Kenya yang’aa kwenye tenisi U-12

Na GEOFFREY ANENE

WANATENISI wa Kenya waling’aa katika mashindano ya Afrika Mashariki ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 12 yaliyokamilika Februari 8, 2018 jijini Kigali.

Wenyeji Rwanda walitwaa taji la wasichana wakifuatwa na Wakenya, Burundi na Uganda katika usanjari huo. Rwanda pia iliibuka mshindi katika kitengo cha wavulana ikifuatiwa na Burundi, Kenya na Uganda, mtawalia.

Katika siku ya mwisho, Kenya ilipepeta Burundi kwa mechi 3-0 katika kitengo cha wasichana na kulaza Uganda kwa mechi 2-1 katika kitengo cha wavulana.

Kwenye kitengo cha wasichana cha mchezaji mmoja mmoja, Anouk Vandevelde alimlima Zaituni Akesa 6-0, 6-0 naye Reha Kipsang’ akamshinda Milka Nkeshima japo kwa jasho 6-4, 6-4. Ushirikiano wa Vandevelde na Kipsang’ uliwabwaga Akesa, ambaye alishirikiana na Kinzey Umuvyeyi, 6-2, 6-0.

Kwenye kitengo cha wavulana, Liberty Kibue alilemea Allan Otto 6-1, 6-0 naye Raqeem Virani akapigwa 6-1, 6-4 na Troy Zziwa. Ushirikiano wa Kibue na Virani ulifanikiwa kuchapa Brian Kimera na Zziwa 7-5, 6-0 katika kitengo cha wachezaji wawili wawili na kushinda Waganda hao kwa mechi 2-1.

Rwanda pia ilikuwa na siku nzuri Alhamisi ilipopepeta Uganda 3-0 (wasichana) na Burundi 2-1 (wavulana).

Mashindano haya yaliyovutia Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda, yalianza Machi 4 na kukamilika Machi 8.

Wanyama ashinda tuzo ya goli bora la Februari EPL

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Wanyama ameshinda tuzo ya goli bora la mwezi wa Februari mwaka 2018 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, Ijumaa.

Nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, aliwapiku mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2017 Mohamed Salah (Liverpool & Misri) pamoja na Sergio Aguero (Manchester City & Argentina), Jose Izquierdo (Brighton & Hove Albion & Colombia), Adam Smith (Bournemouth & Uingereza) na Mario Lemina (Southampton & Gabon).

Kiungo huyu mkabaji wa Tottenham Hotspur alivuta kiki zito kutoka nje ya kisanduku lililosaidia klabu yake kutoka 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield hapo Februari 4.

Katika mchuano huo, Wanyama aliingia kama nguvu-mpya katika dakika ya 79 akijaza nafasi ya Mbelgiji Mousa Dembele. Aliona lango dakika moja baadaye akiisawazishia Spurs 1-1.

Mvamizi hodari Harry Kane alikosa nafasi ya kuweka Spurs 2-1 juu alipopoteza penalti dakika ya 87 kabla ya Salah kupachika bao tamu dakika ya 91 lililowania tuzo ya goli bora la Februari.

Kane alipata nafasi nyingine ya kufuma penalti dakika ya 95 na akaifunga, huku mechi hiyo ikatamatika 2-2. Salah alifunga mabao yote ya Liverpool dhidi ya Tottenham siku hiyo.

Bao la Aguero lilikuwa dhidi ya Leicester City mnamo Februari 10.

Kirwa, Cheshari na Kosgei kushiriki Hannover Marathon

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Gilbert Kirwa, Jacob Cheshari na Recho Kosgei wameingia mbio za kilomita 42 za Hannover Marathon zitakazoandaliwa nchini Ujerumani mnamo Aprili 8, 2018.

Taarifa kutoka Shirikisho la Riadha duniani (IAAF) zinasema Kirwa ataanza kitengo cha wanaume kama mgombea halisi wa taji naye Mjerumani Fate Tola anapigiwa upatu kutetea ubingwa wa wanawake.

Kirwa na Tola pia wamepigiwa upatu kuvunja rekodi za Hannover Marathon za saa 2:08:32 (wanaume) na 2:27:07 (wanawake) zinazoshikiliwa na washindi wa mwaka 2013 Lusapho Aprili (Afrika Kusini) na Olena Burkovska (Ukraine).

Muda bora wa Kirwa ni saa 2:06:14 naye Tola anajivunia kutimka kasi ya juu ya 2:25:14.

Kirwa alinyakua mataji ya Vienna Marathon (Austria) na Frankfurt Marathon (Ujerumani) kwa saa 2:08:21 na 2:06:14 mwaka 2009, mtawalia.

Amekuwa akisumbuliwa na majeraha. Hajashiriki mashindano yoyote mwaka 2018. Mpinzani wake mkuu ni Cheshari, ambaye alishinda Hannover Marathon mwaka 2015 kwa saa 2:09:32.

Anajivunia muda wake bora wa saa 2:07:46 alioweka alipomaliza Frankfurt Marathon katika nafasi ya nne mwaka 2013. Raia wa Poland, Henryk Szost, ambaye anajivunia muda bora wa saa 2:07:39, hawezi kupuuzwa.

Tola, ambaye alibadili uraia kutoka Ethiopia hadi Ujerumani mwaka 2016, alishinda Hannover Marathon mwaka 2017 kwa saa 2:27:48. Alikosa rekodi ya Burkovska pembamba.

Kosgei, ambaye taji la Warsaw Marathon nchini Poland lilimponyoka akiona aliposhiwa nguvu zikisalia mita 800 mwaka 2017, na Mchina Yue Chao ni baadhi wa washindani wakuu wa Tola. Muda bora ya Chao na Kosgei ni saa 2:29:26 na 2:30:09, mtawalia.

Magufuli apiga marufuku maandamano nchini mwake

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli amepiga marufuku maandamano yoyote yasiyoidhinishwa na serikali yake.

Akiongea katika mkutano wa hadhara kaskazini mwa Tanzania, kiongozi huyo Ijumaa alionya kuwa yeyote atakayedhubutu kupanga na kushiriki maandamano, haswa ya kupinga utawala wake, ataadhibiwa vikali.

Alisema maandamano kama hayo ya kisiasa huathiri mkondo wa mageuzi ya kiuchumi aliyoanzisha pamoja na vita dhidi ya ufisadi.

Tangu Bw Magufuli alipoinga mamlakani mnamo Novemba 2015, serikali yake imeanzisha mageuzi ya kiuchumi na vita vikali dhidi ya ufisadi.

JAMVI: Raila apania kujaribu bahati yake Ikulu kwa mara ya tano?

Na BENSON MATHEKA

Kitendawili kuhusu iwapo kinara wa NASA Raila Odinga anapanga kugombea urais kwa mara ya tano kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 kimezonga muungano huo wa upinzani.

Wadadisi wanasema  japo wandani wake wa kisiasa wanamshinikiza kujaribu bahati yake tena 2022 atakapokuwa na umri wa miaka 77, Bw Odinga anajikuna kichwa kwa sababu ya mkataba wa maelewano aliotia  sahihi na vinara wenza katika NASA kwamba hatagombea urais tena.

“Ukifuatilia kwa makini kinachoendelea katika chama cha ODM, utabaini kuna msukumo fulani unaolenga Bw Odinga kugombea 2022 na kukiuka mkataba wake na vinara wenzake.

Kitendawili ni iwapo atafaulu akigombea peke yake au iwapo ni kuunda muungano mpya wa kisiasa na uwezo wa muungano huo kumfaidi,” asema mwanasiasa wa NASA ambaye hakutaka tutaje jina lake kwa sababu ya jukumu analotekeleza katika muungano huo.

Kulingana na mwanasiasa huyo, Bw Odinga mwenyewe anajivuta kukubali mipango ya wandani wake wa kisiasa katika ODM ambao wanapanga mikakati ya chama chao kutema wenzao katika NASA.

“Kwa Bw Odinga, NASA haijafanikiwa katika jukumu lake kuu la kupigania haki katika uchaguzi ambayo vinara wenzake Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wanakubali kwamba ni lazima iwapo uchaguzi wa 2022 utakuwa huru na haki.

Hata hivyo, shinikizo za wandani wake katika ODM wanaowachukulia vinara wenza kama waoga zinamfanya kujikuna kichwa na akiwaachia kuamua mambo, hatakuwa na jingine ila kuondoka NASA. Kitendawili ni kuwa ODM kikiondoka NASA kitaelekea wapi?”  anahoji mdadisi wa masuala ya kisiasa David Wafula.

 

Wasiwasi

Anasema kwamba kwa ODM kuagiza tathmini ya uchaguzi mkuu kuanzia 2007 na ushirikiano wake na vyama vingine vya kisiasa, vyama vingine tanzu vya Wiper, ANC na Ford Kenya vinafaa kuwa na wasiwasi. Bw Odinga mwenyewe amekuwa akasisitiza kuwa NASA ingali imara na kutaja tofauti zinazoshuhudiwa katika muungano huo kama za kawaida.

“Usisubiri Bw Odinga atangaze mara moja kujitenga na vinara wenzake, mwenye macho haambiwi tazama. Kuna moshi katika NASA na ni wakati tu kabla ya moto kulipuka,”asema.

Vyama tanzu vya NASA vinaonekana kutegua kitendawili hicho kwa kueleza jinsi Bw Odinga alivyowapiga chenga vinara wenza kuhudhuria hafla ya kumuapisha kama rais wa wananchi ambayo wanasiasa wa ODM wamekuwa wakitumia kumtaka kujitenga vinara hao kwa kutohudhuria.

Kulingana na Bw Barrack Muluka ambaye ni Katibu Mkuu wa ANC, Bw Odinga aliwachezea shere vinara wenza kuhudhuria hafla hiyo.

“Wanaowaita vinara wenza waoga hawaelewi kilichotendeka. Nilikuwepo na nilikuwa nikisubiri Raila awasiliane na vinara wenza walivyokuwa wamekubaliana lakini badala ya kufanya hivyo, alipenya na kuelekea Uhuru Park kula kiapo, “ Bw Muluka alisema.

Kulingana na Bw Francis Ikedi, mdadisi wa siasa madai ya Bw Muluka yanawiana na ya aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye wiki jana alimlaumu Bw Odinga kwa kuwasaliti vinara wenza katika NASA na kuhudhuria hafla ya kiapo.

 

Mara tano

“Ukifuatilia yaliyotokea katika NASA tangu wakati huo wa kiapo Januari 30, utagundua kuna mwelekeo mpya katika ODM huku vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya vikionekana kujitenga na maamuzi ya chama cha chungwa japo vinara wamekuwa wakitoa taarifa zinazosemekana kuwa za pamoja.

Kuna kitendawili ambacho kitateguliwa muda unaposonga kuelekea 2022 na kinahusu iwapo Raila ana azma ya kuingia katika vitabu vya historia kama mmoja wa watu waliogombea urais kwa zaidi ya mara tano, “ alisema Bw Ikedi.

Mbali na Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Wetangula kuapa kuwa kwenye debe 2022, manaibu wa Bw Odinga, Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya ambao wamehudumu kipindi cha mwisho kama magavana wametangaza kuwania urais 2022.

Bw Ikedi anahoji kuwa huenda ODM ina njama za kumtenga Bw Musyoka kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ambaye chama chake cha Wiper kimekuwa kikimtaka Bw Odinga kumuunga mkono.

“Hii tathmini ya uchaguzi na ushirikiano na vyama vya kisiasa huenda inalenga Bw Musyoka ambaye wanasiasa wa ODM wanamchukulia kama kizingiti kikuu cha Bw Odinga kujaribu bahati tena 2022,” asema Bw Ikedi.

Kulingana na Bw Wafula hata ODM kikijiimarisha bila kushirikiana na vyama vingine hakiwezi kushinda uchaguzi na Bw Odinga anajua hivyo.

TAHARIRI: Mazungumzo ni hatua nzuri ya kukuza utaifa

Na MHARIRI

ALIPOAPISHWA mnamo Novemba 2017 katika uwanja wa michezo wa Kasarani kwa muhula wa pili, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuwaita viongozi wa upinzani na kujadiliana kuhusu mwelekeo wa kuchukua kama nchi.

Kauli yake ilitokana na mgawanyiko mkubwa uliopo hadi sasa, ambao chanzo chake ni kususiwa kwa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017.

Tungetaka kusifu Rais Kenyatta kwa kutimiza ahadi yake na kukutana na kinara wa NASA Raila Odinga, lakini tusisitize umuhimu wa kuhusishwa kwa viongozi wengine, haswa katika upinzani.

Tayari vinara wenza katika upinzani wametaja hatua ya Bw Odinga kukutana na rais peke yake kama usaliti wa kisiasa.

Japo mkutano wa rais na Bw Odinga umewapa wengi matumaini ya kutuliza joto la kisiasa nchini, ni vyema kutopuuza mchango wa vinara wenza katika upinzani Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.

Madhumuni ya kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga yawe kuunganisha Wakenya wote na wala si jamii au familia mbili.

Kilele cha joto la kisiasa kilikuwa hafla ya kumwapisha Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi,’ jambo ambalo lilivutia macho ya ulimwengu mzima.

Ukweli mchungu ni kuwa, Wakenya wamegawanyika katika makundi mawili. Kuna kundi linaloamini kuwa Rais Kenyatta ndiye kiongozi aliyechaguliwa na kuapishwa, kwa mujibu wa katiba. Kwa upande mwingine, wafuasi wa Bw Odinga nao wanasikiza tu kauli ya upinzani.

Uasi wa aina hii si mzuri kwa nchi. Ikiwa tunataka kuendelea mbele, na serikali ifanikiwe katika nguzo zake nne za maendeleo ilizojiwekea, basi lazima kuwe na mandhari tulivu ya kisiasa.

Ni matumaini yetu kuwa mkutano wa viongozi hao wawili ni mwanzo wa kulainisha siasa zetu kabla ya uchaguzi wa 2022.

Kando na wanasiasa, rais anapaswa kuwaita wadau wengine kufanya mazungumzo kuhusiana na masuala ibuka kutokana na uchaguzi uliopita, ili kukomesha hali ya wasiwasi na Kenya isonge mbele.

Mazungumzo ya kijamii pia yanafaa kutekelezwa kwa lengo la kukuza umoja, utangamano na amani miongoni mwa Wakenya.

Mimi ni kigugumizi, Jaji Mwilu afichua kuhusu maisha yake

Na WACHIRA MWANGI na PETER MWANGANGI

NAIBU Jaji Mkuu Philomena Mwilu amezungumzia maisha yake ya kibinafsi na kukiri kuwa yeye ni kigugumizi hasa baada ya kukoselewa kuhusiana na ufasaha wake wa kuongea, na jinsi alivyoibuka kuwa miongoni mwa wanawake watajika nchini.

Jaji Mwili ambaye aliapishwa Oktoba 28, 2016 na kuchukua nafasi iliyokuwa imeshikiliwa na Jaji Kalpana Rawal, ameelezea kuwa mahali alipofikia sasa pametokana na jitihada na nidhamu hata baada ya kupitia changamoto anazosema kuwa hazikustahili.

Wakenya wengi waliofuatilia kwa karibu kesi za uchaguzi wa urais 2017 wanakumbuka akikosolewa kwa mambo kadha ambayo ni pamoja na jinsi alivyokuwa akiongea.

“Mimi ni kigugumizi, Sina ufasaha wa kuongea, Siongei vyema sana, lakini naweza kupata maelezo, na ikiwa wanaonisikiliza wana utulivivu watapata kuelewa ninakoelekea,” alisema.

“Kwa hivyo, huwa ninahakikisha kuwa nina maelezo, kwa kuwa bila maelezo, nitaeleza nini wanaonisikiliza?” alieleza wanawake waliokusanyika katika hoteli ya Sarova Whitesands Resort Beach Resort, Mombasa wakati wa kongamano la Chama cha Mahasibu Wanawake (AWAK).

Hata hivyo, ingawaje anakumbwa na hali hiyo, alisema kuwa kuna watu wengi wanaohisi kuwa ana msimamo mkali.

“Nimejifunza kutotingisika, kwa sababu usipofanya hivyo watasema hakuna mwanamke anaweza kufikia hapa bila ya kusaidiwa na mwanamume chumbani, ama sehemu nyingine ya kushangaza,” alieleza.

Aliongeza, “La, hilo halikunifanyikia mimi, na halitanifanyikia. Sitahitaji mwanamume kunidumisha katika kazi hii, nitamhitaji Mungu.”

Jaji Mwilu ambaye alijiunga kama wakili wa Mahakama Kuu 1984 anasema kuwa alishangaa kusikia baadhi ya watu wakisema kuwa hawamfahamu alipokuwa akihojiwa kwa nafasi anayoshikilia sasa.

“Kuna mtu aliuliza, ‘Mwilu ni Nani’ Mbona unauliza. Mimi ni wakili, nimekuwa jaji na kufanya hili na lile,” anaeleza.

“Kuna nini ikiwa haujawahi kunisikia? Katiba inasema nini kuhusu kutobagua kwa misingi ya hali ama sababu nyingine? Inamaanisha kuwa unahitaji tu kuhitimu. Ikiwa kuna yeyote ambaye anataka kunipinga kwa kazi ninayofanya kila siku, niko tayari kupingana na mtu huyo,” anasema.

Hata hivyo, maisha hayajakuwa shwari kwake wakati wote, kwani alimpoteza babake mapema sana akiwa mtoto, jambo ambalo alisema liliibua changamoto kadha maishani mwake.

“Sikufanya vyema sana katika Darasa la Saba, na nashukuru kuwa sikufanya vyema kwa kuwa hapo ndiyo nilizinduka na kuamua kukomesha mzaha wa alama nilizopata. Kutoka hapo, sijawahi kuangalia nyuma na nimeshindana na wale bora zaidi,” anasema.

Kuhusiana na kazi anayofanya sasa, Jaji Mwilu alisema wanawake hawana nafasi sawa na wanalazimika kung’ang’ana kuweza kufikia nyadhifa za juu.

 

Amerika yataja Wakenya wawili magaidi sugu wa kimataifa

Na KEVIN KELLEY

WIZARA ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika imewaorodhesha Wakenya wawili viongozi wa kundi la Al-Shabaab kuwa “magaidi wa kimataifa.”

Hatua hiyo ya kuwalenga Ahmad Iman Ali na Abdifatah Abubakar Abdi inanuia kuwanyima rasilmali zinazohitajika kupanga na kuendesha mashambulizi yao ndani na nje ya Kenya pamoja na Somalia.

Hatua hiyo inalenga kuwazuia wawili hao kupata pesa za kupanga na kutekeleza mashambulizi yoyote ya kigaidi. Pia mali yao yoyote ambayo huenda iko nchini Amerika itazuiliwa na pia raia wa Amerika hawaruhusiwi kufanya nao biashara yoyote.

Ali ameendesha shughuli za Al-shabaab nchini Kenya kwa miaka sita iliyopita na anaaminika kuhusika na vifo vya mamia ya watu.

Wizara hiyo inasema kuwa Ali aliratibu shambulio la Januari 2016 katika kambi ya Jeshi la Kenya ya El Adde ambayo ndiyo tukio baya zaidi la kushindwa kwa jeshi katika historia ya Kenya. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban wanajeshi 150 wa Kenya waliuawa katika shambulizi hilo.

“Ali pia anawajibika kwa propaganda za Al-Shabaab zinazolenga serikali ya Kenya na rais, kama video ya Julai 2017, ambapo alitoa vitisho kwa Waislamu wanaohudumu katika vikosi vya usalama nchini Kenya,” wizara hiyo ilisema.

Ali alihudumu kama kiongozi wa dini wa kituo cha Muslim Youth Center, Nairobi ambacho mnamo 2012 kilitangaza kuwa kimeungana na Al-Shabaab. Pia alijaribu kuwasajili vijana wa mitaa ya mabanda ya Nairobi kujiunga na kundi hilo.

Naye Abdi anasakwa kuhusiana na mashambulio ya Juni 2014 eneo la Mpeketoni, Kenya ambapo watu zaidi ya 60 waliuawa.

Hatua hiyo ya Alhamisi ya kuwaorodhesha inawanyima Ali na Abdi uwezo wa kufikia mfumo wa kifedha wa Amerika na itasaidia hatua za watekelezaji sheria Amerika na serikali nyingine, wizara hiyo ilisema.

Mbali na kuorodheshwa leo na waziri huyo, Ali na Abdi pia wameorodheshwa katika Kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na maafikiano yaliyofanywa kuhusu Somalia na Eritrea.

Kenya, imeshudiwa mashambulio kadha ya kigaidi ambayo ni pamoja na shambulio kubwa zaidi la 1998 lililolenga ubalozi wa Amerika.

Walimu sasa waacha kutumia vitabu vipya

Na JOSEPH WANGUI

WALIMU wamewacha kutumia vitabu vilivyosambazwa na serikali kwa mtaala mpya wakisema kuwa maelezo yake ni hafifu.

Katibu wa Chama cha Walimu wa Sekondari (Kuppet), kaunti ya Laikipia, Bw Ndung’u Wangenye alisema walimu wamewacha kutumia vitabu vilivyopendekezwa na serikali kwa sababu ya kuwa na makosa na kukosa maelezo ya kutosha ya kuwafunza wanafunzi.

“Walimu wanazuia kutumia vitabu kwa kuwa maelezo yake ni hafifu na wanafunzi wana uwezekano wa kutofanya vyema katika mitihani ya kitaifa ikiwa watatumia vitabu hivyo,” alisema Bw Wangenye, ambaye pia ni mratibu wa Kundi la Walimu wa eneo la Mt Kenya.

Alifichua kuwa walimu wanawashauri wazazi kununua vitabu vingine vya kusoma vyenye maelezo zaidi ili kuongezea kwa vile vilivyotolewa na serikali.

Bw Wangenye pia aliwasihi wachapishaji 100 ambao walichaguliwa na serikali kuchapisha na kusambaza vitabu hivyo, kuajiri watu wenye utaalam wanapounda maelezo na kurekebisha makosa kabla ya kusambaza nakala nyingine mpya.

Katibu huyo alieleza kuwa hakuna umuhimu wa kuendesha mfumo kwa sababu ya unalenga ujuzi badala ya ufahamu.

Alisema kuwa utekelezaji wa mtaala mpya na usambazaji wa vitabu umeharakishwa na kwamba wizara ya Elimu ilikosa kushauriana na wadau wengine katika sekta.

“Wazazi wanaamini kuwa elimu inastahili kuwa ya bure na kila kitu kutolewa na serikali. Wanalalamika baada ya kuambiwa wanunue vitabu vya Kiingereza na Kiswahili kwa fasihi na vitabu vingine kama ‘logarithm’, ramani na kikokotoo maalum,” aliongeza.

Pia alieleza kuwa wazazi walidhania kuwa serikali itatoa vitabu vyote.

“Serikali ilitoa taarufa ya kisiasa kwamba itatoa vitabu vyote. Lakini ukweli ni kuwa wazazi lazima wanunue baadhi ya vitabu,” aliongeza Bw Wangenye.

Wafanyakazi wa kaunti wakosa ujira wa Februari

Waziri wa Fedha Henry Rotich. Picha/ Maktaba

Na SILAS APOLLO na KENNEDY KIMANTHI

MAELFU ya wafanyakazi wa kaunti hawajapokea mishahara yao ya Februari huku serikali hizo za ugatuzi zikikabiliwa na upungufu mkubwa wa pesa, na kuathiri utoaji huduma na utekelezaji miradi.

Kaunti nne zimewaandikia wafanyakazi wao barua za kuwafahamisha kuhusu kucheleweshwa kwa mishahara yao ya Februari, kwa sababu hazijapokea pesa kutoka kwa Serikali ya Kitaifa.

Kaunti hizo za Kericho, Taita Taveta, Kilifi na Busia, katika barua hizo, zimekiri kuwa na mifuko mikavu na kuomba muda zaidi. Zilisema mishahara ya wafanyakazi hao italipwa tu baada ya Serikali ya Kitaifa kutoa pesa, hali ambayo imeshuhudiwa katika nyingi ya kaunti zingine 43 zilizosalia.

Haya yanajiri huku Waziri wa Fedha Henry Rotich – ambaye wiki jana alidokeza kwamba serikali imeishiwa na pesa, isipokuwa Sh200 bilioni za mkopo wa Eurobond ulioidhinishwa mwezi jana – akishauri wizara na idara za serikali kuweka mikakati mikali ya kudhibiti ubadhirifu wa fedha.

Hapo nyuma, magavana walitumia ovadrafti za benki kulipa mishahara ya wafanyakazi lakini mbinu hiyo ilishutumiwa na Wizara ya Fedha ambayo ilishauri wakuu hao wa kaunti kupata idhini yake kabla kufuata mkondo huo wa kuchukua mikopo.

“Hii ni kufahamisha kwamba mishahara ya Februari 2017 itacheleweshwa kwa sababu Wizara ya Fedha imechelewa kutoa pesa,” alisema Katibu wa Kaunti ya Kericho Joel Bett katika barua kwa wafanyakazi.

Huko Kilifi, Katibu wa Kaunti Benjamin Chilumo aliwaomba wafanyakazi kuwa watulivu akisema gatuzi hiyo inatazamia kuwalipa mishahara katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Alieleza Bw Chilumo: “Hii ni kuwafahamisha kuwa mishahara ya Februari 2018 itachelewa. Hii imetokana na kucheleweshwa kwa fedha za Desemba za mgawo wa kaunti kutoka kwa Wizara ya Fedha, pesa ambazo tulikuwa tumepanga kuzitumia kulipa mishahara ya Februari.”

Haya yanajiri huku magavana wakionya kuwa kaunti zinatatizika kutekeleza majukumu yao kwa sababu ya kucheleweshwa kwa fedha hizo, miezi mitatu kabla kukamilika kwa mwaka wa sasa wa fedha.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Josphat Nanok alisema Wizara ya Fedha ilikuwa imetoa asilimia 33 pekee ya fedha hizo kinyume na asilimia 75 zilizotarajiwa kufikia sasa, na kwamba mpango wowote wa kukosa kutoa pesa zote Sh18 bilioni kwa kaunti kutasababisha huduma kusitishwa.

“Kaunti zinakumbwa na mzozo mbaya wa kifedha miezi mitatu tu kabla kukamilika kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Pesa kidogo tulizopokea kufikia sasa zimelipa mishahara na gharama zingine za matumizi ya kawaida,” akasema Bw Nanok.

Ni kaunti za Nairobi, Narok na Trans-Nzoia pekee zimepokea zaidi ya nusu ya mgao wao wa Sh8.7 bilioni, Sh3.2 bilioni na Sh2.8 bilioni mtawalia.

Kaunti 24 zimepokea asilimia 45 ya mgawo huku zingine 20 zikipokea chini ya asilimia 25.

Kaunti iliyopokea kiwango kidogo sana kufikia sasa ni Elgeyo-Marakwet (Sh833,520,000 milioni).

Joho awapongeza Raila na Uhuru

CHAMA cha ODM kimeunga mkono mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wake Raila Odinga kikisema hatua hiyo itaipalilia umoja na kufanikisha maendeleo nchini.

Naibu kiongozi wa chama hicho Ali Hassan Joho pia alitaja hatua hiyo kama ya kijasiri na itasaidia kuondoa tofauti za kikabila, kidini na kisiasa ambazo zilikuwa zikisababisha migawanyiko na uhasama nchini.

“Kwa niaba yangu kama Naibu Kiongozi wa chama cha ODM na kwa niaba ya kaunti muhimu ya Mombasa, ningependa kuwapongeza Mheshimiwa Uhuru Kenyatta na Mheshimiwa Raila Odinga kwa kudhihirisha ujasiri, uzalendo na uongozi na kuweka kando tofauti zao jana (Ijumaa) kwa ajili ya Kenya,” akasema  kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Akaongeza: “Nakubaliana na kauli ya viongozi hawa wawili kwamba taifa letu lilikuwa limegawanyika kwa misingi ya kisiasa, kidini na kikabila na huu ni wakati wa kuchukua uamuzi wa kijasiri ili kuokoa meli ya Kenya ambayo imekuwa ikibiliwa na mawimbi makali.”

Bw Joho ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga aliwataka Wakenya wote kuunga na viongozi hao wawili katika jitihada zao za kurejesha Kenya katika mkondo wa maendeleo.

Hii ni kwa sababu, akasema, mageuzi na maendeleo ambayo Wakenya wanapigania yatapatikana tu ikiwa “tutakubaliana kama Wakenya”.

 

Wagonjwa KNH kuanza kuwekewa vibandiko

Na ELIZABETH MERAB

HOSPITALI Kuu ya Kenyatta (KNH) inatarajiwa kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wanawekwa vibandiko vya majina yao muda wanapolazwa, na wakati wote wakiwa katika hospitali hiyo.

Hospitali hiyo pia inahitajika kuanza kutumia kalamu maalum kuweka alama kwa sehemu za upasuaji kwa wagonjwa wanaotarajia kufanyiwa upasuaji.

Ikitoa ripoti ya uchunguzi wa awali, bodi ya usimamizi ilipatia hospitali mapendekezo manne ambayo inatarajia yaketekelezwe.

Pia kutatua suala hilo, bodi hiyo inayoongozwa na Bw Mark Bor, ilisema kuwa imekamilisha na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wake wa awali kwa Wizara ya

Afya ikiwa na mapendekezo ya kuangaliwa upya kwa saa za kufanya kazi na utaratibu wa kazi wa maafisa wa matibabu.

Kanuni hizo mpya zimefuatia tukio ambapo mgonjwa ambaye hakustahili kufanyiwa upasuaji, aliishia kufanyiwa upasuaji wa ubongo.

Tukio hilo lililotakana na hali ya mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji kuwekwa kibandiko cha jina ambalo halikuwa lake.

Madaktari walisema kuwa hawakugundua kosa hilo hadi saa kadha upasuaji ukiendelea walipogundua hakukuwa na damu iliyoganda kwa ubongo wa mwanamume huyo.

Jumamosi, bodi hiyo pia ilitangaza kuwa imeondoa agizo la kusimamishwa kazi kwa daktari, afisa wa masuala ya matibabu na wauguzi wawili ili kutoa nafasi ya chunguzi huru kufanywa kuhusiana na tukio hilo.

 

KIFO CHA NASA: Dalili zote za muungano kusambaratika

Na CHARLES WASONGA

MKUTANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA Raila Odinga sasa unaonekana kupanua ufa katika muungano wa NASA baada ya vinara wenzake kulalamikia kutohusishwa.

Jumamosi, Mbw Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula walitumia maneno makali na mazito kuelezea ghadhabu zao.

Walisema hawakuwa na habari kuhusu mazungumzo hayo waliyotaja kama ya “watu wawili na NASA haikuwakilishwa kwa njia yoyote ile”.

“Masuala ambayo NASA imekuwa ikipigania kama vile haki katika uchaguzi na utawala bora hayakuangaziwa katika mazunguzo hayo.

NASA imekuwa ikiitisha mazungumzo ya kitaifa yanayowajumuisha wadau wote kwa maslahi ya Wakenya; sio maafikiano kati ya watu wawili,” Bw Mudavadi akasema kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa Jumamosi.

Naye Bw Musyoka alisema katika mkutano wao kesho, watataka maelezo zaidi kutoka kwa Bw Odinga kuhusu mkutano wake na Rais Kenyatta.

“Mkutano wetu wa Jumatatu unatupa nafasi nzuri ya kujadili masuala haya yote katika muktadha mwafaka.

Wale wenye macho wanaweza kuona na wale wenye masikio wanaweza kusikia. Naacha suala hilo hapo huku nikisubiri mkutano wa Jumatatu,” akasema.

Hata hivyo, wabunge na viongozi wengine wa Wiper walimshutumu Bw Odinga wakisema aliwasaliti vinara wenzake kwa kukutana na Rais Kenyatta bila kuwahusisha.

Bw Wetangula alimtaka kinara huyo wa ODM kujitayarisha kwa maelezo ya kina wakati wa mkutano wao wa kesho.

“Raila atatueleza kwa nini hatukuhusisha na nini walichokizungumza na Uhuru,”alisema Bw Wetangula.

 

Wakome kuteta

Hata hivyo, Naibu Rais William Ruto aliwataka vinara hao wakome kuteta na badala yake wajiunge na Bw Odinga kuunga serikali. “Mkutano wa Raila na rais uliashiria kikomo cha msimu wa siasa.

Naomba wenzangu katika upinzani wakome kuteta kuwa hawakuhusishwa na badala yake waje tujenge Kenya pamoja,”alisema Bw Ruto.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba mikakati kuhusu mkutano huo, uliowashangaza wengi, ilianza kuandaliwa wiki kadhaa zilizopita. Lakini mipango hiyo ilishika kasi Alhamisi wiki iliyopita ilipobainika kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Rex Tillerson angefika nchini kwa ziara ya siku tatu.

“Usiri mkubwa uligubika maandalizi ya mkutano huo. Ni msaidizi wa Rais Jomo Gecaga na bintiye Raila Winnie Odinga pekee ambao walikuwa katika mstari wa mbele katika maandalizi hayo,” mshirika mmoja wa Odinga alisema.

Hata hivyo, mnamo Alhamisi wiki jana Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto walijadiliana kuhusu mkutano huo, kabla ya Rais mwenyewe kumfikia Bw Odinga kwa simu na wakapanga kukutana Ijumaa asubuhi.

 

Kioja mwizi wa pikipiki kuirejesha huku akilia

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa sokoni hapa, jamaa aliyeiba pikipiki alipoirejesha kwa mwenyewe huku akilia kutokana na masaibu chungu nzima yaliyomwandama.

Kulingana na mdokezi, mwenye pikipiki hiyo aliiegesha nje ya duka moja mwendo wa saa tatu usiku na kuingia ndani kununua bidhaa. “Polo alijitoma dukani kununua bidhaa na kuacha pikipiki nje ya duka ilivyokuwa desturi yake,’’ alisema mdokezi.

Inasemekana alipotoka nje hakuipata pikipiki yake.

Inadaiwa kwamba, polo aliye mcha Mungu alimwendea pasta mmoja maarufu ili amuombee aweze kuipata pikipiki yake aliyotegemea kujitafutia riziki.

“Mtumishi wa Mungu aliomba na kumuahidi polo kuwa angeipata pikipiki yake baada ya siku tatu,’’ alisema mdaku wetu.

Twaarifiwa kwamba polo alirejea kwake akiwa na matumaini kuwa ‘miujiza’ ingetendeka. Siku tatu zilipotimu, alishangaa alipomuona jamaa mmoja akisukuma pikipiki yake huku akiangua kilio kama mtoto mchanga!’

“Ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni. Mwizi wa pikipiki alimrejeshea mwenyewe huku akilia,’’ alisema mdokezi.

Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, umati ulifika mahali hapo kushuhudia kioja hicho huku wengi wao wakitisha kumtia kiberiti mwizi huyo ili awe funzo kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Hata hivyo, mwenye pikipiki aliwakataza kuchukua sheria mikononi mwao.

Alipohojiwa, mwizi alisema kwamba tangu aibe pikipiki hiyo, familia yake ilikumbwa na mfululizo wa nuksi.

Aliomba radhi na akasamehewa. Alionywa dhidi ya kujihusisha na visa vya wizi na akaenda zake huku akilia kwa simanzi na huzuni nyingi.

“Polo alikiri kwamba alitafuta huduma za pasta mmoja maarufu baada ya kuibiwa pikipiki yake,’’ alisema mdokezi.

WAZO BONZO…

Kidosho pabaya kupapasa polo mbele ya majirani

Na JOHN MUSYOKI

KATHIANI, MACHAKOS

KIDOSHO mmoja kutoka eneo hili, alijipata kona mbaya alipompapasa jamaa na kumbusu hadharani mbele ya wapangaji plotini.

Inasemekana demu huyo alikuwa akijipendekeza kwa jamaa huyo kwa muda mrefu lakini polo alimpuuza kwa sababu alikuwa akipenda pombe kupita kiasi.

Siku ya kioja demu alitoka kwa mama pima na kumpata jamaa akiwa ameketi nje ya chumba chake akipiga soga na majirani. Penyenye zinasema demu alianza kutabasamu kisha akamkaribia jamaa na kuanza kumpapasa kabla ya kumpa busu moto.

Inasemekana jamaa alianza kumfokea. “Shindwe kabisa kahaba wewe. Nani amekupa ruhusa ya kunikaribia na kunipapasa. Ona midomo yako michafu,” jamaa alisema huku akimtemea demu mate usoni.

Jamaa alipandwa na hamaki na kumwangushia demu kofi usoni. “Mimi sikupendi hata ukijipendekeza kwangu kiasi gani. Tabia yako siipendi hata kidogo.

Hauna maadili mema na siwezi kupoteza wakati wangu nikikutongoza.Toka mbele yangu ama nikuharibu sura, shetani wewe. Siku nyingine ukijaribu kunikaribia nitakuonyesha cha mtema kuni,” alisema.

Alitaka kumpokeza kichapo zaidi lakini alizuiliwa na wapangaji waliomwambia demu alikuwa amepata funzo.

Kalameni aliyezaa na dada apanga kumuoa

Na BENSON MATHEKA

RUNDA, NAIROBI

KALAMENI mmoja mjini hapa amefichua kuwa alizaa na dada yake wa kambo na kwamba anampenda sana na ameapa kumuoa.

Jamaa huyo alisema aliamua kumwaga mtama kwa sababu ya mapenzi yake kwa mwanadada huyo ambaye tunafahamishwa ni mrembo ajabu.

Hata hivyo, jamaa alisema japo anampenda mwanadada huyo ana hakika wazazi wake hawatafurahi kufahamu kwamba wamekuwa wakifanya mapenzi hadi wakapata mtoto. “Dada yangu kwa kambo ana mtoto wangu. Tulianza kufanya mapenzi miaka mitatu iliyopita hadi akapata mimba.

Aliniahidi kwamba hakuna atakayejua vituko vyetu lakini sasa ninataka kumuoa kwa sababu ndiye mama ya mtoto wangu,” jamaa alimfichulia rafiki yake ambaye alishtuka.

Kulingana na jamaa huyo mwenye umri wa miaka 26, alianza kumtamani mwanadada huyo akiwa na umri wa miaka 17.

“Kilichoanza kama hisia za kawaida za mahaba miongoni mwa vijana kiligeuka na kuwa uhusiano thabiti wa mapenzi. Siwezi kumtoa katika moyo na mawazo yangu. Nampenda sana dada yangu wa kambo na lazima nitamuoa,” alisema jamaa ambaye ni meneja wa benki moja jijini Nairobi.

Kulingana na jamaa huyo, hataki mtoto wake kuishi bila baba na anajua kwamba ni mwiko kufanya mapenzi na kuoa mtu wa familia.

“Lakini kiwango ambacho uhusiano wangu na dada yangu wa kambo umefika ni tofauti. Kuna mtoto ambaye anakabiliwa na tisho la kuitwa mwanaharamu. Sitaki mtoto wangu aitwe mwanaharamu,” alisema.

Kwa vile anajua kwamba wameiletea aibu familia yake na yeye na dada yake wa kambo wameamua kuhama Kenya na tayari mwanadada huyo na mtoto wako ng’ambo. Jamaa anatarajiwa kuondoka Kenya mwishoni mwaka huu.

WAZO BONZO…

 

 

 

 

Mwanamke aliyeshiriki ngono na mtoto aungama ana Ukimwi

Na TITUS OMINDE

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 24 anayekabiliwa na kesi ya kuishi na kushiriki mapenzi na kijana wa umri wa miaka 15 ameeleza mahakama moja mjini Eldoret kwamba yeye ni hawara na anaugua ugonjwa wa Ukimwi.

Akitoa ushahidi mahakamani, mwanamke huyo alisema kwamba wamekuwa wakitumia kinga kila mara wanaposhiriki mapenzi na kukana kuambukiza kijana huyo ugonjwa.

“Naam, ni kweli tumekuwa tukiishi naye kama mke na mume japo mimi ni hawara hapa mjini Eldoret. Kila tunaposhiriki huba huwa hatukosi kutumia kinga kwa sababu mimi nina utu na namjali sana mpenzi wangu,” akasema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Eldoret Bi Naomi Wanjiru.

Kulingana na ripoti ya uchunguzi wa madaktari kutoka Hospitali ya Moi Eldoret, mwanamke huyo alipatikana na virusi vya ugonjwa wa ukimwi huku hali ya mpenziwe ikikosa kuwekwa wazi.

Wazazi wa kijana huyo waliripoti kutoroka kwa mwanao kutoka nyumbani tarehe 6 mwezi Disemba mwaka jana katika kituo cha polisi cha Kiambaa.

Siku nne baadaye polisi walimfumania akiwa na mpenziwe kwenye nyumba moja ya kukodisha viungani mwa mji wa Eldoret.

Alipofikishwa mahakamani mbele ya hakimu mkazi huyo, mwanamke husika aliyakana mashtaka ya kuishi na kushiriki ngono na mpenzi ambaye hajahitimu umri wa 18.

Bi Wanjiru aliratibisha kusikizwa kwa kesi hiyo tarehe 21 mwezi huu ambapo atatoa mwelekeo zaidi.

 

Ni usaliti mkubwa Raila kukutana na Uhuru – Miguna Miguna

Na BERNARDINE MUTANU

WAKILI mbishani Dkt Miguna Miguna Ijumaa alisema hatua ya Raila Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta na kutangaza ‘kumalizika kwa mgogoro wa kisiasa’ ni usaliti mkubwa kwa wafuasi wa upinzani.

Katika taarifa kutoka Toronto, Canada, Dkt Miguna alisema huo ulikuwa ni uamuzi wa Bw Odinga peke yake na ambao haukuwa na umuhimu wowote.

“Uamuzi wa upande mmoja Bw Odinga, usio na mantiki na usioelezeka ni kusaliti kampeni ya haki ya uchaguzi, kampeni dhidi ya utamaduni wa kutojali na ukiukaji wa haki za kibinadamu ambao umekuwa kawaida chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta na William Ruto sio wa haki,” alisema kiongozi huyo, aliyehamishiwa Canada na serikali wiki kadhaa zilizopita.

Dkt Miguna aliorodhesha visa vilivyotokea wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambapo watu zaidi ya 300 waliangamia wakiwemo Baby Pendo, Stephanie Moraa (9), Geoffrey Mutinda (7), na aliyekuwa mkurugenzi wa habari, mawasiliano na teknolojia wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, marehemu Chris Musando, miongoni mwa wengine.

Alielezea dhuluma dhidi ya baadhi ya wanasiasa kuwa miongoni mwa sababu zinazomfanya kutounga mkono hatua ya Raila Odinga, na kuongeza kuwa waliokufa waliuawa kwa sababu walidhaniwa kumuunga mkono kiongozi huyo.

“Huku Raila Odinga na Uhuru Kenyatta wakisherehekea na kukumbatiana Nairobi, nimetengwa huku Canada kwa sababu nilimwapisha Bw Odinga Uhuru Park Januari 30, 2018,” alisema Dkt Miguna na kuongeza kuwa yumo humo sio kwa sababu ya kutaka lakini kwa kulazimishwa.

“Vinginevyo, makubaliano kati ya Uhuru Kenyatta na Raila ni usaliti kwa mamia ya wananchi wasio na hatia ambao wamepoteza maisha wakipigania demokrasia na kumtetea Raila Odinga baada ya kupokonywa ushindi 2007, 2013 na 2017,” alisema.

 

Udikteta

Alisema kuwa daraja walilosema kujenga litageuza Kenya kuwa taifa la kidikteta chini yake (Raila) na Rais Kenyatta.

Kwingineko, katika Kaunti ya Kitui nyumbani mwa Kinara mwenza wa NASA Kalonzo Musyoka, hatua ya Rais Kenyatta na Bw Odinga iliwakera wengi.

Kamwatu Malonza ambaye ni mhudumu wa teksi mjini Mwingi alisema kuungana kwa wawili hao ni usaliti mkubwa kwa vinara wenza kwani ni dhahiri kuwa kiongozi huyo wa upinzani alichukua hatua hiyo bila kuwahusisha.

“Hatukutarajia kuwa siku moja Raila angekubali kufanya kazi na serikali ya Jubilee, kwetu hatua aliyochukua ilikuwa usaliti mkubwa kwa kiongozi wetu Kalonzo Musyoka,”alisema Bw Malonza kwa ghadhabu.

 

Mbunge atahadharisha kuhusu mkutano wa Uhuru na Raila

Na VICTOR RABALLA

MBUNGE wa Nyando Jared Okello amemtaka Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa NASA Raila Odinga, wafanye mazungumzo ya wazi ili kukomesha mzozo wa kisiasa uliopo.

Alitahadharisha dhidi ya kutofichua maelezo ya mazungumzo baina yao akisema kuwa huenda yakaibua shauku miongoni mwa Wakenya.

Akizungumzia mkutano huo wa jana baina ya viongozi hao wawili, mbunge huyo wa Nyando alielezea haja ya kuendesha mazungumzo yenye mpangilio ambayo yataunganisha Wakenya ambao wamegawanyika sana baada ya marudio ya uchaguzi wa urais uliosusiwa hasa na watu kutoka ngome za upinzani.

“Tunahimiza pande za Bw Kenyatta na Bw Odinga ziwe wazi kwa Wakenya na kufichua mazungumzo yao yanahusu nini,” alisema.

Aliongeza, “Mazungumzo hayo lazima yajumuishe haki katika uchaguzi na kuvunjwa kwa tume ya sasa ya uchaguzi (IEBC) inayoongozwa na Bw Wafula Chebukati.

Bw Okello alisema hayo akiwa Kisumu, huku akitaja kuwa mzozo wa sasa wa kiuchumi na kifedha umetokana na tume ya uchaguzi kukosa kuendesha uchaguzi huru, wenye usawa na wa kuaminika.

Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o alikataa kuzungumzia suala hilo akisema bado hajakutana na kiongozi wa chama cha ODM.

“Habari nilizo nazo bado ni za faragha lakini naweza kukuhakikishia kuwa mkutano huo ulinuia mema kwa Wakenya wote,” alisema.

 

Wiper yasema Raila alisaliti NASA kukutana na Rais Kenyatta

Katibu Mkuu wa chama cha Wiper, Bw Peter Mathuki

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha Wiper sasa kinasema kiongozi wa ODM Raila Odinga aliwasaliti vinara wenzake kwa kukutana na Rais Uhuru Kenyatta bila kuwafahamisha.

Katibu Mkuu wa chama hicho Peter Mathuki alisema kulingana na Wiper mkutano huo haukuwa wa NASA.

“Tangazieni watu kwa haraka sana kwamba vyama tanzu vya NASA, hasa sisi Wiper hatukuhusishwa katika mkutano wa jana. Huu ni usaliti”, Bw Mathuki aliambia Taifa Leo kwa simu.

Alisema kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ni kinara mwenza wa NASA hakufahamu kuhusu mkutano wa Ijumaa.

“Tulishangaa kufahamu kuhusu mkutano huo. Tunashangaa watu wakidai hatuna msimamo ilhali Wakenya wanaweza kujionea ni nani ndiye watermelon,” alisema Bw Mathuki.

Alieleza kwamba Bw Musyoka alikuwa nchini mkutano huo ulipofanyika. “Kiongozi wetu alikuwa na angali nchini. Sababu za kutofahamishwa kuhusu mkutano huo ni ishara haukuwa wa NASA,” alisema.

Bw Mathuki alipuuzilia mbali uwezekano wa mkutano kuandaliwa kwa dharura akisema Bw Odinga alisoma taarifa iliyoandikwa.

“Taarifa hiyo ilikuwa imetayarishwa na kiongozi wa hadhi ya Bw Odinga na hawezi kupapia taarifa ambayo hana uhakika nayo,” alisema Bw Mathuki.

TUKO PAMOJA: Uhuru na Raila walikutana baada ya mashauriano ya kisiri

Na CHARLES WASONGA

Kwa ufupi:

  • Mkutano huo ulikuwa kilele cha msururu wa mashauriano ya kisiri ambayo yamekuwa yakiendelea kwa lengo la kuwaleta pamoja viongozi hao 
  • Mkutano  kati yangu na ndugu Raila utasaidia kutuliza joto la kisiasa lililotokana na uchaguzi wenye ushindani mkali – Rais Kenyatta
  • Wakenya wanataka mabadiliko na hayawezi kupatikana bila amani, umoja na haki. Wakati wa kufanya hivyo ni sasa  –  Odinga
  • Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula wakiri kuwa hawakuwa na habari zozote kuhusu mkutano huo

HATIMAYE Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga Ijumaa waliweka kando tofauti zao za kisiasa na kutangaza kufanya kazi pamoja kuunganisha Wakenya kwa ajili ya maendeleo.

Wawili hao walitangaza hayo walipohutubia wanahabari baada ya kufanya mashauriano ya masaa mawili katika Afisi ya Rais iliyoko jumba la Harambee jijini Nairobi.

Duru zilisema mkutano huo ulikuwa kilele cha msururu wa mashauriano ya kisiri ambayo yamekuwa yakiendelea kwa lengo la kuwaleta pamoja viongozi hao wawili.

Bw Odinga ambaye alikuwa wa kwanza kuwahutubia wanahabari alisema: “Hatufai kuruhusu kuwepo kwa mgawanyiko katika nchi hii kwa sababu ya tofauti za kisiasa. Hii ndio maana leo tumeamua kuweka kando tofauti zote za kikabila na kisiasa,” akasema Bw Odinga.

“Tumetoka mbali na hatuwezi kufika tuendako tukiwa tumegawanyika,” akasema.

Bw Odinga alisema japo Kenya ina Katiba mpya ambayo ilileta mageuzi katika mfumo wa uongozi kupitia kubuniwa kwa asasi mbali mbali za utawala, chaguzi bado zinaleta mgawanyiko nchini.

“Wakenya wanataka mabadiliko na mabadiliko hayo hayawezi kupatikana ikiwa hatulenga kupalilia amani, umoja na haki. Wakati wa kufanya hivyo ni sasa,” Bw Odinga akasema.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alitaja mkutano kati yake na Bw Odinga kama nafasi bora kwa wao kama viongozi kuanza kujadili masuala yenye umuhimu kwa taifa.

Rais Kenyatta pamoja na Raila Odinga walipokutana katika Harambee House, Nairobi ambapo walitangaza kusitisha uhasama kwa manufaa ya ustawi wa nchi. Picha/Hisani

Mwanzo mpya

“Huu ni mwanzo mpya. Mkutano  kati yangu na ndugu Raila utasaidia kutuliza joto la kisiasa lililotokana na uchaguzi wenye ushindani mkali na ambao ulisababisha migawanyiko nchini,” akasema Rais Kenyatta.

“Tunaweza kutofautiana kisiasa lakini sharti tuungane katika masuala yanayowaathiri Wakenya,” akaeleza.

Mshauri wa Bw Odinga Joseph Simekha jana alifichua kuwa kiongozi huyo aliamua kufanya kikao na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuhisi kusalitiwa na wenzake waliokwepa sherehe ya kuapishwa kwake Januari 30.

“Bw Odinga amebadili msimamo wa kuendelea kupinga serikali ya Jubilee baada ya kuhisi kusalitiwa na wenzake watatu waliokosa kufika Uhuru Park, Nairobi wakati wa sherehe ya kuapishwa kwake na badala yake wameanza kulenga uchaguzi mkuu wa 2022.

Na matamshi yao pia yameonyesha kuwa walikuwa wakimezea mate nyadhifa kubwa serikali wala sio kuendeleza ajenda ya mageuzi,” akasema Bw Simekha ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Alikuwa akirejelea kiongozi wa ANC Bw Mudavadi, mwenzake Wetang’ula na Bw Musyoka.

Hata hivyo, Bw Simekha alisema kuwa muungano wa NASA bado utaendelea kudumu hata baada ya mkutano wa jana kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

 

Hawakuwa na habari 

Hii ni licha ya Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula kukiri kuwa hawakuwa na habari zozote kuhusu mkutano huo wa Bw Odinga na Rais Kenyatta. Duru ziliambia ‘Taifa Leo’ kwamba, mkutano kati ya wawili hao ulipangwa kisiri bila kuwahusisha wandani wa karibu wa viongozi hao.

“Niliitwa na Baba (Raila) asubuhi na akanishauri kuvalia nadhifu tayari kwa shughuli fulani.

Aliniambia niandamane na msafara wake na ndipo nikajipata hapa katika jumba la Harambee kwa mkutano na Uhuru,” akasema Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed aliyehudhuria mkutano huo. Hata hivyo, mbunge huyo ambaye ni kiranja wa wachache bunge alidinda kutufichuliwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo.

Ujumbe wa Bw Odinga pia ulijumuisha bintiye Winnie Odinga na msemaji wake Denis Onyango.

Mkutano huo pia unajiri miezi miwili baada ya Bw Odinga kuapishwa kama “Rais wa Wananchi” katika hafla iliyoandaliwa katika bustani ya Uhuru, Nairobi, shughuli iliyosusiwa na vinara wenzake.

Idara ya polisi wa trafiki yavunjwa kuzima hongo barabarani

Na MWANDISHI WETU

INSPEKTA Jenerali wa polisi, Bw Joseph Boinnet, amevunjilia mbali idara ya polisi wa trafiki na kutangaza kuwa, afisa yeyote wa polisi atakuwa akipewa jukumu la kuelekeza magari barabarani.

Mwongozo mpya uliotolewa na Bw Boinnet wasema wakuu wa vituo vya polisi (OCS) ndio watakuwa na mamlaka ya kuongoza usimamizi wa masuala ya trafiki. Jukumu hilo limekuwa likisimamiwa na makamanda wa trafiki ambao sasa watapewa majukumu mengine.

Hatua hii imechukuliwa miezi michache baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuahidi kukabiliana vikali na tabia ya polisi wa trafiki kuitisha hongo kutoka kwa waendeshaji magari.

Idara ya polisi wa trafiki imekuwa ikiongoza kwenye ripoti za tafiti mbalimbali kuhusu ufisadi nchini.

Katika siku za hivi majuzi, maafisa hao wamebuni mbinu mpya za kukusanya hongo ikiwemo kutumia vijana kuwachukulia pesa hizo kutoka kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma.

Ripoti zinaonyesha kuwa, ukusanyaji wa hongo umekuwa ukifanywa kwa mpangilio hivi kwamba, maafisa wa vyeo vya chini walio barabarani hugawa kile wanachokusanya na wakubwa wao ambao huwatuma kazini.

 

Hongo ya Sh3 bilioni

Lalama kutoka kwa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) ni kuwa, wao hupoteza karibu Sh3 bilioni kila mwaka ambazo hupeanwa kama hongo kwa polisi wa trafiki.

Tabia hii huwa imelaumiwa kuchangia ajali za barabarani ambapo raia wengi wamepoteza maisha yao.

Agizo la Bw Boinnet pia limetokea miezi michache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) waondoke barabarani mapema mwaka huu ili kuachia polisi jukumu la kusimamia trafiki.

Rais Kenyatta alitoa amri hiyo kufuatia ajali nyingi za barabarani zilizoshuhudiwa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kuna uwezekano maafisa wa polisi wa trafiki watapinga hatua iliyochukuliwa na Bw Boinnet hasa kwa msingi kwamba, si polisi wote wanafahamu vyema kuhusu mbinu za kusimamia trafiki na sheria zinazohitaji kufuatwa.

KNH yarudisha kazini madaktari iliyowasimamisha kazi

Na BERNARDINE MUTANU

HOSPITALI ya Kenyatta (KNH) Alhamisi ilibatilisha barua za kuwasimamisha kazi madaktari wawili walio katika mafunzo na waliohusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo wa mgonjwa asiyehitaji wiki iliyopita.

Hospitali hiyo ilichukua hatua hiyo na kuwasihi madaktari wote waliogoma kurudi kazini.

“Bodi imesimamisha kabisa hatua za kinidhamu dhidi ya madaktari hao.  Tumeachia jukumu hilo bodi ya chama cha madaktari,” alisema mwenyekiti wa bodi ya KNH Bw Mark Bor wakati wa mkutano wa wanahabari Alhamisi.

Bodi ya KNH ilikutana na KMPDB pamoja na Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki kujadili suala hilo ambalo lilifanya madaktari wote walio katika mafunzo kugoma na kuathiri shughuli za afya hospitalini humo.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alipohutubu baada ya kubatilisha barua ya kuwasimamisha kazi madaktari waliofanya upasuaji kimakosa. Aliwataka madaktari wote waliogoma kutokana na suala hilo kurejea kazini. Hii ni baada ya kuafikiana na KMPDU. Picha/ Bernardine Mutanu

Hii ni baada ya daktari aliyehusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo, lakini kwa mgonjwa ambaye hakuhitaji upasuaji huo, kusimamishwa kazi na KNH.

“Tunawaomba madaktari kurudi kazini, tunawathamini na kuheshimu kazi yenu,” alisema Bw Bor na kuongeza kuwa bodi hiyo pia itafanya mkutano na Baraza la Wauguzi ili kuafikiana kuhusu wauguzi wawili waliosimamishwa kazi.

Kulingana na Waziri wa Afya Bi Kariuki, kisa hicho kinachunguzwa na shirika la nje na kulitaka kutia juhudi ili kumaliza uchunguzi huo.

“Ninatarajia bodi ya KNH itashirikiana na KMPDB kwa kutoa habari inayohitajika katika uchunguzi,” alisema Bi Kariuki.

Lakini alikataa kuzungumzia suala la Mkurugenzi Mkuu wa KNH Bi Lily Koros, ambaye alimsimamisha kazi kuhusiana na suala hilo.

Kusimamishwa kazi kwa Bi Koros kumezua mjadala mkubwa wa kisiasa, suala ambalo mwenyekiti wa KMPDB Prof George Magoha alisema hangeingilia.

“Kutoka kwa bodi, tunataka madaktari kurejea kwa sababu hatutaki kuwa na vifo vinavyoweza kuepukika,” alisema, na kutoa ombi kwa KNH kubatilisha barua dhidi ya daktari aliyehusika.

“Tumepokea faili zote zilizo na ripoti kuhusiana na suala hilo, tunataka kurejea kwa madaktari kurejea kwa nia nzuri, tunataka kufanya haki kwa sababu lazima wahusika wasikilizwe,” alisema Prof Magoha.

Wakenya 1,300 wanaozea jela nchi za kigeni – Serikali

Na WYCLIFFE MUIA

TAKRIBAN Wakenya 1,300 wanazuiliwa katika magereza ya mataifa ya nje, kwa mujibu wa Waziri wa Masuala ya Ndani Monica Juma.
Kati ya 1,300 hao, 79 wamefungwa katika taifa jirani la Tanzania, 47 Uganda na 15 nchini Ethiopia.

“Hatua ya baadhi ya Wakenya kufungwa katika mataifa ya nje si jambo la kushangaza. Kila nchi ina sheria zake na sharti ukienda huko ufuate na kuadhibiwa kulingana na sheria hizo ukizivunja,”alisema Dkt Juma katika kikao na wanahabari jijini Nairobi Alhamisi.

Waziri huyo alisema Kenya imezidisha juhudi za kuwarejesha baadhi ya Wakenya katika jela za humu nchini, lakini akaongeza kuwa mchakato huo huchukua muda mrefu.

“Nawaomba Wakenya wawe watulivu wakati jamaa zao wanafungwa nje kwa sababu Kenya pia imewatia ndani wafungwa 2,000 kutoka mataifa ya nje,”akaongeza.

Alisisitiza jukumu la serikali ya Kenya kuhakikisha Wakenya wanaofungwa nje hawadhulumiwi na pia wanapewa mawakili wa kuwatetea.

“Iwapo kuna Mkenya amekamatwa au kufungwa na hatufahamishwi, lazima tutashutumu taifa husika kwa sababu ni kunyume cha sheria za kimataifa,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Wakenya katika mataifa ya nje Washington Oloo, kati ya Wakenya 1,300 waliofungwa katika jeza za nje, 478 wamefungwa kifungo cha maisha.

Dkt Juma alisema wizara yake imeweka mikakati ya kuhakikisha Wakenya wanaokabiliwa na kesi katika mahakama ya nje, wamepata huduma zifaazo kabla na baada ya kuhukumiwa.

“Ningetaka kuwasihi Wakenya wanaoishi mataifa ya nje kuhakikisha kuwa wanaelewa sheria za nchi wanazoishi ili kuepuka dhuluma wakati wanavunja sheria,”aliongeza Dkt Juma.

Janga la bidhaa feki linavyoilemaza Kenya kiuchumi na kiafya

Na MWANGI MUIRURI

Kwa ufupi:

  • Nyingi ya bidhaa feki hasa vyakula, pombe na bidhaa za urembo hutengenezewa eneo la Kariobangi
  • Februari tahadhari ilitolewa kuhusu uuzaji wa kondomu feki, jambo ambalo linawaweka watumiaji kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa
  • Sekta ya bidhaa feki imewatajirisha wahusika huku uchumi wa nchi na afya ya wananchi ikiwekwa kwenye hatari kubwa
  • Bidhaa feki zimeshuhudiwa katika dawa za magonjwa ya binadamu na mifugo, mbegu za mimea, mbolea, pombe, maji, vinywaji, vipuri vya magari na vifaa vya ujenzi 

WAKENYA wataendelea kukumbwa na ongezeko la maradhi yasiyo na tiba kama vile saratani, uhaba wa ajira, umaskini, ajali za barabarani miongoni mwa matatizo mengine iwapo biashara ya bidhaa feki haitakomeshwa.

Wadadisi wanaonya kuwa kabla ya 2030, sekta hii itakuwa kubwa kuliko ya bidhaa halali na hivyo kuwa na uwezo wa kulazimu maamuzi ya serikali mbali na kudhuru shughuli za kiuchumi na afya.

Kufikia sasa uuzaji wa bidhaa ghushi umekithiri katika nyanja nyingi hasa dawa za magonjwa ya binadamu na mifugo, mbegu za mimea, mbolea, pombe, maji, vinywaji, vipuri vya magari na vifaa vya ujenzi wa nyumba.

Hii inamaanisha kuwa Kenya itashuhudia ongezeko la magonjwa yasiyo na tiba kama vile saratani, uhaba wa chakula kutokana na mbegu na mbolea feki, vifo, kuporomoka zaidi kwa mijengo na ongezeko la ajali za barabarani.

Nyingi ya bidhaa feki hasa vyakula, pombe na bidhaa za urembo hutengenezewa eneo la Kariobangi. Ni vigumu kutofautisha bidhaa feki na halisi kwani upakiaji wake unaiga ule halisi.

Hii imefanya kampuni za bidhaa halali kubadilisha upakiaji kila mara katika juhudi za kukabiliana na bidhaa feki, suala ambalo linasababisha hasara kwao.

Madawa feki nayo huagizwa kutoka nje huku mengine yakitengenezewa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, Sabina Chege anakiri kuwa kuna dawa feki zinazouzwa kwa wingi nchini, hali inayohatarisha afya ya umma.

Ni hapo Alhamisi tu ambapo Wizara ya Afya ilitangaza kuwa kuna dawa feki za kutibu sumu ya nyoka. Dawa hizo mbili zinafahamika kama Puff Under na Ant Venom.

Kondomu feki

Mwezi Februari kampuni ya PSI ilitoa tahadhari kuhusu uuzaji wa kondomu feki, jambo ambalo linawaweka watumiaji kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa ukiwemo Ukimwi na mimba ambazo hazijapangwa.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna anayehusika na ukaguzi wa hesabu katika Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA), Bw Githii Mburu, uchumi unaathirika pakubwa kutokana na biashara ya bidhaa feki.

Anasema kuwa biashara hiyo inahusisha bidhaa ambazo hununuliwa kwa kasi sokoni hasa vileo, sigara na bidhaa za elektroniki akiongeza kuwa ni biashara yenye thamani ya mabilioni ya pesa.

Alisema kuwa kwa sasa KRA inachunguza kampuni zaidi ya 50 ambazo zinashukiwa kuhusika katika biashara hiyo haramu.

Mwenyekiti wa Kampuni ya utengenezaji vileo ya London Distillers, Mohan Galot anasema kuwa nusu ya vileo nchini ni feki na idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

Mamilionea

Kulingana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Watumiaji Bidhaa (Cofek), Stephen Mutoro, sekta ya bidhaa feki imewafanya wanaohusika kuwa mamilionea kwa haraka sana huku uchumi wa nchi na afya ya wananchi ikiwekwa kwenye hatari kubwa.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya kupambana na Mihadarati (Nacada), John Mututho anasema biashara ya bidhaa feki iko na uwezo wa kushinikiza ni nani anayechaguliwa katika vyeo mbali mbali na pia sheria na sera zinazowekwa.

Aliyekuwa Mbunge wa Kigumo, Bw Kihara Mwangi, ambaye ni mtaalamu wa ujenzi anasema visa vya mijengo kuporomoka vinatokana na utumizi wa bidhaa feki.

Mwenyekiti wa Muungano wa Matatu, Dickson Mbugua anasema ajali nyingi zina uhusiano na utumizi wa vipuri feki.

 

Polo agutusha kijiji kuficha ng’ombe kwa kimada

Na TOBBIE WEKESA

EKERENYO, NYAMIRA

KALAMENI mmoja aliwashangaza wenyeji wa hapa alipoamua kuwahamisha ng’ombe wake hadi kwa mpango wake wa kando.

Inasemekana katika tukio hilo lililowaacha wengi vinywa wazi, polo alichukua hatua hiyo akidai kwamba mke wake haaminiki kabisa.

Duru zinasema kalameni alianza kumshuku mkewe mashemeji wake walipoanza kwenda kwake bila kumfahamisha.

“Tangu ninunue hawa ng’ombe, ndugu zako wamekuwa wakija hapa kila wakati. Mbona huniambii wakija na sababu yao ya kuja,” polo alimkaripia mkewe.

Kulingana na mdokezi, sababu aliyoitoa mkewe haikumridhisha polo. “Nahofia sana ng’ombe wangu. Sioni hawa watu wako wakiwa na nia njema,” polo alidai huku akielekea zizini na kuwafungulia ng’ombe.

“Naona leo umewafungulia mifugo mapema sana. Kwani unawepeleka malishoni umbali gani na hii mvua?” mkewe alimuuliza kalameni. Inasemekana polo alimkanya mkewe kuingilia mambo ayafanyayo.

“Achana na mali yangu kabisa. Ikiwa ni malishoni nawapeleka haikuhusu. Ni mimi niliwanunua,” kalameni alimkaripia mkewe.

Maneno ya polo yalimshtua kipusa. “Nahofia sana ng’ombe wangu kuchukuliwa na watu wa kwenu. Heri niwafiche mahali salama,” polo alimueleza mkewe.

Alipotaka kujua mahali salama alikodai kuwapeleka ng’ombe, polo alimueleza mkewe kwamba alikuwa akiwapeleka kwa mwenzake.

“Hii mali yangu naipeleka kwa mwanamke mwenzako ambaye hana njama na watu wao kama wewe. Acha maswali mengi,” kalameni alimueleza mkewe huku akienda.

Duru zinasema baada ya kuwafungulia ng’ombe wake, polo alianza safari kuelekea kwa mpango wa kando katika kijiji jirani kuwaficha humo.

…WAZO BONZO….

Mabilionea nchini waongezeka licha ya serikali kulia haina hela

Na VALENTINE OBARA

IDADI ya mabilionea nchini iliongezeka mwaka 2017 licha ya serikali, wafanyabiashara na wananchi wengi kuzidi kulalamika kuwa kipindi kirefu cha kisiasa na kiangazi zilisababisha hali ngumu ya maisha.

Ripoti ya Utajiri Ulimwenguni iliyotolewa Jumatano usiku na shirika la Knight Frank inaonyesha kuna Wakenya 100 ambao kwa jumla wana utajiri wa Sh964 bilioni, kiwango ambacho ni sawa na karibu nusu ya bajeti ya taifa.

Makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019 yaliyochapishwa Januari 2018 yanaonyesha serikali imepanga kutumia Sh2.2 trilioni.

Kulingana na ripoti hiyo, kuna Wakenya kumi wenye utajiri wa dola 500 milioni (Sh50.5 bilioni) kila mmoja. Hii ni kumaanisha kuwa kwa jumla wakwasi hao ambao hawakufichuliwa wana utajiri wa Sh505 bilioni.

Mbali na hayo, idadi ya Wakenya wenye utajiri wa Sh5.1 bilioni kila mmoja iliongezeka kutoka watu 80 katika mwaka wa 2016 hadi 90 mwaka 2017.

Vile vile, wananchi ambao utajiri wao ni Sh505 milioni kila mmoja waliongezeka hadi watu 1,290 mwaka uliopita kutoka watu 1,110 mwaka wa 2016.

Watafiti walihoji washauri wa uwekezaji katika mashirika ya kifedha nchini ambao walisema inatarajiwa idadi ya wakwasi itazidi kuongezeka katika miaka ijayo.

Ilibainika wengi walipata utajiri kutoka kwa uwekezaji katika sekta ya ujenzi, fedha, viwanda na uuzaji wa bidhaa za nyumbani.

Ripoti hiyo ilitolewa wakati ambapo serikali imetangaza kufilisika na hivyo basi kuleta wasiwasi kuhusu hatima ya wananchi kwani inatarajiwa hali hiyo itaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Imetolewa pia wakati ambapo kampuni mbalimbali zinazidi kuweka mikakati ya kupunguza gharama za matumizi ya fedha hasa kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi kutokana na upungufu wa faida.

Zaidi ya hayo, ripoti hiyo imeonyesha pengo kubwa la kimaisha lililopo kati ya mamilioni ya wananchi wachochole na mabwanyenye wachache.

Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Shirika la Kenya Red Cross, Bw Abbas Gullet, aliomba Sh1 bilioni ili kusaidia wananchi karibu milioni 3.4 wanaokumbwa na janga la njaa katika pembe tofauti za nchi.

USWAHILINI: Ni kweli miwa yaweza kutumiwa kudhibiti Chikungunya?

Na LUDOVICK MBOGHOLIi

Jamii inapokabiliwa na ugonjwa unaozuka ghafla na kuathiri watu , inatafuta mbinu kuhakikisha hauenei ukasababisha maafa. Hali hii ilikumba maeneo ya Uswahilini baada ya ugonjwa ‘mpya’ wa ‘kigeni’ kuzuka na kuathiri jamii Kisiwani Mombasa.

Ugonjwa huu wa ‘Chikungunya’ ulizuka ukahangaisha jamii kiholela huku waathiriwa wakiupuuza na kupuuza ushauri wa wataalamu na maafisa wa afya. Ilibainika walioathirika waliupuuza wakiamini unatibiwa tu na dawa za kawaida.

Hata hivyo kadri siku ziliposonga , ‘Chikungunya’ ilienea kwa kasi huku waathiriwa wakihangaika wasijue tiba halisi ni ipi.

Wataalamu na maafisa wa afya walifanya utafiti wakagundua ugonjwa huo ulienezwa na aina ya mbu wasiokuwa wa kawaida. Walidai mbu hao walitoka ng’ambo wakiwa ndani ya meli wakisafiri na abiria au mabaharia wa kigeni.

Kwa mujibu wa wataalamu Uswahilini, mbu hao huzaana kwa kasi kwenye maji safi yasiyokuwa ya chumvi, ya vidimbwi au ya mabwawa na visima. Kwa utafiti wao, walidai mbu hao waliathiri idadi kubwa ya watu huko walikotoka na ni nadra kupatikana Uswahilini!

Ugonjwa huo ulipobainika , maafisa wa afya walianza mikakati ya kuudhibiti.

Ilisadikiwa mtu akiathiriwa anapooza viungo vyote mwilini ashindwe kutembea, kuongea vyema na kufanya lolote!

Unamfanya alegee na ashindwe kula vyema huku akishinda tu kitandani –Waswahili wakaupatia jina la ‘ugonjwa wa mahaba’ kwa sababu mwathiriwa hushinda kitandani asiweze kujishughulisha!

Lakini watabibu wa kienyeji nao walijibidiisha kutafuta jinsi ya kuukabili , wakagundua ili kuupunguza kasi ya kusambaa mwathiriwa anahitaji ‘kutafuna miwa’ au kunywa ‘marami’ (maji ya miwa iliyosagwa).

Watabibu hao waliarifu mwathiriwa anastahili kunywa gilasi tatu za ‘marami’ kila siku kwa siku saba mfululizo ili kupunguza kasi ya ‘Chikungunya’! Inadaiwa walioathiriwa na kufuata ushauri huo wa kienyeji walifanikiwa kuupunguza kasi ilihali waliopuuza walisalia hospitalini wakitibiwa!

Hata hivyo , inadaiwa maafisa wa afya waliarifu waathiriwa wanywe maji mengi kila siku kwani kufanya hivyo ni kuupunguza kasi yake mwilini na kuzuia maafa ya vifo.

Waliarifu tiba ya ‘Chikungunya’ ni kupata dawa za kupunguza maumivu makali mwilini na kunywa maji mengi kila saa ingawa ugonjwa huo hutesa mwili bila kusababisha vifo!