Mhubiri agunduliwa mkulima wa bangi shambani mwake

KNA na PETER MBURU

Polisi mjini Naivasha wamepata bangi ambayo ina thamani ya Sh500, 000 ikienda kuuzwa na kutetekeza nyingine ya thamani ya mamilioni katika shamba la mhubiri mmoja.

Bangi iliyoharibiwa katika shamba la mhubiri huyo ilikuwa tayari kuvunwa.

Kutokana na operesheni hiyo, polisi waliweza kugundua mfumo wa wauzaji wa dawa za kulevya mjini Nakuru. Kiongozi wa kundi hilo anaaminika kuwa mhubiri wa dini la Akorino.

Akiongoza maafisa wa polisi kutoka kitengo cha Polisi wa Utawala (AP), Naibu Kamishna wa Naivasha Richard Oguoka alisema maafisa wa polisi walidokezewa kuhusu bangi hiyo na wananchi wa eneo hilo.

Wakazi hao walihoji kuwa mhubiri huyo alikuwa akipanda mmea huo katika shamba lake lililokuwa karibu na ufuo wa Ziwa Naivasha.

Akihutubia wanahabari baada ya uvamizi huo, Bw Oguoka alisema ufanisi huo uliimarisha kampeni dhidi ya matumizi ya mihadarati eneo hilo.

Aliongeza kuwa wakati wa uvamizi huo, mshukiwa alitoroka kwa kutumia boti. Alisema maafisa watafanya juu chini mpaka watakapohakikisha kuwa wamemkamata.

“Tumefahamishwa kuwa mhubiri huyo ametoka katika kanisa la Akorino na inakaa amekuwa akifanya biashara hiyo kwa muda mrefu hasa kutokana na habari tuliyopata leo,” alisema Oguoka.

Alisema operesheni hiyo itaendelezwa hadi maeneo mengine Naivasha ili kuhakikisha kuwa mji huo ni salama, kwa kusema kuwa wauzaji wa mihadarati wanatishia vizazi.

Naibu kamishna huyo alisema machifu wataendelea na operesheni hiyo kwa kuingia kila boma eneo hilo.

 

Trump atarajiwa kuzuru Kenya

Na PRAVINDOH NJUGUNATH

RAIS wa Amerika Donald Trump anatarajiwa kuzuru Kenya wiki ijayo katika ziara yake ya kwanza barani Afrika.

Trump anapaniwa kuzindua barabara Kuu ya Mombasa- Nairobi inayoendelea kupanuliwa kwa ufadhili kutoka serikali yake na ile ya Kenya.

Serikali ya Kenya imekaa kimya kuhusu ziara hiyo ya siku tatu ya Rais Trump kwa sababu ya usalama wa kiongozi huyo wa taifa lenye uwezo zaidi duniani.

Uchunguzi wa Taifa Jumapili umebainisha kuwa tayari maafisa wa Federal Bureau of Investigation (FBI) kutoka Amerika wamewasili nchini na wanaendelea kushirikiana na wenzao wa Kenya kulainisha usalama wa Trump.

“Tayari tumepokea zaidi ya maafisa 100 wa FBI na tumewatuma maeneo ambayo Trump atatembelea wakati wa ziara yake,” alisema Mkuu wa Polisi jijini Nairobi Seetanoh Lutchmeenaraidoh.

Bw Lutchmeenaraidoh hata hivyo, hangethibitisha iwapo maafisa hao wa FBI wamekuja kwa sababu ya ziara hio ya Trump, lakini alisema Kenya inatarajia ‘mgeni mashuhuri.’

Duru ziliambia Taifa Jumapili kuwa kutimuliwa kwa Balozi wa Amerika humu nchini Robert Godec kulikuwa sehemu ya kutayarisha ziara ya Trump,kwa kuleta balozi mwingine ‘anayekubalika’ na Wakenya wote.

Hivi majuzi, aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alifika nchini kwa kile kilionekana kama kuandaa ziara ya kiongozi huyo.

Barabara Kuu ya Mombasa- Nairobi imepanuliwa kwa gharama ya Sh380 bilioni na kiasi kikubwa cha fedha hizo kimefadhiliwa na serikali ya Trump.

 

‘Ni kibarua kigumu kumsaidia Miguna’

CHARLES WASONGA na JUSTUS OCHIENG’

MAWAKILI, watetezi wa haki za kibinadamu na baadhi ya wanasiasa wameelezea kutamaushwa kwao na msimamo mkali wa mwanaharakati wa upinzani Miguna Miguna ambao wanadai, unatatiza jitihada za kumsaidia dhidi ya ukandamizaji wa Serikali.

Japo Wakenya wengi wamejitokeza kumtetea Dkt Miguna, wakili huyo amejitokeza kama mkaidi na muasi hata kwa wale wanaoendelea kumsaidia kurejea nchini kama raia wa Kenya.

Licha ya kinara wa upinzani Raila Odinga na chama cha ODM kuweka juhudi za kumkomboa Dkt Miguna, jana wakili huyo anayeendelea kuzuiliwa nchini Dubai, alimkemea vikali Bw Odinga na kumshutumu kwa kushirikiana na wanaomkandamiza.

Katika uwanja wa ndege wa JKIA ambapo sarakasi zilianzia Jumatatu, Bw Odinga alijaribu kumshawishi Dkt Miguna ashirikiane na maafisa wa idara ya uhamiaji katika uwanja wa ndege wa JKIA ili aruhusiwe kuingia nchini lakini akakataa.

Bw Odinga alionekana akipiga simu kila mara kuashiria alikuwa akiwasiliana na viongozi wakuu serikalini, akiwemo, Rais Uhuru Kenyatta ili kumsaidia Miguna.

Jumamosi, chama cha ODM kilisema kimekuwa kikitoa huduma za mawakili kwa Dkt Miguna bila malipo kwa maagizo ya Bw Odinga.

“Tumeorodhesha juhudi zote ambazo kiongozi wa chama chetu zinazolenga kumsaidia Dkt Miguna. Mzee (Raila) amewaamuru mawakili wake wote, nikiwemo mimi kushughulikia kesi ya Miguna.

Mawakili hao, wakiongozwa na Orengo wamekuwa wakishughulikia kesi yake tangu Februari alipokamatwa,” akasema Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna.

Akaongeza: “Tumedhulumiwa na polisi na maafisa wa serikali kiasi cha paspoti zetu kutwaliwa. Mzee amekuwa akihudhuria vikao vya kesi hiyo mahakamani.

Na alikuwa katika uwanja wa ndege akihatarisha usalama akishughulikia kesi hiyo. Kwa hivyo, madai kwamba Mzee amemtelekeza Dkt Miguna hayana msingi.”

Jumamosi, Dkt Miguna alimsuta Bw Odinga kwa kumtelekeza na kutofanya lolote kumsaidia na kuendelea kushirikiana na “watu ambao walimwibia kura na kuwaua wafuasi wake baada ya uchaguzi wa mwaka jana”.

Lakini Bw Sifuna na wabunge; Opiyo Wandayi (Ugunja), Samuel Atandi (Alega Usonga) na Gideon Ochanda (Bondo) walimwonya Miguna dhidi ya kumshambulia Bw Odinga kuhusu masaibu yake.

 

Kumshambulia Raila

“Raila Odinga ni taasisi, hafai kushutumiwa. Yeye na Raila hawachezi katika ligi moja. Miguna anavuka mstari mwekundi sasa kwa kumshambulia Odinga,” akasema Wandayi ambaye pia ni Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika ODM.

Dkt Miguna ambaye aliwasili kutoka Canada Jumatatu alitakiwa kujaza fumo maalum ili apewe viza ya miezi sita lakini akakataa licha ya kudinda kuwasilisha paspoti yake ya Canada.

Licha ya wanahabari kujeruhiwa vibaya na maafisa wa polisi waliofika JKIA kufuatilia masaibu ya Dkt Miguna mapema wiki hii, wakili huyo aliwashambulia wanahabari vikali akidai wameshawishiwa na serikali ya Jubilee ili kupuuza habari kumhusu.

“Nimefanyiwa mahojiano na vituo vya BBC, VOA na Radio France International na hakuna mwanahabari wa Kenya amenihoji hata kupitia kwa simu..wanaendelea kuchapisha tu uwongo kunihusu,” alisema Dkt Miguna licha ya habari zake kupewa kipaumbele katika magezeti, runinga na redio za humu kwa kipindi cha wiki moja sasa.

Duru zinasema ubalozi wa Canada umekuwa na wakati mgumu kumsaidia Dkt Miguna kutokana na misimamo yako mikali.

Kwenye kanda za video zilizonaswa katika uwanja wa JKIA, ilidhihirika kuwa Dkt Miguna alijibizana vikali na mawakili wake. Anasikika akiwafokea walipopendekeza atie saini stakabadhi ambazo zingemruhusu kupewa viza ya kuingia nchini.

 

Kurarua stakabadhi

Alitwaa stakabadhi hizo na kuzirarua akidai maafisa wa idara ya uhamiaji walipaswa kumruhusu aingie nchini bila masharti yoyote.

Mmoja wa mawakili wa Miguna Bi Judy Soweto anakiri mteja wake ni “mtu mgumu’ nyakati nyingine.

“Ni kweli kwamba mara nyingi Miguna hujitokeza kama mtu asiyekubali kulegeza msimamo, ni mkakamavu na mkaidi lakini madai mengine anayowekelewa sio kweli,” akasema Bi Soweto.

Wakili huyo alisema hayo kujibu madai ya Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNHRC) Kagwiria Mbogori aliyemtaja Miguna kama mkaidi aliyedinda kushirikiana na maafisa wa serikali waliotaka kumsaidia.

“Nimetamaushwa na Miguna kwa sababu agizo la mahakama lilimruhusu kutumia paspoti yake ya Canada kuingia humu nchini. Lakini alikataa katakata kuwasilisha stakabadhi hizo za usafiri kusudi aruhusiwe kuingia nchini,” akasema Bi Mbogori.

Wakili Miguna pia alikana watu wa familia yake, wakiongozwa na kakake Eric Ondiek, waliotoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati kumnusuru. Alisema msemaji wake ni “mke wangu anayeishi Canada na sitambui mtu mwingine.”

Joho amtembelea Miguna hospitalini Dubai

WINNIE ATIENO na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Mombasa Ali Hassan Joho Alhamisi alimtembelea mwanaharakati wa NASA Dkt Miguna Miguna ambaye anapokea matibabu katika hospitali moja nchini Dubai. 

Msemaji wa Joho Richard Chacha alisema gavana huyo alimtembelea Dkt Miguna kumjulia hali na kumtia moyo.

“Mheshimiwa Joho yuko nchini Dubai. Atamtembelea Dkt Miguna ambaye amelazwa katika hospitali moja katika uwanja wa ndege wa Dubai. Tutawatumia picha na maelezo zaidi,” Bw Chacha akasema kwa njia ya simu.

Gavana Joho amekuwa katika ziara rasmi ya wiki moja katika eneo la Estonia, Dubai.

Ni kama drama! Miguna akumbana na masaibu zaidi wakati wa Pasaka

Na BENSON MATHEKA

SAKATA ya wakili Miguna Miguna imegeuka kuwa mchezo wa sarakasi ila mchezo wenyewe unahusu masuala mazito ya haki za binadamu na utawala wa kisheria.

Sarakasi hii, ambayo imekuwa ikiendelea filamu ya awamu, maarufu kama series, Alhamisi ilibadilisha mahala pa kuigizia kutoka uwanja wa ndege wa JKIA hadi mjini Dubai, katika msimu huu wa sherehe za Pasaka.

Hii ni baada ya mhusika mkuu, Bw Miguna, kuhamishwa usiku wa manane kutoka chooni ambako alikuwa amezuiliwa kwa takriban saa 48.

Mnamo Jumatano usiku, Bw Miguna alichukuliwa kwa nguvu kutoka chooni uwanjani JKIA, na alipoamka jana alfajiri akagundua hakuwa Nairobi, mbali Dubai katika Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE).

“Nilikuwa nimemuacha ndani ya choo kwenda kumnununua chakula cha jioni kwa sababu hakuwa amekula kwa muda. Niporudi nilipata ameondolewa,” alieleza afisa wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNHCR), Kamanda Mucheke kwenye ujumbe wa Facebook ambao aliambatanisha na picha zake akiwa na Bw Miguna kwenye choo hicho.

Katika picha nyingine ameshika chakula na kikombe cha chai alizonuia kumpelekea Bw Miguna.

 

Azuiwa kuingia chooni

Bw Mucheke alisema dakika chache baada ya kuondoka Bw Miguna alimpigia simu kumtaka arudi haraka akisema alikuwa kwenye hatari. “Wakati niliporudi, polisi walinizuia kuingia katika choo hicho,” akaeleza Bw Mucheke.

Bw Miguna alikuwa amezuiliwa peke yake katika choo hicho tangu Jumatatu jaribio la kumtimua nchini lilipotibuka alipozua kizaazaa na kushuka ndege ya kwenda Dubai aliyoagizwa kuabiri.

Iliibuka kuwa huenda Bw Miguna alileweshwa dawa hadi akapoteza fahamu kabla ya kubururwa hadi ndege ambayo ilicheleweshwa kwa dakika 28 ikimsubiri.

Mawakili wake Nelson Havi, James Orengo na Julie Soweto walithibitisha kuwa Miguna aliondolewa Kenya wakidai alikuwa ameleweshwa.

Mbunge wa Gatundu aliweka picha kwenye mitandao ya kijamii kuthibitisha wakili huyo alikuwa ndani ya ndege EK722 ya kampuni ya Emirate kuelekea Dubai.

Alhamisi asubuhi, Bw Kuria aliweka video zilizoonyesha Miguna akibishana na maafisa wa usalama katika uwanja wa ndege jijini Dubai.

“Niligutuka nikiwa Dubai na wadhalimu hawa wanasisitiza ni lazima niendelee na safari hadi London. Mimi ni mgonjwa, ninahitaji matibabu. Kuna mmoja anayeitwa Njihia anayenitisha. Ninahitaji msaada haraka. Ninataka kurudi Nairobi. Sitaki kwenda kwingine,” Bw Miguna alieleza kwenye twitter.

 

‘Siogopi kifo’

Kwenye moja ya kanda ambazo Bw Kuria alituma, Bw Miguna anasikika akimwambia mtu aliyevalia sare za wahudumu wa ndege wa kampuni ya Emirates kwamba haogopi kufa na anafahamu sheria za viwanja na uchukuzi wa ndege. “Ukitaka kuniua, fanya hivyo, siogopi kufa, siwezi kutembea,” alisema.

Afisa huyo anasikika akimwambia Bw Miguna kwamba yuko tayari kumtafutia kiti cha magurudumu lakini anakataa.

Kwenye taarifa aliyotuma akiwa Dubai baada ya kusaidiwa na maafisa wa ubalozi wa Canada nchini humo kupata matibabu, Bw Miguna alidai kwamba alivamiwa na zaidi ya maafisa 50 akiwa chooni JKIA.

“Hawakujitambulisha, walinipiga mieleka, wakanifinyilia chini, wakanikalia na wanne miongoni mwao waliweka vitu kwenye mapua yanguhadi nikapoteza fahamu,” alieleza Miguna.

Serikali ya Kenya inasisitiza kuwa Bw Miguna sio raia wa Kenya na anafaa kutoa paspoti ya Canada aliyotumia kusafiri, huku naye akisisitiza arudishiwe paspoti ya Kenya ilivyoagiza mahakama.

Paspoti yake ilitwaliwa na kuharibiwa na serikali alipokamatwa Februari na kutimuliwa Kenya.

Bw Miguna alisema madaktari walithibitisha kwamba alileweshwa na akasema alitarajia kurudi Kenya jana au leo.

 

Jombi atisha kutimua mke kwa kukataa kuamini ushirikina

Na LEAH MAKENA

GATUNGA, THARAKA

POLO wa hapa alitisha kumfurusha mkewe akimlaumu kwa kuchochea wanawe kutokubali dawa ya mganga ya kuwakinga kutokana na hatari.

Inasemekana kuwa polo alijulikana kwa kuamini ganga ganga za waganga na alikuwa na mazoea ya kuwaita kuwashughulikia watoto wake wakifuzu masomoni ili awape dawa ya kuwazuia na maovu wakielekea mjini kutafuta ajira.

Duru zasema kuwa awali mkewe alikuwa akishirikiana na mzee japo shingo upande ila akabadilika alipojiunga na dhehebu lililomtaka kuacha ushirikina.

Hivi majuzi, jamaa alimuita mganga kuwapa chanjo wanawe waliokuwa wakielekea mijini kutafuta kazi. Penyenye zasema jamaa alimlipa mganga huyo mbuzi watatu na akachinja wa nne kabla ya kuanza kazi yake.

Hapo ndipo mzee alijipata pekee yake kwani wanawe waliokuwa wamekomaa walidinda baada ya kushauriwa na mama yao kutojihusisha na shughuli za ushirikina.

“Wanawe walikataa katakata mipango ya baba yao huku mama yao akiwaunga mkono,” alieleza mdokezi.

Jamaa hakufanikiwa kumshawishi mkewe kukubali vidosho wake wawili wahudumiwe na mganga.

“Alimwambia kwamba alikuwa ameokoka na kamwe hangerudi kwenye shughuli za ushirikina. Wakati huo wote wanawe walikuwa wamejifungia ndani ya nyumba,” alisema mdokezi.

Baada ya vuta nikuvute kati ya jamaa na familia mganga aliamua kuondoka na zawadi zake huku akiahidi kurejea baada ya familia kuelewana.

Penyenye zasema kuwa polo alianza kumkemea mkewe huku akitisha kumtema akisema alimfanya kupata hasara kubwa.

Hatima ya mzozo huo haikujulikana japo mke na wana wa polo walishikilia msimamo wao huku jamaa akiapa kumtimua mkewe iwapo hatalegeza kamba.

…WAZO BONZO…

 

 

Iweje Kenya impeleke Miguna Dubai akateseke kama yatima? auliza Makau Mutua

Mfanyabiashara maarufu Jimi Wanjigi (kushoto), wakili Prof Makau Mutua, Bw Raila Odinga na watu wengine wakiwa katika kesi ya Miguna Miguna Machi 29, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI mwenye tajriba ya juu anayeishi Marekani Profesa Makau Mutua, kinara wa Nasa Raila Odinga na mamia ya mawakili walihudhuria kesi ya kuadhibiwa kwa waziri wa usalama Fred Matiang’i, mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji meja mstaafu Gordon Kihalangwa na Mkuu wa Polisi  Joseph Boinnet kwa kumfurusha wakili mbishi Miguna Miguna na Jaji George Odunga Alhamisi.

Prof Makau alisema ni ukiukaji mbaya wa haki za binadamu kwa raia kusafirishwa kutoka nchi yake na “kupelekwa nchi ya ng’ambo kuteseka kama yatima.”

Wakili James Orengo anayemwakilisha Miguna aliomba Jaji Odunga akiomba korti iwasukume jela Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet miaka mitatu jela alisema , “nchi ya Canada iko afadhali mara mia kuliko Kenya kwamba sababu inamtunza Miguna ilhali nchi ya Kenya inamtesa.”

Bw Orengo alimrai Jaji Odunga akisema , “Jamaa hawa Boinnet, Kihalangwa na Matiang’i wanapasa kuanza kuenda gereza kuu la Kamiti huko watapewa makao bora sio choo kama vile walimweka wakili wa kimataifa mwenye tajriba ya juu Dkt Miguna.”

Bw Orengo alisema wakuu hao watatu wanaidharau mahakama sana na “korti yapasa kujitetea dhidi ya wakaidi kama hawa.”

Bw Orengo alisema ni jambo la kusikitisha sana kwa maafisa wa usalama kumdunga dawa apoteze ufahamu na kumsafirisha Dkt Miguna.

Bw Odinga hakukaa sana kortini na wala hakuhutubia wanahabari.

Orengo ataka Miguna aundiwe pasi maalum ya usafiri apelekewe Dubai

Wakili na Seneta wa Siaya James Orengo. Picha/ Maktaba

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu iliaombwa Alhamisi iamuru Idara ya Uhamiaji itengeneze pasi ya kusafiria ya wakili Miguna Miguna apelekewe Dubai na mawakili Nelson Havi na Aulo Soweto.

Wakili James Orengo ambaye ni mmoja wa mawakili 14 wanaomtetea Miguna aliyedungwa dawa ya kumfanya apoteze fahamu aliambia mahakama sheria inamruhusu mkurugenzi wa idara ya uhamiaji kumtayarishia  mlalamishi cheti maalum cha kusafiria.

“Naomba hii mahakama imwamuru mkurugenzi wa idara ya uhamiaji Bw Gordon Kihalangwa amtengenezee Miguna pasi ya kusafiria kama alivyoamriwa apelekewe Dubai na mawakili Havi na Soweto,” Jaji George Odunga aliombwa na Seneta Orengo.

Jaji Odunga alimweleza wakili huyo mwenye tajriba ya juu kwamba Jaji Enoch Mwita aliamuru Bw Kihalangwa amtayarishie pasi maalum ya kusafiria kutoka Canada.

Pasi ya Kenya aliyokuwa amepewa Miguna ilitwaliwa na Serikali na kufutiliwa mbali.

Wakili Mutinda aponea kusukumwa jela kwa kuwa ‘mwongo’

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI wa Serikali Charles Mutinda yuko na bahati kama mtende kwa vile aliponyoka kusukumwa jela kwa madai hakuwaarifu Waziri wa Usalama Fred Matiang’I, Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Meja mstaafu Gordon Kihalangwa wamfikishe wakili mbishi Miguna Miguna makamani Alhamisi.

Mawakili Cliff Ombeta, John Khaminwa , Harun Ndubi na James Orengo waliomba Jaji George Odunga amsukume Mutinda jela kwa kukaidi agizo la korti kwa “kutowakabidhi agizo la korti wafike kortini wakiandamana na Dkt Miguna.”

“Huyu wakili wa Serikali anadanganya. Ni mdanganyifu. Alikaidi agizo la hii korti kwamba Miguna afikishwe kortini leo,” alisema Khaminwa.

Dkt Khaminwa alisema Mutinda hakuchukulia suala hilo kwa makini ndipo washtakiwa hawakufika kortini. “Naomba uamuru Mutinda asiwahi kuhudumu kama wakili na kwamba asithubutu kufika mbele ya mahakama yoyote kwa vile amekaidi sheria kama wakuu hao wa serikali waliokwepa mahakama.”

Bw Ombeta alisema Mutinda ni “mwongo na hata hafai kusimama kortini bali anatakiwa kufukuzwa aende nyumbani.”

Ombeta alishangaa jinsi Bw Mutinda hakuwaona Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet ilhali waliapa afidaviti aliyotumia kukata rufaa na kesi nyingine ya kuomba maagizo ya Jaji Roselyn Aburili yatupiliwe mbali. “Huyu wakili Mutinda ni mdanganyifu.”

Bw Orengo alisema Bw Mutinda anapasa kupewa adhabu moja na Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa kwa vile wote wamekaidi agizo la hii mahakama.

“Je, Matiang’i na wenzake wako wapi. Uliwaambia wanatakiwa kufika hapa kortini?” Jaji Odunga alimwuliza.

“Sikuwafikia kwa simu. Nilipiga simu mara 16 na sikujibiwa,” alisema Mutinda.

Bw Mutinda alijililia na kuomba korti isiamuru akome kutoa huduma za uwakili katika afisi ya mwanasheria mkuu ama kama wakili wa kibinafsi.

“Naomba hii mahakama iwachukulie hatua Matang’i, Kihalangwa na Boinnet. Nihurumie. Mimi ni wakili tu na kamwe sijakaidi agizo ka mahakama,” alijitetea Murinda.

Kiburi cha Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa kimeiletea Kenya aibu kuu – Jaji Odunga

Na RICHARD MUNGUTI

KINYUME  na matarajio ya kila mmoja Jaji George Odunga Alhamisi alikataa kuwatimua kazini Waziri Fred Matiang’I , Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Meja Mstaafu Gordon Kihalangwa na badala yake kuagiza walipe faini ya Sh200,000.

Lakini watatu hawa hawapasi kufurahi kwani Jaji Odunga alisema yeyote atakaye kufuatilia suala hilo yuko huru kwani watatu hao wamekaidi vifungu nambari 10 na 6 vya Katiba vinavyowataka watumishi katika nyadhifa za umma waletee sifa na heshima taifa kwa kutii na kutekeleza sheria na maagizo ya mahakama.

“Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet wameiletea nchi hii fedheha na aibu kwa kumsafirisha wakili Dkt Miguna Miguna kinyume cha maagizo ya hii mahakama akubaliwe kuingia nchini pasi masharti yoyote,” alisema Jaji Odunga.

Alisema idara ya uhamiaji ilikaidi agizo imkabidhi Dkt Miguna pasi ya kusafiria chini ya  uangalizi wa tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu.

Jaji huyo alisema maafisa hao wakuu serikalini badala ya kutekeleza maagizo ya korti walimfurusha  Dkt Miguna baada ya kumdunga dawa akapoteza fahamu kisha wakamwingiza kwa ndege na kumsafirisha hadi Dubai.

Jaji Odunga alisema watatu hao walikaidi maagizo ya korti kwa madharau na kiburi kikuu.

Jaji alikataa kuamuru washikwe watumikie kifungo cha miaka mitatu kila mmoja akisema , “Ikiwa watatu hawa walionyesha kiburi kikuu jinsi hii na kukataa sio mara moja bali mara nne kutii maagizo ya korti , ni afisa mgani anayehudumu chini yao atathubutu kuwakamata na kuwasukuma jela kuanza kutumikia kifungo.

Hakuna. Hivyo hii mahakama haiwezi kutoa maagizo ambayo hayatatekelezwa. Sasa kila mmoja atalipa faini kutoka kwa mshahara wake ya Sh200,000.”

Agizo hilo litapelekwa kwa afisi ya rais na naibu wa msajili wa mahakama kuu. Pesa hizo zitawasilishwa kortini.

Kambi za polisi zajengwa katika maeneo yanayolengwa na Al-Shabaab

NA KALUME KAZUNGU

KAMBI za polisi zimebuniwa kwenye maeneo yote hatari ambayo awali yalikuwa yakishuhudia uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa kundi la Al-Shabaab kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alisema serikali tayari imeweka kambi za polisi kwenye maeneo ya Milihoi, Nyongoro na Lango la Simba ambako visa vya Al-Shabaab kushambulia msafara wa mabasi ya usafiri wa umma na magari ya walinda usalama vilikuwa vimekithiri.

Bw Kioi kadhalika alisema serikali imeongeza doria za kutosha za polisi na jeshi kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen ili kuzuia mashambulizi yoyote kutoka kwa Al-Shabaab.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Picha/ Kalume Kazungu

Aliwataka wasafiri wanaotumia barabara hiyo kuondoa shaka na kusema kuwa usalama wao umedhibitiwa vilivyo.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Al-shabaab wamekuwa wakilenga mabasi ya usafiri wa umma na magari ya polisi na kuyashambulia kwa risasi na mabomu ya kutegwa ardhini.

Watu zaidi ya 30 walipoteza maisha yao kwenye maeneo ya Nyongoro, Milihoi na Lango la Simba baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kushambuliwa na Al-Shabaab.

Maafisa wa usalama wakishika doria karibu na msitu wa Boni uliokaribiana na barabara ya Lamu-Garsen. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kioi aidha alisema tangu kambi hizo za polisi kubuniwa, visa vya mashambulizi ya Al-Shabaab havijashuhudiwa tena kwenye maeneo husika.

“Tumeweka kambi za polisi kwenye sehemu za Milihoi, Nyongoro na Lango la Simba. Hizo ni sehemu hatari ambazo zilikuwa zikitumiwa na Al-Shabaab kutekeleza mashambulizi dhidi ya magari ya usafiri wa umma, yale ya kibinafsi na pia yale ya walinda usalama.

Ningewasihi wanaotumia barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen kuondoa shaka kwani usalama umedhibitiwa vilivyo,” akasema Bw Kioi.

Kamanda huyo aidha aliwasihi wasafiri kwenye barabara hiyo kutii amri ya walinda usalama na kukubali kukaguliwa kila wakati wanapofikia vizuiozi vya polisi.

Kamanda Muchangi Kioi akiandamana na maafisa wengine wa usalama kutekeleza doria kwenye msitu wa Boni na karibu na barabara ya Lamu-Garsen. Picha/ Kalume Kazungu

Kamanda Muchangi Kioi akiandamana na maafisa wengine wa usalama kutekeleza doria kwenye msitu wa Boni na karibu na barabara ya Lamu-Garsen

Kadhalika aliwataka madereva kutii amri ya kusafiri kwa mpangilio katika msafara mmoja unaosindikizwa na maafisa wa polisi.

“Kuna baadhi ya wasafiri ambao wamekuwa wakikashifu vizuizi vya polisi barabarani. Wengine wanakataa kupekuliwa. Kuna haja ya wasafiri kutii amri hiyo kwa manufaa yao,” akasema Bw Kioi.

MCK yataka visa vya wanahabari kuvamiwa vichunguzwe

Na BENSON MATHEKA

OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) inafaa kuchunguza visa vya kushambulia wanahabari wakiwa kazini na kuharibu vyombo vyao, Baraza la Wanahabari Kenya (MCK) limesema.

Baraza hilo liliungana na Chama  cha Wanasheria nchini (LSK) na Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNHRC) kushutumu kisa cha Jumatatu usiku ambapo polisi waliwashambulia wanahabari waliokuwa wakinasa na kupeperusha habari za kuwasili nchini kwa wakili Miguna Miguna.

“KNHRC, LSK na MCK tunachukulia vitendo vya hivi majuzi vya polisi kama unyanyasaji wa wanahabari wakiwa kazini.Tunataka kufahamisha serikali na hasa polisi kwamba wanahabari hao wana vibali rasmi na wanaongozwa na mwongozo wa maadili ya uanahabari unaotekelezwa na Baraza la Wanahabari la Kenya,” ilisema taarifa ya pamoja ya mashirika hayo.

Mwanahabari wa runinga ya Citizen  Stephen Letoo, Robert Gichira wa runinga ya  NTV na  Sofia Wanuna wa KTN walinyanyaswa na kupigwa na maafisa wa polisi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Stephen Letoo na Gichira walijeruhiwa  na vyombo vyao kuharibiwa.

KNHRC, LSK na MCK tunasema kuwa vinatambua mazingira magumu ambayo wanahabari wanahudumu katika juhudi za kukusanya habari.

“KNCHR, LSK na MCK tunalaani vikali kunyanyaswa kwa wanahabari na kuchukulia kisa hiki kama tisho kwa usalama wao,” ilisema taarifa yao.

“Tuna imani kwamba Mamlaka Huru ya kuchunguza utendakazi wa polisi (Ipoa) itachunguza kwa kina kisa cha kushambulia wanahabari na watakaopatikana kuwa walivunja sheria watachukuliwa hatua.

Pia, tunaomba DPP na ofisi ya kupokea malalamishi ya umma kuchunguza kisa hiki na kuwachukulia hatua waliohusika,” taarifa hiyo ilisema.

Ni aibu kwa serikali kumnyanyasa raia aliyezaliwa Kenya – Mashirika

Na BENSON MATHEKA
MASHIRIKA ya kutetea haki za binadamu humu nchini na ya kimataifa,  yameshutumu serikali ya Kenya kwa kumnyanyasa wakili Miguna Miguna na kumnyima haki yake ya uraia wa kuzaliwa.

Serikali ilimzuia Miguna kuingia Kenya tangu Jumatatu hadi Jumatano ilipomfurusha nchini kwa nguvu kwa mara ya pili hadi Dubai ikidai hakuwa na paspoti.

Juhudi za kumtaka kuomba uraia wa Kenya ziligonga mwamba alipotaka arejeshewe paspoti yake ya Kenya iliyotwaliwa na serikali na kuharibiwa alipokamatwa na kufurushwa Kenya mara ya kwanza Februari.

Alhamisi, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNHRC) na shirika la Human Right Watch yalisema kwenye taarifa tofauti kwamba Bw Miguna anafaa kuruhusiwa kuingia na kuishi Kenya.

Mwenyekiti wa KNHRC, Kagwiria Mbogori alisema Bw Miguna hawezi kupokonywa uraia wake wa Kenya kwa sababu ni wa kuzaliwa. “Bw Miguna ana haki ya kupatiwa paspoti ya Kenya.

Serikali inafaa kufuata ibara ya 16 ya katiba ambayo inafafanua wazi kuwa mtu hawezi kupokonywa uraia wa kuzaliwa,”alisema Bi Mbogori.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Bi Mbogori alilaumu maafisa wa idara ya uhamiaji kwa kumhangaisha Bw Miguna kwa kumzuia kuingia Kenya mahakama ilivyoagiza.

“Bw Miguna hakunyanyaswa alipotoka kwa ndege na kupitia eneo la abiria isipokuwa alipofika kwa maafisa wa uhamiaji ubishi ulipoanza. Bw Miguna aliwataka wampe paspoti yake ili wapige muhuri,” alisema.

Bi Mbogori alisema kulingana na katiba ya Kenya, raia kwa kuzaliwa hawezi kupoteza uraia wake akipata uraia wa nchi nyingine na kwamba akipata uraia wa nchi nyingine, anabaki kuwa raia wa Kenya.

Kulingana KNHRC, mtu hawezi kupokonywa uraia bila kupatiwa nafasi ya kujitetea ikiwa ni pamoja na kutafuta haki mahakamani.

“Kabla ya mtu kupokonywa uraia anafaa kufahamishwa sababu za na kupatiwa nafasi ya kujibu ikiwa ni pamoja na haki ya kujitetea mahakamani,” alisema Bi Mbogori.

Aidha, alisema haki ya uraia imelindwa na sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu na kwamba hakuna mtu anayefaa kupokonywa uraia kiholela.

KNHRC ilifuatilia hatua za kurejea nchini kwa Miguna ilivyoagizwa na mahakama. Tume ilikuwa imewasiliana na idara za serikali zinazohusika na kuhakikishiwa kuwa Bw Miguna angeruhusiwa kurejea nchini jambo ambalo halikutendeka.

Kwenye taarifa, Human Rights Watch lilisema kwamba  Bw  Miguna Miguna anafaa kuruhusiwa kuingia na kutoka Kenya bila kutatizwa.

“Chini ya katiba ya Kenya iliyopitishwa  2010,  Kenya  haiwezi kumpokonya yeyote aliyepata uraia kwa kuzaliwa nchini humo,” HRW lilisema kwenye taarifa.

LSK yakerwa na mazoea ya maafisa wa serikali kudharau sheria

Na BENSON MATHEKA
CHAMA cha Wanasheria Kenya (LSK), Alhamisi kilisikitishwa na hatua ya maafisa wa  serikali ya kudharau na kupuuza maagizo ya mahakama na kushambuliwa kwa mawakili wakitekeleza kazi yao.

Chama hicho kimesema kwamba katiba inasisitiza kuwa mahakama zinapatiwa mamlaka na raia sawa na serikali kuu na bunge na maagizo ya majaji yanafaa kuheshimiwa.

Naibu Mwenyekiti wa LSK, Bi Harieti Chiggai alisema maafisa wa serikali wanafaa kuheshimu maagizo ya mahakama wanavyoheshimu sheria zinazotungwa na kupitishwa na bunge kama njia ya pekee ya kuimarisha utawala wa sheria.

“Idara zote zilizobuniwa chini ya katiba, ni lazima ziheshimu katiba na sio moja kuhujumu nyingine,” alisema Bi Chiggai akisoma taarifa ya pamoja ya chama hicho, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu na Baraza la Wanahabari kuhusu kuhangaishwa kwa wakili Miguna Miguna.

Maafisa wa serikali walikataa kutii maagizo zaidi ya 10 ambayo mahakama ilitoa kuhusiana na masaibu ya Bw Miguna tangu wakili huyo alipokamatwa kwa kumuapisha kinara wa NASA Raila Odinga kuwa “rais wa wananchi.”

“Hakuna mtu au shirika lolote, iwe katika serikali au shirika la kibinafsi ana uhuru wa kuchagua maagizo anayopaswa kuheshimu. Na ikiwa serikali haikubaliani na agizo lolote, kuna utaratibu wa kutaka lisimamishwe au kukata rufaa. Tunaomba serikali kuonyesha mfano mwema wa kufuata utawala wa sheria na kwa kuheshimu katiba,” alisema.

LSK inamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuonyesha kujitolea kwake kuunganisha nchi alipoahidi kwenye mwafaka wake na kiongozi wa NASA Raila Odinga kwa kuagiza Bw Miguna kurudi Kenya.

“Tunaiomba serikali kushughulikia kwa haraka hali ya Bw Miguna kwa utaalamu wa hali ya juu na kuepuka aibu ambayo tunashuhudia,” alisema.

Chama hicho kinaitaka serikali kutowazuia mawakili kufanya kazi yao. Mnamo Jumatano usiku mawakili James Orengo, Nelson Havi na Julie Soweto walizuiwa na polisi kuwakabadhi maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), agizo la kuwataka wasimfurushe Bw Miguna.

“Tunaomba serikali kuwaruhusu mawakili kutekeleza majukumu yao halali bila kuwekewa vizingiti,” alisema Bi Chiggai.

Gor yakanusha kutowalipa wachezaji licha ya kutatizika kifedha

Na GEOFFREY ANENE

AFISA mmoja wa Gor Mahia amekiri kwamba mabingwa hao mara 16 wa Kenya wanakumbwa na matatizo ya kifedha.

Hata hivyo, Ronald Ngala, ambaye ni naibu wa katibu wa klabu hii, amepuulizia mbali ripoti kwamba Gor haijalipa wachezaji wake.

Amenukuliwa na tovuti ya klabu hiyo akisema, “Ni uongo mtupu (kwamba hatujalipa wachezaji). Tumewalipa na ripoti zinazoenea kwamba hatujalipa wachezaji wetu ni za kupotosha. Timu zote (nchini Kenya) zinapitia ugumu huu wa kifedha, si Gor Mahia pekee yake….”

“Tumewahi kuwa katika hali hii na tukafaulu kujikwamua kwa hivyo naamini tutafaulu tena,” aliongeza.

Gor Mahia, ambayo itapiga mechi yake ya saba ya Ligi Kuu itakapoalika Vihiga United mjini Kisumu hapo Jumapili, inashiriki mashindano ya Afrika ya Confederations Cup.

Itakuwa mwenyeji wa SuperSport United hapo Aprili 6 kabla ya kuelekea nchini Afrika Kusini kwa mechi ya marudiano mnamo Aprili 17.

Jeraha lapona, Cherop sasa kushiriki mbio za Rome Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa Boston Marathon mwaka 2012, Sharon Cherop ameingia mbio za Rome Marathon nchini Italia mnamo Aprili 8, 2018.

Cherop, 34, ambaye amekuwa akisumbuliwa na jeraha la goti, ni miongoni mwa wakimbiaji 14, 100 waliothibitisha kushiriki katika makala haya ya 34. Aliambia shirika la habari la Xinhua kwamba yuko tayari kufufua taaluma yake mjini Rome.

“Nahisi niko katika hali nzuri baada ya kupitia wakati mgumu kwa muda. Hata hivyo, nafahamu haitakuwa rahisi kushindana na majina makubwa,” alisema Machi 28.

Cherop, ambaye muda wake bora katika mbio hizi za kilomita 42 ni saa 2:22:28 kutoka Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2013, atakabiliana na bingwa wa mwaka 2016 na 2017 Muethiopia Rahma Tusa (2:25:12).

Wakenya wengine wanaopigiwa upatu kufanya vyema mjini Rome ni Angela Tanui (2:26:31) na Jafred Chirchir Kipchumba (2:05:48).

Mwaka 2017, Ethiopia ilifagia mataji ya wanaume na wanawake kupitia Shura Kitata na Tusa, mtawalia.

Amos Kipruto na Helena Kirop wanasalia Wakenya wa mwisho kushinda mataji ya Rome Marathon walipotawazwa mabingwa mwaka 2016 na 2013, mtawalia.

Mathare kuchupa juu ya Gor wakiilima Chemelil Sugar

Na GEOFFREY ANENE

MATHARE United na Chemelil Sugar zitavaana Ijumaa, huku Ligi Kuu ya Soka ya Kenya ikiendelea baada ya kipindi cha siku 11 cha mechi za timu za taifa kukamilika.

Mabingwa wa mwaka 2008 Mathare, ambao wanashikilia nafasi ya nne, wana fursa murwa ya kujitosa juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 18, wakipiga nambari saba Chemelil.

Mathare ya kocha Francis Kimanzi imezoa alama 14 kutoka mechi saba. Itaruka viongozi Gor Mahia, ambao wamevuna alama 16 kutoka mechi sita, nambari mbili AFC Leopards, ambayo pia imekusanya alama 16, lakini kutoka mechi saba, na nambari tatu Bandari, ambayo imevuna alama 14 kutoka mechi saba.

Wanasukari wa Chemelil watarukia nafasi ya nne na kusukuma Mathare, mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka, na Kariobangi Sharks nafasi moja chini kila mmoja wakilemea Mathare.

Hata hivyo, matokeo ya mechi kati ya klabu hizi inaonyesha kuna asilimia kubwa itaishia sare. Mechi 10 kati ya 12 zao za mwisho zimemalizika sare kwenye ligi.

Msimu uliopita, klabu hizi ziligawana pointi katika sare ya 0-0 Mathare ilipokuwa nyumbani Aprili 26 kabla ya kupiga sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano Oktoba 1.

Mara ya mwisho Chemelil ilizaba Mathare ilikuwa 2-1 Agosti 16 mwaka 2014. Mathare ililipiza kisasi 1-0 Februari 21, 2016.

Kutokana na takwimu hizi ni wazi kwamba nambari nne Mathare na nambari saba Chemelil inatarajiwa kuwa ngumu.

Ratiba:

Machi 30

Mathare United vs. Chemelil Sugar (3pm, Machakos)

Machi 31

Posta Rangers vs. Thika United (2pm, Camp Toyoyo)

Kariobangi Sharks vs. Ulinzi Stars (4.15pm, Camp Toyoyo)

Kakamega Homeboyz vs. Bandari (3pm, Bukhungu)

Gor Mahia vs. Vihiga United (3pm, Kisumu)

Nzoia Sugar vs. SoNy Sugar (3pm, Sudi)

Nakumatt vs. Sofapaka (3pm, Ruaraka)

Aprili 2

Zoo vs. Wazito (2pm, Kericho)

Tusker vs. AFC Leopards (4.15pm, Kericho)

Girona ya Olunga yaharamisha uvutaji sigara

Na GEOFFREY ANENE

KLABU anayochezea Mkenya Michael Olunga, Girona FC, imeimarisha vita dhidi ya uvutaji wa sigara kwenye sehemu za mashabiki ya uwanja wake wa Montilivi.

Taarifa kutoka klabu hii inayoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania zimesema Alhamisi kwamba Girona inataka wavutaji sigara wabadilishe sigara kwa tufaa.

Girona imeimarisha vita dhidi ya uvutaji wa sigara ndani ya uwanja wake kwa sababu inalenga kulinda mashabiki wasiovuta sigara wakiwemo walio na umri mdogo.

“Ni muhimu kuepuka kuvuta sigara katika sehemu ya mashabiki. Wahusika wanaombwa kukoma kuvutia sigara katika maeneo ya mashabiki. Ikiwa ni lazima wavute sigara, basi tutawatengea sehemu yao maalum, mbali na mashabiki ambao wanataka kufurahia mechi bila ya kukerwa na harufu ya sigara,” Girona imesema kwenye tovuti yake.

Girona imeongeza kwamba itaendeleza mikakati ya kuimarisha mazingira mazuri ya afya na yasiyo na bughudha kwa mashabiki.

“Huu ni mwanzo tu wa baadhi ya hatua tunapanga kuchukua kuhakikisha mashabiki wa umri zote wanafurahia soka pamoja na familia zao ndani ya uwanja wa Montilivi. Tumeanzisha kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu hatua hii kupitia video.

“Katika mechi ijayo, kwa mfano, wavutaji sigara watashawisha kubadilisha sigara kwa kupewa tunda la tufaa. Klabu hii inapanga kuendeleza maadili ya afya, heshima na kulinda watu hasa watu walio na umri mdogo,” Girona imesema kwenye tovuti yake.

Rwanda kutua nchini kwa mchuano wa Kombe la Afrika U-20

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Rwanda ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 itawasili Kenya Ijumaa kwa mchuano wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times, kocha mkuu Vincent Mashami atataja kikosi cha wachezaji 18 Alhamisi kabla ya timu hiyo kufunga safari ya kuelekea jijini Nairobi.

Gazeti hilo limesema kwamba Junior Wasps ilicharaza klabu ya SC Kiyovu 2-1 katika mechi ya kirafiki Jumanne uwanjani Amahoro, huku “Mashami akikiri kwamba bado vijana wake wana kazi ya kufanya mazoezini kabla ya kuwa tayari.”

Timu hiyo, ambayo itakabiliana na Kenya hapo Aprili 1 mjini Machakos na kurudiana Aprili 21 jijini Kigali, ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya klabu nyingine ya Rwanda, Police FC, Machi 24.

Mshindi kati ya Kenya na Rwanda atajikatia tiketi ya kulimana na mabingwa watetezi Zambia katika raundi ya pili mwezi Mei.

Raundi ya tatu itafanyika mwezi Julai ambapo mshindi ataungana na wenyeji Niger katika Kombe la Afrika mwaka 2019. Timu zitakazofika nusu-fainali kwenye Kombe la Afrika zitafuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini Poland baadaye mwaka 2019.

Harambee Stars yarejea nchini baada ya matokeo ya kukera

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars imerejea nchini Alhamisi kutoka Morocco ambako ilisikitisha baada ya kumaliza mechi mbili za kirafiki bila ushindi dhidi ya limbukeni Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Comoros.

Stars, ambayo inashikilia nafasi ya 105 duniani, ilikabwa 2-2 dhidi ya nambari 132 duniani Comoros hapo Machi 24 na kulemewa 3-2 dhidi ya nambari 121 duniani CAR mnamo Machi 27.

Matokeo haya yalishuhudia Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) likitangaza kumtimua kocha wa muda Stanley Okumbi pamoja na kocha msaidizi Frank Ouna na kocha wa makipa Hagai Azande.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Comoros, Kenya iliongoza 1-0 kupitia penalti ya kiungo wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama baada ya kiungo Eric Johanna Omondi wa IF Brommapojkarna nchini Uswidi kuangushwa ndani ya kisanduku.

Wanavisiwa wa Comoros walisawazisha 1-1 kupitia Youssouf M’Changama dakika ya 20 kabla ya kuongoza 2-1 baada ya Djamel Bakar kuona lango dakika ya 73.

Mshambuliaji wa Buildcon nchini Zambia, Clifton Miheso alinasua Stars kutoka minyororo ya kupoteza mchuano huo aliposawazisha 2-2 zikisalia dakika sita kipenga cha mwisho kilie.

Katika mechi ya pili, ambayo Spurs ilikataa Wanyama achezeshwe, Foxi Kethevoam aliweka CAR bao 1-0 juu dakika ya 14. Omondi alisawazisha 1-1 baada ya kumegewa pasi murwa na mvamizi Michael Olunga (Girona, Uhispania).

Eudes Dagoulou alirejesha CAR mbele 2-1 dakika ya 63 kabla ya Hilaire Momi kuimarisha uongozi huo hadi 3-1 kupitia penalti.

Olunga alifungia Stars bao la pili dakika ya 87. Kenya ilimaliza mechi watu 10 uwanjani baada ya mzawa wa Uhispania, Mkenya Ismael Gonzalez kuonyeshwa kadi nyekundu.

Stars, ambayo inatarajiwa kupata mkufunzi wa kigeni kujaza nafasi ya Okumbi, ilitumia michuano hiyo kujiweka tayari kwa mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika dhidi ya Ghana mwezi Septemba mwaka 2018. Kundi la Kenya pia liko na Sierra Leone na Ethiopia. Sierra Leone ilipepeta Kenya 2-1 katika mechi ya ufunguzi mwaka 2017.

Makocha wa timu za raga Kenya watangaza vikosi vya Hong Kong Sevens

Na GEOFFREY ANENE

MAKOCHA wakuu wa timu za taifa za raga za Kenya za Innocent Simiyu (wanaume) na Kevin Wambua (wanawake) wametangaza vikosi vitakayoshiriki mashindano ya Hong Kong Sevens na Jumuiya ya Madola mwezi Aprili.

Simiyu amefanya mabadiliko mawili katika kikosi chake kilichofika fainali ya Raga za Dunia duru ya Vancouver Sevens nchini Canada mnamo Machi 11 akiita Ian Minjire na Augustine Lugonzo kujaza nafasi za Samuel Ng’ethe na Erick Ombasa.

Ni mara ya kwanza kabisa Minjire amejumuishwa katika kikosi kitakachoshiriki Raga za Dunia ambazo zitaingia duru ya saba mjini Hong Kong. Lugonzo alikosa duru za Marekani (Machi 2-4) na Canada (Machi 10-11) kwa sababu za kibinafsi.

Baada ya Hong Kong Sevens mnamo Aprili 6-8, Shujaa itaelekea mjini Gold Coast nchini Australia kwa mashindano ya Jumuiya ya Madola (Aprili 13-15) na kisha duru ya nane ya Raga za Dunia nchini Singapore (Aprili 28-29) kabla ya kurejea nyumbani.

Wambua ametaja wachezaji 12 kwa mechi za kufuzu kushiriki Raga za Dunia za wanawake mjini Hong Kong mnamo Aprili 5-6. Stacy Awuor atajiunga na Lionesses mjini Gold Coast.

Katika mechi za makundi za Hong Kong, Shujaa italimana na Australia, Uhispania na Canada nayo Lionesses imekutanishwa na Afrika Kusini, Mexico na Papua New Guinea.

Mjini Gold Coast, Shujaa itavaana na New Zealand, Canada na Zambia katika mechi za makundi nayo Lionesses ilimane na New Zealand, Canada na Afrika Kusini katika awamu hiyo.

Vikosi:

Shujaa

Oscar Ouma (Nakuru, nahodha), Samuel Oliech (Impala Saracens), Andrew Amonde (KCB), William Ambaka (Kenya Harlequins), Daniel Sikuta (Kabras Sugar), Arthur Owira (KCB), Collins Injera (Mwamba), Eden Agero (Kenya Harlequins), Billy Odhiambo (Mwamba), Jeffery Oluoch (Homeboyz), Nelson Oyoo (Nakuru), Ian Minjire (Impala Saracens), Augustine Lugonzo (Homeboyz).

Benchi la kiufundi – Innocent Simiyu (Kocha Mkuu), Will Webster (Kocha Msaidizi), Geoffrey Kimani (Kocha wa mazoezi ya viungo), Lamech Bogonko (Daktari), Erick Ogweno (Meneja wa Timu).

 

Lionesses

Philadelphia Olando (nahodha), Sheila Chajira (nahodha msaidizi), Grace Adhiambo, Judith Auma, Sinaida Aura, Doreen Remour, Celestine Masinde, Linet Moraa, Rachel Mbogo, Janet Owino, Janet Okello na Camila Cynthia. Stacy Awuor atajiunga na kikosi mjini Gold Coast. Benchi la kiufundi – Kevin Wambua (Kocha Mkuu), Samuel Njogu (Kocha wa mazoezi ya viungo), Ben Mahinda (Daktari), Camilyne Oyuayo (Meneja wa Timu).

Chipu yabandua Madagascar kutinga fainali Namibia

Na GEOFFREY ANENE

CHIPU ya Kenya imetinga fainali ya mashindano ya raga ya Bara Afrika ya ukanda wa Afrika ya Kusini baada ya kulipua Madagascar 51-13 katika nusu-fainali ya kwanza uwanjani Hage Geingob jijini Windhoek, Namibia, Machi 28, 2018.

Vijana wa kocha Paul Odera watakabiliana na mabingwa mara nane Namibia, ambao wameshinda mataji sita yaliyopita, katika fainali hapo Machi 31.

Nahodha Xavier Kipng’etich (no. 9) atambulisha wachezaji wa Chipu kabla ya Kenya kuvaana na Madagascar. Picha/ Hisani

Namibia walitolewa kijasho kabla ya kujikatia tiketi ya kushiriki fainali kwa kulima majirani Zimbabwe 27-17 katika nusu-fainali ya pili uwanjani humu.

Mshindi kati ya Kenya na Namibia atamenyana na mshindi wa Afrika ya Kaskazini kati ya Tunisia na Senegal. Bingwa wa Afrika ataingia mashindano ya dunia ya Junior World Rugby Trophy (JWRT) baadaye mwaka huu.

Chipu na Namibia zikimenyana katika fainali ya mwaka 2017. Picha/ Hisani

Chipu, ambayo iliongoza 24-10 wakati wa mapumziko, ililemea Madagascar kupitia alama za Mark Mutuku (miguso miwili), Xavier Kipng’etich (mikwaju mitatu, miguso miwili na penalti moja), Victor Matiko (mguso na mkwaju), Joshua Macharia (mikwaju miwili) na Monate Akuei na Jeff Mutuku (mguso mmoja kila mmoja) na penalti moja. Madagascar ilifunga penalti mbili na mguso mmoja.

Mechi za Afrika ya Kaskazini, ambazo ziliandaliwa mjini Monastir nchini Tunisia mnamo Machi 28, zilishuhudia Senegal ikibwaga Morocco 30-25 nayo Tunisia ikakung’uta Ivory Coast 15-11.

NDIVYO SIVYO: ‘Makanga’ au ‘manamba’ hayafai katika miktadha rasmi

Na ENOCK NYARIKI

Makanga na manamba ni maneno mawili yatumiwayo sana katika mazungumzo ya watu kuwarejelea wafanyakazi katika magari ya usafiri. Baadhi ya watu huyatumia maneno hayo kwa kutojua maneno mengine sanifu yanayoweza kutumiwa kuwarejelea wafanyakazi hao ambao huwa na majukumu tofauti.

Katika maeneo ya mjini, maneno hayo hutumiwa kwa uchangamano mno hivi kwamba mtu anaweza kudhani kuwa anayerejelewa ni mtu mmoja. Kwa watu wengine, ‘manamba’ na ‘makanga’ ni maneno yatumiwayo kuwabeza wafanyakazi hao wa matatu yamkini kutokana na tabia zao zilizochipuza katika mazingira yao magumu ya utendakazi.

Nimewahi kuliangazia neno manamba katika safu tofauti. Tulisema kuwa hili ni neno sanifu la Kiswahili ila matumizi yake ya kwanza hayakuhusiana na mfanyakazi katika chombo cha usafiri.

Lilitumiwa kuwarejelea wafanyakazi wa muda fulani katika mashamba makubwa. Hii ni fasili ya toleo la kwanza kabisa la Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyojulikana hadi mwanzomwanzo wa karne ya ishirini na moja.

Kamusi zilizoanza kuandikwa katika karne ya ishirini na moja zimeikumbatia maana ya pili ya neno hilo jinsi inavyotumiwa mtaani kurejelea wafanyakazi katika magari ya usafiri ambao kazi yao kubwa ni kuwaita watu waingie kwenye magari.

Yamkini ile hulka ya watu hao ya kuzitaja nambari za magari kila wanapowaita watu kuyaabiri ndiyo iliyowafanya kupewa jina hilo manamba. ‘Namba’ ni neno jingine ambalo limepata ukubalifu kwa maana ya nambari.

Nayo dhana ‘manamba’ ni lugha ya mtaani ya kuutajia wingi wa namba. Nadharia nyingine inayoweza kuelezea kubuniwa kwa neno hilo ni ile ya utaratibu maalumu unaofuatwa na watu hao katika kuyajaza magari.

Neno makanga halimo kwenye kamusi ingawa baadhi ya vyombo vya habari mpaka sasa hulitumia kwa maana ya mfanyakazi katika gari la abiria ambaye kazi yake ni kuwatoza watu nauli. Ijapokuwa neno kondakta ambalo hutumiwa kumrejelea mfanyakazi huyo si geni, watu wengi hupendelea kutumia makanga kutokana na mazoea.

Kanga ni ndege wa mwituni mwenye rangi nyingi afananaye na kuku. Je, kunao uwezekano kuwa asili ya neno makanga lilitokana na mvao wa wafanyakazi wenyewe hasa kabla ya kuibuliwa kwa sare ya makondakta?

Alhasili, anayepakia na kupakua mizigo kwenye chombo cha usafiri ni utingo au taniboi. Anayewatoza abiria nauli ni kondakta. Anayewaita watu waingie kwenye gari ni mpigadebe. Manamba na makanga hayajapata ukubalifu kamili kwa maana ya wafanyakazi wa matatu. Yasitumiwe katika miktadha rasmi.

KAULI YA MATUNDURA: Mkangi aliandika Walenisi kwa mafumbo kuepuka rungu la dola?

Na BITUGNI MATUNDURA

Riwaya ya Walenisi (Katama Mkangi) ndiyo riwaya ya ‘kwanza changamano’ kuwahi kutahiniwa katika somo la fasihi ya Kiswahili katika  kiwango cha shule za upili nchini.

Katika makala yangu ‘Uhusiano wa mwandishi na mazingira aliyolelewa’ (Taifa Leo, Desemba 15, 2003), nilidai kuwa aghalabu watunzi wa kazi kifasihi huakisi tajriba zao maishani katika tungo zao.

Walenisi ni mfano mzuri ambapo Mkangi anatusawiria baadhi ya tajriba na falsafa zilizoyaongoza maisha yake katika uhai wake – lakini kwa kutumia mkwepo au fumbo.

Maswali tunayofaa kujiuliza ni: Riwaya  changamano/dhati ni ipi? Kwa nini mkwepo au fumbo? Riwaya changamano ina muundo mgumu na uhitaji upevu wa akili ili msomaji aielewe.

Msuko wa riwaya hii huwa tata. Mbali na Walenisi, wahakiki wanaelekea kukubaliana kuwa tungo nyingine katika kundi hili ni Nyongo Mkalia Ini (Rocha Chimera), Ziraili na Zirani (W.E. Mkufya), Babu Alipofufuka (S.A.Mohamed), Nagona na Mzingile (E.Kezilahabi) Bina-Adamu! na Musaleo za Kyalo Wamitila.

Mwanafunzi wa fasihi hana budi kuelewa aghalabu kwa kinaganaga hulka na falsafa za Katama Mkangi ili kuielewa Walenisi. Mkangi  alikuwa msomi na mkereketwa wa utetezi wa ‘ukombozi wa pili nchini’.

Kwa kuamini falsafa ya ujamaa (Socialism), tunamwona Mkangi akiuliza katika riwaya yake ya Mafuta (1984), “Ni kwa nini kuna matajiri wachache na maskini wengi katika jamii?”

Akiwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Mkangi alishirikiana na kina Ngugi wa Thiong’o, Maina wa Kinyatti, Micere Githae Mugo, Alamin Mazrui, Abdilatif Abdalla miongoni mwa wengine kushutumu utawala mbaya wa serikali ya Kanu.

 

Mwakenya

Mnamo mwaka 1986, alitiwa kizuizini kwa  tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi haramu la Mwakenya ambalo yadaiwa lilikuwa na nia ya kuipindua serikali ya wakati huo.

Hali hii inajitokeza katika Walenisi ambapo Dzombo (mhusika mkuu)  anahukumiwa kifo kwa kuingizwa katika chombo cha sayari kinachotumiwa na viongozi dhalimu dhidi ya wapinzani wa utawala wao.

Kinaya ni kwamba, chombo cha kifo kinakuwa chombo kinachomwezesha Dzombo kujifahamu zaidi, kuielewa nchi yake na kuyaelewa mazingira yake kwa undani zaidi.

Walenisi ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa fumbo. Katika miaka ya 1980 na 1990, serikali za Kenya wakati huo hazikutakakukosolewa. Wakati huo, vyombo vya dola – mathalan  mahakama, magereza na polisi vilitumiwa kunyanyasa raia.

Kwa hiyo, watu wengi, wakiwemo waandishi waliogopa kukwaruzana na utawala. Mkangi aliamua kutunga Walenisi kwa njia ya fumbo ili kuepuka rungu la dola.  Dzombo, anahukumiwa  kifo na mahakama kwa madai kuwa kavunja sheria za nchi.

 

Ujasiri wa Dzombo

Baada ya kuwekwa kwenye sayari ya mauti, mahakama ilifikiri Dzombo  ameangamizwa na sayari hiyo ya kifo, lakini Ddombo aliimiliki  kwa uhodari na ujasiri mwingi.

Chombo hicho kinampeleka katika ulimwengu  mpya unaokuwa funzo  kubwa kwake – funzo analoweza  kulitumia kuielekeza nchi yake katika mfumo mwingine unaolinda maslahi ya waliowengi.

Wataalamu Njogu na Chimerah wanaiona Walenisi kuwa  taashira ya safari ya maisha ambapo  mtu anajisaka na kujiuliza: yeye ni nani? Anatoka wapi? Anaenda wapi katika mustakabali  wa jamii yake? Ni safari inayoangalia  muumano wa jana (historia) leo na kesho.

Mkangi anaikamilisha hadithi yake  kwa kauli kwamba, Dzombo anaamua  kurudi duniani – bila shaka kuwafundisha Wanawalenisi wenzake. Je, watamsikiliza au watamkana jinsi Yesu wa Uyahudi alivyokanwa na hatimaye kuangikwa msalabani?

Aidha, Chimerah na Njogu wanaifasiri, riwaya ya Walenisi  kwa misingi ya  msimamo wa mshairi T.S. Elliot (1963) katika shairi lake ‘East Cocker’ kuwa mwanzo wa Dzombo ndio mwisho wake na mwisho wake ndio mwanzo wake.

Je, Dzombo atafanikiwa kuleta mageuzi?

 

Bitugi Matundura ni msomi, mtafiti, mkereketwa wa lugha na mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. mwagechure@gmail.com

 

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili kitakwezwa tu kupitia ari na juhudi za wasemaji wake

Na PROF KEN WALIBORA

Mhakiki wa Kinaijeria Obi Wali aliwahi kuuliza: “Kiingereza kingekuwa wapi kama waandishi wa Kiingereza wangeamua kuandika kwa lugha za Kifaransa au Kilatini, lugha ambazo zilikuwa na hadhi zamani zile kuliko Kiingereza?” Obi Wali alilalamikia kudhalilishwa kwa waandishi wa Kiafrika waliozitumia lugha za Kiafrika.

Kilichochochea kauli ya Obi Wali ni kongomano la fasihi ya Kiafrika lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Makerere, 1962.

Wali alilalamika ni kwa nini waandishi wanaoandika kwa lugha za Kiafrika hawakualikwa kwenye kongomano. Mnamo 1986, Mkenya Ngugi wa Thiong’o aliandika katika kitabu, Decolonising the Mind, kwamba yeye alikuwa ameandika hadithi fupi mbili tu kwa Kiingereza nazo zilitosha kufanya aalikwe.

Nani walioachwa nje? Ni waandishi wakongwe na wabobezi wa lugha za Kiafrika kama vile Fagunwa aliyeandikwa kwa Kiyoruba na Shaaban bin Robert aliyeandika kwa Kiswahili.

Mhakiki wa Kinaijeria Obi Wali aliwahi kuuliza: “Kiingereza kingekuwa wapi kama waandishi wa Kiingereza wangeamua kuandika kwa lugha za Kifaransa au Kilatini, lugha ambazo zilikuwa na hadhi zamani zile kuliko Kiingereza?” Obi Wali alilalamikia kudhalilishwa kwa waandishi wa Kiafrika waliozitumia lugha za Kiafrika.

 

Sababu ya kutoalikwa 

Kilichochochea kauli ya Obi Wali ni kongomano la fasihi ya Kiafrika lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Makerere, 1962. Wali alilalamika ni kwa nini waandishi wanaoandika kwa lugha za Kiafrika hawakualikwa kwenye kongomano.

Mnamo 1986, Mkenya Ngugi wa Thiong’o aliandika katika kitabu, Decolonising the Mind, kwamba yeye alikuwa ameandika hadithi fupi mbili tu kwa Kiingereza nazo zilitosha kufanya aalikwe.

Nani walioachwa nje? Ni waandishi wakongwe na wabobezi wa lugha za Kiafrika kama vile Fagunwa aliyeandikwa kwa Kiyoruba na Shaaban bin Robert aliyeandika kwa Kiswahili.

Turejelee kauli ya Obi Wali: Kiingereza kingekuwa wapi kama waandishi wa Kiingereza wangeamua kuandika kwa lugha za Kifaransa au Kilatini ambazo zilikuwa na hadhi kubwa zaidi kuliko Kiingereza zamani zile? Kiingereza kingekuwa wapi kama William Shakespeare na Charles Dickens wangeandika kwa lugha isiyokuwa yao?

Hili ni swali kuhusu kile ambacho kingetokea ingawa kwa kweli hakikutokea. Nini hasa kilichotokea basi? Kwanza lugha iliyoonekana kuwa ya washenzi, ya makabwela, na walalahoi iliinuka ikakwea sana kwa juhudi za wasemaji wake kujitolea mhanga kuitumia.

Hii leo lugha hii ya Kiingereza iliyokuwa lugha ya washenzi, ndicho Kiswahili cha dunia, chambilecho rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, yaani lugha ya dunia.

 

Lugha ya wachache

Nini kingetokea? Isingekuwa lugha hii ya Washenzi imekua na kunawiri kwa kadiri kubwa namna hiyo. Ingekuwa lugha ya watu wachache katika kisiwa kidogo kiitwacho England au Uingereza.

Kiingereza kingekuwa lugha isiyokuwa na maandishi mengi maarufu kama kilivyo Kiibo cha Chinua Achebe. Kiibo cha Achebe hakijulikani sana wala hakijatumiwa sana katika maandishi.

Achebe mwenyewe alidai kwamba kapewa Kiingereza na kwamba hiyo alikuwa hana budi kukitumia. Naye alikitumia sana katika maandishi yake. Alikitajirisha Kiingereza na kutoa mchango unaofanana na ule Shakespeare na Dickens kwa kadiri fulani.

Aliwafanyia kazi yao ya kukikweza Kiingereza na kukifanya lugha ya dunia. Waingereza hao walipokufa walikuwa na  deni la kukikuza na kukweza Kiibo cha Achebe.Mbona hali kama  hii inatokea ya Waingereza kusaidiwa na wengine?

Hao wengine, kama Achebe, wana lugha zao, lakini hayamkiniki kupata msaada  wa Waingereza kuzikweza lugha zao.  Kisa na maana?  Waingereza walitiisha maeneo mengi ya dunia na kuyafanya makoloni.   Ushawishi wao wa kikoloni bado ungalipo mpaka leo.

 

Prof. Ken Walibora ni msomi wa fasihi, mwanahabari na mwandishi mtajika katika ulimwengu wa Kiswahili.

GWIJI WA WIKI: Timothy Kinoti M’Ngaruthi

BIDII na maombi huandamana kwani imani bila matendo imekufa! Huu ndio ushauri wa Dkt
Timothy Kinoti M’Ngaruthi – mwandishi, mtafiti, mhariri na mhadhiri wa Kiswahili.

MAISHA YA AWALI
Dkt Kinoti alizaliwa kijijini Kanthungu, kata ya Ruiri, katika Kaunti ya Meru mnamo 1967 akiwa kitindamimba katika familia ya watoto tisa. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Loire (1975-1983), Shule ya Upili ya Chuka (1984-1987) na Shule ya Upili ya Kanyakine (1988-1989).

Ana Shahada ya Elimu (Kiswahili na Jiografia) kutoka Chuo Kikuu cha Egerton (1990-1994), Uzamili katika Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta, 2008) na Uzamifu katika Kiswahili (Chuo Kikuu cha Chuka, 2015).

 

HUJAFA HUJAUMBIKA
Dkt Kinoti hakufanya vyema katika mtihani wa Darasa la Saba wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Shule ya Msingi (CPE) mnamo 1982 kwani aliambulia jumla ya alama 21 kwa 36. Baada ya kukosa nafasi ya kuendelea na masomo ya shule ya upili, aliamua kujiunga na chuo cha ufundi kujifunza uashi.

Siku chache kabla ya kujiunga na Isiolo Village Polytechnic, aliyekuwa mwalimu wake wa shule ya msingi, Bw Justus Murira aliwasili nyumbani kwao na kumshawishi kurudia Darasa la Saba.

Aliporejea shuleni shingo upande, hakujua kwamba katika mtihani wa CPE wa 1983, angeibuka kuwa mwanafunzi wa pili bora katika shule yao kwa kuzoa jumla ya alama 28! Lakini furaha yake iliyeyuka ghafla baada ya kukosa karo ya kujiunga na Shule ya Upili ya Chuka kwani mnamo 1984, kulitokea baa la njaa nchini Kenya linalokumbukwa hadi leo kutokana na kuwasili kwa msaada wa mahindi ya manjano kutoka Marekani.

Iliwabidi wazazi wake Kinoti – mzee M’Ngaruthi M’Kirigia na mama Grace Kaguri, kuuza kipande cha ardhi walichokuwa wakikitegemea sana kwa chakula katika kata ya Kambakia.

Alipojiunga na Kidato cha Kwanza, alikuwa tayari amepitwa na mengi kwani ilichukuwa muda mrefu kupata mnunuzi wa ardhi yao. Ingawa alipitia changamoto tele, bidii za wazazi wake zilizoandamana na maombi zilimwezesha kupata jumla ya alama 20 katika Kiwango cha Kwanza (Division One) katika mtihani wa Kidato cha Nne (KCE) wa 1987.

Alipojiunga na Shule ya Upili ya Kanyakine, alifanya vyema katika mtihani wa Kidato cha Sita (KACE) mnamo 1989 kwa kuzoa jumla ya alama 13 kwa 18.

Vitabu alivyochapisha hadi sasa ni Fasihi Simulizi na Utamaduni (Jomo Kenyatta Foundation, 2008) kinachotumiwa na wanafunzi na walimu katika shule za upili na vyuo vikuu nchini na ughaibuni, na Miale ya Mashariki:Mashairi na Mwongozo wa Uchambuzi (Nsemia Inc. Ontario, 2012). Picha/ Chris Adungo

UALIMU
Dkt Kinoti amewahi kufunza katika Shule ya Upili ya Mataara, Thika (1994-1996), Shule ya Wasichana ya Kanjalu, Meru (1996-1999) na shule ya Wasichana ya Ruiri, Meru (2000-2010). Kwa miaka kadha, alikuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi yaTatu ya KCSE (Fasihi ya Kiswahili).

Aidha, alikuwa akitunga mashairi na kuwaandaa wanafunzi kwa mashindano ya kitaifa ya muziki na drama, mbali na kuwa mkaguzi katika tamasha mbalimbali, yakiwemo mashindano ya muziki na ushairi makanisani.

Amewahi kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kimethodisti (KeMU) ambamo alikuwa Mkuu wa Idara ya Elimu (2015-2016) kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Embu mnamo Septemba 2016 na kuteuliwa katika kamati mbalimbali za chuo.

Hizi ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha za Kitamaduni, Kamati ya Uhariri wa Miswada ya Sera za Chuo Kikuu, Mhariri wa Jarida la Flashlight na Mlezi wa Chama cha Kiswahili, miongoni mwa majukumu mengine.

Isitoshe, amewahi kufunza kozi kadha za Uzamili katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya na Chuo Kikuu cha Chuka akiwa mhadhiri wa muda.

 

UANDISHI
Aligundua kipawa chake cha uandishi alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Insha alizoziandika kwa Kiingereza zilisifika sana shuleni kote na pia kuongoza katika mitihani ya mwigo tarafani. Wakati huo, somo la Kiswahili halikutiliwa maanani katika shule za msingi kwani halikuwa likitahiniwa mwishoni mwa Darasa la Saba.

Hata hivyo, palikuwepo walimu wawili – Bi Jacinta Muthamia na Bw Rwigi, ambao walijitolea kuwafunza Kiswahili wakati walimu wengine walipokosa kuona maana ya somo hilo.

Juhudi za walimu hao pamoja na zile za babaye mzazi ambaye alimfunza kuhesabu kwa Kiswahili zilimfanya Kinoti kuvutiwa na somo hilo. Pia alipenda kusikiliza mashairi yaliyoghaniwa redioni na mzee Abdalla Mwasimba.

Mwalimu wake wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Chuka, Bw Kaimenyi Marete ndiye aliyemsaidia kutambua kipawa chake hasa alipompa nafasi ya kushiriki katika kipindi cha

Sanaa ya Kiswahili kilichopeperushwa na runinga ya VoK (sasa KBC) mnamo 1987. Dkt Kinoti alishiriki mjadala ‘Kiswahili ni Lugha ya Kibantu’ na kutambuliwa na waamuzi James Kanuri na Bakari Mwarandani kuwa mwanafunzi bora zaidi miongoni mwa waliokuwa washiriki. Kipindi hicho kilimpa umaarufu mkubwa katika shule hiyo ambayo ilikuwa na zaidi ya wanafunzi 800.

Katika Shule ya Upili ya Kanyakine, alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kiswahili na Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari. Isitoshe, yeye na mwanafunzi mwenzake, Kamau Munyua (mtangazaji maarufu wa Redio Citizen) walitambuliwa kuwa waandishi rasmi wa habari na kutengewa viti maalum ndani ya basi wakati timu za shule ziliposafiri kwa mashindano ya muziki, drama na michezo.

Dkt Kinoti alipata fursa ya kipekee ya kuwa mwanahabari katika ukumbi wa KICC wakati wa Tamasha za Kitaifa za Muziki mwaka wa 1989! Walimu wake – Bi Ngaku, Bw Murugu na Bw Nkanata pia walikipalilia kipawa chake cha uandishi kwa kumuomba kutunga mashairi yaliyowasilishwa na wanafunzi wenzake katika tamasha za muziki na kupata tuzo mbalimbali.

Aidha, alishiriki katika vitengo vya nyimbo za kitamaduni na mazungumzo pamoja na kukariri na kughani mashairi aliyotunga.

Kutangamana kwake na wasomi maarufu wakiwemo Chacha Nyaigotti Chacha, Abdulaziz Lodhi, Kimani Njogu, Rocha Chimerah, Ken Walibora, John Habwe, Rayya Timammy, Catherine Ndungo, Clara Momanyi, Richard Wafula, Mwenda Mukuthuria, John Kobia na Bitugi Matundura kumemchochea kujiendeleza zaidi katika utafiti na uandishi akilenga kufikia ngazi ya uprofesa.

Vitabu alivyochapisha hadi sasa ni Fasihi Simulizi na Utamaduni (Jomo Kenyatta Foundation, 2008) kinachotumiwa na wanafunzi na walimu katika shule za upili na vyuo vikuu nchini na ughaibuni, na Miale ya Mashariki:Mashairi na Mwongozo wa Uchambuzi (Nsemia Inc. Ontario, 2012).

Diwani hii yenye mashairi 82 imeidhinishwa na KICD kutumika katika shule za upili nchini Kenya.

Pia amechapisha makala ya kitaaluma katika majarida ya kimataifa na kushiriki makongamano ya kimataifa yaliyoandaliwa na Baraza la Wanataaluma wa Kiswahili (BAWAKI), Taasisi ya Utafiti na Masomo ya Kiswahili Afrika Mashariki (RISSEA), Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Kongamano la Kwanza la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Zanzibar.

 

JIVUNIO
Dkt Kinoti ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shule ya Upili ya Rwarera na Mlezi wa Shule ya Msingi ya Kanthungu. Pia huhubiri neno la Mungu na kutoa ushauri katika makanisa na taasisi mbalimbali, mbali na kuwa mfawidhi (MC) katika sherehe mbalimbali. Katika shughuli zote, mke wake – Bi Hellen Kinoti pamoja na mabinti zake – Karwitha, Kajuju, Joy na Rehema wamekuwa nguzo kuu.

 

Kila mwanahisa wa Eveready apokea Sh1 kwa kila hisa

Na PETER MBURU

WENYEHISA wa kampuni ya kuuza betri ya Eveready East Africa PLC walipokea Sh1 kwa kila hisa, kutokana na pesa za mauzo ya shamba la ukubwa wa ekari 18.5 ililokuwa ikimiliki kampuni hiyo eneo ghali mjini Nakuru.

Baada ya kuuza shamba hilo kwa Sh1.14bilioni, kampuni hiyo ilitumia Sh525 milioni kulipa madeni yaliyokuwa yakiisakama baada ya kutengana na kampuni ya Energizer Holdings, na kubakisha Sh210milioni kama faida kwa wenye hisa.

Habari hizi zilitolewa wakati wa mkutano wa mwaka wa kampuni hiyo (AGM) ulioandaliwa katika hoteli ya Merica mjini Nakuru Jumatano.

“Lakini tuna furaha kufahamu kuwa sasa hatuna deni na mtu kwani tulilipa madeni yote na hata kubakisha Sh150 milioni za kupanua biashara,” akasema mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Jackson Mutua.

Bodi ya wakurugenzi aidha ilisema kampuni hiyo ilikuwa ikijikokota kushika mizizi sokoni, kwani licha ya kuwepo kwa zaidi ya miaka 50, nyingi za biodhaa zao zilizinduliwa kwa kipindi cha mwaka uliopita baada ya kutofautiana na kutengana na kampuni ya Energizer Holdings.

Bodi hiyo ilisema kampuni hiyo iliingiza hasara ya zaidi ya Sh300 milioni kipindi cha mwaka uliopita wa pesa, kutokana na gharama nyingi za kubadili uongozi, kugharamia kesi nyingi kortini na hali ya biashara kuvurugwa na uchaguzi wenye utata.

“Sisi ni biashara ambayo bado ipo utotoni kwani tumeingiza bidhaa nyingi sokoni mwaka uliopita, lakini bado tuna ubora wa betrii na wateja wengi wanatuamini,” akasema Bw Mutua.

Kampuni hiyo aidha ilitangaza mpango wa kuondoa betriizijulikanazo kama D-sized sokoni, kutokana na ugumu wake wa kutupwa zinapoharibika na badala yake kuingiza betri ndogo.

Bodi ya uongozi ilitilia hofu deni wanalodai kampuni ya Nakumatt kuwa huenda likapotelea, baada ya Nakumatt kuanguka kwa viwango vikubwa na kutoonyesha dalili za kulipa.

Mwenyekiti wao Bi Lucy Waithaka, hata hivyo, alitetea kampuni hiyo kuwa sasa baada ya kujitenga na Energizer Holdings walikuwa na nafasi kufanya vyema sokoni.

“Hii ni kwa kuwa sasa sisi ndio waamuzi wa biashara yetu kinyume na mbeleni ambapo maamuzi yalifanywa na watu wasiofahamu changamoto na mahitaji ya sokoni,” akasema Bi Waithaka.

 

Wakenya sasa kufanya biashara popote Afrika bila vikwazo

Na CECIL ODONGO

HATIMAYE Serikali imeidhinisha mkataba wa kibiashara ambao utawezesha Wakenya kufanya biashara katika mataifa mengine ya Afrika bila vikwazo vya usafiri.

Baraza la Mawaziri lilipitisha makubaliano ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitia saini wiki jana kwenye mkutano wa Biashara Huru Barani Afrika, jijini Kigali, Rwanda.

Kwenye mpango huo, raia wa Afrika watasafiri kutumia paspoti moja. Pia sarafu moja ya barani itazinduliwa kurahisisha ununuzi na uuzaji.

Mswada ulioidhinishwa na mawaziri, sasa utapelekwa bungeni kujadiliwa na kupitishwa ili kuifanya Kenya kuwa mojawapo ya nchi 22 ambazo zimeanza kuitumia kama sheria.

Rais Uhuru Kenyatta aliongoza mkutano wa baraza hilo uliohudhuriwa pia na Naibu Rais William Ruto ambapo sekta ya kibinafsi ilitakiwa kutumia nafasi kutiwa saini kwa makubaliano hayo kuwekeza katika mataifa yote barani.

Makubaliano hayo ya Kigali yatawezesha bara la Afrika kupanua soko lake la kibiashara, kuimarisha miundo msingi na kuimarisha uchumi kwa zaidi za wananchi wake 1.2 bilioni.

Ikitekelezwa, vile vile itakuwa rahisi mno kutatua mizozo iliyokithiri sana miongoni mwa mataifa ya barani ikiwemo mizozo ya kila mara kuhusu mipaka na mapinduzi ya kijeshi.

Mkutano huo pia uliidhinisha uhuru wa kibiashara kwa Mashirika ya COMESA, SADC na EAC na bajeti la ziada kwa lengo la kupunguza gharama ya matumizi.

Baada ya kupitisha bajeti ya ziada, bajeti ya mwaka 2017-2018 pia itaangaliwa upya ili kupunguza nchi kukimbilia mikopo na kufanya nchi kushughulikia miradi yake kutokana na uwezo wake kiuchumi.

guzo nne za muhimu za awamu ya pili ya Rais Kenyatta pia zitatekelezwa kikamilifu ili kuimarisha uchumi wa nchi.

Baraza la Mawaziri pia lilijadili mswada wa kustaafu kwa maafisa wa kaunti na ripoti iliyotolewa majuzi kuhusu viwango vya umaskini nchini na Shirika la Takwimu Nchini(KNBS)

Mkutano huo ulipendekeza serikali itumie matokeo ya ripoti hiyo kutekeleza na kuipa kipaumbele miradi inayowainua wananchi kiuchumi ili kupunguza kiwango cha umaskini.