Wafanyakazi watapoteza kazi wakikatwa ada ya nyumba – Waajiri

Na BERNARDINE MUTANU

Waajiri wameonya kuwa huenda wafanyakazi wengi wakapoteza kazi ikiwa serikali itatekeleza pendekezo la kukata asilimia 0.5 ya mshahara kufadhili hazina ya nyumba.

Kulingana na waajiri hao, hatua hiyo itazidisha gharama ya kufanya biashara na kuwapunguzia wafanyikazi mapato yao.

Kulingana na pendekezo hilo, waajiri na waajiriwa watakatwa hadi Sh5, 000 kufadhili mradi huo.

“Mapendekezo hayo yatazidisha gharama ya leba kwa waajiri na gharama ya maisha kwa wafanyikazi ambao hawajui jinsi mpango huo utakavyowafaidi,” alisema Rais wa Shirikisho la Waajiri (FKE) Mark Obuya Alhamisi.

Kwa sasa, waajiri huwalipia wafanyikazi Sh200 kufadhili Hazina ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF).

Ikiwa pendekezo hilo litapitishwa, wafanyikazi wote ambao wanapata Sh100, 000 watachanga Sh500 kwa mwezi kufadhili mradi huo.

Pendekezo hilo linatarajiwa kuwaathiri vibaya zaidi wafanyikazi wanaopata chini ya Sh50, 000.

DASH 100 Bombardier: FlySax yarejelea safari zake Kitale

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya ndege ya FlySax, tawi la Fly540, imerejelea safari zake za Kitale baada ya zaidi ya majuma mawili, tangu ajali mbaya ya ndege yake Juni 5, ambayo ilipelekea vifo vya watu 10.

Ndege hiyo ilirejelea safari zake Alhamisi ambapo kurejea kwa huduma zake kulipokelewa vyema na wateja wake.

FlySax ilitoa ndege kubwa, DASH 100 Bombardier, kwa ziara kati ya Wilson na Kitale.

Ndege iliyoanguka Aberdares FlySax  5Y-CAC ilikuwa ikiendeshwa na Barbara Kamau, 28 na Jean Mureithi.

Ndege DASH 100 ambayo ina nafasi 37 za abiria itakuwa ikimaliza safari kati ya Nairobi na Kitale katika muda wa dakika 50 ikilinganishwa na FlySax iliyoanguka ambayo ilikuwa ikichukua dakika 75 kati ya Nairobi na Kitale.

Pigo kwa Kamau korti kuamuru Kesi dhidi yake iendelee

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Waziri wa Uchukuzi Bw Michael Kamau alipata pigo kubwa Ijumaa baada ya Mahakama ya rufaa kutupilia mbali ombi lake ya kuzuia akishtakiwa upya kwa matumizi mabaya ya mamlaka yaliyopelekea Serikali kupoteza zaidi ya Sh33milioni za mradi wa barabara miaka kumi iliyopita.

Majaji Majaji Mohammed Warsame, William Ouko na Kathurima M’Inoti waliakataa kumzima Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP) Noordin Haji akimfungulia mashtaka upya Bw Kamau.

Majaji hao walisema kesi ya kwanza dhidi ya Bw Kamau halikutupwa mbali iliondolewa baada ya ripoti kuwa aliposhtakiwa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) haikuwa na makamishna inavyotakiwa kisheria.

Bw Kamau alishikwa na kushtakiwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta alipohutubia bunge mnamo Mei 26 2015 na kusema kulikuwa na watumishi wa umma 175 waliohusika na ufisadi wakiwamo mawaziri watano miongoni mwao Bw Kamau.

Majaji Warsame , Ouko na M’Inoti walifahamishwa wakati huo EACC haikuwa na makamishna.

Walikuwa wamejiuzulu wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw Mumo Matemu.

Bw Kamau alisema haki zake zilikiukwa aliposhtakiwa wakati wa kwanza na hata sasa alidai DPP hakuwa na mamlaka kisheria kufufua kesi iliyokuwa imeondolewa.

Katika uamuzi wao majajaji hao walisema kuwa “ Bw Kamau hakuwa ameponyoka kabisa makali ya sheria.Hii korti imechambua ushahidi wote aliowasilishwa Bw Kamau na kufikia suluhu kuwa kesi ya awali dhidi yake haikuwa imetamatishwa mbali ilikuwa imeondolewa tu na inaweza fufuliwa wakati wowote baada ya EACC kupata makamishna.”

Korti iliamuru kesi iliyowasilishwa upya dhidi ya Bw Kamau iendelee kusikizwa na kuamuliwa katika mahakama ya kusikiza kesi za ufisadi.

Majaji Warsame , Ouko na M’Inoti,” aliyeshtakiwa pamoja na wahandisi wawili kwa kubadili ramani ya ujenzi wa barabara ya Kamukuywa-Kaptana-Kapsokwony-Sirisia mwaka wa 2008 katika kaunti ya Bungoma.

Kutupwa kwa kesi hiyo sasa kumeipa afisi ya DPP kuwasilisha ushahidi mbele ya hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi aliyesitisha kusikizwa kwa kesi hiyo asubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Wakili wa Serikali Bw Ashimoshi Shitambashi alipinga ombi la Bw Kamau katika mahakama ya rufaa akisema kushtakiwa kwa waziri huyo wa zamani hakukaidi haki zake.

Katika kesi hiyo Bw Kamau alikuwa ameshtaki DPP , mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) na EACC akisema wamekandamiza haki zake kuamuru afunguliwe mashtaka upya ilhali alikuwa ameachiliwa huru na korti hii ya pili kwa ukuu.

“Naomba hii mahakama itetee haki zangu sisihujumiwe na EACC iliyoamuru nishtakiwe tena baada ya mashtaka dhidi yangu ya kwanza kutupiliwa mbali na hii mahakama,” majaji hao walifahamishwa na wakili wa Bw Kamau.

Ameshtakiwa kubadili barabara Kamukuywa-Kaptana-Kapsokwony-Sirisia mwaka wa 2008 katika kaunti ya Bungoma.

SAKATA YA NYS: Dhamana ya Lillian Omollo yakubaliwa,aondoka gerezani

Na RICHARD MUNGUTI

KATIBU mkuu Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bi Lillian Omollo alikuwa wa kwanza kuruhusiwa kuondoka gerezani baada ya dhamana alizowasilisha kukubaliwa na mahakama.

Bi Omollo na washukiwa wengine wawili watapumua hewa safi wakiwa huru baada ya kukaa gerezani siku 26 tangu Mei 28, 2018 walipozuiliwa baada ya kushtakiwa kwa sakata ya NYS iliyopelekea zaidi ya Sh460milioni kupotea.

Bi Omollo ataondoka gereza la Langata anakozuiliwa baada kutupiliwa mbali kwa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwamba dhamana zote watakazowasilisha washtakiwa zikaguliwe na kuidhinishwa na shirika la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa ARA.

Katika barua aliyokuwa ameandikia mahakama Alhamisi Bw Haji alikuwa ameitaka korti iruhusu ARA iidhinishe dhamana hizo  alizosema huenda zilinunuliwa na pesa zilizoibwa NYS.

Ombi hili lilipingwa vikali na mawakili wanaowatetea washtakiwa wakisema Bw Haji anajaribu kuhujumu maagizo ya korti.

Akitupilia mbali ombi hilo la Bw Haji hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi ni mahakama tu iliyo na mamlaka ya kukataa dhamana na kuruhusu zoezi la ukaguzi liendelee.

Bw Mugambi alisema DPP hana mamlaka kisheria kuweka masharti mapya katika utaratibu wa kuwahoji wadhamini na uhalali wa dhamana walizowasilishwa washtakiwa.

Alisema kuwa Bw Haji atakiuka sheria ikiwa ataruhusiwa kuvuruga maamuzi ya mahakama kuu iliyoweka masharti ya kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa hao wa sakata ya NYS ambapo zaidi ya Sh400milioni zillibwa kwa kulipia huduma ambazo hazikutolewa.

Mahakama kuu iliwaachiliwa washtakiwa hao Juni 19 2018.

Akiwaachilia kwa dhamana Jaji Hedqig Ong’udi aliamuru kila mshukiwa awasilishe dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa Sh2 milioni pamoja na dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni.

Bw Mugambi alisema suala alilozua DPP ni nzuri katika jitihada za kupambana na ufisadi lakini halikuwa moja ya masharti ya Jaji Ong’undi.

Alisema kama DPP angelitaka ARA ishirikishwe katika ukaguzi wa dhamana , angeliomba Jaji Ong’undi atoe agizo kwamba dhamana zote ziidhinishwe na shirika hili la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa.

“Sitamruhusu DPP awe kizingiti katika utekelezaji wa maagizo ya Mahakama kuu katika ukaguzi wa dhamana na mahojino na wadhamini,” alisema Bw Mugambi.

Hakimu huyo alisema Jaji Ong’undi alikuwa ameamuru wadhamini wakaguliwe na mahakimu wa mahakama zinazosikiza na kuamua kesi za ufisadi.

Wakipinga masharti hayo mapya aliyowasilisha DPP, mawakili Dunstan Omari, Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi walisema kinara huyu wa mashtaka anavuruga utenda kazi wa mahakama akiwa na nia “ washtakiwa wote 47 washindwe kulipa dhamana waliyopewa.”

Bw Omari aliomba korti imwekee muda Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI)  muda wa siku tatu au wiki moja akamilishe kukagua uhalali wa dhamana walizowasilisha washtakiwa na kutoa ripoti kwa mahakama.

“Tutakaa hapa muda wa miezi mitatu au minne na hata mwaka ikiwa Polisi na DPP wataruhusiwa kuvuruga utaratibu wa kuidhinisha dhamana zilizowasilishwa na washtakiwa hawa 47,” alisema wakili Assa Nyakundi.

Lakini mahakama iliamuru shughuli ya kukagua wadhamini iendelee na ikiwa kutaimbuka suali kuhusu dhamana yoyote ile basi DPP atakuwa huru kuapa Afidaviti akiomba ARA ichunguze dhamana husika.

“Kila mshtakiwa atakaguliwa kivyake. Ikiwa kutazuka swali kuhusu dhamana zitakazowasilishwa na washtakiwa basi DPP kupitia afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Paul Waweru atahoji stakabadhi hiyo,” Bw Mugambi aliamuru.

Chiloba sasa ataka Chebukati asukumwe jela kwa kumpiga kalamu

Na RICHARD MUNGUTI

Afisa mkuu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw  Ezra Chiloba aliwasilisha kesi tena mahakamani akipinga kusimamishwa kazi kwake.

Katika kesi hiyo Bw Chiloba anaomba mahakama imsukume jela mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati na makamishna wawili kwa kukaidi agizo wamrudishe kazini.

Bw Chiloba amewashtaki Mabw Chebukati na Makamishna Abdi Yakub Guliye na Boya Molu.

Bw Chiloba aliyewasilisha kesi hiyo chini ya sheria za dharura alisema maagizo yaliyotolewa wiki iliyopita iliuupuzwa na Mabw Chebukati, Guliye na Molu.

Wakili Andrew Wandabwa anayemwakilisha Bw Chiloba amesema kuwa maagizo ya mahakama arudishwe kazini yamepuuzwa.

Mahakama ya kuamua mizozo baina ya wafanyakazi na waajiriwa (ELRC) iliamuru Bw Chiloba arudishwe kazini huku ukaguzi wa ununuzi wa vifaa vilivyotumika wakati wa uchaguzi ukiendelea.

Siku hiyo IEBC iliamriwa imrudishe kazini Bw Chiloba alimwandikia barua aendelee kukaa nyumbani.

“Huku wakidharau maagizo ya hii korti washtakiwa walimwandikia barua nyingine ya kumsimamisha kazini Bw Chiloba,”  alisema Bw Wandabwa katika ushahidi aliowasilisha kortini.

Bw Wandabwa alisema hatua hii ni madharau ya hali ya juu na ukiukaji wa vipengee vya katiba.

Wakili huyo anaomba kesi hiyo isikizwe upesi kwa vile haki za Bw Chiloba zimekandamizwa na heshima kwa mahakama imeendelea kutiwa ndoa.

Jaji Onesmus Makau aliamuru mnamo Juni 14, aliamuru washtakiwa wamrudishe Bw Chiloba kazini.

Mnamo Oktoba 2017 Bw Chiloba alichukua likizo ya wiki tatu miito ajiuzulu ilipozidi. Wakati huo kampeini za uchaguzi wa kiti cha urais ulikuwa umepamba moto baada ya Mahakama ya Juu kuharamisha ushindi wa Rais Kenyatta.

Viongozi wa upinzani walikuwa wamechacha wakimtaka Bw Chiloba ajiuzulu baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta.

Bw Chiloba anaomba mahakama ibatilishe uamuzi wa kusimishwa kazi kwa mara ya pili.

Walioshtakiwa kununua rukwama za Sh900,000 warudishwa ndani

Na RICHARD MUNGUTI

KUHUKUMIWA kwa waliokuwa wafanyakazi wa kaunti ya Bungoma waliopatikana na hatia ya kununua rukwama tisa kwa gharama ya Sh983,880 kuliahirishwa kwa mara ya nne Ijumaa baada ya hakimu kusemekana ni mgonjwa.

Kutosomwa kwa hukumu hii iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu kuliimbua manung’uniko makali kutoka kwa familia za washtakiwa hata ikabidi hakimu aamuru wanyamaze na kuheshimu korti.

Adhabu ilikuwa inatarajiwa kupitishwa na hakimu mkuu wa Kakamega Bw Bildad Ochieng’.

Kesi hiyo ilitajwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Thomas Muraguri aliyewajulisha washtakiwa kuwa Bw Ochieng’ hajihisi vizuri na hakufika kortini.

“Hakimu aliyesikiza kesi hii hajisikii vizuri. Hakufika kazini leo. Itabidi kesi hii itajwe Juni 25 2018 ,” alisema Bw Muraguri.

Alipoahirisha kusomwa kwa uamuzi huo Bw Ochieng’ alisema hakuwa ametayarisha  uamuzi huo kutokana na kazi nyingi.

Lakini nje ya mahakama kulikuwa na sokomoko huku washtakiwa wakiwapungia mikono jamaa wao huku wakisukumwa kuingia seli na maafisa wa polisi.

Baadhi ya jamaa wa washtakiwa waliwaambia wajipe moyo vita vinaendelea (Aluta Continua).

Washtakiwa hao walipatikana na hatia ya kufuja pesa za umma kwa kununua Wilubaro tisa kwa bei ya ShSh 983,880, kumaanisha kila moja ilinunuliwa kwa bei ya Sh109,350.

Walioshtakiwa ni Bw Howard Lukadilu (mwenyekiti wa kamati ya utoaji zabuni), Bw Oscar Onyango Ojwang’ (naibu wa mwenyekiti) na Bw John Juma Matsanza (afisa mkuu).

Wengine walioshtakiwa ni Ayub Tuvaka China, Arlington Shikuku Omushieni, Jacquueline Nanjala Namukali na Reuben Cheruyiot Rutto.

Upande wa mashtaka unaoongozwa na Bw Paul Juma uliomba korti iwasukumie kifungo cha miaka 10 gerezani akisema makosa waliyoyafanya ni mabaya

#LewaMarathon kufanyika Juni 30

Na BERNARDINE MUTANU

Mbio za 19 za Lewa zitafanyika Jumamosi Juni 30, 2018 katika Hifadhi la Wanyamapori la Lewa.

Mbio hizo (nzima na nusu) ambazo zimefadhiliwa na Safaricom zitashirikisha wananchi kutoka mataifa mbali mbali ulimwenguni.

Watakaoshiriki sio lazima wawe wanariadha mahiri, wanaweza kuwa wanariadha wowote wanaotaka kushiriki.

Mashindano hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuchangisha kusaidia jamii na kuhifadhi wanyama wa mwituni.

Watakaoshiriki wanaweza kujiandikisha katika tovuti ya hafla hiyo.

Kenya yapata mkopo mwingine kutoka Ufaransa

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeongeza kiwango cha mkopo kufikia Sh2.54 trilioni baada ya kupewa mkopo wa Sh47 bilioni na Mamlaka ya Maendeleo ya Ufaransa (FDA).

Mkopo huo ulioidhinishwa na Mkurugenzi Mkuu wa FDA  Alhamisi utagharamia miradi ya uzalishaji wa kawi, maji, uchukuzi na usimamizi wa fedha za umma.

Shirika hilo liliingia katika mkataba na KenGen kufadhili uzalishaji wa kawi ya upepo Meru. KenGen ilipata Sh7 bilioni kufadhili ujenzi wa kiwanda hicho kitakachozalisha kawi ya uwezo wa 80 MW.

Kampuni ya kusambaza umeme(Ketraco) ilipata Sh10.9 bilioni ambazo zitatumiwa kujenga kituo kidogo Makindu na kituo cha kudhibiti shughuli cha kampuni hiyo.

Pia itafadhili mradi wa mfumo wa kusambaza stima wa Nairobi Ring. Mkurugenzi Mkuu pia alitia sahihi mkataba wa Sh14 bilioni kufadhili mradi wa Mwache, chini ya Bodi ya Maji ya Coast Water, kwa lengo la kumaliz upungufu wa maji Mombasa kwa kuongeza kiwango cha maji kinachotolewa kutoka lita milioni 50 kwa siku hadi lita milioni 190 kwa siku.

Kwa sasa, mji huo unahitaji lita milioni 150 za maji kila siku.

IGAD yabuni sera kurahisishia wanachama wake biashara mipakani

Na BERNARDINE MUTANU

JUMUIYA ya Mamlaka ya Kimataifa kuhusu Maendeleo (IGAD) imepitisha sera ya biashara isiyo rasmi nje ya mipaka pamoja na usimamizi wa pamoja wa kiusalama miongoni mwa mataifa husika.

Sera hiyo ilipitishwa Ijumaa na mawaziri kutoka mataifa husika na itawasilishwa kwa marais wa IGAD kabla ya kuwasilishwa kwa Muungano wa Afrika (AU).

Mawaziri hao kutoka Kenya, Djibouti, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Somalia na Uganda walikutana Mombasa, Kenya  walikopitisha sera hiyo.

Viongozi hao walisema sera hiyo itasaidia katika kuimarisha eneo la biashara huru Barani Afrika (FTA).

Mnamo Machi 21, zaidi ya mataifa 40 kutoka Afrika yalitia sahihi mkataba wa kuunda FTA ili kuimarisha biashara kati ya mataifa washirika.

M-Tiba ya Safaricom yatambuliwa ulimwenguni

Na BERNARDINE MUTANU

Huduma ya matibabu ya Safaricom, M-Tiba, imetambuliwa ulimwenguni kama teknolojia inayobadilisha maisha.

Huduma hiyo imeungana na huduma zingine zilizotambuliwa ulimwenguni kama vile Twitter, Spotif na Google, ambazo zimebadilisha maisha katika jamii.

Huduma hiyo inayotolewa kwa njia ya apu ilitambuliwa na World Economic Forum (WEF).

M-Akiba ni miongoni mwa kampuni tatu kutoka Barani Afrika ambazo zilitambuliwa mwaka huu.

Kampuni nyingine ya Kenya iliyotambuliwa ni BitPesa.

Mpango huo huwaruhusu watumiaji kulipia huduma za matibabu kwa M-Pesa.

M-Akiba haijafikia malengo tuliyoweka – Rotich

Na BERNARDINE MUTANU

Utafiti mpya kuhusu matumizi ya M-Akiba umeonyesha kuwa huduma hiyo haifanyi vyema kama ilivyotarajiwa.

Kulingana na Waziri wa Fedha Henry Rotich, wawekezaji katika M-Akiba wanasumbuka kupata wanunuzi.

Waziri huyo alisema ili M-Akiba iweze kuimarika, lazima hati za dhamana za muda mfupi- zilizo na uwezo wa kukomaa katika muda wa chini ya miaka mitatu, kama ilivyo katika soko la rejareja.

Kutokana na hilo, Hazina ya Fedha inatathmini kugeuza mfumo M-Akiba ili kukabiliana na mahitaji katika soko la reja reja, alisema Bw Rotich Alhamisi.

Utafiti huo ulifanywa na Shirika la Financial Sector Deepening Africa likishirikiana na serikali ya Uingereza.

Mwaka 2017, ni wawekezaji 303,534 pekee ambao waliwekeza katika M-Akiba.

Kundi la wenye magari kuwapa chakula wakazi wa pato la chini

Na BERNARDINE MUTANU

Klabu ya magari ya Bundu Rovers imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wananchi kuhusu athari za mafuriko ya hivi majuzi, ikiwa ni pamoja na njaa.

Klabu hiyo ilizindua kundi la magari 25 aina ya land rover katika ziara ya kilomita 2000 inayofahamika kama ‘Desert Drive against Hunger’.

Kundi hilo njiani litagawa chakula na bidhaa zingine kwa jamii zinazohitaji. Akiongea wakati wa uzinduzi  huo Alhamisi, mwenyekiti wa Bundu Rovers Rikky Aguda alisema, “Ajenda yetu ni kuacha historia njema katika jamii ambazo tutapitia. Tutasaidia katika kuimarisha viwango vya chakula nchini.”

Mafuriko yalisababisha uharibifu mkubwa wa mimea katika baadhi ya maeneo hali inayotishia usalama wa chakula maeneo hayo.

“Tunajua hatuwezi kusaidia kila mtu, lakini tutasaidia washikadau wetu kama vile Misheni ya Katoliki North Horr. Tutatoa kidogo tulicho nacho kuzisaidia jamii,” aliongeza.

Safari hiyo inatarajiwa kuanza Jumamosi Juni 23, 2018 Nairobi na magari hayo yatapitia North Horr, Kaunti ya Marsabit, Chalbi Desert, Mbuga ya Wanyamapori ya Sibiloi, Loiyangalani, Laisamis, Nanyuki  na kurejea Nairobi Julai 1 baada ya siku tisa kichakani.

Faxe Gold, bia mpya yatua mitaani kushindana na Tusker

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya kutengeneza pombe ya Demark, Royal Unibrew imezindua mauzo ya bia mpya nchini Kenya.

Kampuni hiyo ilizindua pombe Faxe Gold ambayo itashindana na aina za pombe zilizoko nchini zenye uwezo wa kiwango cha wastani kama Tusker, Pilsner, White Cap na Allsops.

Kiwango cha pombe kilichoko ndani ya kileo hicho ni asilimia 5.5 na itapatikana ndani ya chupa ya milimita 330 na chupa za milimita 500.

Tayari, kuna pombe Faxe 10 na Faxe Stout 7.7 nchini Kenya.

Faxe Gold itasambazwa na Patiala Distillers, na inatarajiwa kushindana na pombe zingine nchini zenye uwezo huo.

Jamii zilizobaguliwa kunufaika na sera ya kugawa rasilimali

Na BERNARDINE MUTANU

Tume ya Kugawa Rasilimali (CRA) Ijumaa ilizindua sera ya pili ambayo inalenga kutambulisha maeneo yaliyobaguliwa.

Sera hiyo pia inatambulisha utaratibu wa kugawa rasilimali kutoka kwa hazina ya usawazishaji.

Kupitia kwa sera hiyo, maeneo 1424 yametambulishwa katika wadi 366, kaunti 34, kama yaliyoachwa nyuma zaidi kimaendeleo.

Sera hiyo inalenga kuimarisha upataji wa huduma za kimsingi miongoni mwa wananchi 5.6 milioni.

Baadhi ya jamii zilizotambulishwa na kuorodheshwa kuachwa nyuma kimaendeleo ni Waat, Makonde, Elmolo na Dorobo-Saletia.

Kulingana na sera hiyo, jamii hizo zinahitaji miradi maalum ili kuimarisha hali zao za kijamii na kiuchumi.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa sera hiyo, Dkt Jane Kiringai alisema, “Tume hii ina wajibu wa kukuza sera ambayo inabainisha utaratibu wa kutambulisha maeneo yaliyoachwa nyuma kwa lengo la kugawa rasilimali kutoka kwa hazina ya usawazishaji.”

Wakazi wafurahia biashara ya mafuta ndani ya Bahari Hindi

NA KALUME KAZUNGU

WAUZAJI mafuta ya petroli, diseli na gesi ndani ya Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu wamekiri kupata kivuno kutokana na idadi ndogo ya wanabiashara ambao wamejitolea kuwekeza kwenye biashara hiyo.

Wafanyabiashara wa petroli, diseli na gesi katika kisiwa cha Lamu hawaruhusiwi kuendeleza biashara hiyo ndani ya mji huo na badala yake wanatakiwa kuweka vituo vyao vya mafuta ndani ya Bahari Hindi.

Mmoja wa wahudumu wa vituo vya mafuta ndani ya Bahari Hindi, Crasmy Wanje (kulia) akihudumia wateja. Asema kwa siku anaweza kuhudumia hadi wateja 3000 na kuzoa zaidi ya Sh 200,000 kwa kuuza mafuta baharini. Asema biashara ya mafuta ndani ya bahari hindi imenoga. Picha/ Kalume Kazungu

Sababu kuu ya kaunti kuafikia marufuku hiyo ni kwamba mji wa kale wa Lamu ni mdogo.

Isitoshe, nyumba nyingi ziko pamoja pamoja, hatua ambayo inaleta ugumu kwa magari ya kuzima moto kuhudumu ndani ya mji endapo mikasa ya moto itazuka.

Ni biashara ambayo wakazi wengi wanaifurahia, hapa ni njoo nikupimie. Picha/ Kalume Kazungu

Kufuatia ughali wa kuwekeza vituo vya mafuta ndani ya Bahari Hindi, ni wafanyabiashara wachache pekee ambao wanaendelea biashara hiyo.

Katika kisiwa cha Lamu ambapo zaidi ya wakazi 10,000 wanaishi, vituo vitano pekee vya mafuta ndivyo vinavyohudumia idadi hiyo kubwa ya wakazi.

Mmoja wa manahodha wa boti akisimamisha boti yake ambayo imejaa abiria huku akiweka mafuta kituoni ili kuendelea na safari ndani ya Bahari Hindi kisiwa cha Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Utafiti uliofanywa na Taifa Leo juma hili ulibaini kwamba biashara ya vituo vya mafutya ndani ya bahari ni miongoni mwa uwekezaji unaofanya vyema zaidi kwenye mji wa Lamu.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na wanahabari walisema wanahudumia mamia ya wateja kila siku, hatua ambayo imewafanya kuvuna faida kubwa.

Mmoja wa wamiliki wa biashara hizo, Bw Omar Abdalla alisema licha ya kupata ugumu katika kuanzisha na kuendeleza kituo vya mafuta baharini, bado wanapata faida ambayo inawawezeka kuiendeleza biashara hiyo.

Jahazi la kununua na kuuza mafuta likielea ndani ya Bahari ya Hindi. Picha/ Kalume Kazungu

“Mwanzo wa kubuni kituo cha mafuta baharini huwa ndio mgumu lakini kuendeleza biashara hiyo si shida. Utahitajika kusafirisha mafuta kutoka Mombasa hadi Lamu.

Kisha utahitajika kuyavukisha hadi kwenye kituo chako cha mafuta ndani ya bahari. Zote hizo ni gharama lakini licha ya yote bado tunapata faida baada ya kuuza mafuta hayo,” akasema Bw Abdalla.

Mojawapo ya vituo vya mafuta ya petroli, diseli na gesi ndani ya Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu. Wawekezaji kwenye biashara hiyo wakiri kuvuna pakubwa kutokana na kukosekana kwa ushindai wa kibiashara. Picha/ Kalume Kazungu

Mmoja wa wahudumu wa kituo cha mafuta ndani ya Bahari Hindi, Crasmy Wanje alikiri kuhudumia hadi wateja 3000 kwa siku.

“Wateja wangu wengi ni wahudumu wa boti, waendeshaji pikipiki na hata watalii wanaozuru eneo hili wakitumia boti zao za kisasa. Mimi huuza mafuta na kupata hadi Sh 200,000 kwa siku.

Biashara ya mafuta ndani ya Bahari inafanya vyema kwani hatuna ushindani wa kibiashara hapa,” akasema Bw Wanje.

KDF wanatuhangaisha usiku,walia wakazi wa Mpeketoni

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa miji ya Mpeketoni, Hongwe na Kibaoni Kaunti ya Lamu wamelalamikia mateso wanayopitia mikononi mwa maafisa wa jeshi (KDF) wanaoshika doria eneo hilo hasa majira ya usiku.

Wakiongozwa na Mwakilishi wa Wadi ya Hongwe, James Komu, wakazi wamelalamika kwamba KDF wamekuwa wakiwapiga na kuwalazimisha kuogelea au kunywa maji chafu ya vidimbwi barabarani punde wanapowapata wakitembea barabarani usiku.

Bw Komu alimtaka waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang’i kuingilia kati na kukomesha madhila yanayoendelezwa na KDF dhidi ya wananchi wa Mpeketoni.

Pia aliitaka serikali kueleza waziwazi iwapo sheria ya kutotembea usiku almaarufu kafyu bado inaendelezwa eneo la Mpeketoni.

Mnamo Juni, 2014 siku chache baada ya Al-Shabaab kushambulia na kuua wakazi zaidi ya 100 mjini Mpeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi, serikali iliamrisha kafyu kuendelezwa kwenye kaunti ya Lamu.

Mojawapo ya sehemu ya mji wa Mpeketoni. Wakazi wanadai KDF wamekuwa wakiwahangisha na kuwadhulumu usiku. Picha/ Kalume Kazungu

Sheria hiyo hata ghivyo iliondolewa tangu Oktoba, 2015 baada ya usalama kudhibitiwa Lamu.

Bw Komu alisema inashangaza kwamba wakazi wa Mpeketoni na sehemu zingine za Lamu bado wamekuwa wakinhyimwa uhuru wa kutembea.

“Ikifika saa mbili za usiku na ukiwa Mpeketoni, Kibaoni au Hongwe basi una kesi ya kujibu. Maafisa wa KDF wakikupata wanakupiga na kukudhalilisha. Wakazi hapa wamekuwa wakinilalamikia na lazima dhuluma hizo zikome.

Kwa nini watu wetu wanyimwe uhuru wa kutembea sehemu yao ilhali hakuna kafyu? Hatujaridhishwa na tabia za KDF na ningeomba Waziri Matiang’i achunguze na kukomesha visa hivyo hapa Mpeketoni. Tunaumia,” akasema Bw Komu.

Naye Simon Kimani alisema idadi kubwa ya wananchi wanalazimika kujikaza kubakia majumbani mwao kufikia saa kumi na mbili unusu jioni ili kuepuka kichapo kutoka kwa walinda usalama.

Kwa upande wake aidha, Msemaji wa KDF, David Obonyo alikana kuwepo kwa dhuluma zozote zinazoendelezwa na KDF dhidi ya wananchi wa Mpeketoni na Lamu kwa jumla.

Badala yake, Bw Obonyo alisema wamejitahidi kuendeleza ushirikiano bora na raia eneo hilo.

“Madai hayo si ya kweli. KDF hawawezi kudhulumu mwananchi bila sababu. Hiyo itakuwa ni kuzidisha ugumu wa kazi yetu. Jumatano tulikuwa na kikao na wananchi na hata viongozi eneo hilo na malalamishi yao yalikuwa ni kuhusu polisi. Wanadai polisi wanaitisha hongo kutoka kwa raia eneo hilo. Hakukuwa na malalamishi yoyote yaliyohusisha KDF,” akasema Bw Obonyo.

Aliwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na walinda usalama eneo hilo ili kuhakikisha vita dhidi ya Al-Shabaab vinafaulu na Lamu isalie kuwa na amani.

Vyuo vyatakiwa kubuni ofisi za kusaidia wanafunzi kuhusu ajira

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Amina Mohamed ameamuru vyuo vikuu na vyuo vya kadri kote nchini kuanzisha afisi za kuwashauri wanafunzi kuhusu mahitaji ya soko la ajira (Offices of Career Services-OCS) kuanzia mwezi Julai.

Alisema huduma zitakazotolewa katika afisi hizo zitawawezesha wanafunzi kupata ajira kwa urahisi baadhi ya kukamilisha kozi zao, hatua ambayo itapunguza tatizo la sasa ambapo idadi kubwa ya vijana hawana ajira baadhi ya kuhitimu kwa shahada za juu.

“Takriban vijana milioni moja hutimu kila mwaka kutoka vyuo vikuu na vyuo vingine vya kadri. Lakini inasikitisha kuwa ni mmoja pekee kati ya watano kuweza kupata ajira katika sekta ya umma. Idadi kubwa hukosa ajira kwa sababu ya kukosa ujuzi na maarifa zinazohitajika katika soko la ajira nyakati hizi,” akasema Bi Mohamed.

Akaongeza: “Hii ndio maana Wizara yangu kwa ushirikiano na vyuo husika na wahisani wengi imebuni mpango huu wa kuanzishwa kwa afisa maalum za kutoa mwongozo na ushauri kwa wanafunzi kuhusu kozi ambazo zitawapa ujuzi na maarifa zinazolandana na mahitaji ya soko la ajira.”

Bi Mohamed alivitaka vyuo hivyo kutumia sehemu ya bajeti zao kufadhili uanzishwaji wa afisi hizo katika mabewa yao huku akiongeza kuwa wizara yake itavipa rasilimali zinazohitajika, “endapo patatokea haja ya kufanya hivyo.”

Waziri huyo alisema hayo Alhamisi alipozindua mpango huo kuanzishwa kwa afisi hizo, katika hafla iliyoandaliwa katika ukumbi wa Taifa Hall, katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Bi Amina ambaye aliandamana na Waziri Msaidizi Simon Kachapin na makatibu katika wizara hiyo, alisema mpango huo ni sehemu ya mabadiliko ambayo serikali imeanzisha katika sekta ya elimu ya juu.

“Wanafunzi wataelekezwa na kufundishwa mbinu ambazo zitawawezesha kupata ajira kwa urahisi. Hii ina maana mitaala ya masomo katika vyuo vya masomo ya juu vitahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kulandana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa pamoja na malengo ya maendeleo nchini Kenya,” akasema.

SHANGAZI: Nimegawia wengi asali lakini sijawahi kuhisi utamu

Na SHANGAZI SIZARINA

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 28 na nimekutana na wanaume kadhaa tangu nijue masuala ya mahaba. Ajabu ni kuwa sijawahi kufurahia utamu wa burudani hata siku moja. Je, nina kasoro?
Kupitia SMS

Kusema kweli sijawahi kukutana na mtu mwingine aliye katika hali kama hiyo yako. Wengi wao hasa hulalamika kwamba hawatosheki. Inawezekana kwamba unaokutana nao hawana ujuzi unaohitajika kusisimua hisia zinazoleta utamu wa shughuli hiyo. Kuwa na subira, siku moja utakutana na pwaguzi akushughulikie ipasavyo.

Hana muda wa kusema nami

Hujambo shangazi. Nilikuwa na mpenzi na nikaenda kazi mbali. Nikiwa huko alikuwa akinipigia simu kuniambia jinsi anavyonipenda na hata kuniahidi kuwa tutaoana. Nilirudi majuzi kwa likizo na nilipompigia simu akakata na kunitumia SMS akisema hana wakati wa kuongea nami. Baadaye nilimpigia simu akazima. Nifanyeje?

Tabia ya mpenzi wako ni ishara kwamba hataki tena uhusiano kati yenu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba alishikana na mwanamume mwingine ulipokuwa mbali naye. Mapenzi hayalazimishwi kwa hivyo itabidi ukubali uamuzi wake.

Amenizidi umri, je nimkubali?
Shangazi nina mpenzi lakini kuna jambo linalonitia wasiwasi. Amenizidi umri kwa mwaka mmoja na ninashangaa iwapo ninaweza kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa kunishinda. Nishauri.

Nimesema mara nyingi katika safu hii kuwa umri si hoja sana wawili wanapopendana. Isitoshe, tofauti ya mwaka mmoja ni ndogo sana na hilo si jambo linalofaa kukutia wasiwasi. Ondoa hofu na ushughulikie uhusiano na ndoa yenu.

Rafiki alimnyaka sasa wameachana

Vipi shangazi. Kuna msichana niliyempenda lakini akanyakuliwa na rafiki yangu kabla sijamdoekezea hisia zangu kwake. Sasa wameachana na bado nampenda. Ninajua pia nikimwambia nampenda atanikubali. Nishauri.
Kupitia SMS

Sijui unahitaji ushauri gani ilhali kila jambo liko wazi kutokana na maelezo yako. Unasema kuwa wameachana sasa hana mpenzi, bado unampenda na una hakika ukimwambia atakubali. Unangoja nini? Ukizubaazubaa atanyakuliwa tena. Shauri yako.

Hakutaka nijulikane na watu wa kwao

Shangazi pokea salamu zangu. Ni mwaka mmoja sasa tangu nilipooa. Ajabu ni kuwa mke wangu huwa hataki jamaa zake wajue kuwa ameolewa. Amekuwa akiwadangaya yuko kazini na pesa anazowatumia huwa zinatoka kwangu. Juzi alisafiri kwao na amekataa kurudi. Nifanye nini?

Ukweli ni kuwa huyo unayemuita mke wako hakupendi bali alikuchezea akili tu ili kwanza avune pesa kutoka kwako. Ndiyo maana hakutaka ujulikane kwao wala jamaa zake wajue kuwa ameolewa kwa sababu hiyo haijawa nia yake kwako. Kama ameenda kwao na amekatalia huko, usimngojee kwani hatarudi. Ameshapata alichokuwa akitaka kutoka kwako.

Mamake anapinga

Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na mpenzi wangu ana miaka 21. Yeye yuko tayari kunioa lakini mama yake anapinga akisema bado hajafikisha umri. Nifanye nini?

Mimi pia nahisi ni mapema kwa mwanamume huyo kuoa kwani bado hajakomaa kiakili kiasi cha kuweza kushughulikia masuala ya ndoa. Labda pia hana uwezo wa kukimu familia na ndiyo maana mama yake anapinga. Ikiwezekana subiri labda afikishe angalao miaka 25.

Nampa pesa lakini hanipakulii

Shikamoo shangazi? Mimi nina mpenzi lakini nimegundua kuwa haja yake kwangu ni pesa tu hakuna mapenzi. Nikimuomba asali anaruka. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Kama huna habari, si lazima mwanamke akulambishe asali ili kuthibitisha penzi lake kwako. Tendo hilo hasa linafaa kusubiri hadi watu wanapooana. Hata kama unampa pesa mpenzi wako, unafanya hivyo kwa hiari wala si kumhonga ili akulambishe asali. Ukihisi kwamba anakutumia vibaya acha kumpa pesa ama uachane naye.

ANGLO LEASING: Githu na Wako waeleza mabilioni yalivyotoweka

Na RICHARD MUNGUTI

WALIOKUWA wanasheria wakuu Mabw Amos Wako na Prof Githu Muigai Alhamisi walieleza jinsi waliomba mataifa ya kigeni kusaidia Kenya kuchunguza kashfa ya Anglo-Leasing na kutambua zilikokuwa zimefichwa pesa zilizolipwa kampuni zilizohusika na sakata hiyo.

Bw Wako na Prof Muigai walifichua kuwa pesa hizo zilikuwa zimefichwa katika mataifa ya Uswizi , British Virgin Islands na Amerika.

Maafisa wakuu kutoka nchi hizo waliwasilisha ushahidi kwa Prof Muigai , alioupeana kwa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuwachunguza wakuu serikalini na wenye makampuni hayo.

Bw Wako na Prof Githu waliotoa ushahidi mmoja baada ya mwingine walisema “ ushahidi ulipoletwa uchunguzi ulianza na washukiwa wakatiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.”

“Niliomba Kenya isaidiwe na Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Uswizi mwenye tajriba ya juu Dkt Mark Henzline aliyechunguza kampuni ya Anglo-Leasing na kuipa Kenya ushahidi. Pesa zilizokuwa zimelipwa kampuni hiyo Euro 5.2milioni (Sh506milioni) zilirudishwa nilipofutilia mbali kandarasi hiyo ya kuuzia idara ya polisi vifaa,” alisema Bw Wako.

Alitoa kama ushahidi wa vyeti 47 vya kandarasi tano kati ya Kenya na InfoTalent vya ununuzi wa vifaa vya usalama vya idara ya polisi.

Seneta wa Busia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu akiwa mahakamani Juni 21, 2018. Picha/ Richard Munguti

Wanasheria hawa wakuu walieleza jinsi waliandika mabarua ya kuomba Kenya isaidiwe kupokea ushahidi wa makampuni yaliyokuwa yanahusika kutoka ng’ambo.

Wawili hawa waliotoa ushahidi mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku walisema mataifa hayo ya kigeni yaliipa Kenya ushahidi kuhusu makampuni yaliyokuwa yamehusika katika sakata hiyo ya Sh3.8bilioni.

Wastaafu hawa walisema hayo walipotoa ushahidi dhidi ya wafanyabiashara watatu wa kimataifa Mabw Deepak Kamani, Rashmi Kamani na baba yao Chamanlal Kamani wanaoshtakiwa kwa kashfa hiyo pamoja na waliokuwa makatibu wakuu wizara za fedha na afisi ya rais Mabw David Onyonka na Dave Mwangi.

Watano hawa wamekanusha kufanya njama za kuilaghai Serikali zaidi ya Euros 40milioni (Sh3.8bilioni) kupitia mradi wa kununulia idara ya polisi vifaa vya mawasiliano na maabara almaarufu E-Corps.

“Nilifutilia mbali kandarasi iliyokuwa imetiwa saini kati ya Kenya na kampuni ya kimataifa ya InfoTalent iliyomilikiwa na familia ya Kamani,” alisema Bw Wako.

Bw Wako alisema afisi yake wakati huo mwaka wa 2003 iliombwa na aliyekuwa katibu Afisi ya Rais Bw Mwangi isome na kuidhinisha kandarasi iliyokuwa imetayarishwa kati ya Serikali na InfoTalent inayomilikiwa na familia hiyo ya Kamani  yenye afisi nchini Geneva , Uswizi.

“Bw Mwangi aliomba afisi yangu isome na kutoa ushauri wa kisheria kuhusu kandarasi kati ya Kenya na InfoTalent,” alisema Bw Wako.

Kandarasi hiyo, Bw Wako alisema ilisomwa na mawakili wa Serikali Bw D Achapa na Bi Roselyn Amadi wote wa kitengo utengenezaji kandarasi kati ya Kenya na Nchi za Kigeni.

Kandarasi hiyo ilisomwa na Bi Amadi na kuirudisha OP irekebiswe.

“ Ilirudishwa tena na Amadi akaikosoa kisha akarudisha OP,” alisema Bw Wako.

Hatimaye ilitiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu David Mwiraria , aliyekuwa Katibu mkuu Wizara ya hazina Bw Joseph Magari, Bw Mwangi  na InfoTalent.

Kesi itaendelea Agosti 20 2018 mashahidi wanane watakapotoa ushahidi.

Mkuu wa ATPU aamriwa kufika kortini

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA anayesimamia kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU)  Alhamisi aliamriwa afike kortini kueleza sababu ya kutowaachilia washukiwa watano wa ugaidi.

Hakimu mwandamizi alitoa agizo hilo baada ya kufahamishwa na wakili Albert Makori kuwa “ Polisi wamekaidi agizo lake.”

“Polisi wa kitengo cha ATPU wamekataa kuwaachilia washukiwa watano wa ugaidi ambao wamekaa rumande mwezi mmoja sasa,” alisema Bw Makori.

Bw Makori alisema polisi hawakuwapata na hatia washukiwa hao Mabw Abdi Aziz Bule Ali, Abey Rashid Ibrahim,Hassan Osman Mohamud  Abdirahaman , Bashir Mohammed na Qadro Jamal Gaite na wamekataa kuwaachilia kinyume cha sheria.

Bi Mutuku aliamuru Juni 18 washukiwa hawa waachiliwe huru lakini polisi wanaendelea kuwazuilia.

“Naomba hii mahakama iamuru msimamizi wa ATPU afike kortini kueleza sababu ya kukaidi maagizo ya mahakama,” Bw Makori alimweleza hakimu.

Nitakaa na Ruto sako kwa bako, aapa Jumwa

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Malindi, Aisha Jumwa ameapa kuendelea kumpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022. Hii ni licha ya tishio kutoka kwa chama chake cha ODM la kuwaadhibu wabunge waasi.

BI Jumwa alizungumza siku moja baada ya kiranja wa walio wachache bungeni Junet Mohamed kueleza nia ya ODM kumwondoa mbunge huyo katika kamati ya Utumishi wa Bungeni (PSC) yenye mamlaka makubwa.

Katika kikao cha wanahabari jana mjini Malindi, mbunge huyo, ambaye alikuwa mmoja wa wandani wakuu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo la Pwani, alisema hatakubali kutishwa na mtu yeyote kuhusu misimamo yake ya kisiasa.

“Hatutakubali kutishwa. Kama nilivyosema awali, sina mgogoro wowote na ODM wala kiongozi wa chama. Lakini msimamo wangu kumuunga mkono Bw Ruto kuwa rais 2022 hautabadilika. Huo ni uamuzi wangu,” akasema.

Bi Jumwa aliongeza kuwa haijalishi kama ODM kitakuwa na mgombeaji wa urais 2022 lakini msimamo wake wa kisiasa utabaki kuwa anamuunga mkono naibu rais.

“Sioni kama kuna shida yoyote na msimamo huo, na hili halifai kuwa suala linaloibua utatanishi katika ODM,” akasema.

Kulingana naye, ripoti kwamba chama kimenuia kumwondoa katika kamati ya bunge ni uvumi kwani hajapokea mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa Spika wa Bunge Justin Muturi kuhusu suala hilo.

“Sijafanya kosa lolote. Ninafuata tu nyayo za Raila Odinga, na ninataka kusema kuwa sina ubishi wowote dhidi ya chama, viongozi wake wala wanachama wengine. Wadhifa niliopewa katika PSC haukuwa wa hisani bali ni haki ya Wapwani baada ya kukipa chama kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita,” akasema.

Aliongeza: “Sisi ni washirika katika ODM na kila mmoja anajua tulivyochangia pakubwa chamani wakati wa uchaguzi uliopita. Kwanza tulipewa nafasi chache sana katika ODM.”

Kulingana naye, msimamo wake kumfuata Bw Ruto ulitokana na muafaka wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuleta umoja wa kitaifa, na pia unalenga kufanikisha malengo ya maendeleo yanayoendelezwa na serikali kuu.

Kwenye barua iliyoandikwa kwa spika wa bunge, Bw Mohammed, ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki, alitaka apewe mwongozo wa jinsi ya kumwondoa Bi Jumwa kutoka wadhifa huo wa PSC.

Kuna wabunge karibu kumi wa upinzani kanda ya Pwani ambao wamekuwa wakihudhuria msururu wa hafla za Bw Ruto katika eneo hilo, huku wengine wao wakitangaza wazi kuunga mkono maazimio yake ya urais.

Baadhi yao, akiwemo Bi Jumwa, walihepa kuhudhuria mkutano wa chama cha ODM mnamo Jumatatu uliosimamiwa na Bw Odinga mjini Mombasa.

Lakini Bi Jumwa alisema alikuwa amearifu chama mapema kwamba hakuwa nchini kwa hivyo hangehudhuria mkutano huo.

‘Mchungaji’ achoma nyumba mkewe kumtomzalia watoto wa kiume

Na MAGATI OBEBO

MWANAUME katika Kaunti ya Nyamira alichoma nyumba zake mbili kutokana na ghadhabu za kutozaliwa mtoto wa kiume na mkewe.

Alitenda ukatili huo baada ya kuchimba kaburi ili kumzika mkewe ndani na wasichana wake watatu alioapa kwamba lazima angewauwa.

Jamaa wa familia hiyo walisema Joshua Misati kwa jina la utani ‘mchungaji’ alikuwa ameishi na mkewe Rebbeca Kerubo kwa zaidi ya miaka 12 bila kujaaliwa mtoto wa kiume lakini hakuonekana kama aliyejawa na msongo wa mawazo kuhusu suala hilo.

Mkewe wa kwanza alimtoroka katika hali ya kutatanisha kufuatia ugomvi wa kila mara kuhusu kutojifungua mtoto wa kiume baada ya kujaaliwa wasichana tisa.

Hata hivyo, siku ya Jumanne usiku, mwanaume huyo kwa hasira alionekana kukosa subira na kumgeukia mkewe ambaye alifanikiwa kuponyoka kutoka mikonono mwake.

Hapo hapo alichukua kiberiti na kuchoma nyumba zake mbili, kisa kilichowashtua mno wanakijiji wa Bondeni eneo la Kebirigo, Nyamira.

Jamaa na wanafamilia walisema Bw Misati alianza ukatili wake wiki mbili zilizopita alipochimba kaburi hilo katika shamba la matunda na kuapa kuwazika mke na watoto wake wote humo.

Baadaye alilazimishwa kulifunika baada ya tambiko kufanywa na wazee ili kuwaepusha wanafamilia dhidi ya nuksi kutokana na kitendo cha Bw Misati.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’, mkewe Bw Misati Bi Rebecca Kerubo alisimulia jinsi mumewe alivyorejea nyumbani siku hiyo kama amelewa na kuzua ugomvi naye kuhusu kukosa kujifungua mtoto wa kike.

“Alifika akigombana kuhusu chakula kisha baadaye akaanza kuuliza kwa nini nimemzalia wasichana watatu na kukosa kumzalia wa kiume,” akasema Bi Kerubo katika hali ya huzuni.

Mambo yaliharibika siku hiyo saa nne usiku alipochukua upanga na kuwafungia ndani ya nyumba kwa nia ya kuwateketeza. Waliponea kwa tundu la sindano baada ya kufanikiwa kutoroka alipokuwa akijishughulisha kuwateketeza.

“Tuliweza kutoroka wakati alipoondoka kidogo akijitayarisha kutuchoma na aliporejea alichoma nyumba zote,” akasema Bi Kerubo.

Bw Misati tayari ametoroka na anaswaka na polisi.

wa Nyamira wakiazisha msako wa kumkamata.

Watalii 7,000 watarajiwa kunogesha biashara Lamu

NA KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya watalii 7000 wanatarajiwa kuzuru eneo la Lamu katika kipindi cha ziara nyingi za watalii kinachotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, anasema hatua hiyo inatokana na imani ambayo imerejeshwa kwa watalii hasa baada ya usalama kudhibitiwa kote Lamu.

Sekta ya Utalii ya Lamu imekuwa ikipokea changamoto tele hasa tangu Al-Shabaab walipovamia na kuua wakazi zaidi ya 100 kwenye miji ya Mpoeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi kati ya 2014 na 2015.

Akizungumza wakati wa kongamano la washikadau kwenye hoteli ya Majlis eneo la Shella Alhamisi, Bw Mwasambu aliwashauri wenye mahoteli kote Lamu kujiandaa vilivyo ili kupokea watalii wengi zaidi kutoka kutoka sehemu mbalimbali za nchi na ng’ambo punde Julai itakapoanza.

Mmiliki wa hoteli ya Bush Gardens, Ghalib Alwy akiwa na wafanyakazi wake hotelini wakiendeleza ukarabati wa hoteli hiyo. Asema anatumaini kunoga kwa biashara hiyo ifikapo Julai. Picha/ Kalume Kazungu

“Ningewashauri wenye hoteli kutengeneza mahoteli yao vizuri na hata kupanua hoteli hizo mapema ili kukimu idadi kubwa ya wageni tunaotarajia kupokea eneo hili kuanzia Julai. Tunatarajia zaidi ya watalii 7000 wa hapa nchini na ng’ambo kuzuru eneo hili msimu wa Julai hadi Disemba,” akasema Bw Mwasambu.

Baadhi ya wadau wa utalii waliohojiwa na Taifa Leo kwenye miji mbalimbali ya Lamu walieleza matumaini ya kunoga kwa biashara hiyo punde Julai itakapofika.

Wamiliki wa mahoteli kwenye miji ya Lamu, Ras Kitau, Shella, Manda, Mkokoni, Kiwayu, Matondoni, Kipungani na viungani mwake tayari wameanza kukarabati hoteli zao ilhali wengine wakizijenga upya ili kuvutia watalii wanaotarajiwa kuwa wengi msimu wa Julai.

Bw Ghalib ALwy ambaye anamiliki hoteli ya Bush Gardens mjini Lamu anasema wameanza kupokea kodi ya vyumba vya kulala kwa watalii kutoka ng’ambo mapema ikilinganishwa na miaka ya kawaida.

Alisema hiyo ni dalili tosha kwamba biashara ya utalii itanoga mwaka huu.

Asema wamezindua kampeni ya kusafisha fuo za bahari na hata kuelimisha umma wa Lamu kuepuka kutupa ovyo taka kwenye fuo. Picha/ Kalume Kazungu

“Tunasubiri kipindi cha Julai kufika. Tayari tumepokea kodi za mapema kwenye hoteli zetu kwa watalii wa ng’ambo ambao wanazuru Lamu ifikapo mwezi Julai. Tunaishukuru serikali ya kitaifa kwa juhudi zake kudhibiti usalama eneo hili la Lamu,” akasema Bw Alwy.

Naye mmiliki wa hoteli ya Sunsail, Bw Ali Bunu ambaye kwa sasa anaendeza upya ujenzi wa hoteli yake alisema kuna dalili njema ya sekta ya utalii kuimarika kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya awali.

Vijana wa Huduma za matembezi ya watalii ufuoni pia wameahidi kutoa huduma bora zaidi kwa watalii wanaozuru Lamu mwaka huu.

Wakiongozwa na Bw Salim Ali, walisema wanaendeleza mikakati kuhakikisha kuwa usafi wa fuo za bahari kote Lamu unadhibitiwa vilivyo.

“Tumejiandaa kukaribisha watalii ambao tayari wameanza kuja hapa Lamu kwa msimu wa mwezi Julai na Disemba. Tumezindua kampeni ya kusafisha fuo zetu za bahari na hata kuelimisha umma wa Lamu kuepuka kutupa ovyo taka kwenye fuo zetu. Watalii wote wanakaribishwa Lamu,” akasema Bw Ali.

Ni juma hili ambapo idara ya utalii ya Kaunti ya Lamu ilitangaza ongezeko la kiwango cha watalii wanaozuru Lamu kwa hadi asilimia 70.

Fedha za wanasiasa mnazotumia kujenga makanisa ni chafu, Keter aonya

Na LEONARD ONYANGO
MBUNGE wa Nandi Hills Alfred Keter sasa ametaka viongozi wa kidini kukoma kujenga makanisa kwa kutumia pesa ‘chafu’ kutoka kwa wanasiasa.

Kulingana na Bw Keter wanasiasa wanaojihusisha na biashara ya sukari ya magendo inayodaiwa kuwa na sumu, ndio wanaotoa michango makanisani kila wikendi bila kuishiwa na fedha.

“Ukiona mwanasiasa anaongoza mikutano zaidi ya minne ya harambee  kwa siku na kila harambee anatoa fedha zisizopungua Sh2 milioni, huyo mwanasiasa anatoa wapi fedha hizo?” akauliza Bw Keter katika mahojiano na runinga ya NTV, Alhamisi asubuhi.

“Napenda kuwakumbusha viongozi wa kidini kwamba fedha mnazotumia kujenga makanisa ni chafu. Inasikitisha kuwa mnajenga makanisa matakatifu kwa kutumia fedha chafu,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo aliwataka viongozi wa kidini kuwahoji wanasiasa hao wanapotoa fedha ili kuthibitisha ikiwa pesa zinazotolewa katika michango zilipatikana kwa njia halali auni za wizi.

Bw Keter alidai kuwa maafisa wafisadi serikalini wanaiba Sh2 bilioni kila wikendi ambazo wanatumia kutoa katika harambee

“Kila mwaka Sh400 bilioni hupotelea katika mifuko ya wafisadi. Ikiwa wezi hao watapumzika kuiba siku ya Jumamosi na Jumapili, kila Wikendi Kenya itaokoa Sh2 bilioni. Kwa mwaka tutaokoa Sh96 bilioni,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo machachari kutoka Bonde la Ufa amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kutimua mawaziri husika walioshindwa kuzuia uingizaji wa bidhaa ya magendo nchini.

“Rais Kenyatta asilegeze kamba kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi na uingizaji wa sukari ya magendo nchini. Kadhalika, namsihi rais kuwaachisha kazi baadhi ya mawaziri walioshindwa kuzuia uingizwaji wa bidhaa ghushi nchini,” akasema.

Bw Keter pia anataka maafisa wanaosimamia Shirika la Kuhakiki Ubora wa Bidhaa (Kebs), Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) na idara nyinginezo watimuliwe kwa kuzembea kutekeleza majukumu yao huku sukari ya magendo ikiingizwa nchini.

“Ili kuzuia siasa inayoendelea kuhusiana ikiwa sukari hiyo ya magendo ina sumu au la, waziri wa Usalama Fred Matiang’i ajitokeze aweke wazi ripoti kuhusiana na vipimo vilivyofanywa na kubaini kuwa sukari hiyo imechanganywa na madini ya mekyuri au la,” akasema Bw Keter.

Madai kuwa sukari ya magendo inayoendelea kunaswa katika maeneo mbalimbali imechanganywa na mekyuri, yaliyotolewa na Dkt Matiang’i, yamepuuziliwa mbali na mwenzake wa Viwanda Adan Mohamed na kuwaacha Wakenya katika njiapanda.

Mbunge wa Nandi alidai kuwa wafanyabiashara na wanasiasa wanaohusika na biashara ya sukari ya magendo wanawekeza fedha zao katika mataifa ya kigeni kama vile Dubai, Afrika Kusini, Zambia, Botswana kati ya mengineyo kwa kuhofiwa kukamatwa.

Kampeni ya kuwabamba wazee wanaooa wasichana matineja yaanza

NA KALUME KAZUNGU

IDARA ya usalama ya kaunti ya Lamu imezindua kampeni kabambe ya kuwasaka na kuwakamata wazee wanaowaoa wasichana wa umri mdogo eneo hilo.

Kampeni hiyo pia inalenga kuwanasa wahusika wa ubakaji, washukiwa wa ulawiti wa watoto na wazazi wanaoendeleza ndoa za mapema kwa wasichana wao badala ya kuwahimiza kuzingatia masomo.

Akizungumza na wanahabari ofisini mwake Jumanne, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alitaja kukithiri kwa visa hivyo hasa kwenye maeneo ya Hindi na Mokowe.

Bw Kioi alifichua kuwa zaidi ya watoto saba wamebakwa kwenye vijiji vya Hindi na Mokowe mwezi huu wa Juni pekee ilhali makumi ya wasichana wakiwa wameozwa na wazazi wao.

Alisema operesheni waliyozindua itaangazia sana maeneo hayo mawili.

Alisema inashangaza kwamba baadhi ya wazazi kwenye maeneo hayo wamekuwa mstari wa mbele kuficha ubakaji na ulawiti wa watoto wao badala ya kuripoti visa hivyo kwa polisi ili hatua mwafaka zichukuliwe dhidi ya wahalifu.

Badala yake, wazazi wamekuwa wakishirikiana kisiri na wabakaji, walawiti na hata wale wanaotunga mimba wasichana wa shule ili wasifikiwe na mkono wa sheria.

Kamanda huyo wa polisi alionya vikali wazazi wa namna hiyo kwamba wakipatikana pia watakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Alizitaka jamii za Lamu kuheshimu haki za watoto na kuwahimiza wakazi kusomesha wasichana wao ili kujinasua kutoka kwa umaskini uliokithiri.

“Kuna unajisi na ulawiti unaofanywa dhidi ya watoto wadogo hasa eneo la Hindi na Mokowe. Tayari tumerekodi visa zaidi ya saba vya watoto kubakwa na kulawitiwa eneo la Hindi. Wazazi kwenye maeneo hayo pia wamekuwa wakiendeleza itikadi ya kuwaoza mabinti zao wa umri mdogo kwa wazee.

Tumeanzisha kampeni inayolenga kuwakamata wazee wanaooa wasichana wa shule, wazazi wanaooza wasichana wao, wabakaji na wale wanaoendeleza ulawiti wa watoto kote Lamu. Kampeni yenyewe hasa tutaielekeza zaidi Hindi na Mokowe ambapo visa hivyo vimekithiri,” akasema Bw Kioi.

Aliomba mashirika yasiyo ya kiserikali na yale yanayohusika na masuala ya kijamii kuendeleza hamasa kwa wakazi hasa kwenye miji ambayo visa vya ndoa za mapema, ubakaji, ulawiti na mimba za mapema vimekithiri Lamu.

Mnamo Aprili mwaka huu, Shirika la World Vision eneo hilo lilifichua kuwa wasichana wapatao 25 tayri walikuwa wamenajisiwa na wazazi wao kwenye divisheni ya Hindi.

Shirika hilo pia liliorodhesha ndoa za mapema kuwa kizingiti kikuu katika kuendelezwa kwa elimu ya mtoto msichana eneo hilo

Outering Road iaongoza kwa idadi ya ajali barabarani – NTSA

Na BERNARDINE MUTANU

Idadi ya watu waliofariki barabarani kati ya Januari 1 na Juni 11, 2018 imefikia 1,348 kulingana na Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) Jumatano.

Eneo lililo na idadi kubwa ya waliofariki dunia katika ajali za barabarani ni Nairobi ambapo barabara ya Outering ina idadi kubwa zaidi .

Idadi kubwa zaidi ya waliofariki barabarani ni watu wanaotembea kwa miguu (515) wakilinganishwa na 497 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Idadi ya abiria waliofariki ni 297, wakilinganishwa na 335 katika kipindi hicho mwaka jana, ilisema NTSA, ilhali idadi ya madereva walioaga dunia ilikuwa ni 145 ikilinganishwa na 147 mwaka jana.

Walioaga dunia katika ajali za bodaboda walikuwa ni 115 wakilinganishwa na 118 mwaka wa 2017, ilisema NTSA.

Waendeshaji 25 wa baiskeli waliaga dunia katika kipindi hicho, ongezeko la asilimia 21 katika kipindi hicho mwaka jana.

Barabara ya Outering ilikuwa na asilimia ya juu zaidi ya vifo, ambapo watu 23 waliaga dunia ikilinganishwa na barabara zingine Nairobi, ilisema ripoti hiyo.

Jubilee Insurance kuwapa bima Wakenya wa pato la chini

Na BERNARDINE MUTANI

Kampuni ya bima ya Jubilee Jumatano ilizindua mpango wa bima kwa watu wa mapato ya chini zaidi nchini.

Kampuni hiyo inashirikiana na kampuni ya Bluewave Microfinance kutekeleza mradi huo.

Huduma hiyo, Imarisha Jamii itapatikana kwa njia ya simu na itafadhili bima ya maisha, ajali ya kibinafsi, ulemavu, na bima ya afya ili kusaidia wananchi wa mapato ya chini kuepuka baadhi ya changamoto maishani.

Watakaochukua huduma hiyo watalipa hata Sh20 kwa wiki na wataweza kunufaika kwa kupata pesa za kufadhili matibabu, mazishi na ulemavu hadi Sh100,000.

Pia wataweza kupokea Sh10,000 pesa za kusimamia matibabu wanapolazwa hospitalini siku tatu au zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa Jubilee Holdings Juliua Kipng’etich alisema huduma hiyo itafanya rahisi kulipa ada ya bima(premium) na upokeaji wa malipo kwa sababu inatumia simu.

Huduma hiyo inatarajiwa kugeuza sekta ya bima nchini kwa sababu inalenga mahitaji ya wateja, alisema Bw Kipng’etich.

Tenda za serikali sasa kushindaniwa na wananchi

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeanzisha mpango wa kuweka wazi tenda zake kwa wananchi.

Mpango huo utaweka wazi kandarasi zote na mikataba iliyotiwa sahihi na serikali. Hiyo itawezekana kupitia kwa wavuti maalum, alisema Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich Jumanne.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa wakati ambapo serikali ina miradi mingi ya muundo msingi, ambayo inatarajia kutekeleza kwa kushirikiana na sekta ya kibinafsi.

Habari zitazowekwa katika tovuti hiyo ni kuhusiana na utambulisho, utaratibu wa kutayarisha na uagizaji wa huduma na bidhaa, utiaji sahihi wa kandarasi, ujenzi na uzinduzi wa miradi hiyo.

Kwa sasa kuna miradi zaidi ya 70 ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali, umma na sekta ya kibinafsi(PPP).

Alisema hatua hiyo ni ya kuimarisha uwazi katika operesheni za serikali. Baadhi ya miradi ni kama ujenzi wa barabara na bandari.