Mamaye Wanyama abwagwa uchaguzini

Na GEOFFREY ANENE

MWENYEKITI wa Shirikisho la Mpira wa Pete (Netiboli) la Kenya (KNF) Mildred Ayiemba Wanyama Jumatatu amepoteza kiti hicho.

Mama huyu wa viungo Victor Mugubi (Tottenham Hotspur, Uingereza) na McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), aliambulia kura saba dhidi ya 54 za mshindi Immaculate Kabutha katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliofanywa katika ukumbi wa City Hall jijini Nairobi mnamo Machi24, 2018.

Mbali na mama ya viungo hao wa Harambee Stars kupoteza nyadhifa zao, katibu wa muda mrefu wa KNF Lilian Anupi pia hakuwa na lake.

Anupi, ambaye amehudumu KNF kwa zaidi ya miaka 20, alibwagwa kwa kura 52-9 na Millicent Busolo.

Kiti cha Mwekahazina pia kimepata afisa mpya baada ya Anne Bett kulemea Sophie Makoba 53-7. Esther Mukene hakutetea kiti hiki chake.

Bett atasaidiwa na Evelyn Cherono aliyepata kura 43 dhidi ya wapinzani wake Eunice Okal (13) na Silphosa Omollo (tano).

Jonah Chemagut ni naibu wa rais. Hakuwa na mpinzani. Juma Amollo ni katibu msaidizi na John Makau (mpanga ratiba) na Suleiman Hassan (naibu mpanga ratiba).

Ajenti wa M-Pesa kizimbani kuhusu njama ya kumtapeli Sabina Chege

Na RICHARD MUNGUTI

AJENTI wa Mpesa wa kampuni ya Safaricom Jumatatu alishtakiwa kwa kusajili nambari ya simu ya mbunge mwakilishi wa wanawake kaunti ya Murang’a Bi  Sabina Chege kwa lengo la kumlaghai pesa pamoja na wabunge wengine katika kashfa ya kimitandao.

Catherine Nyaboke Omwene ameshtakiwa siku 12 baada ya wanafunzi wawili wa chuo kikuu kufunguliwa shtaka la kujaribu kupokea Sh100,000 kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo.

Bi Omwene alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku. Alikabiliwa na mashtaka matano ya ufisadi wa kimitandao na kujaribu kumtapeli Bi Chege.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Veda alimweleza hakimu kwamba kabla ya kukamatwa kwa mshtakiwa wabunge walikuwa wamelalamika kwa polisi kwamba nambari zao zinatumikiwa na walaghai kujipatia mamilioni ya pesa kutoka kwa wananchi na wabunge.

“Wabunge walidai wamefujwa mamilioni ya pesa na matapeli,” alisema Bi Veda.

Mshtakiwa ambaye hakuwa na wakili wa kumtetea alidaiwa mnamo Machi 3, 2018 katika duka la kuuza bidhaa za urembo za wanawake lijulikano Update Beauty Shop katika mtaa wa Donholm kaunti ya Nairobi aliandikisha nambari ya simu ya Bi Chege.

Bi Omwene aliandikisha nambari ya mbunge huyo kwa mmoja Bw Waziri Benson Masubo. Shtaka lilisema mshtakiwa alikuwa na lengo la kuwatapeli umma alipoandikisha simu hiyo ya Bi Chege kwa jina la Bw Masubo.

Bw Omwene alikabiliwa na shtaka la kukubali sajili ya Safaricom itumike kwa njia ya uwongo kwa kuandikisha nambari ya Bi Chege kwa jina la Bw Masubo.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka yote na kuomba aachiliwe kwa dhamana. Bi Mutuku aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000 na kuorodhesha kesi isikizwe Aprili 26, 2018,

Korti iliamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi aandae utetezi wake.

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Multi-Media Mabw Derick Kimutai Ng’etich na Edwin Ndiritu walikana walijaribu kumlaghai Bw Midiwo wakijifanya wametumwa na Bi Chege kupokea Sh100,000.

Mkali wa kriketi motoni kwa kubadilisha hali ya mpira kwa manufaa yake

Na GEOFFREY ANENE

MCHEZAJI wa kriketi wa Australia, Steve Smith amepigwa marufuku mechi moja na kupoteza Sh1, 435,408 baada ya kupigwa faini ya asilimia 100 kwa sakata ya kubadilisha hali ya mpira ili kujinufaisha Machi 24, 2018.

Cameron Bancroft, ambaye ni mchezaji mwenza, alikwepa marufuku, lakini akapigwa faini ya Sh1, 076,556 (asilimia 75 ya ada yake ya mechi) baada ya kupatikana akidanganya mchezoni kwa kusugua mpira ili kufanya Australia iwe na kazi rahisi kupata pointi dhidi ya wenyeji Afrika Kusini mjini Cape Town.

Bancroft, 25, alinaswa kwenye runinga akiwa na kifaa fulani akisugua mpira kabla ya kukificha katika mfuko wa long’i yake.

Smith, 28, alipokonywa unahodha wa Australia kutokana na kisa hicho. David Warner, 31, pia alijiuzulu majukumu ya naibu ya nahodha. Inaaminika wachezaji hawa viongozi walimsukuma Bancroft kuvunja sheria hiyo.

Akizungumzia hatua ya kuadhibu Smith na Bancroft, Afisa wa marefa kutoka Shirikisho la Kriketi duniani (ICC) Andy Pycroft alisema, “Kubeba kifaa ambacho si cha mchezo wa kriketi uwanjani kwa nia ya kubadilisha hali ya mpira ili kukuwezesha kushinda mpinzani wako ni kinyume na sheria na pia inavunja maadili ya mchezo huu.”

Mwaka 2016, raia wa Afrika Kusini Faf du Plessis alijipata pabaya dhidi ya Australia mjini Hobart akijaribu kubadilisha hali ya mpira kwa kutumia mate akiwa na peremende kinywani. Alipoteza asilimia ya ada ya mechi, ingawa aliepuka marufuku.

Maumivu ya tumbo hayapo tena, Kipsang’ ashinda Tokushima Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI shupavu Wilson Kipsang’ alinyakua taji la mbio za Tokushima Marathon nchini Japan mnamo Jumapili, mwezi mmoja baada ya kusalimu amri katika Tokyo Marathon.

Raia huyu wa Kenya, ambaye maumivu ya tumbo yalifanya ashindwe kutetea taji la Tokyo Marathon mnamo Februari 26, alitawazwa bingwa wa Tokushima kwa saa 2:19:35.

Muda huu ulikuwa nje ya rekodi ya Tokushima Marathon ya 2:15:25, ambayo Mjapani Yuki Kawauchi alitimka mwaka 2014

Bingwa huyu wa London Marathon mwaka 2012 na 2014 alifuatwa unyounyo na Mjapani Takumi Matsumoto katika mbio hizi zilizovutia wakimbiaji 12,400.

Mshikilizi huyu wa zamani wa rekodi ya dunia yuko katika harakati za kuanzisha hazina ya kusaidia kulinda mazingira na masomo ya watoto nchini Kenya kupitia mbio mbalimbali anazoshiriki.

Katika makala ya Tokyo Marathon mwaka 2018, Kipsang’ alikuwa ameahidi kuvunja rekodi ya dunia ya Mkenya mwenzake Dennis Kimetto ya saa 2:02:57 iliyowekwa mwaka 2014 jijini Berlin, Ujerumani. Hata hivyo, baada ya kilomita 15, aliumwa tumbo na kuamua kujizulu. Mkenya Dickson Chumba aliibuka bingwa kwa saa 2:05:30.

Maafisa ndani kwa kumeza hela za makaburi

Afisa wa usoroveya Cephas Kamande (kushoto) na afisa wa masuala ya ununuzi katika wizara ya serikali za mitaa Boniface Okerosi Misera waliofungwa kwa kuilaghai serikali pesa za makaburi. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wakuu katika kaunti ya Nairobi Ijumaa walihukumiwa kifungo cha miaka miwili kwa kuilaghai serikali zaidi ya Sh283 milioni katika kashfa ya ununuzi wa shamba la kuwazika wafu katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos miaka tisa iliyopita.

Mbali na kifungo hicho cha miaka miwili kavu wawili hao waliagizwa walipe faini ya Sh77milioni.

Mahakama ilisema baraza la jiji la Nairobi NCC iliyokuwa inauziwa shamba hili ilipata liko na mawe na “makaburi hayangechimbika”

“Lilikuwa shamba la mawe. Hakuna mfu angelizikwa mle. Serikali ilipoteza mamilioni ya pesa kununua shamba la mawe. Maiti hutakiwa kuzikwa katika ardhi iliyo na mchanga mwingi,” alisema hakimu mwandamizi Feliz Kombo.

Wafungwa hao miwili ni  afisa wa usorovea Cephas Kamande na afisa wa masuala ya ununuzi katika wizara ya serikali za mitaa Boniface Okerosi Misera.

Akipitisha hukumu, Bw Kombo alisema maafisa hawa walikuwa wamepewa jukumu la kutunza pesa za umma lakini wakazifuja.

“Wawili hawa walikuwa wamepewa jukumu la kutunza pesa za umma lakini walizitumia vibaya waliponunua shamba lenye mawe la kuwazika wafu,” alisema Bw Kombo.

Wawili hao walikuwa wameshtakiwa pamoja na aliyekuwa Meya wa Nairobi Bw Geoffrey Majiwa, aliyekuwa naibu wa katibu mkuu wa lililokuwa baraza la jiji la Nairobi sasa kaunti ya Nairobi Bw Charo Kahindi.

Wengine wanaoshtakiwa kwa kupokea pesa katika kashfa na kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya ni  pamoja na katibu wa zamani  Sammy Kirui, aliyekuwa katibu wa baraza la jiji la Nairobi Bw John Gakuo na katibu mkuu wa zamani Bw William Mayaka.

Viongozi wa kidini: Weta na Mudavadi wakomeshe siasa za ukabila

Na JUSTUS OCHIENG’

VIONGOZI wa dini eneo la Nyanza wamewalaumu vinara wawili wa Nasa- Musalia Mudavadi na Moses Wetenga’ula kwa kuendeleza siasa za ukabila kumlenga kiongozi muungano huo wa Nasa Raila Odinga katika eneo la magharibi.

Wahubiri hao wa baraza la viongozi wa kanisa waliwashutumu Mudavadi na Wetang’ula kwa kuendeleza kampeini za mgawanyiko na uchochezi dhidi ya Bw Odinga.

“Tunamtaka Bw Wetang’ula aendeleze kampeni zinazolenga kuwaunganisha wakenya. Hii ni kwasababu nchi hii inahitaji kuletwa pamoja baada ya siasa za migawanyiko na chuki kutokana na kampeni za mwaka uliopita,” kiongozi wa baraza hilo Askofu Washington Ongonyo-Ngede alisema.

Mnamo Jumamosi, Mabw Mudavadi na Wetang’ula waliambia jamii ya Walhuya wamkatae Bw Odinga na kumlaumu “kwa kuitumia jamii hiyo na kuitema.”

Shambulizi hili dhidi ya Bw Odinga linatokana na kung’atuliwa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wake wa kiongozi wa walio wachache katika bunge la Seneti.

Wadhifa huo umetunukiwa Seneta wa Siasa James Orengo.

Lakini jana viongozi wa dini kutoka Nyanza wakiongozwa na Askofu Ngede walimtahadharisha dhidi ya madai kwamba ataimbua kampeini za kumpinga Bw Odinga.

Katika taarifa iliyotiwa saini na maaskofu saba Ogonyo-Ngede, Julius Otieno, Dkt Hesbon Omwandho Njera, Habakuk Abogno, Dkt William Abuka, Geoffrey Owiti na Rev Job Othatcher viongozi walimtakaka Bw Wetang’ula akome “mara moja kuendeleza kampeni za mgawanyiko na badala yake aanze mikakati ya kuwaunganisha wananchi kwa minajili ya maendeleo.”

Maaskofu hao waliwashauri wakenya wakumbatie uhusiano uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuimarisha nchi hii.

Wahubiri hao walisema Bw Odinga yuko huru kushauriana na Rais Kenyatta kutafuta namna ya kuleta uuwiano nchini.

“Seneta Wetang’ula anapasa kujua aliyekuwa waziri mkuu ni kiongozi wa kitaifa anayeongoza watu na wala sio wananchi wanaomwongoza,” alisema Askofu Ngede.

Kizaazaa Miguna kuzuiwa JKIA akitoka Canada

Na WANDERI KAMAU

KIZAAZAA kilizuka Jumatatu katika Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya maafisa wa Idara ya Uhamiaji kumzuilia wakili Miguna Miguna aliyewasili nchini.

Bw Miguna aliwasili katika uwanja huo mwendo wa saa nane mchana kama alivyopangiwa, ila hakuruhusiwa kuondoka mara moja, “hadi pale angetimiza kanuni fulani.”

Muda mfupi baada ya kufika, maafisa hao walimtaka Bw Miguna kutia saini stakabadhi fulani na kusalimisha paspoti yake ya nchi ya Canada, ila mawakili wake walisema walimwonya dhidi ya kufanya hivyo.

Kulingana na wakili wake, Nelson Havi, huo ni mpango wa serikali kumpa visa ya muda ili kumfanya kuupoteza uraia wake baada ya miezi sita.

“Tumemwagiza mteja wetu dhidi ya kutia saini stakabadhi zozote, kwani njama iliyopo ni ya kumpa stakabadhi ya muda, ili kumnyang’anya uraia wa Kenya, ili serikali imrejeshe Canada tena baada ya kipindi cha miezi sita kuisha,” akasema Bw Havi.

Na hadi tukienda mitamboni, Bw Miguna alikiuwa angali anazuiliwa katika uwanja huo.

Bw Miguna alirudishwa ghafla nchini Canada mwezi uliopita, baada ya kuzuiliwa kwa siku tano na polisi kwa kumlisha kiapo kinara wa Nasa Raila Odinga kama ‘Rais wa Wananchi’ mnamo Januari 30.

Tangu kurejeshwa nchini humo, amekuwa akihutubia vikao katika miji mbalimbali katika nchi za Amerika na Canada, ambako amekuwa akiilaumu serikali ya Jubilee kwa ‘kumhangaisha’ bila sababu.

Bw Miguna pia amekosoa vikali muafaka wa kisiasa kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, akiutaja kutokuwa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili nchi.

Aidha, alimlaumu Bw Odinga kwa “kuwasaliti” wafuasi wake kwa hatua yake kukubali kuingia katika muafaka huo.

 

Mahakama yasitisha uchaguzi wa awamu ya pili Sierra Leone

FREE TOWN, SIERRA LEONE

MAHAKAMA Kuu ya Sierra Leone, Jumamosi ilitoa agizo la kusimamisha awamu ya pili ya uchaguzi wa urais hadi iamue kesi iliyowasilishwa na wakili wa chama tawala.

Taharuki imetanda kabla ya uchaguzi huo huku kampeni zikikumbwa na ghasia. Wanasiasa na wafuasi pia wamekuwa wakitishwa na chuki za kikabila zimeongeka kufuatia kura hiyo.

Agizo la mahakama linazuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuandaa uchaguzi huo hadi kesi isikilizwe na kuamuliwa. Linazuia tume kuandaa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kusambaza karatasi na vifaa vya kura.

Mahakama iliahirisha kesi hadi Jumatatu kupatia tume muda wa kuwasilisha swali katika Mahakama ya Juu na baadaye itaketi kushughulikia kesi hiyo.

“Kwa kuzingatia kuwa kesi hii itarudi kortini Jumatatu Machi 26, tume itasitisha kwa muda maandalizi ya awamu ya pili ya kura ya urais,” tume ilisema kwenye taarifa.

Wakili Ibrahim Sorie Koroma, mwanachama wa chama tawala cha All Peoples’ Congress (APC), alisema kwenye kesi yake kwamba madai ya wizi wa kura yanafaa kuchunguzwa kabla ya uchaguzi kuandaliwa.

Waangalizi wa kimataifa na wa Sierra Leone walisema kwamba uchaguzi wa raundi ya kwanza ulikuwa huru na wa haki.

Mgombea urais wa APC Samura Kamara, alikuwa wa pili nyuma ya Julius Maada Bio wa chama cha upinzani cha Sierra Leone People Party (SLPP) kwenye raundi ya kwanza Machi 7 lakini hakuna aliyepata asilimia 55 ya kura kutangazwa mshindi.

Kamara aliambia AFP kwamba alitarajia mahakama zitahakikisha NEC itaondoa makosa yaliyoshuhudiwa Machi 7 kabla ya awamu ya pili ya uchaguzi.

Tayari, upinzani unadai kwamba polisi wamekuwa wakitumiwa na APC baada ya kuingia ofisi za NEC na kuwahoji wafanyakazi wiki jana. Upinzani pia unasema kwamba chama tawala kinatumia mahakama kuchelewesha uchaguzi.

“Tunachukulia haya yanayoitwa maagizo ya muda ya mahakama kama njama za Rais Ernest Koroma za kutaka kuongeza muda wake mamlakani kinyume cha sheria,” SLPP ilisema kwenye taarifa Jumamosi.

“Dalili zote zinaonyesha kwamba Koroma hatapeana mamlaka bila shinikizo za jamii ya kimataifa kwa sababu ameingilia asasi zote za serikali ikiwa ni pamoja na Mahakama,” ilisema taarifa hiyo.

Polisi walivamia boma la mgombeaji wa SLPP, Bio baada ya raundi ya kwanza ya uchaguzi lakini hawakumkamata.

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Magharibi mwa Afrika (UNOWAS), Mohamed Ibn Chambas, Alhamisi alisema tume ya uchaguzi inakabiliwa na changamoto teke katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alitaka pande zote kutoingilia au kutatiza uhuru na uadilifu wa NEC.

 

Kidume mkono gamu amhepa kisura wake dukani

 Na TOBBIE WEKESA 

ROYSAMBU, NAIROBI

Mrembo mmoja alitamani ardhi ipasuke immeze kuepuka aibu aliyopata katika supamarket moja mtaani hapa baada ya polo aliyesemekana kuwa mpenzi wake kumhepa.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa amemtembelea mrembo anakoishi. Inadaiwa mrembo alimuomba polo amnunulie bidhaa fulani za matumizi  nyumbani.

Duru zinaarifu polo alimueleza mrembo waandamane naye supamaketi ili wakavinunue.

Ripoti zinasema mrembo alipofika supamaketi, aliamua kujaza troli na vitu visivyo na maana.

“Nilifikiri utachukua vitu unavyohitaji tu.  Sasa vibanzi, biskuti sharubati na popkons ni vya nini. Ama unapanga kununua supamaketi nzima,” polo alimuuliza mrembo. Badala ya kujibu swali, mrembo aliendelea kuongeza bidhaa kwenye troli.

Jamaa alilazimika kuanza kuondoa baadhi ya bidhaa kutoka kwenye troli.

Darling unajua tu si rahisi wewe kunifanyia shopping. Acha nijaze tu troli ndiposa vinisukume mwezi mzima,” mrembo alimueleza jamaa.

Duru zinasema jamaa aliamua kutoka nje ya supamaketi huku akimueleza demu asubiri akatoe  hela kwenye ATM.

Kipusa aliamua kumngoja polo hadi akachoka. Aliamua kumpigia simu lakini alikuwa mteja kwa muda mrefu na alipofaulu kumpata hakujibu.

Baada ya kugundua kuwa jamaa alikuwa amemhepa, alianza kuondoa bidhaa kwenye troli na kuvirudisha alikovitoa. Wahudumu wote kwa hiyo supamaketi walimrushia macho huku walinzi wakimakinika.

Kabla ya kumaliza kurudisha vitu, jamaa alimtumia  ujumbe kwenye simu akimuonya dhidi ya kutofuata maagizo yake.

“Wakati mwingine tukienda shopping, niulize kwanza nina pesa ngapi. Tabia yako ya kufanya mambo kwa kiburi ikome,” jamaa alimuonya mrembo kwa ujumbe.

Demu alilazimika kuondoka polepole bila kununua chochote.

…WAZO BONZO…

TAHARIRI: Tuongeze juhudi kuangamiza TB

Na MHARIRI

ULIMWENGU ulipoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani Jumamosi, jambo moja lililojitokeza wazi ni kwamba Wakenya 29,000 walikufa mwaka jana kutokana na ugonjwa huo.

Hata takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonyesha kuwa TB ni ugonjwa wa pili kwa kuua watu duniani, ambapo 4,500 huaga dunia kila siku.
Ugonjwa huu umekuwa hatari zaidi, kutokana na kuzuka kwa Kifua Kikuu ambacho hakisikii dawa.

Tatizo kubwa linalowakumba Wakenya wengi ni kuwa, hata mtu anapoanza kukohoa mfululizo, huogopa kwenda kumwona daktari kutokana na itikadi isiyokuwa ya ukweli kuwa mtu akiugua TB bila shaka atakuwa ana virusi vya Ukimwi.

Ni kweli kwamba mtu anapokuwa na virusi vya HIV, huwa na kinga dhaifu na maradhi mengi humpata kikiwemo Kifua Kikuu. Lakini si lazima anayeugua Kifua Kikuu awe na Ukimwi.

Hapa Kenya, mojawapo ya mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa maambukizi ya TB ni watu kuwa kwenye mazingira yenye hewa isiyotosha. Ndani ya maduka ya jumla katika miji mingi, orofa za chini au juu hushuhudia msongamano wa wateja, lakini madirisha huwa machacho au wakati mwingine hayapo.

Ndani ya magari ya usafiri wa umma, abiria huamua kufunga vioo kwa kuhofia wachomozi ambao hunyakua simu au bidhaa nyingine za thamani kupitia madirishani.

Japokuwa wananchi wana jukumu katika suala hili, ipo haja kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuunga mkono juhudi za maafisa wa afya kuhamasisha raia kuhusu hatari ya kutokuwa na mzunguko wa kutosha wa hewa safi.

Kwa hivyo, kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni ‘Viongozi Wahitajiwa: Ili kuwa na Ulimwengu bila TB’ yafaa kuzingatiwa na viongozi wote, bila kujali tabaka au uwakilishi wao katika jamii.

Viongozi wan auchawishi mkubwa kwa wananchi. Tungependa kuona MCA, chifu, mzee wa kijiji, viongozi wa vijana na hata rais wa Jamhuri ya Kenya wakijitokeza na kuwaeleza wananchi madhara ya kutozingatia kanuni za kukabiliana na kusambaa kwa TB.

Kwa mfano wanapaswa kuhamasisha watu kwamba wakati mtu anakohoa katika eneo la umma, awe akiziba mdomo kwa kuwa vidudu vinavyosababisha TB hurukakupitia hewa tunayovuta.

Ni kupitia juhudi za pamoja tu, ndipo tutaangamiza Kifua Kikuu.

 

 

Mwaka mmoja baada ya Wamakonde kutambuliwa, bado ni kilio

KAZUNGU SAMUEL na FADHILI FREDRICK

Kwa ufupi:

 • Wamakonde walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru
 • Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho
 • Sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa 2017 na Rais Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa tena
 • Wanalia kuwa kumiliki ardhi kwao ni tatizo kuu huku wakitengwa na majirani zao licha ya kukubaliwa kama kabila la 43 nchini

MWAKA mmoja si kipindi kirefu katika maisha ya kawaida, hawa iwapo katika muda huo, mtu anasubiri kutimiziwa ahadi fulani.

Kauli hii ni sahihi zaidi kwa watu wa kabila dogo kutoka taifa la Msumbiji, ambao juhudi zao za kutaka kutambuliwa zilizaa matunda mwaka jana, wakati wa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Jamii ya Wamakonde, ambao walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru, ilijikuta ikiendelea kuzaana na kujazana katika kijiji cha Makongeni, kando mwa barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga, katika kaunti ya Kwale.

Taifa Leo ilipowatembelea wakazi hao mwaka mmoja tangu watambuliwe kuwa kabila la 43 la Kenya, wakazi wa kabila hilo walikuwa wengi wa matumaini kwamba labda walikuwa wamefikishiwa habari njema.

Kijiji hicho ambacho hakikuonekana kuwa na shughuli nyingi, ndiyo makao ya jamii hiyo ya Wamakonde.

Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari maeneo ya Msambweni na Ramisi mtawalia lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho.

Ingawa wamekuwa wakisoma katika shule za Kenya na kupata elimu na ujuzi, safari yao imekuwa ikifikia darasa la nane au kidato cha nne, kwa kuwa baada ya hapo wamekuwa hawapati ajira kwa vile hawakuwa na vitambulisho vya kitaifa.

Katikati ya kijiji hiki kuna kibao chenye ujumbe unaosema hivi ‘Kama kumbukumbu ya kukumbuka jamii ya Wamakonde ambao walikuja Kenya kama wafanyikazi katika mashamba ya makonge. Jamii hii ilipewa rasmi uraia wa Kenya mwaka wa 2016,’ kinasema kibao hicho.

Hata hivyo, sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa mwaka jana Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa kwa kipindi cha pili cha uongozi.

Kuna mti kando ya kibao hicho ambao ulipandwa siku ambapo jamii hiyo iliidhinishwa na serikali kuwa mojawapo ya jamii za Kenya.

Mwenyekiti wa jamii ya Wamakonde, Kwale, Mzee Thomas Nguli aelezea masaibu ya jamii hiyo alipohojiwa na Taifa Leo katika kijiji cha Makongeni. Picha/ Kazungu Samuel

Matumaini

Kwa hivyo, baada ya kutambuliwa, kulikuwa na matumaini makubwa kwamba sasa Wamakonde wangenufaika na miradi na mambo mengine ambayo jirani zao Wadigo na Wakamba wamekuwa wakinufaika nayo.

Hata hivyo msemaji wa jamii hiyo, Bw Thomas Nguli, anasema kuwa Wamakonde hawajaona yale matunda waliyokuwa wakitarajia kupata, ambayo yalifaa kuandamana na wao kufahamika rasmi Wakenya.

“Tunashukuru kwamba kwa sasa sisi ni Wakenya lakini bado tuko na changamoto nyingi ambazo zinatuathiri kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano sasa hivi sisi hatuna mashamba wala ardhi. Hatuna hati miliki za kijiji hiki ambacho sisi tumepaita nyumbani kwa miaka mingi,” akasema Mzee Nguli.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa jamii hiyo kwa sasa iko na zaidi ya watu 1,000 ambao wamepata vitambulisho vya kitaifa.

“Tunamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kutuwezesha kupata uraia wa taifa hili, lakini hatuwezi kusema kwamba tumepata uhuru wetu wakati ambapo bado tunatatizika kumiliki ardhi. Hii ni shida kubwa,” akasema Mzee Nguli.

Wanawake wa jamii ya Wamakonde wakipiga soga nyumbani wakati Taifa Leo ilizuru kijiji cha Makongeni, kaunti ya Kwale. Picha/ Kazungu Samuel

Kutengwa

Alisema kuwa changamoto nyengine ambayo inawakabili ni kutengwa na majirani zao na hilo halijakuwa jambo jema kwao.

“Hapa wanatuita watoto wa Uhuru lakini tungeomba tu kama majirani zetu wanaweza kutambua kwamba sisi sasa ni Wakenya kama wao na wanafaa kututambua,” akasema Mzee Nguli.

Aliongeza kwamba jumla ya wakazi 1,875 kutoka kwa jamii hiyo tayari wamepata vitambulisho na hata wengine wakijisajili kama wapiga kura katika kaunti hiyo.

“Kutokana na mateso mengi tuliyopitia kama watu tusio na makao katika nchi hii ambayo tumeishi maisha yetu yote, tunadhani kwamba matakwa yetu sharti yaangaliwe kikamilifu na suluhisho la kudumu lipatikane,” akasema Bw Nguli.

Tutalala tu na amani ikiwa tutahakikishiwa kuajiriwa na serikali na kila aina ya jambo ambalo litatuwezesha kimaisha,” akaongeza.

Kitongoji cha Makongeni, Msambweni chenye watu wengi zaidi wa jamii ya Wamakonde waliohamia Kenya kutoka Mozambique. Picha/ Kazungu Samuel

Kupata kazi za serikali

Alisema kuwa kutambuliwa kwao hata hivyo kumewapatia faida kiasi kwani kuna watu sita miongoni wao ambao wamepata kazi baada ya kupewa uraia.

“Tuko na vijana wawili ambao wamejiunga na idara ya huduma za polisi na wane wameingia katika idara ya magereza. Zaidi ya vijana 200 sasa wameingia katika mradi wa huduma kwa taifa (NYS),” akasema Mzee Nguli.

Kulingana na Rose Boniface aliye na umri wa miaka 50, ilikuwa furaha kuu baada ya kupata kitambulsho tangu azaliwe. Hatua hiyo alisema ilimwezesha kushiriki katika uchaguzi wa wa mwaka 2017.

Alisema kabla ya kupata stakabadhi hiyo muhimu, maisha yalikuwa yamejaa usumbufu kwa vile hakuweza kupata huduma muhimu katika ofisi ya umma na vile vile alikuwa mara nyingi akisumbuliwa na polisi.

“Ilikuwa ni vigumu sana na tuliteseka sana miongoni mwetu ila sasa hali ni tofauti,” akasema.

Aliongeza kwamba mradi muhimu kama vile malipo kwa wazee walikuwa hawapati lakini sasa wamewekwa kaitka mpango huo.

Julieta Simenya, katibu wa kundi hilo alisema kuwa jamii bado inapitia changamoto kadhaa ambazo bila kuangaliwa vyema, zitatizika.

Katika eneo hili la Msambweni, Wamakonde huitwa watoto wa Uhuru na kutengwa na jamii zingine. Picha/ Kazungu Samuel

Kumiliki ardhi 

“Shida yetu kuu ilikuwa ni kupata uraia wa Kenya lakini pia tulikuwa na nyengine kama vile umiliki wa mashamba. Kwa sababu sasa tumepata vyeti vya kuzaliwa na kuwa raia kamili, serikali sasa haina budi kuangalia jinsi ambavyo itatusaidia tupate mashamba,” akasema Bi Simenya.

Jamii hiyo ina ukoo kutoka nchini Msumbuji na walikuja Kenya kupitia Tanzania Kusini ili kuja na kufanya kazi katika mashamba ya Makonge katika kaunti za Kwale na Kilifi.

Hata hivyo jamii hizo zilikumbana na hali ngumu baada ya kampuni za miwa na makonge kufilisika ambapo walijikuta wakiosa mahali pa kwenda.

Baada ya miaka mingi ya kutengwa, Bw Nguli alisema kuwa kwa kushirikiana na mashirika ya haki za kibinadamu, serikali iliwapatia uraia mwaka wa 2016.

“Tulianza safari hii mwaka wa 1995 na mimi sasa hata nikifa nitakuwa na furaha kwamba nilifanya kazi uyangu kubwa ya kufikisha watu wangu mahali walipotamani,” akasema Mzee Nguli.

 

Mashoga 6,000 hatarini kuambukizwa HIV kuliko makahaba

Na CHARLES LWANGA

KARIBU watu 6,000 wanofanya ushoga mjini Malindi wako katika hatari ya kuambukizwa na virusi vya Ukimwi kutokana na ongezeko la vijana wanaofanya biashara ya ushoga katika mji huo wa kitalii.

Mtaalamu wa maswala ya Ugonjwa wa Ukimwi katika hospitali ya Malindi, Dkt Godfrey Njoroge, alisema idadi hiyo imeongezeka kutokana na ukosefu wa ajira.

“Kulingana na utafiti, karibu watu 6,000 wanakisiwa kufanya mapenzi na wanaume wenzao na nambari hiyo huenda ikawa kubwa ikilinganishwa na idadi ya wanawake wanaofanya ukahaba mjini humu,” alisema.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, aliitaka serikali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali wagawe mipira za kondomu na mafuta kwa mashoga hao ili ipunguze usambazaji ukimwi mjini humo.

“Kama unavyofahamu, sehemu inayotumiwa haikuumbwa kwa ajili ya kufanyia mapenzi na kwa hivyo ni mahali ambapo virusi vya ukimwi vinaweza kuigilia kwa urahisi wakati wa mapenzi,” alisema.

Dkt Njoroge alisema wateja wao ni watu matajiri mjini Malindi na watalii wanaozuru mji huo kwa likizo.

Bi Evans Onyango, ambaye pia ni mtaalamu wa janga la Ukimwi hospitalini humo aliwasihi watu wanaofanya ushoga watembelee vituo vya afya ili wapime hali yao ya virusi vya HIV wapate madawa.

“Baadhi yao hawapendi kwenda hospitali kupimwa na ingekuwa vyema waje hospitali ili tuweze kuwasaidia,” aliongeza.

Kulingana na Shirika la kupambana na janga la Ukimwi nchini, uambukizaji wa Ukimwi katika Kaunti ya Kilifi iko katika asilimia 4.2, kumaanisha kuwa katika kila watu 100 wanne wao wanabeba virusi vya Ukimwi.

 

Shule mbioni kupaka mabasi rangi ya manjano muda ukiyoyoma

KALUME KAZUNGU na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

 • Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31
 • Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule
 • Katika maeneo mengiya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi
 • Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano

ZIKIWA zimesalia siku tano kabla ya kukamilika kwa makataa kwa shule zote nchini kupaka rangi magari ya kubeba wanafunzi, walimu wakuu na wamiliki wa shule wamo katika harakati za mwisho kutimiza agizo hilo.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31.

Dkt Matiang’i alisema kwamba agizo hilo linalingana na Sheria ya Trafiki, ambayo ilipitishwa na Bunge mnamo 2016.

Hatua hiyo inaonekana kuchangiwa na ongezeko la ajali za barabarani, ambapo iligunduliwa kuwa baadhi ya magari yaliyokuwa yamekodishwa kusafirisha abiria, yalikuwa ya shule.

Kulingana na sheria hiyo, jina la shule husika linapaswa kuandikwa kwa rangi nyeusi.

 

Rahisi kutambulika

Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule, na kwa hivyo hatua za haraka zinaweza kuchukuliwa iwapo madereva wa magari hayo watapatikana wakiendeleza mambo yanayoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

Sheria hiyo pia inayahitaji mabasi hayo kuwa na mikanda ya usalama katika viti vyake vyote.

“Shule zote zinapaswa kuhakikisha kwamba zimetimiza kanuni hizo kufikia Machi 30, kama inavyohitajika kisheria. Hatutakubali visingizio vyovyote kuhusu suala hili,” akasema waziri.

Sheria hiyo pia inasema kuwa mabasi hayo yanapaswa kuendeshwa kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa.

Mwendo wa kasi umekuwa mojawapo ya mambo ambayo yamechangia ongezeko la ajali za barabarani. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, kumekuwa na ajali kadha ambazo zimehusisha mabasi ya shule katika maeneo ya Nyanza na Kisii.

Kanuni nyingine ni kwamba yataruhusiwa kuhudumu kati ya saa 12 asubuhi na jioni pekee, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Basi la Shule ya Msingi ya Twfiq Muslim mjini Malindi. Picha/ Hisani

Kuiga mataifa ya Magharibi

Kulingana na wadadisi wa masuala ya elimu, Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano.

Katika kaunti ya Lamu, shule zote za mzingi na za upili zinazomiliki mabasi zimetimiza amri hiyo.

Akizungumza Jumapili na Taifa Leo, Afisa wa Elimu wa Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, Bw Josphat Ngumi, alisema ni shule mbili pekee za upili – ile ya wavulana ya Mpeketoni na shule ya sekondari ya Mokowe ambazo zinamiliki mabasi kati ya jumla ya shule 26 za umma zilizoko Lamu.

Alisema shule ya kibinafsi ya Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ndiyo shule ya msingi ya kipekee ambayo inamiliki basi kati ya shule 104 zilizoko eneo hilo.

Kwa mujibu wa Bw Ngumi, shule zote tatu kwa sasa zimehakikisha mabasi yao yamepakwa rangi ya manjano kama ilivyoamriwa.

“Hapa Lamu kuna shule mbili pekee za upili zinazomiliki mabasi ambazo ni Mpeketoni na Mokowe. Pia kuna shule moja pekee ya msingi ya kibinafsi ambayo ni Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ambayo ina miliki basi. Shule zote tatu zimetii sheria kwa kuhakikisha magari yao yanapakwa rangi ya manjano,” akasema Bw Ngumi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya wavulana ya Mpeketoni, Bw Macharia Kagutha alisema basi lao lilipakwa rangi takriban wiki tatu zilizopita.

 

Gharama ya kupaka rangi

“Tulisafirisha basi letu hadi Mombasa ambako lilipakwa rangi na kampuni ya Assosiated Motors. Tulitumia Sh127,000 katika kutekelezewa huduma hiyo. Kwa sasa liko sawa,” akasema Bw Kagutha.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mokowe, Bw Thaddeus Mogute, alisema shughuli ya kulipaka rangi gari hilo tayari ishaanza na itakamilika juma hili.

“Tunalenga kutumia kati ya Sh 130,000 na Sh 150,000 ili kupaka rangi ya manjano basi letu na pia kulikarabati. Tayari niko Mombasa na shughuli itakuwa imekamilika kufikia mwishoni mwa wiki hii,” akasema Bw Mogute.

Katika maeneo mengine ya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi ya kupaka rangi hiyo ya manjano kwenye magari yaliyopelekwa katika gereji zao.

Kulingana na kanuni zilizotolewa na serikali, hata matatu na magari ya kibinafsi yatakayotumiwa kuwabeba wanafunzi wa shule, yatahitajika kuwa na rangi hiyo ya manjano.

Mkutano wapangwa kuunganisha viongozi wa Pwani

Waziri msaidizi wa Wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro. Picha/ Maktaba

NaMOHAMED AHMED

VIONGOZI wa Pwani wanapanga kukutana kujadili masuala yatakayowaunganisha, Waziri msaidizi wa wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro amesema.

Bw Mung’aro alisema kuwa mwezi ujao viongozi wote wa kutoka pwani watakutana katika kaunti ya Kwale ili kujua mustakabali wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa mazishi ya mke wa aliyekuwa waziri wa utalii marehemu Karisa Maitha, Bi Alice Maitha mnamo Jumamosi, Bw Mung’aro alisema kuwa mkutano huo unatazamiwa kuunganisha viongozi hao kwa ajili ya matakwa ya mpwani.

“Tusifurahie kukutana kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Inafaa sisi wenyewe kama viongozi tusalimiane ndio tujue kuwa kweli tumeungana. Tunafaa kufurahia pia tukiona Mung’aro, Joho na Kingi wanasalimiana,” akasema Bw Mung’aro.

Bw Mung’aro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Kilifi Kaskazini alizungumzia muungano huo baada ya viongozi wa kaunti hiyo ya Kilifi na Mombasa kueleza kuwa kuna haja ya kuungana kama Wapwani.

Naibu gavana wa Mombasa William Kingi alisema kuwa kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga ni “fursa nzuri kwa Wakenya na kwa Wapwani”.

“Inapaswa tutumie fursa hii kuendesha mambo yetu mbele. Sisi kama Wapwani tuna kila sababu ya kutumia nafasi hii kuona tunaungana ili tuweze kutambulika nafasi yetu kitaifa,” akasema Dkt Kingi.

Naibu gavana wa Kilifi Gideon Saburi alisema kuna haja ya wakazi wa Pwani na viongozi kuwa kitu kimoja ili waweze kutatua matatizo yao na yaweze kusikizwa katika mazungumzo ya kitaifa ambayo yanapaswa kufanyika kufuatia kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana alisema kuwa kuna haja ya kuungana kwa Wapwani kwa sababu ya maendeleo ya eneo hilo.

“Sisi tutafuata hatua zile zile kama za Baba za kuunganisha Wakenya. Na sisi kama Wapwani lazima tushikane ili tulete maendeleo kwa watu na bila hivyo hatuwezi faidika,” akasema Bw Katana.

Mbunge wa eneo bunge la Kilifi Kusini Ken Chonga alisema kuwa mazungumzo ya kutaka kuungana kwa Wapwani yamekuwa kwa muda na kuongeza kuwa hilo litafanyika wakati Wapwani wataunda chama chao.

 

Jumapili ya Mitende ilivyoadhimishwa nchini

PETER MBURU na BRIAN OCHARO

Waumini wa kanisa Katoliki Jumapili walifurika kwenye barabara kote nchini wakibeba matawi ya mitende kuadhimisha siku ya ‘Jumapili ya mitende’ na mwanzo halisi wa ‘wiki takatifu’.

Mjini Nakuru, mamia ya waumini hao, wakiongozwa na askofu Maurice Muhatia wa dayosia ya Nakuru walitembea mjini humo kwa saa chache, kabla ya kufululiza hadi kwenye kanisa la Christ the King kwa ibada.

Sherehe hiyo iliandaliwa kukumbuka tukio la kishujaa yesu kristo kuingia mji wa Yerusalemu kwa unyenyekevu kabla yake kuuliwa, katika Biblia takatifu.

Matawi yaliwakilisha amani na ukaribisho mwema aliopokea Yesu alipoingia mji wa Yerusalemu na ushindi wake.

Kutembea kwa miguu nako kuliashiria unyenyekevu, hata wenye pesa na magari wakijitolea kutembea kwa mapenzi ya wokovu.

Wakati wa misa hiyo, askofu Muhatia aliwataka waumini kumwiga Yesu Kristo kwa kuwa na vitendo vya unyenyekevu, mbali na kuwasaidia wasiojiweza.

“Kwa kuwasaidia wale waliokosa katika jamii, tutakuwa tunatimiza mapenzi ya Mungu kwa kutoa kafara ya maisha ili waokoe ulimwengu,” akasema.

Mjini Mombasa, Padri Marsallius Okello wa Kanisa la Holy Ghost, aliwaomba Wakenya kuombea amani.

“Tumeanza kuona matokeo ya sala ambazo wakenya wamekuwa wakifanya  tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na tunatarajia kuwa Kenya itapata amani ambayo tumekuwa tunayotamani na kuomba,” alisema.

Padri Okello aliwaomba Wakenya kuwapa  Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga muda wa kufanya mazungumzo ili kupata suluhisho la muda mrefu ambalo litaleta utulivu wa kisiasa nchini.

Aliwahimiza  wanasiasa wote na viongozi wa kidini nchini kuhubiri amani, umoja na upatanisho ili nchi iimarishe a ki uchumi.

Kulingana na tamaduni za dhehebu la Katoliki, matawi hayo yatachomwa na jivu yake kuhifadhiwa kisha itumiwe kuighinisha siku ya jumatano ya jivu, mwaka ujao.
Waumini nao wanatarajiwa kujifungia vitu wanavyopenda kama chakula na vingine, kama mbinu ya kumtolea mungu kafara.

 

Wanasiasa wataka Jubilee iwe macho Raila asije akazima ndoto ya Ruto 2022

GAVANA wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

BAADHI ya wanasiasa wa Jubilee sasa wamesema kuwa hawamwamini kinara wa NASA Raila Odinga kwani huenda akavuruga mpango wa Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.

Wakiongozwa na Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu ‘Babayao’, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na Mwakilishi Mwanamke wa Nyeri Rahab Mukami, wanasiasa hao walisema japo wamefurahishwa na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kukubali kufanya kazi pamoja, kuna haja kwa Jubilee kuwa waangalifu.

“Tumefurahishwa na viongozi hao wawili kukubali kufanya kazi pamoja lakini Bw Odinga haaminiki,” akasema Bw Waititu.

“Naibu wa Rais, Bw Raila akikuambia ufumbe macho muombe usifunge macho kwani anaweza kutoweka na kukimbia na kila kitu,” akasema Bw Waititu. Bw Ichungwa alimtaka Bw Odinga kuwa mwaminifu na asiwe na ‘mguu mmoja nje’.

Bi Mukami alimtaka Bw Odinga kushirikisha vigogo wenzake wa Nasa katika meza ya mazungumzo na Rais Kenyatta ikiwa kweli ana nia ya kuunganisha Wakenya wote.

Lakini Bw Ruto ambaye alikuwepo wakati wa ibada katika kanisa la PCEA mtaani Runda, Nairobi alikwepa na madai ya viongozi hao huku akisema kuwa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unalenga kuleta amani ambayo ni muhimu kwa maendeleo.

“Ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga si wa manufaa ya kibinafsi bali ni wa kuhakikisha Kenya inapata amani hivyo kupisha maendeleo,” akasema Bw Ruto.

Uingereza yawapa onyo raia wake kuhusu shambulio la kigaidi Kenya

Na STELLA CHERONO

UINGEREZA imetoa tahadhari ya usafiri kwa raia wake wanaoishi ama wanaotembelea Kenya dhidi ya tishio la ugaidi na utekajinyara.

Aidha, taifa hilo liliwashauri kuwa waangalifu dhidi ya mashambulio ya kundi la kigaidi la Al Shabaab, kwani huenda wakalenga baadhi ya maeneo muhimu kama hoteli, vilabu, maduka ya jumla, na maeneo ya Pwani kama fuo za bahari.

“Mashambulio hayo huenda yakawa katika maeneo ya kuabudu; kama vile makanisa na misikiti, kwani yamekuwa yakilengwa. Mnapaswa kuwa na tahadhari kubwa,” ikasema taarifa.

Tahadhari hiyo inajiri baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet kutangaza kwamba vikosi vya usalama vimefanikiwa kuzima shambulio kubwa la kigaidi ambalo lilipangiwa kutekelezwa jijini Nairobi.

Kufikia sasa, zaidi ya watu 12 wamekamatwa kwa kuhusishwa na shambulio hilo ambapo wamefikishwa mahakamani lilifanyika baada gari moja lililojaa vilipuzi kunaswa katika eneo Merti, Isiolo.

 

Wazee wateta kunyimwa hela kwa sababu ya vidole chakavu

Na FADHILI FREDRICK

BAADHI ya wazee wanaofaidika kutokana na mpango wa pesa kila mwezi kupitia mpango maalum wa serikali kutoka kaunti ya Kwale wamelalamikia kukosa fedha hizo kutokana na uchakavu wa vidole vyao unaosababibishwa na madhara ya kuzeeka.

Wazee hao wamechoshwa na hali hiyo na wametoa wito kwa mawakala wa benki waliopewa kandarasi ya kuwapa pesa kutafuta mbinu mbadala ili wapate pesa hizo bila kuhangaishwa.

Walisema hayo siku ya Jumamosi wakati wa kuwasilisha malalamishi yao kwa Kamati ya Bunge la kitaifa la Leba na Ustawi wa Jamii.

Kamati hiyo iko katika ziara ya kaunti za Pwani ili kutathimini maendeleo ya mpango wa uhamisho wa fedha wa Inua Jamii.

Katibu Mkuu wa Ulinzi wa Jamii, Bi Susan Mochache, alisema kwamba malipo ya wazee yatafanywa kupitia akaunti za benki za walengwa kutoka Oktoba mwaka huu ili kukabili changamoto zinazojitokeza katika mpango huo.

“Serikali bado inafanya kazi ya kuboresha mpango huo ili kuhakikisha kuwa matokeo yake yanafaa kwa watu wake,” alisema.

Mwenyekiti wa kamati hio Bw Ali Wario na pia Mbunge wa Bura alisema kuwa watajumuisha ripoti kulingana na matokeo yao kutoka ziara ya majimbo ya Pwani kwa lengo la kuhakikisha mpango huo umeboreshwa ili kukidhi mahitaji ya makundi yaliyotekelezwa katika jamii.

“Madhumuni ya ziara hii ni kuthathimini maendeleo na changamoto zinazotokana na mradi huo kwa wazee ili kutafuta mbinu za kuuboresha,” alisema Bw Wario.

Wazee hao walieleza faida wanazozipata kupitia mpango huo wa kijamii na kuipongeza serikali kwa kuwajali.

Hata hivyo, waliiomba serikali kuzingatia kuongeza fedha kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000 wakisema gharama ya maisha imepanda.

“Tunathamini msaada wa serikali lakini tunahimiza kufikiria kulipa zaidi kwa sababu kile tunachopata sasa ni kidogo sana ili kukidhi mahitaji yetu yote,” alisema Bw Salim Mwariko wa miaka 72.

 

Mapuuza ya sheria huleta ufukara, aonya Maraga

Na BENSON MATHEKA

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga amesema kwamba kupuuzwa kwa utawala wa sheria na ufisadi barani Afrika kumechangia umaskini na kulemaza maendeleo.

Kwenye hotuba yake katika kongamano kuhusu maendeleo barani Afrika lililoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Harvard, Amerika, Bw Maraga alisema ni vigumu kutenganisha utawala wa sheria na maendeleo ya dhati.

“Utawala wa sheria na maendeleo vimeunganishwa na vinatiliana nguvu. Utawala wa sheria unatoa mazingira bora ya kushamiri kwa vitendo vyote vya binadamu na ni nguzo ambayo ustawi hujengwa,” alisema Bw Maraga.

“Hata hivyo, katika nyanja ya maendeleo Afrika, haki na utawala wa sheria havichukuliwi kwa umakinifu unaofaa,” aliongeza Bw Maraga.

Alisema kwamba ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa zimetambua kuwa utawala wa sheria na maendeleo haviwezi kutenganishwa.

Bw Maraga alisema kwamba kuimarishwa kwa utawala wa sheria katika viwango vya kitaifa na kimataifa ni muhimu kwa ukuaji na udumishaji wa uchumi, kupiga vita umaskini na njaa.

“Imetambuliwa kuwa utawala wa sheria huleta haki za binadamu ikiwemo haki ya maendeleo zote ambazo huwa zinaimarisha utawala wa kisheria,” alisema.

Alisema utawala wa sheria ni nguzo ya demokrasia. “Umehusishwa na upunguzaji wa mamlaka na nguvu za serikali, uhuru wa mahakama na usawa mbele ya sheria, kulinda haki za kimsingi ziwe za kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na haki ya mali,” alieleza.

Bw Maraga aliyealikwa kutoa hotuba kuu kwenye kongamano hilo alisema utawala wa sheria unahakikisha kwamba haki za binadamu zinapatiwa uhai kama njia moja ya kupiga vita ubaguzi, kutengwa kwa maeneo na jamii ambazo ni chanzo cha umasikini.

Alisema kwa kuelewa vibaya maana ya utawala wa sheria, sheria hutumiwa kukandamiza wananchi. Bw Maraga alisema Kenya imepiga hatua kubwa chini ya katiba mpya iliyopitishwa 2010 ambayo alisema ilisisitiza utawala wa sheria na jukumu lake katika maendeleo.

Alisema mahakama barani Afrika zinafaa kusaidia bara kufikia utawa bora na kutekeleza haki za kiuchumi na kijami.

“Mahakama ni asasi zinazotoa mchango muhimu katika utawala na hili ndilo jukumu ambazo zinafaa kutekeleza kulingana na sheria. Nchini Kenya, ugatuzi, fedha za umma, masuala ya jinsia zina jukumu muhimu katika kuimarisha utawala bora,” alisema.

Bw Maraga alisema ufisadi na kutekwa kwa asasi muhimu na wanasiasa na kumelemeza maendeleo.

“Ufisadi na vitendo vya ufisadi huendelezwa na wale ambao hawaheshimu sheria na kwa hivyo kupalilia umaskini. Kenya mhasibu mkuu wa serikali ameripoti kuwa thuluthi tatu ya bajeti ya taifa hupotea kupitia ufisadi,” alisema Bw Maraga.

 

 

Sitaki kiti chenu, nitawapa dawa yenu, Weta aiambia ODM

Na WYCLIFF KIPSANG

Kwa ufupi:

 • Bw Wetang’ula asema hatahudhuria kongamano la maseneta la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha NASA
 • Amshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi
 • Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha -Wetang’ula
 • BwMudavadi asema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

MPASUKO katika muungano wa NASA ulipanuka wazi Jumapili baada ya Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula kukata tamaa ya kupigania kiti cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti na kutangaza kwamba hatapigania tena wadhifa huo.

Bw Wetangula alisema hatahudhuria kongamano lililopangwa la maseneta wa NASA la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha muungano huo.

“Ni nini cha kujadili (katika kongamano hilo)? Sitahudhuria. Nikienda itakuwa kama kondoo kujipeleka katika mahakama ya fisi,” alisema Bw Wetangula.

“Hata nikipewa kiti hicho sitakichukua, wakae nacho; asante. Sasa mchezo uanze; tutawapa dawa yao polepole lakini hatari sana,” aliongeza kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya.

Alisisitiza kuwa hakuomba kiti hicho cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti lakini akiwa mmoja wa vinara wa NASA, uamuzi wa kumpa wadhifa huo ulinuiwa kutia nguvu shughuli katika bunge hilo.

Bw Wetangula alimshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi.

Wiki iliyopita, maseneta wa ODM walimng’oa Bw Wetangula katika wadhifa wa Kiongozi wa Wachache na kumteua Seneta wa Siaya James Orengo kuchukua wadhifa huo. Bw Wetangula alisema Ford Kenya iliungana na ODM kwenye uchaguzi wa 2013 sawa na 2017.

“Tuliweka mali na nguvu zetu kwa suala hili lakini kama jamii ya Mulembe hakuna la kutufaidi,” Bw Wetangula alisema alipohutubia wanahabari mjini Bungoma.

“Imesemekana ninapigwa vita. Ninataka kutangaza hapa na sasa kwamba nina amani katika moyo wangu,” alisema Bw Wetangula.  Alitaja mkutano wa vinara wa NASA na maseneta wa muungano huo Alhamisi kama duka la kelele.

“Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa katika mkutano huo yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha,” alisema Bw Wetangula.

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa chama cha ANC ambaye ni mmoja wa vinara wa NASA Musalia Mudavadi, Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na aliyekuwa seneta wa Kakamega, Bonnie Khalwale.

Wengine walikuwa wabunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Eseli Simiyu (Tongaren), Ayub Savula (Lugari).

Bw Mudavadi alikosoa mazungumzo kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wa kuwatenga vinara wenza wa NASA.

“Hatupingi mazungumzo lakini tunataka yahusishe watu wote. Hakuna aliye na haki ya kushiriki mazungumzo. Canaan yetu si harambee house, bado tunaendelea mbele, “ alisema Bw Mudavadi.

Hata hivyo, akiongea katika kanisa la CITAM, mjini Rongai Jumapili, Bw Odinga alisema mwafaka wake na Rais Kenyatta ni wa kuunganisha Wakenya.

Bw Mudavadi alisema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Maeneo mengine yamefanya hivyo. Sioni sababu yetu kukosa kuungana hapa. Sisi kama viongozi wa Magharibi tunamuunga Bw Wetangula,” alisema Bw Mudavadi.

Alisema walipoungana katika NASA lengo lao lilikuwa mageuzi, kuimarisha uhuru wa asasi za kikatiba na mageuzi ya polisi. “ Tunasikitika kusema kwamba ndoto ya NASA haijatimizwa, nchi yetu inakabiliwa na changamoto tele ikiwa ni pamoja na vijana kukosa ajira,” alisema.

 

Shujaa watawazwa washindi wa Victoria Falls Sevens Zimbabwe

Na GEOFFREY ANENE

SHUJAA ya Kenya imeibuka mshindi wa makala ya pili ya raga za wachezaji saba kila upande za Victoria Falls Sevens nchini Zimbabwe, Jumapili.

Kenya ilivuna taji kwa kuzaba wenyeji na mabingwa watetezi Zambezi Cheetahs 10-5 katika fainali ngumu mjini Victoria Falls.

Ushindi huu muhimu ulipatikana kupitia miguso ya wachezaji wapya kikosini Levy Amunga na Brian Wahinya katika kipindi cha kwanza.

Ingawa Zimbabwe ilianza kipindi cha pili kwa kishindo kwa kupachika mguso kupitia Rian O’Neill, ufufuo wake ulizimwa na ulinzi imara kutoka kwa Shujaa.

Kenya, ambayo haikusafiri na kocha mkuu Innocent Simiyu, ililemea mabingwa wa Afrika Uganda 17-10 katika nusu-fainali. Ilihitaji mguso katika sekunde ya mwisho kutoka kwa Samuel Ng’ethe kuingia fainali.

Shujaa, ambayo ilishinda taji la Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015, iliongoza 10-0 wakati wa mapumziko.

Hata hivyo, Uganda ya kocha Mkenya Tolbert Onyango, ambayo ni bingwa wa Afrika mwaka 2016 na 2017, iliziba mwanya huo kupitia mguso miwili bila mikwaju kutoka kwa Solomon Okia 10-10 kabla ya Ng’ethe kupata mguso wa ushindi na mkwaju wake.

Katika mechi ya robo-fainali, Kenya ilibwaga Spartans ya Botswana 43-0 kupitia miguso ya Mark Kwemoi, Frank Wanyama, Bush Mwale, Derrick Mayar, Augustine Lugonzo na Ian Minjire.

Shujaa ilikuwa alama 19-0 juu wakati wa mapumziko kupitia miguso ya Kwemoi na Wanyama kabla ya Mwale, Mayar, Lugonzo na Minjire kuongeza alama zaidi katika kipindi cha pili.

Kenya ilifuzu kushiriki robo-fainali baada ya kupepeta False Bay (Afrika Kusini) 17-0, Zambia B 31-0, Lesotho 26-0 na Zambezi Cheetahs ya Zimbabwe 14-12 katika mechi za makundi Jumamosi.

Shujaa, Uganda na Zimbabwe zilitumia Victoria Falls Sevens kujiandaa kwa mashindano ya dunia ya Hong Kong Sevens yatakayofanyika Aprili 6-8. Kenya inashiriki Raga za Dunia msimu 2017-2018 nazo Zimbabwe na Uganda zitakuwa zikipigania tiketi ya kuingia Raga za Dunia msimu 2018-2019.

Timu za Kenya, Uganda na Zambia pia zinajitayarisha kwa mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili 13-15 nchini Australia.

Matokeo (Machi 25)

Fainali

Kenya 10-5 Zambezi Cheetahs (Zimbabwe)

Nusu-fainali

Shujaa (Kenya) 17-10 Uganda

Zambezi Cheetahs (Zimbabwe) 19-0 Zambia A

Robo-fainali

Shujaa (Kenya) 43-0 Spartans (Botswana), Zambezi Cheetahs (Zimbabwe) 31-0 Zambezi Steelers (Zimbabwe), False Bay (Afrika Kusini) 14-19 Uganda; Spartans (Botswana) 14-33 False Bay (Afrika Kusini), Goshawks (Zimbabwe) 21-17 Zambezi Steelers (Zimbabwe). Mechi ya kuorodhesha nambari tisa na 10 – Zambia B 28-7 Lesotho.

BI TAIFA MACHI 08, 2018

MAUREEN Wairimu, 22, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anaenzi kujipodoa, kutazama filamu na kucheza densi. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 07, 2018

MARY Mueni, 21, ni mwanamitindo wa jijini. Anapenda kucheza densi, kutazama filamu na kusoma vitabu. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 06, 2018

LYDIA Wairimu, 20, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anaenzi kusikiliza muziki, kutazama video na kuimba. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 05, 2018

LYDIA Alila, 21, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Uraibu wake ni kusoma vitabu, kuchakura intaneti na kushiriki mashindano ya urembo. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 04, 2018

LISA Mutia, 21, anatupambia tovuti yetu mwezi huu. Uraibu wake ni kushirika maonyesho ya urembo, kucheza densi na kujipodoa. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 03, 2018

LEAH Wanjiku, 22, ni mpenzi wa uanamitindo. Anapenda kusoma vitabu, kutalii na kutazama filamu. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA MACHI 2, 2018

IRENE Wanjiru, 20, ni mwanamitindo mjini Thika. Uraibu wake ni kucheza gitaa, kucheza densi na kusikiliza muziki. Picha/ Anthony Omuya