo hayo kutolewa.

Mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya naibu wa rais pia alishikilia kuwa utafiti huo ulifadhiliwa na watu walio na nia ya kujenga dhana kuwa Bw Ruto ni mfisadi miongoni mwa wakenya ili kumharibia juhudi za kufika ikulu.

“Matokeo hayo ni hila za waliofeli kisiasa, wawezaje kupima dhana?” akauliza Bw Mugonyi.

Lakini akitoa matokeo hayo, mtafiti mkuu wa Ipsos Prof Tom Wolf alisema mtu hawezi kuwashtaki kwani matokeo yao yaliakisi wanavyofikiria wakenya, akisema hayo ni maoni tu ila si hukumu kwa waliotajwa.

“Kazi ya kudhibitisha ikiwa mtu aliyetajwa ni mfisadi au la ni ya idara nyingine kama mahakama, letu ni kusema wanavyodhani wakenya tu,” akasema Prof Wolf.

Babu Owino na wenzake watisha kuandamana Kampala kumnusuru Bobi Wine

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Wabunge Vijana (KYPC) kitaandaa maandamano jijini Kampala Uganda Jumatatu na kuvuruga shughuli katika ubalozi wa nchi hiyo humu nchini kupinga kuzuiliwa kwa Mbunge wa Kyandodo Mashariki Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine.

Wakilaani kukamatwa kwa mbunge huyo, maarufu kama Bobi Wine wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Fred Okello (Nyando) na Gideon Keter (Mbunge Maalum) waliukosoa utawala wa Rais Yoweri Museveni kwa kunyanyasa na kukandamiza viongozi vijana.

“Kitendo cha kukamatwa, kuzuiliwa na kuteswa kwa mwenzetu ni kielelezo cha ukiukaji wa haki za kibinadamu. Dhuluma dhidi ya kiongozi yeyote kijana ni dhuluma kwa vijana kote ulimwengu… hii ndio maana tumempa Museveni makataa ya hadi Jumatatu kumwachilia huru Bobi Wine la sivyo tutaongoza maandamano makubwa nchini Kampala Jumatatu,” akasema Bw Owino ambaye ni Katibu Mkuu wa KYPC.

“Isitoshe, endapo kufikia Jumatatu dikteta Museveni hatakuwa amememwachilia mwenzetu tutavuruga shughuli katika ubalozi wa Uganda humu nchini. Tutaamuru kufungwa kwa ubalozi huo kwa sababu Kenya haiwezi kuendelea kushirikiana na taifa ambalo linakiuka haki za kibinadamu za rais wake,” akaongeza.

Naye Bw Okello alisema wao kama wanachama wa KYPC wamekuwa wakiwasiliana na wenzao nchini Uganda kupanga maandamano ya kulaani utawala wa Museveni.

“Wabunge vijana wenzetu nchini Uganda wanafahamu kuhusu mipango yetu na Jumatatu wako tayari kuungana nasi katika maandamano ya kutetea Bobi Wine. Kamwe hatuogopi kushikwa na polisi na wanajeshi,” akasema Mbunge huyo wa Nyando.

Bw Keter alisema ilisema ingekuwa bora kama Serikali ya Uganda ingemwasilisha Bobi Wine na kumfungulia mashtaka kwa mujibu wa sheria badala ya kumfungia korokoroni.

“Serikali ya Uganda kuendelea kumtesa mwenzetu, kumnyima chakula na hata huduma za wakili. Huu ni unyama ambao haufai kuendelea katika ulimwengu wa sasa,” akasema Mbunge huyo wa chama cha Jubilee.

Akaongeza: “Uganda ni mojawapo ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambayo yametia sahihi mkataba wa kulinda haki za kibinadamu na kuheshimu utawala wa sheria. Kwa hivyo, hatutakubali haki kama hii kuendelea katika taifa hili jirani.”

Tangu wiki jana maafisa wa usalama wamekuwa wakipambana na mamia ya watu ambao wamekuwa wakiandamana nchini Uganda kupinga kukamatwa kwa Bobi Wine ambaye ni mbunge wa mrengo wa upinzani.

Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika maandamano hayo huku wengine zaidi ya 100 wakikamatwa.

Bobi Wine alikamatwa wiki jana kwa madai kuwa alipatikana na bunduki kinyume cha sheria. Hatua hiyo ilichukulia muda mfupi baada ya msafara wa Rais Museveni kupigwa mawe na umati baada ya mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo katika eneo la kaskazini mwa Uganda.

Wabunge wapinga wakulima kupigwa msasa kabla ya kulipwa

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu kutoka eneo la North Rift wamepinga agizo la serikali kwamba wakulima waliwasilisha mahindi kwa mabohari ya Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) msimu uliopita wapigwe msasa kabla ya kupokea malipo yao.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano Mbw Alfred Keter (Nandi Hills, Jubilee), Silas Tiren (Moiben, Jubilee) na Ferdinand Wanyonyi (Kwanza, Ford Kenya) walidai kuwa hatua hiyo inalenga kunyanyasa wakulima hata zaidi.

“Wakulima wamesubiri wakisubiri kulipwa kwa muda wa miezi minane sasa na kunashangaa ni kwa nini serikali inataka wakulima wakaguliwe kwanza kabla ya kulipwa ilhali walipitia mchakato huo kabla ya kuwasilisha mahindi yao kwa NCPB,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo mbishani alisema serikali ina mbinu na mikakati ya kuwatambua wakulima bandia ambao huenda wakadai malipo ilhali hawakuwasilisha mahindi na haifai “kuwasumbua wakulima tena ikitaka wapigwe msasa”

“Serikali inafahamu wakora ambao wamekuwa wakijitokea kudai malipo. Inafaa kuwaandama wakora hao badala ya kuwasumbua wakulima ambao wamesubiri tangu mwaka jana kabla ya kulipwa,” akasema Bw Keter.

Naye Bw Tiren alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati suala hilo ili kuwaondolea usumbufu wakulima wa mahindi ambao wanangojea kulipwa kwa mahindi yao tangu mwaka jana.

“Serikali imetoa pesa ili wakulima walipwe. Sasa mbona tena waambiwe kuwa wanafaa kukaguliwa. Sielewi zoezi hili ni la nini. Naomba Rais aingilie suala hilo ili wakulima wetu walipwe haraka iwezekanavyo,” akasema Mbunge huyo.

Wiki jana, serikali ilitoa Sh1.4 bilioni kwa ajili ya kuwalipa zaidi ya wakulima 600 ambao waliwasilisha mahindi yao kwa depo za NCPB mwaka jana lakini mpaka sasa hawajalipwa.

Pesa hizo ni sehemu ya Sh3.5 bilioni ambazo wakulima hao kutoka kaunti za Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia na Nakuru wanadai serikali tangu mwaka jana.

Mapema mwaka huu, kulifichuliwa sakata ambapo zaidi ya Sh1.9 bilioni ambazo zilinuiwa kulipwa wakulima hao zililipwa wafanya biashara walaghai waliowasilisha mahindi katika NCPB wakidai hao ni wakulima.

Sakata hiyo inachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Kamati maalum iliyoundwa na Seneti.

Wiki hii serikali iliwataka walikulima ambao wanapania kufaidi kutokana na malipo hayo kuwasilisha nakala za vitambulisho vyao vya kitaifa, nambari za siri za KRA, picha ndogo, tiketi za upimaji uzani na maelezo ya benki kabla ya kulipwa pesa zao.

Wakulima pia wamepinga sharti hilo na kutaka liondolewe la sivyo wafanye maandamano katika miji mikuu katika eneo zima la North Rift.

Taabani kwa kujaribu kulaghai kampuni ya bima

Na RICHARD MUNGUTI

DEREVA mmoja alishtakiwa Alhamisi kwa kujaribu kuilaghai kampuni ya bima Sh380,000 akidai alihusika kwenye ajali iliyohusisha magari matatu.

Bw Antony Maina Nyambura alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi.

Alidaiwa alijaribu kuilaghai kampuni ya bima ijulikanayo Resolutions iliyoko jijini Nairobi.

Pia alikabiliwa na shtaka lingine la kutoa habari za uwongo kwa Konstebo Charles Nyambane kwa alihusika kwenye ajali katika barabara ya Souther Bypass inayounganisha barabara kuu ya Mombasa na ile ya Thika mjini Ruiru.

Mshtakiwa alikana mashtaka mawili na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000

Kesi ya tatu ya sakata NYS kuanza Februari 2019

Na RICHARD MUNGUTI

MOJA ya kesi tatu dhidi ya waliokuwa maafisa wa shirika la huduma ya  vijana kwa taifa ya sakata ya Sh469 milioni itaanza kusikizwa Februari 7, 2019.

Kesi hiyo ilitengewa siku hiyo washukiwa 44 walipofika kortini. Baadhi ya walioshtakiwa ni aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu NYS Dkt Richard Ndubai na washukiwa wengine 41..

Kiongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu alieleza Bw Ooko kuwa atatayarisha cheti kingine cha mashtaka kitakachowashirikisha washukiwa wote 47.

Faili tatu zimeunganishwa kuwa kesi moja baada ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kumwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji agawanye kesi 10 zinazowakabili washukiwa hao wanaojumuisha wafanyabiashara wa Naivasha wa Familia ya Ngirita kuwa tatu.

“Kufuatia maagizo ya Bw Ogoti nimeunganisha kesi tatu kusikizwa kwa pamoja kwa vile mashahidi ni wamoja,” alisema Bw Riungu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa kuna washukiwa watatu ambao hawajajibu mashtaka.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na wakili Migosi Ogamba walisema wamepokea nakala za mashahidi kutoka kwa afisa anayechunguza kesi hiyo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa nakala za usahidi ambazo hazijapokewa zitachukuliwa katika afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI).

EACC yapewa fursa ya mwisho kuwakamata Wakhungu na Waluke

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) Jumatano iliipa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) fursa ya mwisho kumkamata Bi Grace Wakhungu anayeshtakiwa pamoja na Mbunge wa Sirisia John Waluke kwa kuilaghai Halmashauri ya Nafaka na Mazao NCPB Sh300 milioni katika kashfa ya mahindi.

Hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi alitoa agizo hilo wakati wa kutajwa kwa kesi dhidi ya Bw Waluke.

Mahakama ilifahamishwa kuwa maafisa wa EACC wanaendelea kuweka bidi kumsaka Bi Wakhungu anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa ushahidi wa uwongo kwa jopo lililochunguza mzozo kati ya kampuni yao na Bw Waluke iliyodai ilihuifadhia NCPB tani 40,000 za mahindi kwa gharama ya zaidi ya Sh300 milioni

Wameshtakiwa walipokea pesa hizo kwa njia ya udanganyifu. Kesi itatajwa Septemba 25, 2018.

“Ikiwa Bi Walukhe hatakuwa ametiwa nguvuni ifikapo Septemba 25 basi kesi dhidi ya Bw Walukhe itaendelea,” alisema Bw Mugambi.

Hakimu alisem mahakama haitakuwa na budi na kuendelea na kesi dhidi ya mbunge huyo na hatimaye Bi Wakhungu akikamatwa ataadhibiwa kivyake.

EACC yaagizwa impe Kidero nakala za ushahidi

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mwandamizi Bw Lawrence Mugambi Jumatano aliamuru Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) impe aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero na washtakiwa wengine 10 nakala za ushahidi katika kesi inayomkabili ya ulaghai wa Sh213 milioni.

Bw Mugambi alitoa agizo hilo baada ya kujulishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Muteti kuwa nakala za mashahidi zitakuwa tayari ifikapo Ijumaa.

Bw Muteti alisema kuwa nakala hizo zaweza kupokewa na mawakili wanaowatetea washtakiwa mnamo Ijumaa.

Bw Mugambi aliamuru kesi hiyo itajwe Agosti 29 mawakili wa washtakiwa waeleze mahakama ikiwa walizipata nakala hizo.

Dkt Kidero na wenzake wamekanusha walilipa kampuni mbili Ngurumani na Lodwar mamilioni hayo bila kutoa huduma zozote kwa gatuzi hili la Nairobi.

Washtakiwa walikanusha mashtaka 34 na wakaachiliwa kwa dhamana ya Sh3 milioni.

Masaibu ya Sofapaka yaipa Gor ushindi, ubingwa wanukia

NA CECIL ODONGO

NYOTA ya jaha ilirejea na kumulika kambi ya Mabingwa mara 16 wa KPL Gor Mahia  baada ya kuwalaza mabingwa  wa mwaka wa 2009, Sofapaka mabao 3-0 katika mechi ya KPL iliyosakatwa Agosti 22 kwenye uga wa Narok.

Mabingwa hao walifunga mabao yao kupitia kiungo Joakim Onyango katika dakika ya 33 kisha beki wa kushoto Innocent Wafula akatia msumari moto kwenye kidonda cha Sofapaka kwa kuyafunga mabao mawili safi yaliyozamisha kabisa chombo cha wapinzani katika dakika ya 63 na 84 kipindi cha pili.

Bao la pili la K’Ogalo lilifungwa kupitia penalti baada ya kipa wa Sofapaka Wycliffe Kasaya kumchezea rafu mshambulizi wa Gor Lawrence Juma kwenye boksi.

Kosa hilo liliwaponza mabingwa hao wa zamani kwa kuwa Kasaya alipokezwa kadi nyekundu na ikawalazimu Sofapaka kumaliza mechi wakiwa watu tisa uwanjani.

Masaibu zaidi yaliandama Sofapaka dakika ya 15 baada ya kocha John Baraza  kumwingiza kipa Mathias Kigonya na kumwondoa kiungo  Justin Mico.

Mlinzi Mohamed Kilime aligongana na mlinzi wa Gor Mahia Samuel Onyango na kushindwa kuendelea na mechi dakika kumi za mwisho wa mtanange huo.

Vijana wa Kocha Dylan Kerr sasa wamefungua mwanya wa alama 20 na wanahitaji sare ya aina yoyote katika mechi zao  zilizosalia ili kutwaa ubingwa wa KPL kwa mwaka wa pili mfululizo.

Ushindi huo unawapa matumaini mashabiki wa K’Ogalo ambao  walikuwa wakiendelea kuomboleza kichapo cha Jumapili Agosti 19 mikononi mwa mibabe wa soka ya Rwanda, Rayon Sports kwenye mechi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika, CAF.

K’Ogalo sasa watalazimika kurejelea mazoezi kabambe siku ya Alhamisi na Ijumaa kuyanoa makali yao dhidi ya mechi kubwa ya debi ya Mashemeji itakayowakutanisha na watani wao wa jadi AFC Leopards  Jumamosi Agosti 25 katika uga wa MISC, Kasarani kuanzia saa tisa jioni.

Sofapaka walilazimika kumaliza mechi hiyo wakiwa wachezaji kumi

Kichapo hicho sasa kinazima kabisa azma ya Sofapaka ya kuwa wagombezi halisi wa ubingwa wa KPL  msimu wa 2017/18. Batoto ba Mungu wanaonolewa na kocha John Baraza wanaendelea kushikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la ligi kwa alama 44 baada ya kujibwaga uwanjani mara 27.

Kocha Dylan Kerr alifanya mabadiliko kadhaa kwa kikosi kilichoicharaza Sofapaka ikiwemo  kumpumzisha kipa Shaban Odhoji na kumtumia Fredrick Odhiambo katika nafasi yake.

Mnyakaji huyo alidhihirisha umahiri wake na kuwanusuru  vijana wa K’Ogalo dhidi ya kufungwa goli la mapema alipookoa penalti iliyozawidiwa Sofapaka na kuchanjwa na mshambulizi matata Kepha Aswani.

Google sasa yawezesha watumiaji kutuma baruapepe za siri

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya Google imebadilisha mfumo wake wa baruapepe za Gmail, na kuongeza chaguo la kutuma au kupokea ujumbe kwa njia ya siri, na katika hali salama zaidi.

Kulingana na taarifa ya kampuni hiyo,  baruapepe za siri zitafutika baada ya miaka mitano. Pia, aliyetuma ujumbe huo atakuwa na uwezo wa kuufuta ujumbe huo wakati wowote.

Zaidi, wanaopokea jumbe hawatakuwa na uwezo wa kutumia watu wengine, kuzinakili, kuzichapisha au kuzidondoa.

Watumiaji wa Gmail pia wataweza kutengeneza muda wa mwisho wa baruapepe waliyotuma kusalia katika akaunti ya aliyetumiwa. Hii ina maana kuwa baruapepe itajifuta yenyewe baada ya muda huo kukamilika.

Barua pepe kutoka kwa mtumiaji wa Gmail itakuwa ya kawaida, lakini kutoka akaunti nje ya Gmail, kama Yahoo, baruapepe hizo zitakuwa zikifunguliwa nje ya akaunti, katika wavuti salama, imesema Google.

Huenda mtumaji wa baruapepe akawahitaji waliopokea ujumbe kutumia neno siri  kuweza kufungua barua hiyo. Nywila (password) hiyo itatumwa kwa njia ya simu au baruapepe.

Kwa watumiaji wa Gmail, nambari hiyo ya siri itakuwa ikitumwa kupitia kwa simu (ujumbe mfupi). Kwa watumiaji wa akaunti nje ya Gmail, watapokea kodi hiyo kwa baruapepe au kwa ujumbe mfupi.

Lakini watakaopokea kodi hiyo ni wanaoishi Uingereza, India, Japan, Marekani Kaskazini, na Marekani Kusini.

Aidha, unaweza kupiga picha jumbe huo  (screenshot). Ukifungua akaunti yako, ukienda kuandika ujumbe mpya kwa simu au kwa kompyuta, utapokea chaguo (option) la kuandika ujumbe huo kwa namna ya siri (confidential) kwa kutumia nukta tatu upande wa kulia wa skrini ya simu yako, ambapo unaweza kubadilisha usiri wa baruapepe yako.

Kwa kutuma ujumbe kutumia kompyuta, utafungua ‘andika ujumbe’, pale chini kuna kidude mfano wa kufuli. Ikiwa barua hiyo ni ya siri, bonyeza kidude hicho, kitakupa chaguo la jinsi unataka kutuma ujumbe wako.