BI TAIFA MACHI MOSI, 2018

DEBBIE Kwamboka, 22, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anaenzi kutalii, kuendesha baiskeli na kuogelea. Picha/ Anthony Omuya

Starlets waumiza She-polopolo 3-0 kwao nyumbani

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets ya Kenya imetuma onyo la mapema kwa wapinzani wake wa raundi ya kwanza ya mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2018 kwa kupepeta wenyeji Zambia 3-0 katika mechi ya kirafiki uwanjani Arthur Davies mjini Kitwe, Jumapili.

Kenya, ambayo itaalika Uganda mjini Machakos mnamo Aprili 4 na kupiga mechi ya marudiano Aprili 8 ugenini, imezima She-polopolo kupitia mabao ya Mwanahalima ‘Dogo’ Adam na Corazone Aquino.

Mvamizi hodari Adam aliipa Starlets uongozi dakika ya 18 kabla ya kiungo Aquino kuzamisha chombo cha Zambia kabisa na mabao mawili dakika 10 za mwisho.

Ni kisasi kitamu dhidi ya Zambia kwa sababu warembo wa kocha David Ouma walilazwa 4-2 kwa njia ya penalti katika mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba kwenye mashindano ya Cosafa mwaka 2017.

Starlets ilitumia mchuano huu kujipiga msasa kabla ya kulimana na Uganda.

Ikibandua Uganda nje, Kenya itamenyana na mabingwa wa Afrika mwaka 2008 na 2012 Equatorial Guinea katika raundi ya pili Juni 4 na Juni 9. Mshindi wa raundi ya pili atajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika litakalofanyika Novemba 17 hadi Desemba 1 katika miji ya Accra na Cape Coast.

Starlets ilipepeta Uganda 4-0 mjini Jinja zilipokutana katika mechi ya makundi ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Septemba mwaka 2016.

Esse Akida, ambaye alifunga mabao mawili katika mechi hiyo, alikosa ziara ya Zambia kwa sababu ya jeraha, lakini Ouma ni mwingi wa matumaini kwamba mshambuliaji huyu atapata afueni kabla ya kukutana na Uganda.

Kenya ilishiriki Kombe la Afrika kwa mara yake ya kwanza kabisa mwaka 2016 nchini Cameroon.

Ilijikatia tiketi ya kuelekea Cameroon baada ya mpinzani wake wa raundi ya kwanza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiondoa. Ililemea Algeria katika raundi ya pili kupitia mabao ya ugenini baada ya kutoka 2-2 nchini Algeria na 1-1 jijini Nairobi.

Ikiwa itapiga Uganda katika raundi ya kwanza, Starlets itavaana na mabingwa wa zamani wa Afrika Equatorial Guinea katika raundi ya pili Juni. Mshindi wa raundi ya pili ataingia Kombe la Afrika litakalofanyika Novemba 17 hadi Desemba 1 katika miji ya Accra na Cape Coast.

Vikosi: 

Kenya – Wachezaji 11 wa kwanza – Pauline Atieno, Pauline Musungu, Wincate Kaari, Lilian Adera, Dorcas Shikobe, Caroline Omondi, Cheris Avilia, Cynthia Shilwatso, Neddy Atieno, Wendy Ann Achieng na Mwanahalima Adam; Wachezaji wa akiba – Maureen Shimuli, Vivian Nasaka, Caroline Kiget, Vivian Corazone Aquino, Mercy Achieng, Doris Anyango na Sheryl Angachi.

Zambia – Wachezaji 11 wa kwanza – Catherine Musonda, Mary Mwakapila, Theresa Chewe, Misozi Zulu, Rhoda Chileshe, Hellen Chanda, Margaret Belemu, Lweendo Chisamu, Jacqueline Nkole, Jane Chalwe na Racheal Kundananji

Pasta aalika mganga atibu wanawe walevi

Na CORNELIUS MUTISYA

NZAIKONI, MACHAKOS

Pasta mmoja maarufu eneo hili, aliwaacha majirani wakiwa wameduwaa alipomualika mganga nyumbani kwake ili awagange wanawe waliokuwa wamezama katika ulevi wa kupindukia.

Kulingana na mpambe wetu, pasta alikuwa maarufu kwa mahuburi yake yaliyowagusa wengi wakabadili mienendo yao. Hata hivyo, licha ya pasta huyo kusifika  mitaani, wanawe  wawili walikuwa wakipenda pombe kupindukia.

Walikuwa wakirauka  asubuhi na mapema kila siku kwenda kubugia mvinyo na kushinda kwa mama pima mchana kutwa.

Inasemekana kila siku, walikuwa wakirejea nyumbani usiku wa manane wakibwabwaja maneno ya kilevi na kuwatusi majirani.

“Uraibu wa pombe wa wanawe ulimkera mno pasta huyo. Alishindwa hatua ambazo angewachukulia wanawe ili wakomeshe tabia ya ulevi huo wa chakari kwa sababu walikuwa wakimwaibisha,’’ alisema mdaku wetu.

Inasemekana kwamba pasta huyo alijitahidi kiasi cha uwezo wake kuwaombea wanawe wakomeshe ulevi bila mafanikio mpaka akakata tamaa.

Alipowaza na kuwazua, aliona ni heri atundike wokovu kando kwa muda ili atafute suluhisho la kudumu. Alikata kauli kutafuta huduma za mganga amtatulie masaibu yaliyowasibu wanawe.

“Pasta alimualika mganga maarufu kutoka kaunti jirani ili amsaidie kumaliza ulevi wa wanawe. Aliwaacha waumini, majirani na marafiki vinywa wazi kwa sababu kwao alikuwa mfano wa kuigwa,’’ alisema mdaku wetu.

Tunaarifiwa kwamba mganga alitekeleza vimbwanga vyake na kuondoka. Wakazi wanasubiri kuona iwapo vijana hao wataacha pombe.

“Pasta ameacha kuhubiri mitaani kama ilivyokuwa kawaida yake. Wakazi wanashuku huenda akaacha huduma kabisa baada ya kuonyesha imani tofauti na anayohubiri,’’ alisema mdaku wetu.

…WAZO BONZO…

JAMVI: Baada ya kumnasa Jumwa, Ruto sasa alenga kumkumbatia Sultan wa Pwani

Na WYCLIFFE MUIA

MUAFAKA wa kusitisha uhasama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga unaendelea kuwaleta pamoja mahasimu wa kisiasa kwa matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Umoja wa viongozi hao wawili umempa Naibu Rais William Ruto mwanya wa kunyemelea ngome za upinzani ili kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wandani wa Bw Odinga.

Na sasa, Bw Ruto anadaiwa kumlenga Gavana wa Mombasa Hassan Joho anayechukukuliwa kuwa ‘Sultan’ wa siasa za Pwani.

Washirika wa naibu rais walidokeza kuwa Waziri wa Utalii Najib Balala ametumwa na Bw Ruto kuwaunganisha kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Siku chache baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kukutana, Bw Ruto aliekea Pwani kwa ziara ya siku tatu ambapo alilakiwa kwa heshima na Wabunge wa chama cha ODM.

Baadhi ya wale waliomlaki Bw Ruto walidokezea Jamvi la Siasa kuwa naibu rais analenga kushirikiana na Bw Joho kuelekea siasa za 2022.

“Wakati Ruto alizuru Pwani, Joho alikuwa amesafiri nje ya nchi lakini naibu rais alitutuma tuongee na yeye ili tujipange kuhusu 2022,”mbunge mmoja wa Pwani asiyetaka kutajwa alisema.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema Joho amejikuza kisiasa kiasi cha kumnyima usingizi Bw Ruto kuhusu ndoto yake ya 2022.

 

Joho alivyong’aa

Mhadhiri wa chuo cha Pwani, Hassan Mwakimako anaamini kukosekana kwa Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses  Wetang’ula katika bustani ya Uhuru wakati Bw Odinga alikula kiapo mnamo Januari 31, kulikuwa kilele cha Joho kung’aa kisiasa.

“Kile Joho alifanya siku hiyo ni sifa wapigakura wengi hutafuta kwa kiongozi. Joho aliwapiku vinara wenza wa NASA na huenda akawa na umuhimu mkubwa wa kisiasa kuwaliko kuelekea 2022,”alisema Prof Mwakimako.

Kwa mujibu wa  Maimuna Mwidau, mchanganuzi wa siasa za Pwani, utiifu wa Joho kwa Bw Odinga umepandisha hadhi yake ya kisiasa na kando na kuwa ‘Sultan’ wa Pwani, huenda akadhibiti kura za Nyanza.

Ili kudhihirisha mandhari ya kisiasa eneo la Pwani ni tulivu kwa Bw Ruto kufanya urafiki na wapinzani wake, mwenyekiti wa wabunge wa Pwani  Suleiman Dori alifichua kuwa Bw Odinga aliwashauri wakomeshe kampeni za kujitenga hata kabla ya kukutana na Rais Kenyatta mnamo Machi 9.

“Alikuwa ashatuambia tuunge ajenda ya serikali na hivyo ndio tunafanya. Kama chama, ni sharti tufuate kile kinara wetu anatuambia,”alisema Bw Dori.

Zaidi ya wabunge 10 wa ODM walimlaki Bw Ruto katika ziara yake ya kaunti za Mombasa, Kwale na Taita Taveta  huku wengine wakiahidi kumuunga mkono ifikiapo 2022.

 

Kuzamisha ndoto ya Joho

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir aliliambia gazeti moja la humu nchini kuwa, kuna juhudi zinaendelea kumshawishi Bw Ruto apangue ndoto yake ya kuwa rais 2022 na badala yake amuunge mkono Joho.

Bw Nassir ambaye ni mwandani mkubwa wa gavana huyo alisema hatua hiyo itahakikisha Ruto amekumbatiwa kikamilifu na Wapwani.
“Msimamo wetu ni wazi. Tunamtaka Ruto amuunge Joho mkono ili awanie urais 2022,” akasema.

Bw Nassir alisema wabunge wa Pwani walijadiliana na Bw Ruto kuhusu mapendekezo hayo kabla ya kuambatana naye katika ziara yake Pwani.

Hata hivyo, msemaji wa naibu rais, David Mugonyi, alipuuzilia mbali kuwepo na mipango kama hiyo.

Ili kuhakikisha ushirikiano kati ya rais na Bw Odinga una maana kwa watu wa Pwani, wabunge wa ODM walisema sharti Bw Joho ashirikishwe.

“Karibu Pwani Bw Ruto, lakini ni vyema tukufahamishe kuwa eneo hili lina kiongozi wake,” alisema Asha Hussein alipomlaki naibu rais Ijumaa iliyopita, eneo la Jomvu Kuu-Rabai .

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alijipata pabaya alipomuidhinisha Ruto kuwania urais 2022, lakini alijitetea kuwa huo ulikuwa uamuzi wake binafsi.

 

Asubiri 2022

Mbunge wa Kaloleni  Paul Katana alidinda kumuidhinisha Ruto  na badala yake akamshauri angoje hadi 2022. Haya yanajiri huku ikifichuka kuwa Bw Joho kwa ushirikiano na mwenzake wa Nairobi walichangia pakubwa kuja pamoja kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Mbunge wa  Makadara George Aladwa alinukuliwa akisema kuwa, magavana hao wawili walikutana siku chache kabla ya rais na kiongozi wa ODM kufanya mazungumzo.

“Nilifanya mkutano na Sonko afisini mwake Machi 8, kabla ya rais na Raila kukutana na akanifichulia kuwa vinara hao wawili wako tayari kufanya kazi pamoja,”alisema Bw Aladwa.

Sonko anaonekana kuwa mwandani wa rais huku Joho ambaye ni naibu kinara wa chama cha ODM, akionekana kuwa mtiifu kwa Bw Odinga.

Inadaiwa Joho anaendela kumshawishi mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kupuuzilia mbali juhudi zake za kuanzisha chama cha Pwani na badala yake amuunge mkono katika chama cha ODM.

Eneo la Pwani lenye takriban wapigakura 1.7 ni ngome ya NASA na litakuwa muhimu sana katika siasa za 2022.

JAMVI: ‘Jenerali’ kutua nchini bila gwaride wala fataki…

Na LEONARD ONYANGO

MWANASIASA wa Upinzani Miguna Miguna atarejea humu nchini Jumatatu huku kukiwa na dalili kwamba hatalakiwa kwa mbwembwe na wafuasi wa National Super Alliance (Nasa).

Umaarufu wa Dkt Miguna ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee ulididimia mara tu baada ya kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza kuwa atafanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta wiki mbili zilizopita.

Dkt Miguna ambaye amejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la NASA, National Resistance Movement (NRM), alifurushwa na serikali kwa nguvu kutoka Kenya hadi Canada mwezi jana kutokana na madai kuwa hakuwa Mkenya.

Kabla ya kufurushwa, mwanaharakati huyo wa NASA alikamatwa na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi katika kaunti za Kiambu na Nairobi na kisha kufikishwa katika mahakama ya Kajiado baada ya siku tatu ambapo alifunguliwa mashtaka ya uhaini.

Bw Miguna ndiye aliapisha Bw Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ uwanjani Uhuru Park mnamo Januari 30, mwaka huu. Hata hivyo, serikali ilisisitiza kuwa kiapo hicho kilikuwa haramu na kisha kuwapokonya bunduki, paspoti na walinzi baadhi ya wanasiasa wa NASA huku vuguvugu la NRM likiharamishwa.

Tangu kusafirishwa nchini Canada kwa lazima, Dkt Miguna amekuwa akizunguka katika mataifa ya Amerika, Uingereza na Ujerumani ambapo amekuwa akihutubia makundi mbalimbali kuhusiana na hali ya kisiasa ya Kenya na yaliyojiri wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26, mwaka jana.

“Machi 24, 2018, vuguvugu la NRM litakuwa jijini London, Uingereza kabla ya kutua jijini Nairobi Machi 26,” akasema Dkt Miguna.
Mwanaharakati huyo alitangaza kurejea wiki mbili baada ya Mahakama ya Rufaa kumwondolea vikwazo huku ikisema kuwa yuko huru kurejea.

Wafuasi wa NASA walimkumbatia DktMiguna na kumtaja shujaa alipojitokeza kukabiliana na serikali ya Jubilee huku akidai kuwa uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na dosari chungu nzima.

Lakini tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, wafuasi wa NASA wameonekana kumtelekeza Miguna huku wengi wakiunga mkono hatua ya kiongozi wa Upinzani kukubali kushirikiana na serikali.

Wengi wa wafuasi wa NASA wamemchukulia Bw Odinga kama mpenda amani huku baadhi wakimwona kama msaliti kwa kuamua kushirikiana na serikali.
Bw Odinga pia ameonekana kujitenga naye tangu Miguna alipopasua mbarika kuwa baadhi ya maafisa wa NASA walipokea fedha za hongo kutoka kwa Jubilee kabla ya kuapishwa kwa Bw Odinga Januari 30.

Tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta, Dkt Miguna amekuwa mkosoaji mkubwa wa kiongozi wa Upinzani huku akimtaja kuwa msaliti kwa wafuasi wake.

Amesisitiza kuwa vuguvugu la NRM litandelea kupigania haki katika masuala ya uchaguzi licha ya Bw Odinga ‘kujiunga’ na serikali.

“Kwa kukubali kufanya kazi na Rais Kenyatta ‘aliyemwibia’ ushindi wake, Bw Odinga amesaliti mamia ya Wakenya waliouawa na kuhataraisha maisha yao baada ya uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26,” akasema Dkt Miguna.

Mwanaharakati huyo pia alitangaza kuongoza maandamano katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia kesho ili kushinikiza kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa uchaguzi huku akisema kuwa: “ushindi haupatikani kwa kusalimiana (kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga) katika chumba cha mikutano katika afisi ya rais kwenye Jumba la Harambee.”

Dkt Miguna ambaye alibwagwa na Mike Sonko katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi wa Agosti 8, huenda akajizolea maadui zaidi; kutoka upande wa Jubilee na chama cha ODM atakaporejea kesho humu nchini.

Kulingana na aliyekuwa waziri na mwaniaji wa urais 2013, James Ole Kiyiapi, Dkt Miguna atakabiliwa na upinzani kutoka kwa Jubilee na ODM kutokana na mtindo wake wa kutaka kusema ukweli.

“Miguna Miguna anasema mambo ambayo wanasiasa hawataki kusikia uwe upande wa Jubilee au NASA. Miguna ni mwaminifu na ndiye kiongozi anayefaa kuongoza Kenya,” alisema Prof Kiyiapi.

JAMVI: Uhuru afanikiwa kupunguza makali ya vinara wa upinzani kwa utawala wake

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye amefaulu kudhoofisha upinzani dhidi ya serikali yake kwa kumshawishi kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunga ajenda zake.

Wadadisi wanasema, japo viongozi hao wawili walisema nia yao ni kuunganisha Wakenya,  Rais Kenyatta ndiye mshindi kwa sababu hatakuwa na upinzani wenye nguvu wa kukosoa serikali yake.”

Jubilee ilijaribu kusambaratisha upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana lakini ikashindwa. Kwa kukutana na Bw Odinga na kufikia muafaka, Rais Uhuru amefaulu kulemaza upinzani,” asema Bw Godfrey Aliwa, mdadisi wa masuala ya siasa na wakili jijini Nairobi.

Anaeleza kuwa waliopanga mazungumzo hayo walielewa kuwa upinzani bila Raila ni butu. “Raila ndiye nguzo ya upinzani Kenya na kwa kumleta karibu na serikali ni kusambaratisha upinzani.

Lengo hapa ni kuhakikisha Rais Kenyatta hatakuwa na upinzani wenye nguvu kumsumbua katika kipindi chake cha pili na cha mwisho uongozini,” alisema Bw Aliwa.

Mbali na upinzani kuwa na wabunge wachache, wengi wao ni wa chama cha ODM cha Bw Raila ambao tayari wameanza kuchangamkia muafaka wake na Rais Kenyatta.

Washirika wa Bw Raila katika NASA, Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic Movement, Moses Wetang’ula wa Ford-Kenya na Musalia Mudavadi wa Amani National Congress hawakuhusishwa katika muafaka huo.

Baadhi ya washirika wa kisiasa wa Bw Musyoka, Bw Wetangula na Bw Mudavadi wamenukuliwa wakitaka chama cha ODM kuondoka NASA ili wachukue nafasi ya upinzani rasmi. Hata hivyo, kulingana na Bw Aliwa, hata kama wangeachiwa NASA, hawataweza kukosoa serikali alivyokuwa akifanya Bw Raila.

“Aliyenufaika pakubwa ni Rais Kenyatta kwa sababu atakuwa na mteremko kwa kukosa upinzani thabiti katika kipindi chake cha mwisho mbali na Raila kumtambua kama rais,” alisema.

Chini ya Bw Raila na wanasiasa wake wa ODM, upinzani uliongoza maandamano yaliyong’oa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) chini ya aliyekuwa mwenyekiti Isaack Hassan.

Ni Bw Odinga ambaye alifichua kashfa mbali mbali serikalini ikiwa ni pamoja na ile ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS na Eurobond. “Sidhani kama kuna anayeweza kufuata nyayo za Raila kati ya Musyoka, Wetangula na Mudavadi. Kumbuka ni Raila aliyekuwa akisukuma kubuniwa kwa mabunge ya wananchi yaliyokuwa yakikosesha Jubilee usingizi,” asema Bw Geff Kamwanah, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Anasema masuala ambayo NASA imekuwa ikipigania kama haki katika uchaguzi ni mazito na yanahitaji kiongozi mwenye ujasiri kama Raila.

Bw  Musyoka, Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi wanasema wako tayari kusukuma ajenda za NASA bila Bw Odinga lakini hii ni kama mzaha,” asema mwanahabari na mdadisi wa masuala ya siasa Macharia Gaitho kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation.”

“Wamekasirika kwa sababu Bw Odinga alizungumza na Bw Kenyatta bila kuwahusisha,” alisema Bw Gaitho.

Bw Kamwanah anasema ishara kwamba Musyoka, Wetangula na Mudavadi hawana ujasiri wa kukabiliana na serikali ni kujitenga kwao na Raila alipokula kiapo kama rais wa wananchi.

“Huo ulikuwa mtihani waliofeli. Raila amejaribiwa mara nyingi kwa moto, ameteswa na kutupwa jela na kuibuka jasiri zaidi. Kwa kuzika tofauti zake na Rais Uhuru ni kama kuua upinzani,” aeleza.

Raila amesisitiza kuwa hajahama NASA akisema muafaka wake na Rais Kenyatta ni wa watu wawili na sio mirengo ya kisiasa. Hata hivyo, matamshi yake na washirika wake wa kisiasa, wakiwemo wabunge wa chama cha ODM, yanatoa ujumbe tofauti. Kulingana na mbunge wa Lugari Ayub Savula, Wiper, ANC na Ford Kenya viko tayari kuunda upinzani rasmi bila ODM.”

ODM ikioana na Jubilee tuko tayari kuunda upinzani rasmi,” alisema. Hata hivyo, wadadisi wanasema wanachotaka wabunge hao wapatao 40 bila ODM ni vyeo vya upande wa upinzani bungeni.

“Kenya imerejea ilipokuwa 1997 upinzani ulipodhoofishwa Raila alipojiunga na serikali ya Kanu. Jukumu la kukosoa serikali lilichukuliwa na vyombo vya habari na mashirika ya kijamii na yasiyo ya Serikali.

Jinsi hali ilivyo wakati huu, uhuru wa wanahabari na mashirika ya kijamii umedidimizwa. Kwa ufupi, hakutakuwa na upinzani Kenya iwapo Raila atamezwa na Jubilee,” asema Bw Kamwanah.

Hisia za wadadisi ni kuwa, muafaka wa Raila na Uhuru ulipangwa ili  kupangua upinzani ukose makali ya kukosoa Serikali.

Jirongo asimulia Raila alivyomsaidia kupata kazi Tanzania

Bw Cyrus Jirongo akihutubu awali. Picha/ Maktaba

Na BARACK ODUOR

ALIYEKUWA mgombeaji urais Cyrus Jirongo amempongeza kiongozi wa NASA Raila Odinga kwa kumsaidia na kumwezesha kupata ajira. Jirongo ambaye ni Mbunge wa zamani wa Lugari alidai kuwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto walimtelekeza.

Mwanasiasa huyo alidai viongozi hao wawili wa Jubilee, ambao wamekuwa wandani wake, walimpuuzilia alipowageukia akitaka wamsaidie.

“Nitaendelea kuwa kushirikiana na jamii ya Waluo kwa sasa hata juzi nilimtembelea Bw Odinga na nikamwelezea jinsi viongozi wakuu wa Jubilee wamenitelekeza,” akasema Bw Jirongo.

Akiongea wakati wa mazishi ya Mama Julia Amayo, mkewe aliyekuwa Mbunge wa Karachuonyo Okiki Amayo, Jirongo alifichua jinsi alivyosafirishwa na Bw Odinga hadi Tanzania ambapo kiongozi huyo wa NASA alimfahamisha kwa Rais John Magufuli.

“Ni Bw Odinga alinisaidia kwa kunijulisha kwa Rais wa Tanzania na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye baadaye alinipa kazi,” Bw Jirongo akawaambia waombolezaji katika kijiji cha Kakdhimu, eneo bunge la Karanchuonyo, kaunti ya Homa Bay.

Ingawa hakufichua ni kazi gani alipewa, alisema anamshukuru Bw Odinga na kuunga mkono mwafaka kati yake na Rais Kenyatta.

“Naunga mkono ushirikiano kati ya Odinga na Rais Kenyatta kwani nafahamu utaleta manufaa makubwa kwa Wakenya wote,” akasema.

Bw Jirongo alisema Odinga sasa anafaa kupewa heshima na wanasiasa wa mirengo ya Jubilee na NASA kutokana na hatua yake ya kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya kuunganisha nchi.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Rangwe Shem Ochuodho alipongeza ushirikiano kati ya viongozi hao wawili lakini akawataka kuutumia kuunganisha nchini.

“Mazungumzo kati ya Kiongozi wa NASA Raila Odinga na Rais Kenyatta yanafaa kuwa zaidi ya salama ya mkono ili yaweze kuafaidi Wakenya,” akasema Bw Ochuodho ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Wakenya wanaoishi Ughaibuni.

Aliwataka wanasiasa nchini kuepukana na siasa za migawanyiko bali waungane na viongozi hao wawili kuleta maridhiano nchini baada ya kukamilika kwa kipindi cha uchaguzi.

“Wanasiasa wote nchini hawana jingine ila kuwaunga mkono Rais Kenyatta na Odinga katika mchakato wa kuleta maridhiano miongoni kwa Wakenya,” akasema.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Gavana wa Homa Baye Cypria Awiti, aliyekuwa Mbunge wa Rangwe Philip Okundi, kati ya wengine.

Kalonzo aandaliwa kuwarithi Uhuru na Raila

Na PIUS MAUNDU

BAADA ya mkondo wa kisiasa kuonekana kubadilika katika Muungano wa NASA, Wiper imeanzisha mikakati ya kuhakikisha kinara wake Kalonzo Musyoka amerithi ngome za kisiasa za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mwenyekiti wa chama cha Wiper, ambaye ni Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana sasa anasema kuwa Bw Musyoka, atahitaji baraka za Rais Uhuru Kenyatta na pia Raila Odinga kushinda urais 2022.

Mnamo Ijumaa, Prof Kibwana aliambia mkutano wa kamati za maendeleo kutoka vijijini kote kwa kaunti yake na viongozi waliochaguliwa katika eneo, kuwa hatua ya maridhiano iliyofanywa kisiri kati ya viongozi hao wawili, ndiyo itaamua siasa za 2022.

Ingawaje awali gavana huyo hakuwa amefurahishwa na hatua hiyo hasa kwa Bw Odinga kukosa kuwahusisha vinara wenza, alionya jamii ya Wakamba dhidi ya kumshtumu Bw Odinga ama kumhujumu Rais Kenyatta.

“Tunastahili kukosa kumshtumu Bw Odinga na badala yake tuanze kumuambia kuwa sisi ni sehemu ya salamu zile na Rais Kenyatta,” alieleza huku akiepuka kuhusu hatma ya muungano wa Nasa.

 

Mchezo safi

“Pia tunahitaji mabaraza za Rais Kenyatta,” alisema akiongeza, “Kuna njia tunaweza kupata baraka za Rais Kenyatta kwa kucheza vyema mchezo wetu kwa sasa.”

Wakati huo huo, akiongea kwa lugha ya Kikamba, Prof Kibwana alionya jamii hiyo dhidi ya kutojali jamii nyingine ambazo itazihitaji kwa Bw Musyoka kuweza kuingia Ikulu.

“Kuendelea mbele, lazima tujitahidi kuhusiana vyema na jamii zingine kwa sababu tutahitaji usaidizi wao kwa kijana wetu kuingia Ikulu,” alisema.

Pia aliunga mkono maoni ya Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na mbunge wa Mbooni Erastus Kivasu, ambao wamekumbatia wazi maridhiano kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta na kusema yanafaa kutuliza na kuendeleza nchi.

Pia amekuwa akiwahimiza wenzake katika Wiper na Nasa kuangalia dhamira kubwa ya hatua hiyo na kuwacha manung’uniko.

“Hatutaki kiongozi wetu awachwe nje ya mkataba kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta tunapoelekea 2022,” Bw Kilonzo Junior aliambia mkutano katika kituo cha mafunzo ya Kilimo cha Kwa Kathoka, ambao ulihudhuriwa na viongozi waliochaguliwa.

Kulingana na Prof Kibwana, Wiper inashirikiana na vyama vingine vilivyowachwa nje ya mkataba wa awali na rais na wanalenga kufanya mkutano naye.

 

Tahadhari

Mbunge wa Kitui Kusini, Rachael Kaki na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Makueni, Bw Stephen Ngelu wamemtahadharisha Bw Musyoka dhidi ya kuweka masharti akiwa anategea kuhusishwa kwa mkataba wa Bw Odinga na Rais.

Kuweza kusalia na umuhimu kisiasa, Bw Musyoka lazima akubali kufanya kazi na rais kwa sababu hatua ya hivi punde ya Bw Odinga imetia doa upinzani.

Bw Musyoka anatarajiwa kuongoza viongozi wote wa Ukambani kwa kongamano katika kaunti ya Machakos juma lijalo kujadili msimamo wa kisiasa wa eneo hilo kufuatia yaliyojiri.

Duru zimeambia Taifa Jumapili kuwa mojawapo ya ajenda kuu ni jinsi ya kumwandaa upya Bw Musyoka kumrithi Rais Kenyatta.

Bw Odinga amewaacha Wakenya wakiendelea kubahatisha kuhusu msimamo na mipango yake, hata ingawa tayari amezuru maeneo ya Kisii na Kisumu na kujaribu kufichua wazi mkataba baina yake na rais unahusu nini.

Takwimu: Siaya yaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya vifo nchini

Na DOROTHY OTIENO na JOSHUA MUTISYA

IKIWA unaishi Siaya, una uwezo mkubwa zaidi kufariki kabla ya muda wako ikilinganishwa na yeyote anayeishi katika kaunti nyingine nchini Kenya, utafiti wa Nation Newsplex umebaini.

Kulingana na utafiti huo, idadi ya vifo ni asilimia 20 miongoni mwa wananchi 1,000 mwaka wa 2016, huku mkazi wa Siaya akiwa na uwezo mara tatu wa kuaga dunia akilinganishwa na mkazi wa Nairobi.

Jiji la Nairobi lina idadi ndogo zaidi ya watu wanaoaga dunia, ambapo ni watu sita kati ya 1,000. Hali hiyo imeshuhudiwa Siaya tangu 2011 ambapo kila mwaka huongoza kwa idadi ya vifo.

Kwa kipindi hicho, Nairobi imeorodheshwa miongoni mwa kaunti tatu ambazo zina idadi ndogo zaidi ya vifo nchini katika kipindi hicho.

Kwa kuzingatia visa vya watu wanaoua wengine, Kaunti ya Siaya iliorodheshwa ya saba. Kitaifa, visa hivyo ni 14 kati ya 100,000.

Kaunti zingine tatu Nyanza zimo miongoni mwa kaunti 10 za mbele zilizo na idadi kubwa ya vifo kwa watu 1,000.

Kisumu imeorodheshwa ya tano ambapo ina viwango vya vifo kuwa asilimia 14.1, Homabay ni ya saba kwa asilimia 13.5 na kufuatwa na Migori kwa asilimia 13.
Kaunti ya pili ni Vihiga ambayo idadi ya vifo ni 17 kwa watu 1,000 na kufuatwa na Elgeyo-Marakwet(15) na Taita Tavet(14.7).

Vihiga imekuwa nambari hiyo tangu 2011. Kaunti ya Turkana imo katika nafasi ya sita(14) na Bungoma imo nambari tisa(12.4).

Kaunti ya Kakamega ni nambari 10 (12). Idadi ya mauaji kwa watu 100,000 katika Kaunti ya Vihiga ni 11, ambapo kaunti hiyo ni miongoni mwa kaunti 10 zilizo na visa vingi zaidi vya mauaji.

Viwango hivyo vilikadiriwa kwa kuzingatia idadi ya watu wanaoishi katika maeneo ya kaunti, idadi ya vifo vilivyoripotiwa katika ripoti ya takwimu za kitaifa miaka ya 2015 na 2017.

Idadi ya vifo ilizingatiwa katika utafiti huo kwa sababu sio vifo vyote vilivyoripotiwa katika sajili ya kitaifa. Kwa mfano, asilimia 76 ya vifo vyote viliripotiwa na kusajiliwa 2016, idadi ya juu Zaidi nchini. Hata hivyo, idadi ya vifo iliyoripotiwa Mandera na Wajir ilikuwa chini ya asilimia 10.

Kaunti iliyo nambari mbili kwa viwango vya chini vya vifo kati ya watu1,000 ilikuwa Isiolo(6.8) na kufuatwa na Narok(6.9), Kajiado(7.3) na Embu(7.9).
Isiolo ndio kaunti ya pekee ambayo hakuna kisa hata kimoja cha mauaji kiliripotiwa mwaka wa 2016.

Kaunti za Garissa, Mandera na Wajir hazikuzingatiwa katika utafiti huo kwa sababu makadirio ya idadi ya watu 2011 na 2015 yalilandana na hesabu ya watu wote katika uchunguzi wa hesabu ya watu nchini (KNBS) wa 2009.

Hivyo, ni kaunti 44 ambazo zilijumuishwa katika utafiti wa Nation Newsplex.

 

Vifo jijini Nairobi

Ingawa Nairobi ina idadi ndogo zaidi ya vifo nchini, kifo kimoja kati ya 14 mwaka wa 2016 kilitokea jijini, idadi ya juu zaidi.

Hata hivyo, mmoja kati ya watu 10 nchini wanaishi Nairobi, kumaanisha ikilinganishwa na kiwango cha watu cha kitaifa, idadi hiyo ilikuwa ya chini zaidi.

Mwaka wa 2016, jumla ya vifo 189,930 vilisajiliwa, ambavyo vilikuwa takriban asilimia 42 ya vifo vyote mwaka huo ambavyo viliripotiwa bila kusajiliwa(452,214).

Katika miaka sita, Kaunti ya Nyeri iliripoti upungufu mkubwa zaidi wa vifo katika muda wa miaka sita, hadi 2016. Idadi hiyo ilipungua kwa thuluthi moja, hadi tisa, kutoka 14 kwa watu 1,000.

Idadi ya vifo iliongezeka zaidi katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet kutoka 11 hadi 15 kati ya watu 1,000. Kitaifa, idadi ya vifo iliongezeka kwa asilimia 10 hadi 10 kwa watu 1,000 katika kipindi hicho.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO), uwezekano wa mwanamke Mkenya kuishi hadi miaka 65 ni asilimia 72, kiwango kilichoshuka kwa asilimia 10.

 

Mauaji

Wakati wa kuzingatia kiini cha vifo, Kaunti ya Lamu ilikuwa na idadi ya juu zaidi ya mauaji huku Nakuru na Isiolo zikuwa na viwango vya chini zaidi.

Hii ni kumaanisha kuwa una uwezo mara 58 kufa kutokana na mauaji katika Kaunti ya Lamu ikilinganishwa na Isiolo au Nakuru.

Kulingana na ripoti ya polisi, visa 76 vya mauaji viliripotiwa Lamu, ambapo ni watu 59 kati ya 100,000.

Visa vinane pekee vya mauaji viliripotiwa Nakuru, ambavyo ni chini ya asilimia moja pekee.

Idadi ya mauaji ya kaunti hizo mbili ilikuwa chini zaidi ikilinganishwa na viwango vya kitaifa, cha asilimia sita pekee kwa watu 100,000.

Viwango hivyo kwa kaunti 23 vilikuwa chini ya viwango vya kitaifa vya 6 kati ya watu 100,000.

 

Viini vikuu vya vifo nchini
Pneumonia-vifo 21,295,
Malaria -vifo 16,000
Kansa- vifo 15,762
Ukimwi -vifo 9,471
Ukosefu wa damu mwilini -vifo 8,165

Uchunguzi waanika uozo unaokumba shule za umma

Na WAANDISHI WETU

MAAFISA wa elimu wa ngazi za juu waliozuru kaunti 46 wameshtushwa na uozo unaokumba taasisi za elimu nchini Kenya.

Kundi hilo ambalo lilijumuisha maafisa kutoka Wizara ya Elimu, Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC), Taasisi ya Kuunda Mtaala (KICD) na Taasisi ya Elimu Maalum (KISE), limebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mimba za mapema, ndoa za mapema, utumizi wa dawa za kulevya na pia wanafunzi kukosa kufika shuleni.

Katika baadhi ya kaunti, takriban asilimia 60 ya wasichana wachanga wanaozwa mapema na kukosa kutumia nafasi ya elimu bila malipo, matokeo ya mijadala ambayo imekuwa ikiendelea kuhusu ubora wa elimu iliyomalizika Ijumaa yameonyesha.

Waziri wa Elimu, Amina Mohamed alisema midahalo hiyo ni muhimu katika kukusanya maelezo ambayo yatasaidia mageuzi yanayoendelea shuleni, baadhi ambayo yameegemezwa katika mitazamo iliyopitwa na wakati.

“Mageuzi yetu lazima yatekelezwe kulingana na data iliyokusanywa moja kwa moja kutoka kwa wadau walioathiriwa,” alisema.

Midahalo hiyo iliyohudhuriwa na wafanyakazi wa kitaifa na kaunti ilibainisha kuwa idadi ya wanafunzi wanaokosa kufika shuleni ni kubwa katika baadhi ya kaunti zaidi ya inavyotarajiwa.

“Tulishtushwa na viwango vya wanafunzi kukosa kufika shuleni katika baadhi ya shule, hali ambayo imechangia idadi ya wanaojiandikisha shuleni kupungua kwa sababu wanafunzi wengine wanaacha shule,” alisema mkurugenzi wa Elimu ya Mahitaji Maalum, Bi Maria Cherono.

Hali ni mbaya zaidi katika kaunti ya Kirinyaga ambapo wadau waliafikiana kuunda kundi maalum la kuchunguza changamoto za dawa za kulevya na wanafunzi kukosa kufika shuleni.

Katika Kaunti ya Meru, kundi hilo lilibaini kuwa mimba za mapema, utafunaji miraa, ukeketaji wa wasichana na ajira ya watoto kuwa changamoto zinazoathiri watoto.

Walimu kadha katika Kaunti ya Mombasa walilalamikia kukosa vitabu vya kutosha kuweza kufunza vilivyo. Katika Kaunti za Kisii na Nyamira, makanisa yalipigwa darubini kufuatia tuhuma kuwa yanaingilia kati usimamizi wa shule.

Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu Kaunti ya Kisii, Dkt Henry Onderi alisema baadhi ya wadhamini wanawajibikia kuanguka kwa shule zilizotambuliwa kwa sababu ya kuvuruga usimamizi.

Katika Kaunti ya Kilifi, mila na desturi za Wamijikenda zilitajwa kuchangia mimba za mapema na matokeo mabovu, hasa disko zinazochezwa matangani.
Gavana wa Kilifi, Amason Kingi ambaye alihudhuria kikao katika kaunti yake aliwahimiza wakazi kuachana na desturi potovu. Aliongeza kuwa ukosefu wa miundomsingi na walimu umeongeza kudorora kwa elimu.

Katika Kaunti ya Nakuru, msongamano madarasani ulibainika kuwa shida kubwa, darasa moja likiwa na wanafunzi zaidi ya 100.

Taarifa ya Ouma Wanzala, Diana Mutheu, Magati Obebo, Kalume Kazungu, Charles Lwanga, Barack Oduor, Francis Mureithi, Ruth Mbula, Francis Mureithi na Steve Njuguna.

27 wakamatwa kufuatia ghasia Kakamega

Na SHARON OKOLLA

Watu 27 walikamatwa mjini Kakamega kwa kuhusika katika rabsha baada ya waombolezaji kukabiliana na polisi wa kupambana na fujo.

Machafuko yaliibuka mjini wakati mwili wa Sharlyne Mwanzia ulipokuwa ukitolewa chumba cha kuhifadhia maiti kupelekwa nyumbani kwao, mtaa wa Scheme mjini humo.

Vitoa machozi vilirushwa na milio ya risasi ilisikika wakati vijana walikuwa wakiandamana kuwataka maafisa wa polisi kumkamata mshukiwa wa mauaji hayo.

Msimamizi wa polisi eneo la Kakamega Joseph Chebii Jumamosi alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao 27. Alisema watafikishwa mahakamani Jumatatu.

Hata hivyo, alikana madai kwamba baadhi ya vijana walifyatuliwa risasi na maafisa wa polisi Ijumaa.

“Hakuna ripoti iliyowasilishwa kwetu kuhusiana na suala hilo kufikia sasa, kwamba kuna mtu aliyejeruhiwa wakati wa vurugu iliyoshuhudiwa Ijumaa,” alisema.

“Hata hivyo, maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa kidogo walipopigwa kwa mawe na vijana waliokuwa na ghadhabu,” aliongeza.

Aliwashauri wakazi wa eneo hilo kuepuka kukabiliana na maafisa wa polisi. Bw Chebii alisema wanawataka washukiwa kuwapa habari zaidi ambayo inaweza kupelekea kukamatwa kwa washukiwa zaidi.

Alishutumu mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi. Waombolezaji walionekana kulemewa na hisia kwani walilia kwa uchungu mwingi na kushutumu mauaji hayo ya mtoto huyo wa miaka tisa.

Mtoto huyo aliuawa na mwili wake kutupwa ndani ya tanki la maji, nyumbani kwao. Sharlyne aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya St Joseph’s Academy, alipotea nyumbani kwao Machi 11, 2018 alipokuwa akicheza na ndugu zake. Mwili wake ulipatikana Machi 16.

Waombolezaji hao waliwashtumu polisi kwa kushindwa kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama .

Msichana huyo wa darasa la tatu katika shule ya St Joseph’s Academy, Kaunti ya Kakamega, alitoweka nyumbani kwa wazazi wake siku 13 zilizopita na anashukiwa kuhadaiwa na mtu asiyejulikana.

Ijumaa, vurumai zilizuka baada ya kundi la vijana kuanza kuharibu nyumba ambapo mwili wa mtoto huyo uligunduliwa, waombolezaji walipokuwa wakikaribia mtaa huo.

Mtu mmoja alijeruhiwa mikono alipojaribu kuchukua mkebe wa gesi hiyo ya kutoza machozi walipokuwa wakikabiliana na polisi.

Mkuu wa Polisi Kaunti, Bw Johanah Tonui hata hivyo alipuuzilia mbali mdai hayo akisema kuwa polisi walitumwa kuwatawanya vijana ambao walikuwa wakipora kutoka kwa duka kuu.

“Kile tulichofanya ni kuwatawanya vijana waliokuwa wamezuia barabara na kuwapiga mawe maafisa ili kuwachanganya akili na kisha kupora,” alitetea afisa.

Atakayefichua mwanamume anayewatapeli wabunge kutuzwa Sh20,000

Na STELLA CHERONO

MKURUGENZI Mkuu wa Ujasusi(DCI) George Kinoti ametoa Sh20,000 kwa yeyote aliye na habari kuhusu aliko mwanamume aliyetuhumiwa kuwalaghai wabunge.

Benson Wazir Chacha Masubo anahitajika kwa kudaiwa kupata pesa kwa kujifanya, na kwa kutumia vitisho katika intaneti.

Bw Masubo alishutumiwa kwa kuwalaghai wabunge kwa kujifanya kuwa Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Bi Sabina Chege.

Alhamisi, Bw Kinoti aliambia Kamati ya Bunge ya Usalama kwamba baada ya uchunguzi wa kina, walibaini kuwa kulikuwa na uhusiano maalum kati ya mshukiwa na walalamishi.

“Tumefanya uchunguzi wa kina kuhusiana na suala hili na tumetamatisha kuwa kuna uhusiano maalum kati ya walalamishi na mshukiwa ambao na sihisi vyema kujadili suala hilo hadharani,” alisema Bw Kinoti.

Ni kutokana na kauli hiyo ambapo wanahabari walishauriwa kuondoka nje ili Bw Kinoti aweze kueleza zaidi.

Miongoni mwa wa waliolaghaiwa na mwanamume huyo ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye alimtumia Sh30,000, aliyekuwa mbunge wa Gem MP Jakoyo Midiwo (Sh20,000), na mawaziri Eugene Wamalwa (Ugatuzi), Peter Munya (Jumuia ya Afrika Mashariki), Margaret Kobia (Huduma ya Umma) na Sicily Kariuki (Afya).

Mwezi Februari, mshukiwa aliweka mtandaoni picha zake alizopigwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Bomet Cecilia Ng’etich na kuonekana kusingizia uhusiano kati yao.

Picha hizo zilisambazwa sana katika mitandao ya kijamii. Wakati wa mahojiano, Bi Ng’etich alisema mwanamume huyo alikuwa laghai na alikuwa akitaka Sh2 milioni kwa kumtishia.

Aliwataka maafisa wa polisi kumchunguza, na kuongeza kuwa alikuwa mtu wa kutiliwa shaka.

 

Msituhusishe kwa mzozo wenu, Mutula awaambia vinara wa NASA

Na PIUS MAUNDU

KIRANJA wa Wachache Seneti Mutula Kilonzo Junior ameonya vinara wa Muungano wa NASA dhidi ya kuwahusisha maseneta na mzozo wao.

Seneta huyo alisema hatima ya Seneta Moses Wetangula tayari imeamuliwa akiongeza kuwa uamuzi wa kumwondoa mwenzao ambaye ni “anajionyesha kuwa bora” hauwezi kubatilishwa.

Baadhi ya wahusika wa Nasa wamewakosoa maseneta wa upinzani kwa kuendesha ‘mgawanyiko’ wa upinzani baada ya kuamua kumng’oa Bw Wetangula kama Kiongozi wa Wachache Seneti.

Nafasi hiyo walimpa Seneta wa Siaya, James Orengo, hatua ambayo pia haijawafurahisha vinara wa muungano.

Kinara wa Nasa Raila Odinga na naibu wake Kalonzo Musyoka wamemsihi Bw Orengo asikubali kuangamiza Nasa kwa kukubali kuchukua nafasi hiyo, maoni ambayo yameibua hisia kali kutoka kwa maseneta ambao ni pamoja na Bw Kilonzo Junior.

“Vinara wa Nasa wanastahili kukoma kuona maseneta wanahusika katika vita vyao,” alisema Seneta huyo wa Makueni.

Bw Kilonzo pia alizungumzia wajibu wake katika utaratibu huo wa kumuondoa Bw Wetangula.

“Wajibu wangu ulikuwa kuwasilisha hoja ya kumuondoa Seneta Wetangula kama inavyoelezwa katika sheria bila hofu ama mapendeleo,” alieleza Taifa Jumapili.

Pia alionekana kupuuzilia mbali juhudi zinazoendelea katika muungano huo wa upinzani kumrejesha Bw Wetangula, na kuonekana kudumisha kuwa uamuzi huo hauwezi kubadilishwa.

 

Wavuvi wa Kenya wavamiwa tena na polisi wa Uganda

Na KNA

WAVUVI 20 wa Kenya walivamiwa Alhamisi usiku na kunyang’anywa taa zao zinazokadiriwa kuwa za thamani ya Sh70,000 na maafisa wa usalama wa Uganda katika Ziwa Victoria.

Wavuvi hao kutoka ufuo wa Kinda, kaunti ndogo ya Suba Kusini walishikwa walipoenda kuvua Omena.

Mwanachama wa kamati simamizi ya ufuo huo wa Kinda, Bw Boni Sidika alisema tukio hilo lilifanyika wakati maafisa watatu wa usalama ambao walikuwa na bunduki walivamia boti tano zilizokuwa zimebeba wavuvi wanne kila moja.

Alisema wavuvi hao waliumizwa walipojaribu kujitetea kwa kueleza kuwa walikuwa wakivua katika maji ya Kenya.

Bw Wycliffe Aila, mmoja wa wamiliki wa boti hizo na taa, alisema maafisa hao walijaribu kwanza kuchukua taa za kuvua lakini wavuvi walipokataa waliwapiga.

“Waliwaumiza wavuvi kwa kutumia mbao baada ya wavuvi hao kukataa kuhangaishwa. Wavuvi hao walijeruhiwa sehemu kadha mwilini,” Bw Aila alieleza.

Alisema wavuvi hao pia walilazimishwa kutupa majini samaki waliokuwa wamevua. Wavuvi hao sasa wanataka serikali itatue mzozo wa mipaka ya ziwa hilo kati ya Kenya na Uganda.

“Tunasihi serikali itafute suluhisho la kudumu kwa mizozo inayohusu mpaka kati ya Kenya na Uganda,” Bw Sidika alisema.

OCPD wa Suba Kusini, Bw Paul Kipkorir alisema wavuvi hao hawajaandikisha taarifa kwa polisi.

“Hakuna mvuvoi ameandikisha taarifa lakini tunaulizia ili tuweze kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema Bw Kipkorir.

 

 

Ziara ya Rais Uhuru na Raila mjini Kisumu yaahirishwa

Na JUSTUS WANGA

MKUTANO wa pamoja kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA Raila Odinga uliotaribiwa kufanyika wiki hii mjini Kisumu umeahirishwa kutoa nafasi kwa muda wa kushughulikia masuala ibuka yanayotisha kuathiri muafaka kati yao.

Wandani wa Bw Odinga wameanza kushuku kujitolea kwa Jubilee katika mchakato wa mazungumzo baada ya kiongozi wa wengine bunge Aden Duale kupinga kujumuishwa kwa suala ya mageuzi  katika mfumo wa uchaguzi ambalo ni mojawapo yale ambayo Rais na Odinga walikubali kujadili.

Akiongea katika runinga moja ya humu nchini Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini pia alipuuzilia mbali mageuzi katika mfumo wa uongozi nchini.

Wakati huo huo, mpango wa balozi Martin Kimani na Wakili Paul Mwangi kuwahutubia wanahabari Ijumaa ili kuelezea hatua iliyopigwa kuhusu suala hilo iliahirishwa dakika zake mwisho.

Mbw Kimani na Mwangi waliteuliwa na Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga kutayarisha mwongozo ambao utasaidia kufanikisha malengo ya mwafaka huo.
Duru zilisema kuwa “kuna masuala ambayo pande husika hawajakubaliana.” Walipofikiwa kwa njia ya siku wawili hao hawakutaja sababu ya kufutilia mbali kikao na wanahabari.

Taifa Jumapili pia imegundua kuwa Kamati hiyo itapanuliwa kwa kujumuisha angalau wanachama watano kutoka kila upande huku akianza kibarua rasmi.

Shauku ya kambi ya Bw Odinga inatokana na hali kwamba japo ameshawishi uongozi wa chama hicho kuunga mkono ushirikiano huo, kufikia sasa Rais Kenyatta hajaitisha mkutano wa kundi la wabunge wake (PG) au asasi yoyote ya chama hicho kuhimiza wafuasi wake kuunga mkono mwafaka huo. Vile vile, wanasema Rais Kenyatta hajaitisha kikao maalum cha baraza la mawaziri kuwajuza kuhusu yaliyomo ndani ya mkataba kati yake na Bw Odinga.

“Tunataka kuona taarifa kutoka afisi ya Rais ikielezea hatua ambazo zimewekwa kuafikia uwiano na masuala ambayo yalikubaliwa. Sawa na Odinga, tunaamini kwamba Rais ana nia njema. Tunataka kuona wakianza kazi,” mmoja wa wandani wa Bw Odinga alisema.

Chama cha ODM kinashikilia kuwa hatima ya mwafaka huo utategemea kama iwapo Rais alielekeza nchini kufunua ukurasa mpya huku masuala ya serikali yakiendeshwa kwa namna tofauti.

Hata hivyo, hakuna kiongozi kutoka kambi ya Kenyatta ambaye amepinga mwafaka huo isipokuwa Seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki ambaye ameonya Rais kutahadhari anapojadiliana na Bw Odinga kwa sababu, “ni mwanasiasa mjanja”.

Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga aliwaonya Rais Kenyatta na kiongozi huo wa upinzani kuwaonya wafuasi wao dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kusambaratisha mwafaka huo.

 

Niliporwa mamilioni niliyochangiwa na Wakenya – Miguna Miguna

Na CHRIS WAMALWA

MWANAHARAKATI wa vuguvugu la NRM, Miguna Miguna amedai kuibiwa Sh2 milioni alizochangiwa na Wakenya wanaoishi Amerika.

Dkt Miguna, ambaye anarejea nchini Jumatatu, alielekeza kidole cha lawama kwa kundi la Wakenya waliopanga mikutano kadhaa aliyoandaa katika mji wa Dallas katika jimbo la Texas kwa wizi huo uliofanyika Machi 10.

Bw Steve Aseno ndiye alikodi ukumbi wa mkutano na kupanga safari za Dkt Miguna.

Mwanasiasa huyo alitoa hotuba mjini Dallas, shughuli iliyofuatwa na mchango wa fedha za kuwalipa mawakili wake na kukarabati makazi yake katika mtaa wa Lavington, Nairobi yaliyoharibiwa na polisi waliotumwa kumkamata.

Dkt Miguna alidai kwa sauti ya juu kwamba, Bw Aseno ndiye alipora pesa zilizokusanywa katika mkutano wa Dallas.

Hata hivyo, Bw Aseno amekana madai hayo, akisema yeye ndiye alilazimika kutumia Sh100,000 zake mwenyewe.

Promota huyo alisema hafla ya kuchanga pesa ilifeli Dkt Miguna alipoanza kumshambulia kiongozi wa NASA Raila Odinga kwa kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Aseno alisema wafuasi wengi wa Bw Odinga ambao walikuwa wamethibitisha kuhudhuria shughuli hiyo walibadili nia Dkt Miguna alipoanza kushambulia Bw Odinga.

 

Adhabu ya kumkejeli Raila

“Ni wageni 114 pekee walihudhuria. Walitozwa Sh2,000 kila mmoja kama ada ya kungia ukumbini, Sh1,000 kwa kupiga picha na Miguna na Sh500 ili kupewa picha ya Raila. Kwa sababu Miguna alikuwa akitoa matusi dhidi ya Raila, hakuuza picha zozote wala kupata nafasi ya kupigwa picha na wageni waliohudhuria.

Hii ndio maana michango ilikuwa finyu zaidi,” Bw Aseno akesema kwenye mahojiano na “Taifa Jumapili”.

Promota huyo alisema alimkabidhi Dkt Miguna Sh119,500 zilizopatikana kutokana na mchango na Sh15,000 za mauzo ya picha, akisema haelewi ni kwa nini mwanasiasa huyo anadai kuwa yeye na wasaidizi wake walimwibia Sh2 milioni.

Wakati huo huo, Msomi Profesa David Monda anayeishi Amerika asema, huenda Dkt Miguna akakumbana na hali tofauti kabisa ya kisiasa baada ya Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta.

“Mandhari ya kisiasa nchini Kenyatta yamebadilika baada ya Rais Kenyatta kusalimiana kwa mkono na Bw Odinga. Miguna atabaini kuwa bila Raila hakuna NASA, na hata vuguvugu lake la NRM halipo tena.

Vijana wengi kutoka Luo Nyanza wanaweza kuhatararisha maisha yao kwa sababu ya Raila lakini hawawezi kufanya hivyo kwa Miguna,” akasema Profesa Monda.

Aliongeza: “Hulka yake ya makabiliano kila wakati, kando na ujasiri wake, ilidhihirika wakati wa ziara yake. Hali hiyo ilionekana wazi jinsi alivyopuuza maswali kutoka kwa washiriki na kuwashambulia wanasiasa akiwemo Bw Odinga. Amejitenga na wafuasi wa NASA,” alisema.

Weta na Mudavadi waapa kusambaratisha ndoa ya Uhuru na Raila

Na DERRICK LUVEGA na JUSTUS OCHIENG’

Kwa ufupi:

  • Mudavadi asema Raila ni msaliti na kama jamii ya Waluhya inafaa kuepukana kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee
  • Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”
  • Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila 
  • Ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa

VINARA wa NASA kutoka jamii ya Waluhya sasa wametangaza vita vikali vya kisiasa dhidi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kuwataka wafuasi wao kukataa chama hicho kuelekea uchaguzi wa 2022.

Wakihutubia mikutano ya hadhara katika vituo kadha vya kibiashara kaunti ya Vihiga, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi, walisema Bw Odinga ameikosea heshima jamii ya Waluhya kwa kuisaliti na kuitelekeza.

Walitaja kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti na wao kutajwa kama waoga kama ishara tosha kuwa ODM imetelekeza jamii ya Waluhya.

“Mliona vile alituhepa na kwenda kuzungumza na Uhuru Kenyatta. Na juzi mliona alivyochochea kuondolewa afisini kwa ndugu yangu Weta kama kiongozi wa wachache katika seneti.

Huyo ni msaliti na sisi kama jamii ya Waluhya tuepukane kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee,” Bw Mudavadi akawaambia wafuasi wake mjini Mbale bila kumtaja Bw Odinga kwa jina.

Aliandamana na wabunge, Alfred Agoi (Sabatia), Ernest Ogesi (Vihiga), aliyekuwa seneta wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale, Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka miongoni mwa wengine.

Nao viongozi wa ODM wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, waliwajibu kwa kupuuzilia mbali malalamishi yao.
“Watu wanafaa kuungana kwa masuala yenye umuhimu kwa wananchi kama vita dhidi ya umasikini unaowazonga watu wetu.

Sio masuala potovu kama kuwashambulia wanasiasa wengine,” akasema Bw Sifuna.

Naye Bw Wandayi akasema: “Hakuna aliyeisaliti jamii ya Waluhya. Hakuna mwanasiasa aliye na uwezo kama huo. Hili suala la mabadiliko ya uongozi katika seneti linashughulikiwa na maseneta wenyewe, haifa kutumiwa kumchafulia jina kinara wetu Bw Odinga”.

 

Kusambaratisha ndoa

Na akiongea mjini Chwele awali, Bw Wetang’ula alisema yeye na vinara wengine wa NASA watafanya juu chini kusambaratisha ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM.

Bw Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”.

Migawanyiko imekuwa ikitokota katika muungano wa NASA baada ya Bw Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kwa mazungumzo Machi 9 bila kuwahusisha vinara wenzake.

Akiwahutubia walimu katika kituo cha kibiashara cha Chwele wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha ushirika cha Ngarisha, Bw Wetang’ula alisema uamuzi wa Bw Odinga kukutana na Rais bila kuwafahamisha na kuondolewa kwake kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti ni usaliti “ambao hauwezi kuvumiliwa”.

 

Kulipiza kisasi

“Licha ya sisi kupambana kwa bidii na baadhi ya watu kupoteza maisha yao, mienendo ya mgombea wetu wa urais inashangaza na inaashiria usaliti wa kiwango cha juu,” akasema Bw Wetang’ula huku akiapa kulipiza kisasi.

Alisema ingawa yeye, Mudavadi na Kalonzo wamekuwa wakihimiza kuandaliwe mazungumzo ya kitaifa, utaratibu ufaao haukutumika kuanzisha mchakato huo.

Bw Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila mnamo Januari 30.

Alisema ni Raila mwenyewe aliyewashauri kutohudhuria halfa hiyo katika bustani ya Uhuru, Nairobi, ili waweze kumtetea endapo angekamatwa.

“Ni Raila aliyetushauri kukaa kando, kwa hivyo ni makosa kwa wanachama wa ODM kututaja kama waoga kwa kutohudhuria sherehe hiyo ambayo kwa kweli haikuwa na maana,” Bw Wetang’ula akasema.

 

Fisi

“Kama fisi anataka kuwala wanawe, kwanza huanza kuwashutumu kwamba wananuka harufu inayofanana na ya mbuzi,” akaeleza kwa mafumbo.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alisema yeye na wenzake hawatakubali kutolewa kafara na Raila, akisema wamejipanga kukabiliana naye na Rais Kenyatta bila woga.

“Sasa hafai kujihushisha na masuala ya NASA. Aelekeze nguvu zake katika ushirikiano kati yake na Jubilee na sasa tuko tayari kuendelea na ajenda za upinzani,” Bw Wetang’ula amasema.

Seneta huyo alisema ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa.

“Kondoo amekuwa na wasiwasi kuhusu mbwa mwitu kwa miaka mingi lakini aliishia kuliwa na mchungaji,” Wetang’ula akasema.

 

Matano aitaka Ingwe imfidie Sh4.9 milioni kwa kumsimamisha kazi

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Robert Matano anataka fidia ya Sh4.9 milioni kutoka kwa klabu ya AFC Leopards iliyomsimamisha kazi kabla ya kandarasi yake kumalizika.

Kulingana tovuti ya Goal, Matano, ambaye alijiunga na Ingwe tena mnamo Julai 10 mwaka 2017 baada ya kuinoa mwaka 2010 na 2011, ametumia kampuni ya mawakili ya Kiplagat & Company Advocates kushtaki waajiri hao wake wa zamani.

“Barua kutoka kwa kampuni hiyo, ambayo imeandikiwa maafisa wa Leopards, inaamrisha klabu hiyo ilipe Matano Sh700, 000 kwa kumfuta kazi, marupuru ya Sh63, 000 ya kushinda mechi ambayo hakuwa amelipwa na fidia ya kusimamishwa kazi kwa njia isiyofaa ya Sh350, 000 kila mwezi kwa miezi 12 (Sh4.2 milioni).

Ukijumlisha utapata Leopards inafaa kulipa Matano Sh4.9 milioni chini ya siku saba zijazo,” tovuti hiyo imenukuu mawakili hao wakisema.

Msimu huu, Matano aliongoza Leopards katika mechi tatu za ligi akipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Ulinzi Stars, sare ya 1-1 dhidi ya Posta Rangers na kulemewa 2-1 na Sofapaka.

Aliandikisha sare mbili katika mashindano ya Afrika ya Confederations Cup baada ya Ingwe kukabwa 1-1 mjini Machakos kabla ya kupiga sare tasa dhidi ya Fosa Juniors ya Madagascar.

Tangu Matano aondolewe majuma mawili yaliyopita, Leopards imepepeta SoNy Sugar 2-0, Mathare United 4-3, Wazito 3-2 na Kakamega Homeboyz 2-1 chini ya kocha Mtanzania Dennis Kitambi.

Starlets wasalia 108 duniani viwango vya FIFA

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets ya Kenya imekwamilia nafasi ya 108 kwenye viwango bora vipya vya soka ya wanawake duniani vilivyotangazwa na Shirikisho la Soka duniani (FIFA), Ijumaa.

Wapinzani wa Kenya katika mchuano wa kirafiki utakaopigwa Machi 25, Shepolopolo ya Zambia, wameteremka nafasi mbili hadi nambari 98 duniani.

Kenya, ambayo inanolewa na makocha David Ouma na Richard Kanyi, iliondoka nchini Alhamisi mapema asubuhi kuelekea Zambia kwa mchuano huo utakaochezewa mjini Kitwe.

Starlets itatumia mechi hii kujipiga msasa kabla ya kupepetana na Uganda kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2018 litakaloandaliwa nchini Ghana kutoka Novemba 17 hadi Desemba 1.

Kenya itaalika Uganda hapo Aprili 4 kabla ya kuelekea ugenini kwa mechi ya marudiano mnamo Aprili 8.

Uganda imeshuka nafasi saba katika viwango bora vya FIFA. Iko katika orodha ya mataifa ambayo hayajajishughulisha kusakata mechi za kimataifa kwa zaidi ya miezi 18.

Mechi ya mwisho ya Kenya ya kimataifa ilikuwa dhidi ya Zambia mnamo Septemba 23, 2017. Starlets, ambayo ilikuwa imealikwa kushiriki mashindano ya Afrika ya Kusini (Cosafa) nchini Zimbabwe, ililemewa 4-2 na Zambia kwa njia ya penalti katika mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba baada ya muda wa kawaida kumalizika 1-1.

Kabla ya kupigwa breki na Zambia, Kenya ilikuwa imetesa katika mashindano hayo kwa kuzaba Msumbiji 5-2, Mauritius 11-0 na Swaziland 1-0 katika mechi za Kundi B. Ilipepetwa 4-0 na Zimbabwe katika nusu-fainali.

Vikosi:

Kenya

Makipa – Pauline Atieno, Maureen Shimuli;

Mabeki – Dorcas Shikobe, Wendy Achieng, Carolyne Anyango, Lilian Adera, Vivian Nasaka, Esther Nadika, Pauline Musungu, Wincate Kaari;

Viungo – Cheris Avilia, Dorris Anyango, Sheryl Angachi, Caroline Kiget, Corazone Aquino;

Washambuliaji – Mwanahalima Adam, Mercy Achieng, Phoebe Owiti, Neddy Atieno, Cynthia Shilwatso.

Zambia

Makipa – Catherine Musonda, Annie Namoonje, Bupe Mwanza, Maleta Muwindwa, Yolanta Haankanga;

Mabeki – Jacqueline Nkole, Margaret Belemu, Mercy Nthala, Lweendo Chisamu, Jane Chalwe, Esther Siyafukwe, Mweemba Lushomo;

Viungo – Mary Mwakapila, Maylan Mulenga, Hellen Chanda, Rachael Lungu, Prisca Chilufya, Rabecca Nyirenda, Rexina Lutaka, Mary Mambwe, Rhoda Chileshe, Aliness Kasoma, Womba Chimuachi;

Washambuliaji – Misozi Zulu, Racheal Kundananji, Theresa Chewe, Agness Musesa, Avel Chitundu, Lydia Mubanga, Muyoi Luwi.

Itawabidi Stars kujikakamua zaidi kuzima Comoros na CAR, asema Wanyama

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars italenga kujisukuma hata zaidi kupata matokeo mazuri katika mechi zijazo kutokana na motisha ya kunyakua taji la Afrika Mashariki na Kati mwezi Desemba mjini Machakos, nyota Victor Wanyama amesema.

Akizungumza Alhamisi nchini Morocco kabla ya Stars kupimana nguvu na Comoros (Machi 24) na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) hapo Machi 27, kiungo huyu wa Tottenham Hotspur amesema, “Tuna motisha kutokana na ushindi wa mashindano ya Cecafa Senior Challenge Cup. Tunataka kuonyesha bidii hiyo na kuendeleza fomu hiyo katika mechi zijazo.”

Wanyama ni mmoja wa wachezaji 16 kutoka nchi za kigeni walioitikia mwito kocha Stanley Okumbi kushiriki michuano hii itakayoathiri msimamo wa Kenya kwenye viwango bora vya soka duniani.

Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya 105 duniani, itatumia michuano hii kujipiga msasa kabla ya kupepetana na Ghana katika mechi yake ya pili ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019.

Vijana wa Okumbi watajipata pabaya kwenye viwango bora vya dunia wakipoteza dhidi ya nambari 132 Comoros na nambari 121 Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwezi Juni mwaka 2017, Kenya ilizimwa 2-1 na Sierra Leone katika mechi ya ufunguzi ya Kundi F ya kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2019. Timu nyingine katika kundi hili ni majirani Ethiopia, ambao waliaibishwa 5-0 na Ghana katika mechi yao ya kwanza.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa

Patrick Matasi (Posta Rangers), John Oyemba (Kariobangi Sharks), Faruk Shikalo (Bandari)

Mabeki

Harun Shakava (Gor Mahia), Musa Mohammed (FK Tirana, Albania), Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), David Ochieng, (IF Brommapojkarna, Uswidi), David Owino (Zesco, Zambia), Abud Omar (Slava Sofia, Bulgaria)

Viungo

Patilah Omoto (Kariobangi Sharks), Francis Kahata (Gor Mahia), Duncan Otieno (AFC Leopards), Samuel Onyango (Gor Mahia), Athuman Ismael Gonzales (CF Fuenlabrada, Uhispania), Anthony Akumu (Zesco, Zambia), Victor Wanyama (Tottenham Hotspurs, Uingereza), McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), Johanna Omollo (Cercle Brugge KSV, Ubelgiji), Paul Were (FC Kaisar, Kazakhstan), Eric Johana Omondi (IF Brommapojkarna, Uswidi)

Washambuliaji

Ayub Timbe (Heilongjiang FC, Uchina), Cliffton Miheso (Buildcon FC, Zambia), Erick Kapaito (Kariobangi Sharks), Jesse Were (Zesco FC, Zambia), Michael Olunga (Girona FC, Uhispania).

Pigano la Okwiri na Ouma laahirishwa hadi Aprili 18

Na GEOFFREY ANENE

PIGANO la kimataifa la uzani wa ‘welter’ kati ya Mkenya Rayton Okwiri na Mganda Kassim Ouma hapo Machi 30 limeahirishwa hadi Aprili 18, 2018.

Okwiri, ambaye anaishi na kufanyia mazoezi yake Marekani, alitangaza kubadilishwa kwa tarehe hiyo Machi 21 kupitia mtandao wake wa Facebook.

“Pigano langu, ambalo liliratibiwa kufanyika Machi 30 limesukumwa mbele hadi Aprili 18,” alisema Okwiri, ambaye siku chache zilizopita alikuwa ametangaza amejiandaa vyema na yuko tayari kutua jijini Nairobi kwa pambano hilo lililopangiwa kuandaliwa katika Jumba la Mikutano la KICC.

Okwiri na bingwa wa zamani wa taji la kimataifa la IBF, Ouma, walipangiwa kulimana katika pigano lisilo la taji, lakini muhimu sana.

“Ni pigano litakaloamua bondia atakayepata tiketi ya kuwania taji la dunia la WBA mwezi Juni. Pigano kati yangu na Ouma ni mechi ya kufuzu kushiriki pigano la Juni,” Okwiri aliambia Taifa Leo katika mahojiano ya kipekee kutoka Marekani.

Utepetevu hospitalini KNH unavyomsababishia mama uchungu

Na GEOFFREY ANENE

HOSPITALI ya Kitaifa ya Kenya (KNH) inamulikwa tena kwa madai ya kumfanyia mama mmoja upasuaji vibaya wakati wa kujifungua.

Susan Nekesa anasema alitembelea hospitali hii maarufu akihisi uchungu wa uzazi Januari 25 na kujifungua watoto wawili pacha siku iliyofuata.

Hata hivyo, saa chache baada ya upasuaji huo, tumbo lake lilivimba na akaanza kusikia maumivu makali.

Uchungu aliohisi, aliambia runinga ya Citizen, ulikuwa mbaya sana kiasi cha kumfanya asiongee.

Katika ripoti yake, Nekesa anajikokota kukaa kwenye kitanda chake, huku machozi yakimtoka.

Huku akilia, anasimulia kisa hicho akisema, “Naomba Mungu nisipoteze uwezo wangu wa kukumbuka.”

“Nilipokuja kumuona, nilipata amefura tumbo,” dadake Nekesa, Evelyn Anindo anasema.

“Tumbo lake pia lilikuwa moto sana na hakuwa anaweza kuzungumza. Tuliwasiliana kupitia ishara.”

Baada ya kulalamikia maafisa wa matibabu wa KNH, Nekesa alirudishwa katika chumba cha kufanyiwa upasuaji, na ni wakati huo madaktari walikiri walikuwa wamefanya kosa.

“Iligunduliwa kwamba upasuaji ulifanywa vibaya,” anasema Robert Sitati, bwanake Nekesa.

“Sehemu ya matumbo madogo, karibu sentimita 50, ilikuwa nje ya mahali inatakiwa kuwa,” anasema.

Kurekebisha hali hiyo, madaktari waliondoa sehemu iliyoathirika na kuacha mwanya mdogo (unaoitwa stoma) kumwezesha kupitisha uchafu kupitia mfuko maalum (colostomy).

Mgonjwa huyu pamoja na familia yake walisalia na matumaini kuwa atapata afueni na kurejea nyumbani na watoto hao pacha.

Ndani ya Hospitali Kuu ya Kenyatta. Picha/Hisani

Hata hivyo, familia ilipokea habari za kuhuzunisha Jumanne kwamba mtoto mmoja ameaga dunia.

“Walisema kwamba mtoto wangu alikuwa na shimo kwenye moyo wake,” anasema Nekesa kwa huzuni.

Hata hivyo, mumewe Nekesa anasema aliambiwa na mfanyakazi mmoja wa KNH kwamba mtoto wao alisongwa na maziwa.

“Mtu aliniambia kwamba mtu aliyekuwa akimpa mtoto wangu maziwa hakuwa na ujuzi,” Sitati anasema.

Kilichofuata masaibu ya Nekesa, ambaye anaomboleza kifo cha mtoto wake, ni kipindi cha huzuni, kutelekezwa na machungu dhidi ya madaktari wa KNH, ambao hawakufanya kazi yao vyema.

“Hakuna anayemshughulikia,” anasema Anindo.

“Mfuko huo maalum ukijaa, mzigo ni wake mwenyewe kujikokota hadi kwenye chumba cha kujisaidia kuufanya uwe tupu.”

Kwa wakati huu, familia yake imeshindwa la kufanya, huku hospitali hii ikiwaomba wawe na subira kwa sababu haina washauri wa kushughulikia Nekesa.

Mapema mwezi huu wa Machi, madaktari wanaojiongeza masomo waligoma baada ya wenzao kusimamishwa kazi kwa muda kutokana na upasuaji wa kichwa uliofanyiwa mgonjwa tofauti na yule alistahili kufanyiwa.

Sitati anasema hospitali hiyo imemuonya dhidi ya kuhamisha mke wake ikisema atalipia ada yote ya hospitali mwenyewe akiondoka KNH.

Nekesa anatumai siku moja atapata kuona watoto wake tena. “Wameniweka hapa kwa muda mrefu sana…Nimekuwa nikivumilia nikitumai kwamba siku moja nitaenda kuona watoto wangu,” anasema.

KNH mashakani tena kufuatia upasuaji ovyo wa utumbo

Eneo la matibabu ya dharura katika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

HOSPITALI Kuu ya Kenyatta imejipata mashakani tena kufuatia madai kwamba mwanamke aliyekuwa akijifungua kupitia upasuaji aliathirika baada ya kupasuliwa visivyo.

Mwanamke huyo, Susan Nekesa anasema alifika katika hospitali hiyo Januari 25 na akajifungua siku iliyofuata.

Hata hivyo saa kadhaa baada ya upasuaji, tumbo lake lilivimba na akapata maumivu makali.

Akiongea na runinga ya Citizen Jumatano, mwanamke huyo alisema maumivu yalimzidi akashindwa kuongea.

Kwenye mahojiano na runinga hiyo Nekesa alionekana akitatizika kuketi kitandani huku akitokwa machozi na kusema anachoomba ni asipoteze uwezo wa kukumbuka mambo.

“Nilipokuja kumuona, nilipata tumbo lake likiwa limevimba. Tumbo lilikuwa na joto sana na hangeweza kuongea,” dadake Evelyn Anindo, alisema.

Alipolalamikia hospitali ya KNH, Nekesa alirudishwa katika chumba cha upasuaji na madaktari wakakiri kwamba walikuwa wamefanya makosa.

“lligunduliwa kuwa upasuaji haukuwa umefanywa vyema,” alisema Robert Sitati, mume wa Nekesa.

“Sehemu ya utumbo wake, yaani sentimita 50 ilikuwa nje ya unapopaswa kuwa,” alisema.

Ili kurekebisha hali, madaktari walitoa sehemu iliyoathiriwa na kuacha shimo ndogo

( inayofahamika kama stoma) ili aweze kupitishia choo kupitia mfuko. Familia yake iliomba aweze kupona  ili aruhusiwe kwenda nyumbani na watoto wake pacha.

Hata hivyo, mnamo Jumanne familia ilifahamishwa kuwa mmoja wa watoto hao alikuwa amekufa.

 “Walisema mtoto wangu alikuwa na tundu kwenye roho,” alisema Nekesa kwa uchungu.

Hata hivyo, mumewe alisema alifahamishwa na mfanyakazi wa KNH kwamba mtoto huyo alilishwa na mtu asiyekuwa na ujuzi wa kulisha watoto akasakamwa na maziwa kooni.

Huku akiendelea kuomboleza kifo cha mtoto wake, Nekesa anakabiliwa na wakati mgumu na uchungu kwa madaktari anaodai wamempuuza hata baada ya kusababishia hali hiyo.

 “Hakuna anayemshughulikia,” alisema Evelyn.

Baada ya mfuko anaotumia kupitishia choo kujaa, ni yeye anayeng’ang’ana kwenda chooni kutupa uchafu.

Familia yake imechanganyikiwa huku hospitali ikiwafahamishwa kuwa haina wataalamu wa kumhudumia  na kuwataka wawe na subira.

Sitati anasema hospitali imemuonya dhidi ya kumhamishia mkewe hospitali nyingine .

Ni kivumbi Kenya na Uzbekistan zikiumiza nyasi

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache kabla ya timu za soka za Olimpiki za Kenya na Uzbekistan kupimana nguvu, kambi zote mbili zimeapa kuonyeshana kivumbi Machi 23 na Machi 26, 2018.

Kipa wa Ulinzi Stars, Timothy Odhiambo, ambaye ni nahodha wa timu ya Kenya, amenukuliwa na Shirikisho la Soka la Uzbekistan (UFF) akisema, “Hatuko hapa kutalii, bali tunataka kurejea jijini Nairobi na ushindi. Lengo letu ni kubwaga Uzbekistan.”

“Tulikuwa na habari finyu kuhusu timu ya Uzbekistan hadi pale iliposhinda taji la Bara Asia mapema mwaka huu,” Odhiambo aliongeza na kushukuru wananchi wa Uzbekistan kwa mapokezi mema.

Mvamizi wa Uzbekistan Bobur Abdukhalikov amebashiri kwamba michuano hiyo ya kirafiki ya Under-23 haitakuwa rahisi.

Katika mahojiano na UFF, mshambuliaji huyu wa klabu ya Nasaf amesema, “Mechi dhidi ya Kenya si rahisi. Hata hivyo, tutajikakamua kuweka tabasamu katika nyuso za mashabiki wetu.”

Kocha mkuu wa Uzbekistan, Ravshan Haydarov anaamini vijana wake wamejiandaa vyema. “Tuna mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu ya Olimpiki ya Kenya. Tumechukulia maandalizi yetu kwa uzito mkubwa. Tutajaribu kufurahisha mashabiki wetu kwa kutandaza soka safi na pia kupata ushindi,” Haydarov amesema.

Kenya, ambayo inanolewa na kocha Francis Kimanzi, na Uzbekistan zinajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020. Droo ya michujo hiyo bado haijatangazwa.

Gor kukabana na SuperSport United Confederations Cup

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia watapigania tiketi ya kuingia mechi za makundi za mashindano ya Afrika ya Confederations Cup dhidi ya SuperSport United.

Vijana wa kocha Dylan Kerr walikutanishwa na mabingwa hawa mara tatu wa Afrika Kusini katika droo iliyofanywa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) Jumatano jioni jijini Cairo, Misri.

Gor ilijipata katika mashindano haya ya daraja ya pili baada ya kupigwa 1-0 na Esperance ya Tunisia mnamo Machi 18, 2018 na kubanduliwa nje kwa jumla ya bao 1-0.

Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya Gor na Esperance ilimalizika 0-0 uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Machi 7.

Gor ilirejea nchini kutoka Tunis hapo Machi 19 asubuhi. Mabingwa hawa mara 16 wa Kenya wataalika SuperSport nchini Kenya mnamo Aprili 6 kabla ya kusakata mechi ya marudiano nchini Afrika Kusini hapo Aprili 17.

Klabu zingine kutoka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) zinazoshiriki Confederations Cup ni Rayon Sport (Rwanda), Al-Hilal Al-Ubayyid na Al-Hilal (Sudan) na Young Africans (Tanzania).

Rayon itakabiliana na Club Deportivo Do Sol kutoka Msumbiji nayo Yanga ichapane na Welayta Dicha kutoka Ethiopia katika mechi za kuingia makundi.

Al-Hilal Al-Ubayyid na Al-Hilal zitalimana na UD Songo (Msumbiji) na Akwa United (Nigeria), mtawalia.

Droo ya Klabu Bingwa Afrika pia imefanywa Jumatano. Kampala Capital City Authority (KCCA), ambayo ilipimana nguvu na Gor kabla ya kuanza kampeni yake, itapepetana na miamba Al Ahly (Misri) na Township Rollers (Botswana) na Esperance (Tunisia) katika Kundi A.

Kundi B linaleta pamoja TP Mazembe (DR Congo), Moulidia (Algeria), Difaa Hassani El Jadidi (Morocco) na E.S. Setif (Algeria).

Togo Port de Lome (Togo), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Wydad (Morocco) na Horoya (Guinea) ziko katika Kundi C nayo Zesco United, ambayo imeajiri Wakenya Jesse Were, Anthony Akumu na David Owino, iko Kundi D pamoja na Primeiro de Agosto (Angola), ESS (Tunisia) na Mbabane Swallows (Swaziland).

Seneta Linturi apambana mahakamani kuhusu digrii

Mawakili Profesa Tom Ojienda (kulia), James Orengo na Seneta Mithika Linturi wakiwa na watu wengine kortini Machi 21, 2018. Picha/ RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Meru Mithika Linturi Jumatano alipambana katika Mahakama Kuu kufa kupona aruhusiwe kuhitimu digirii ya uzamili katika somo la Uanasheria.

Jaji George Odunga aliombwa akishurutishe Chuo Kikuu  cha Nairobi (UoN) kimkubalie ahitimu huku Bw Linturi akisema jina lake liliondolewa katika orodha ya mahafala mnamo Desemba 22, 2017 na “kumuaibisha sana.”

Mwanasiasa huyo anayewakilishwa na mawakili wenye tajriba ya juu Seneta James Orengo na Profesa Tom Ojienda alisema hakupewa fursa ya kujitetea dhidi ya madai kwamba alikuwa ameghushi digrii ya kwanza kutoka chuo kikuu kimoja cha ng’ambo.

Bw Linturi alisema UoN kilimdhihaki pakubwa kilipoondoa jina lake katika orodha ya mahafala dakika ya mwisho.

“Wakufunzi wa Bw Linturi walisema alikuwa amepita mitihani na kuidhinishwa kisha jina lake likachapishwa katika orodha ya waliohitimu,” alisema Prof Ojienda.

Wakili  huyo aliwasilisha mbele ya Jaji Odunga karatasi za mitihani iliyokuwa imesahihishwa na kuomba mahakama ifutilie mbali uamuzi wa kumzuia Bw Linturi kuhitimu.

Mawakili Orengo na Prof Ojienda waliwasilisha risiti za kuonyesha jinsi Bw Linturi alikuwa amelipa karo na  kutimiza masharti yote ya chuo kikuu.

Lakini wakili Donald Kipkorir anayekitetea chuo hicho cha UoN, Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC), afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) alipinga kesi ya Bw Linturi  na kusema hatua ya kuondoa jina la mwanasiasa huyo kutoka kwa orodha ya mahafala ilifaa.

“UoN kilipashwa habari za kutohitimu kwa Bw Linturi alipokuwa akisoma ng’ambo kabla ya kukubaliwa kuendelea na masomo ya juu humu nchini,” alisema Bw Kipkorir.

Wakili huyo alimsihi Jaji George Odunga atupilie mbali kesi ya Bw Linturi kwa vile alifukuzwa kutoka chuoni na ‘sio mwanafunzi tena wa Chuo Kikuu cha Nairobi.”

Bw Kipkorir alieleza korti kwamba ufisadi ukiguduliwa hatua huchukuliwa na “hivyo ndivyo UoN kilifanya kilipofahamishwa na EACC na IEBC kuhusu vyeti vya mlalamishi.”

Kiongozi wa mashtaka kutoka afisi ya DPP Ashimoshi Shitambashi aliomba Jaji Odunga  atupilie mbali ombi la Bw Linturi la kuzuia akichukuliwa hatua ya kisheria ikiwa ni pamoja na kushtakiwa.

EACC na IEBC ziliomba korti iruhusu sheria ifuate mkondo na hatua ichukuliwe dhidi ya Bw Linturi.

Jaji Odunga atatoa uamuzi Aprili 25, 2018.

Wakazi wa Githurai 45 waiomba mahakama imwachilie polisi akawahudumie

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Jumatano iliombwa imwachilie afisa wa polisi Titus Ngamau Musila na mwanamuziki wa bendi ya ‘Kithangaini Lipua Lipua’  anayekabiliwa na shtaka la mauaji.

Jambo la kushangaza ni kwamba wakazi wa Githurai ambapo afisa huyo alikuwa akifanyakazi waliiomba korti imwachilie ndipo arudi kuwahudumia.

“Naomba hii mahakama itilie maanani wito na kilio cha wakazi wa Githurai 45 kwamba Katitu aachiliwe arudi kuwatumikia,” alisema wakili Cliff Ombeta.

Na wakati huo huo kiongozi wa mashtaka Catherine Mwaniki aliambia korti “amua kulingana na kilio cha wakazi wa Githurai na wito wa jamii ya mshtakiwa.”

Wote walikubaliana kuwa  “Katitu ni mzuri aachiliwe.”

Facebook yashtakiwa huku thamani yake ikishuka kwa kuruhusu Cambridge Analytica kudukua akaunti

Na REUTERS na CHARLES WASONGA

FACEBOOK na kampuni ya kutoa ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica zimeshtakiwa nchini Amerika kwa kutoa habari za siri za zaidi ya watu 50 milioni wanaotumia huduma za mtandao huo wa kijamii, bila idhini yao.

Kesi hiyo iliyowasilishwa Jumanne jioni na Lauren Price, mkazi wa Maryland, ni ya kwanza dhidi ya Facebook kutokana na kutomakinika kwake kulinda data za wateja wake.

Pia ni kesi ya kwanza dhidi ya kwa kutumia data hiyo, bila idhini, kwa ajili ya kupiga jeki kampeni za Rais Donald Trump katik kampeni za kuelekea uchaguzi wa Novemba 2016.

“Kila mtumiaji mtandao wa Facebook ni mhusika katika kesi hii kwani data zao zilitwaliwa bila idhini yao. Kwa hivyo, haki yao ya usiri imeingiliwa,” John Yanchunis, ambaye ni wakili wa Price, alisema kwenye mahojiano kwa njia ya siku Jumatano.

Kesi hiyo imewasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya San Jose, jimboni California, Amerika.

Iliwasilishwa saa kadhaa baadaya  Facebook kuelekezewa lawama katika kesi nyingine iliyowasilishwa na mwenyehisa mmoja aliyedai bei ya hisa zake zilishuka baada ya sakata hiyo kufichuliwa. Kesi hiyo ya pili iliwasilishwa katika mahakama ya San Francisco.

Bei ya hisa za Facebook  ilipungua kwa takriban dola 50 bilioni (Sh5 bilioni) kwa kipindi cha siku mbili pekee.

Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, Facebook na Cambridge Analytica (yenye makao yake jijini London) hazikuwa zimetoa kauli zao kuhusu tuhuma hizo.

Bi Price anazisuta Facebook na Cambridge Analytica kwa kutokamikinika na kukiuka sheria kuhusu ushindani sawa unaotumika jimboni California.

Alisema Facebook ilikiuka sera yake kuhusu usiri kwa kutoa maelezo/data za wateja wake bila idhini yao.

“Mteja wetu alikuwa akipata jumbe za kisiasa katika ukurasa wake wa facebook wakati wa kipindi cha kampeni. Hukuwa amewahi kuona jumbe kama hizo wakati mwingine,” Yanchunis akasema.

“Hakuelewa kilichokuwa kikiendelea wakati huo lakini saa ameng’amua kuwa jumbe hizo zilenga kumshawishi kupitia upande kura kura.

 Mlalamishi anataka kulipwa ridhaa ya kiwango ambacho hakutaja, pamoja na adhabu kali kwa Facebook na Cambridge Analytica.