NDIVYO SIVYO: Idadi nne za asili ya kigeni hazichukui viambishi vyovyote katika matumizi

Na ENOCK NYARIKI

Viambishi awali huwakilisha dhana mbalimbali katika lugha ya Kiswahili. Dhana hizo ni pamoja na nafsi, ngeli na umoja au wingi. Hakika, dhana ya nafsi na umoja au wingi zinaweza kujitokeza chini ya ngeli ila tumezigawa hivyo ili kurahisisha maelezo yetu.

Viwakilishi nafsi ni maneno kamili au viambishi vinavyosimamia nomino za viumbe vyenye uhai. Kwa upande mwingine, viambishi vya idadi husaidia katika kubainisha iwapo sentensi inayohusika iko katika hali ya umoja au wingi.

Ni rahisi sana kuhesabu nambari au takwimu katika lugha ya Kiingereza kuliko ilivyo katika lugha ya Kiswahili. Jambo hilo hutokea hivyo kwa sababu lugha ya Kiingereza haina upatanisho wa kisarufi ambao ni lazima uzingatiwe wakati wa kuzitaja idadi.

Kosa la kuhesabu nambari hujitokeza sana katika idadi za msingi. Hizi ambazo tumezirejelea hapa kama idadi za msingi ni kuanzia moja hadi kumi.

Kosa linalotokea wakati wa kuhesabu nambari limerithiwa kutoka mfumo wa zamani wa uainishaji wa maneno katika ngeli ambapo mkazo ulitiwa katika viambishi vya nomino wala si aina nyingine za maneno.

Baadhi ya wanafunzi walioupitia mfumo huo hawafahamu wakati wa kuviongeza viambishi katika idadi fulani na wakati wa kuviacha nje viambishi hivyo.

Matokeo yake ni kufanyika kwa makosa yafuatayo:
*Wanafunzi kumi na moja wamewasili shuleni.
*Watu wasaba waliangamia katika ajali hiyo.
*Madereva wasita wametiwa mbaroni kwa kosa la kuendesha magari wakiwa walevi.
*Wanafunzi tano wametimuliwa shuleni kwa kuhusika katika mgomo.
*Vitabu nne havina majalada.

Baadhi ya idadi zimetokana na asili za kigeni yalivyo pia maneno mengine ya Kiswahili. Kutoka moja hadi kumi, kuna jumla ya idadi nne ambazo zimetokana na asili ya kigeni. Hizi ni pamoja na sita, saba, tisa na kumi.

Idadi hizi hazichukui viambishi vyovyote. Tunasema watu sita, vitabu sita, vichwa sita, miguu sita, miti sita, nywele sita, nyuzi sita, ndizi sita na kadhalika. Hali hiyo hujirudia katika idadi tisa, saba na kumi. Idadi nyingine ambayo haina viambishi ngeli ni thelathini.

Idadi nyingine zote zilizosalia huchukua viambishi kutegemea ngeli mbalimbali. Kwa hivyo, wanafunzi ni kumi na mmoja wala si kumi na moja; vitabu ni vinne wala si nne; watu watano wala si tano miongoni mwa idadi nyingine.

Alhasili, idadi ni suala la msingi mno katika lugha ya Kiswahili wala halipaswi kupuuzwa katika mawasiliano ya kila siku.

 

VITUKO: Nia fiche ya Farida kumfichulia Pengo njama ya Mwinyi na Tumbo

Na SAMUEL SHIUNDU

Walifika faraghani na kuagiza chakula. Pengo hakula nyama kwa sababu za kidini. “Huu ni mwezi mtukufu wa pasaka aisee! Lazima tususie kila jambo linalotupa raha’ Hili lilimgutusha Farida.

Akatambua kuwa kakutana na mwanamume mwenye msimamo mkali wa kidini. Hakujua kama hii kauli ya Pengo kuhusu ‘kila jambo la raha’ ilihusisha pia yale yaliyomsumbua roho.

Hapo naye akaomba apewe soda baridi kwa keki. Hakutaja pombe asije akadhaniwa mhuni na muumini huyu. Hakuna mwanamke ambaye hujiachilia na kuonyesha udhaifu wake kwa mwanamume kwa mara ya kwanza. Kwake stara ilikuwa ngao iliyomsaidia kuvishinda vita vingi vya aina hii. Akajitunza na kunyenyekea.

Baada ya jambo-sijambo, Farida alimfichulia mwenzake lililowakutanisha katika mkahawa huo. Alimweleza jinsi alivyoyasikiliza mazungumzo kati ya Tumbo na Mwinyi.

“Nilisikia wakizungumzia kitu kama ‘interdiction’. Mwanzoni sikujua maana ya neno hilo. Lakini baada ya kulitafitia, nikagundua kuwa ni jambo kama, kufutwa kazi.” Farida alimfafanulia mwenzake kabla ya kuendelea, “Na anayepangiwa njama hii si mwingine ila wewe mpenzi” akampasulia mbarika hatimaye.

‘Yakoje haya masikio basi?’ Pengo alijiuliza kwa mshangao. Alijua kuwa Mwinyi hakumpenda, lakini hakujua kuwa uhasama wao ulikuwa umefikia kiwango hiki. Akameza mate machungu huku akimsikiliza Farida aliyekuwa akirogonya kama muumini aliyepandwa na roho wa ndimi, “Nilipogundua hili nikajiambia kuwa si haki kabisa!

Si haki kwa kijana mwema kama wewe kupatwa na nakama hii! Ndipo nilipoikumbuka methali ya kikwetu isemayo kuwa, asiyetahadhari hugaagaa kwenye mapito ya majitu.

Nimekuita nikujuze utahadhari kabla ya hatari. Wajua tena ilivyo vibaya kukumbwa na balaa huku mwenyewe huna habari? Wanasema wahenga kuwa, nzi asiye na mshauri huuandama mzoga hadi kaburini. Singetaka uwe nzi huyu.”

Pengo alikumbuka siku aliyokutana na huyu binti Farida kwa mara ya kwanza. Hakuwahi kufikiria kuwa angemfaa. Aliaibika kwa kumpuuza awali. “Sasa nitafanyaje maskini?” Pengo alishangaa.

Kwa kulisikia swali hili la Pengo, Farida alijiwa na matumaini ya kuvuna alilolilenga. Akampa habari nyingine nzuri. “Swala lako lilinikeshesha na kuniliza hadi kisima changu cha machozi kikakauka. Nimekwishazungumza na mkuu wa shule ya Baraka kule Sidindi. Akaniambia umwone.

Mwinyi aliposema wewe wa nini kumbe kunao wanaojiuliza watakupata lini?” Farida alimliwaza kwa misemo ya kikwao.

Pengo alimshukuru Farida kwa fadhila zake. Shilingi mia tatu zikamtoka kulipia chakula chao. Wakaagana na kuahidiana wakutane kesho yake Pengo atakaporejea kutoka Sidindi.

KAULI YA MATUNDURA: Mradi wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia masomo yote umefikia wapi?

Na BITUNGI MATUNDURA

MIAKA kumi na mitano hivi imepita tangu mdahalo mkali ulipoibuka baina ya wataalamu wa lugha kuhusu ufaafu wa matumizi ya Kiswahili katika ufundishaji wa masomo yote yakiwemo ya sayansi katika asasi za elimu Afrika Mashariki.

Watafiti wa lugha wamekuwa wakikipigia upatu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia masomo yote isipokuwa yale ya lugha za kigeni katika shule za msingi na upili.

Kwenye kikao cha wataalamu wa Kiswahili kilichofanyika mapema 2003, wanachama wa Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (Chakama) waliazimia kuanzisha shule za kimajaribio – ya msingi ya ya upili kutumiwa kutekeleza mradi huo.

Kwenye kikao hicho, iliazimiwa kwamba Kenya na Uganda zianzishe kila moja shule za majaribio katika utumiaji wa Kiswahili katika kufundishia masomo yote; nayo Tanzania ianzishe shule ya upili kutekeleza mradi huo.

Hivyo basi Chakama kiliteua kamati ya wanakamati watano kuchunguza mpango wa utekelezaji wa mradi huo.

Kamati hiyo iliwahusisha Prof Kimani wa Njogu ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Kiswahili cha Taifa, Chakita- Kenya, Dkt Issa Ziddy wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Prof Austin Lwanga Bukenya wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na Maprofesa Mugyabuso Mulinzi Mulokozi na Fikeni Senkoro wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wanataaluma hao walisema lugha ya Kiswahili ilikuwa inakua na kuenea haraka katika mataifa ya Maziwa Makuu hususan Rwanda, Burundi na Kongo-Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Msumbiji na Zambia.

Walisema kuwa Afrika Mashariki inapaswa kuwa kwenye msitari wa mbele katika shughuli za utafiti na kufanikisha azma ya matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika taasisi za elimu.

 

Mgawanyiko

Hata hivyo, azimio la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia lilizua mgawanyiko mkubwa baina ya wataalamu wa Kiswahili – mgawanyiko ambao naamini ungalipo hadi wa leo.

Dkt Casmir Lubagumya, mhadhiri mkuu katika Idara ya Isimu na Lugha za Kigeni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, haikuwa vyema wanataaluma wanaounga mkono matumizi ya Kiswahili katika kufundishia kuchukulia kwamba Kiswahili ni lugha ya kwanza au lugha mama kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na upili Afrika Mashariki, au kuchukulia kwamba wanafunzi wote katika viwango hivyo ni weledi wa Kiswahili.

Alisema, nchini Tanzania ambapo Kiswahili kimekubalika na kusambaa sana, ni asilimia 10 pekee ya watu wanaokizungumza Kiswahili kama lugha yao ya kwanza.

Mbali na hayo, mdahalo kuhusu matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia ulipanda na kufikia viwango vya juu pale ambapo baadhi ya wataalamu walihoji ubora wa kuitumia lugha hiyo kufanya hivyo.

Isitoshe wanataaluma wengine walidai kwamba kuna istilahi chache mno za kuelezea dhana sa kisayansi mbali na kutokuwepo kwa vitabu vya kiada kutumiwa katika mtaala huo.

Mantiki ya uamuzi wa kutumia Kiswahili kufundishia inatokana na ukweli kwamba, kuna mataifa ambayo yametegemea lugha zao kupiga hatua kubwa kisayansi na kiteknolojia.

Inaaminika kwamba, kuna maarifa ya kiasili ambayo yamefumbatwa tu na lugha zetu za kiasili na hayawezi kwa vyovyote kuelezwa au kufafanuliwa kwa lugha nyingine za kigeni. Baadhi ya mataifa yanayosukuma mbele ajenda ya kutegemea lugha zao kufundishia na uvushaji wa maarifa ni pamoja na Japan na Uchina.

Na kwa hakika mataifa haya yamevunjilia mbali imani kwamba ni lazima utegemee lugha za kigeni kama vile Kiingereza – tunavyofanya hivi sasa kupiga hatua kubwa katika maendeleo.

 

KAULI YA WALIBORA: Tasnia ya uandishi itazidi kupiga hatua tu iwapo waandishi chipukizi na wale wabobezi wataandika sambamba, kwa sawia

Na PROF KEN WALIBORA

Mwanafunzi aitwaye Boniface wa Shule ya Upili ya St Peter’s Mumias alinidokezea hivi karibuni kuhusu mawanio yake ya kuwa mwandishi. Si aghalabu kukutana na mwanafunzi ambaye mawanio yake si taaluma tamanifu kama uhandisi au uanasheria.

Boniface ni miongoni mwa wale wanaowania kujitosa katika ulingo wa uandishi, watuandikie vitabu tuvisome kwa lazima au kwa raha zetu. Hawa ndio William Shakespeare, Milton, Chaucer, Victor Hugo, K.W. Wamitila, Jeff Mandilla, John Habwe, na Euphrase Kezilahabi watarajiwa.

Nilikutana na Euphrase Kezilahabi kwa mara ya kwanza nilipozuru Botswana mwaka 2010 kwa kongomano la kiakademia.

Huyu ndiye mwandishi ambaye Bitugi Matundura alijasiria kusema amewapiku wote katika ulingo wa bunilizi za Kiswahili. Kaandika Rosta Mistika, Dunia Uwanja wa Fujo, Kichwani Maji, Kichomi, Kaptula la Karl Marx mbali ya hadithi ya “Mayai Waziri wa Maradhi.”

Ilikuwa fahari yangu kukutana na mkongwe huyu wa tasnia ya uandishi wa Kiswahili. Nikamuuliza alikuwa anaandika nini tukitarajie. Akaniambia kachoka, haandiki tena.

Nililikumbuka jibu lake nilipokutana na mwandishi mtarajiwa Boniface. Boniface aliniambia kwamba alitaka kuwa mwandishi maana anaona waandishi wakongwe kama vile Said A. Mohamed na mimi Ken Walibora tumekonga na karibu tufe.

Kwa hiyo, bora yeye na waandishi wengine chipukizi waanze kuandika, yaani tuwapishe wao sisi wakongwe au vikongwe. Naam, kauli ya Kezilahabi, ambaye nilivisoma vitabu vyake tangu nikiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari, ilinijia akilini: je ina maana kuwa kuchoka na kustaafu katika kuandika bunilizi? Je, sharti tuwapishe waandishi wengine ndipo tasnia ikue?

Je, uandishi ni kama mbio za kupokezana vijiti ambapo huanzia hadi pale unapopokezwa kijiti? Au inawezekana waandishi chipukizi na wabobezi kuandika kwa sawia, kuandika sambamba, pamoja?

Huenda ikawa ni kweli baadhi ya waandishi huridhika na kuandika idadi fulani ya vitabu kisha wakaacha kabisa.

Mohammed Suleiman Mohammed aliandika Kiu, Nyota ya Rehema na Kicheko cha Ushindi akaridhika. Abdilatif Abdalla aliandika Utenzi wa Adamu na Hawaa na Sauti ya Dhiki akaridhika.

Lakini sio wote wanaoridhika na vitabu viwili vitatu au wanaosema kama Kezilahabi wamechoka hawaandiki tena.

Kuna waandishi walioandika vitabu kocho lakini ambao bado wana mawanio ya kuendelea kuandika zaidi kuchangia tasnia hii ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili. Je, tuwashikie mtutu wa bunduki na kuwaambia kachokeni msiandike, staafuni msiandike?

Kwa waandishi kama hao kuandika ndio uhai wao, ndio pumzi ya uhai wao.

Huwezi kuwatakia kufa ili nawe uishi. Ukitaka kuishi katika ulimwengu wa uandishi lililopo ni kusema “jamani nami naja ulingoni, niachie niishi pamoja nanyi nichangie.” Kwa waandishi wa mawanio kama haya ya kuandika mpaka siku ya kufa, kuandika kwao ni kama karamu.

Usiwaambie, “acheni kula ili nami nile.’ Unajuzu kusema, “niachie nami nile pamoja nanyi.” Unapaswa kusema, “nisubiri naja” sio “ondokeni naja.” Karibu Boniface.

Jombi mlevi pabaya kutukana wakweze

Na CORNELIUS MUTISYA

MITABONI, MACHAKOS

POLO wa hapa alijitia mashakani alipoenda nyumbani kwa wakwe zake akiwa mlevi chakari na kuwatupia cheche za matusi akidai walikuwa wakiroga familia yake!

Kulingana na mdaku wetu, familia ya polo ilianza kukumbwa na mikururo ya nuksi na visirani. Kila wakati alikuwa akivurugana na mkewe na ikawalazimu watoto wao wahamie kwa majirani ili wapate utulivu.

“Nyumbani kwa polo kulikuwa hakukaliki. Kila siku kulikuwa kukizuka vurumai na ikabidi watoto watorokee kwa majirani,’’ alisema mdokezi.

Hivi majuzi polo alifika nyumbani akiwa mlevi na akaanza kumtusi mkewe. Vurugu zilizuka na mama watoto akafunganya virago vyake na kurudi kwao.

Inasemekana kwamba polo alienda kulala na akarauka alfajiri kwenda kwa mganga mashuhuri kupiga ramli ili amtatulie masaibu ya familia yake.

Ni mganga aliyemjulisha kwamba matatizo ya familia yake yalisababishwa na wakwe zake.

Penyenye zasema kwamba polo alipopashwa habari hizo, alikasirika sana. Alienda kwa mama pima kubugia mvinyo ili ajiliwaze nafsi. Alipiga mtindi mpaka akalewa chakari na kwa sababu ya ulevi akili ikamhadaa aende kwa wakwe zake kuwakemea kwa kuroga familia yake.

“Polo alipepesuka hadi kwa wakwe zake huku akibwabwaja maneno ya kilevi,’’ alisema mdokezi.

Kilichowakera wakwe zake hata hivyo ni polo alipoanza kuwaita wachawi akidai ndio waliokuwa chimbuko na asili ya nuksi zote za familia yake. Walitwaa nyahunyo na wakamcharaza mpaka pombe ikamtoka kichwani na akakimbia kunusuru maisha yake.

Kwa sasa, polo na mkewe wametengana kabisa huku kila mmoja akifuata njia zake.

          …WAZO BONZO…

SHANGAZI AKUJIBU: Nahisi mapenzi yake kwangu yameingia baridi

Na SHANGAZI SIZARINA

Mwanaume mpenzi wangu amenichanganya kwa tabia zake, sijui iwapo ananipenda au la. Siku za mwanzo za uhusiano wetu alikuwa akinipigia simu na kunitumia SMS karibu kila siku. Lakini siku za hivi majuzi ni mimi nimekuwa nikimtafuta kwa simu na mara nyingine hata anapuuza. Nimeanza kuhisi hanipendi na ni kama ninajipendekeza kwake. Nafikiria kumuacha. Naomba ushauri wako shangazi.
Kupitia SMS

Mapenzi yanapoonekana kutoka upande mmoja kamwe huwa hayana raha. Ni jambo la kushangaza kwamba awali ndiye alikuwa akikutafuta lakini sasa amekuachia mzigo huo. Inawezekana kuwa hisia zake kwako zimepungua na amekosa jinsi ya kukwambia. Ushauri wangu ni kuwa umwelezee unavyohisi kabla ya kukata kauli kuwa hakupendi.

 

Jirani amenizuzua
Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 22 na nina uhusiano na msichana jirani yetu mtaani. Nampenda sana naye pia ameungama kuwa hapati usingizi kwa sababu yangu. Ajabu ni kwamba amekataa kabisa kunionyesha kwa vitendo mahaba aliyo nayo kwangu. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Masuala ya mahaba ni kuelewana wala hayalazimishwi. Mwenzako ameungama mwenyewe kuwa anakupenda na huna shaka kuhusu hilo. Kwa sababu hiyo itakuwa vyema kwako umuelewe akikwambia hayuko tayari kwa jambo hili au lile iwapo unathamini uhusiano wenu na unataka kuudumisha. Kuwa na imani kwamba siku atakayokuwa tayari atakutimizia ombi lako.

 

Anakuja kwangu tu anapotaka pesa
Nina mpenzi lakini ninashuku kuwa hana mapenzi ya dhati kwangu nia yake ni kufaidi kutokana na pesa zangu. Sababu ni kuwa kila anapokuja kwangu akiwa na haja ya pesa nikimpa hutoweka na hurudi tu akitaka zingine. Nipe ushauri.
Kupitia SMS

Bila shaka mwanamke huyo hana mpango wowote wa uhusiano wa kudumu kati yenu iwapo hivyo ndivyo anavyofanya. Naona umefunguka na ningekuwa wewe ningejiondoa mara moja katika uhusiano huo.

Penzi letu ni la simu pekee
Shangazi natumai wewe ni mzima. Kuna mwanaume ambaye tulijuana tu kupitia kwa simu na tukapendana. Tumepanga kukutana na nina wasiwasi kwani sijui anakaa vipi, huenda nikapata kwamba maumbile yake si ya mwanaume ninayemtaka. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Sielewi ulimpenda namna gani mwanaume huyo kama hujamuona umekuwa uskisikia sauti yake tu kwa simu. Kupendana kunatokana na watu kuonana na kuzungumza ana kwa ana. Ni vyema kuwa mmepanga kukutana. Baada ya hapo utajua iwapo anakufaa. Usiwe na hofu kwani ukigundua siye unayemtaka una haki ya kumwambia ukweli huo.

 

Hataki kuniona na mwingine ingawa tuliachana
Hujambo shangazi? Nilikuwa nimeolewa lakini tukaachana. Sasa kila mwanaume huyo anaponiona na mwanaume mwingine hutishia kunipiga. Nifanye nini na simtaki tena?
Kupitia SMS

Hiyo ina maana kuwa mwanaume huyo anakutishia maisha. Kama mliachana na humtaki, hawezi kukuzuia kuendelea na maisha yako. Unafaa kumchukulia hatua ya kisheria kwa kupiga ripoti kwa polisi kwamba anakutishia maisha.

 

Nimependana na mjomba wangu
Hujambo shangazi. Mimi nimependana na mjomba wangu lakini wazazi wamepinga vikali uhusiano wetu. Ninampenda kwa moyo wangu wote na sidhani ninaweza kumuacha. Nishauri.
Kupitia SMS

Mapenzi yenu hayo ni haramu na hatari. Huwezi kamwe kuwa na uhusiano na mjomba wako kwani huyo ni sawa na baba yako. Ni lazima utii agizo la wazazi wako kwa kuvunja uhusiano huo mara moja la sivyo utajiletea laana maishani.

 

Ataka burudani tu!
Hujambo shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa miezi kadhaa sasa. Nilidhani ananipenda lakini nimegundua nia yake ni kunitumia tu. Sababu ni kuwa hunitafuta tu anapohitaji asali. Ninapokuwa na shida simuoni. Nishauri.
Kupitia SMS

Hayo kamwe si mapenzi ya dhati na ni vyema umegundua mapema nia ya mwanamume huyo. Itabidi uchunguze moyo wako na kuamua kuhusu iwapo utaendelea na uhusiano huo ama utajiondoa.

TAHARIRI: Serikali kupungukiwa na hela ni hatari kuu

Na MHARIRI

MATAMSHI ya Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich kwamba serikali haina fedha Za kutosha kugharimia miradi yake hapa nchini ni fedheha na hatari zaidi kwa wananchi wa taifa hili.

Akihojiwa mbele ya kamati ya seneti inayosimamia bajeti na fedha, Waziri huyo alisema kwamba kipindi kirefu cha kupinga uchaguzi kuliathiri nchi kiuchumi, hivyo basi akatangaza kuwa analenga kupunguza mgao unaotengewa kaunti 47 kutoka Sh302 bilioni hadi Sh285 bilioni.

Mwanzo ni kinaya kwamba serikali imedidimia kifedha ilhali baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa miaka ya nyuma kupunguza gharama ya matumizi hayajatekelezwa.

Baadhi ya mapendekezo hayo ambayo haijabainika kama yalitekelezwa, ni kupunguzwa kwa mshahara wa Rais,naibu wake na maafisa wa ngazi za juu serikalini mapema mwaka wa 2014.

Viongozi wetu wanaohudumu bungeni walipoona pendekezo la Tume ya Mishahara nchini (SRC) kupunguza mshahara wao walifanya kila juhudi kuhakikisha kwamba hilo halitimii.

Wakati wa mjadala huo bungeni, tofauti za mirengo zilitupwa kando na kuhakikisha kuwa maslahi yao yanadumishwa.

Waziri anapotaja kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) imefeli kufikia viwango lengwa ina maana kuna nia fiche ya kuongeza kodi ama kuhakikisha mabwenyenye wanaokwepa kutozwa ushuru wanakabiliwa.

Lakini suala zito linalofaa kuzingatiwa baada ya waziri huyo kutangaza hayo ni, je,serikali za kaunti zitatumia mbinu zipi kuhakisha kwamba pengo hilo la hela linazibwa? Iwapo hamna chochote kitakachofanyika, basi huenda kaunti zikajipata kwenye matatizo chungu nzima.

Tamko hilo la Bw Rotich linahofisha zaidi kwa sababu nchi ambayo haiwezi kumudu gharama ya huduma kwa raia wake ndiyo hukimbilia mikopo kiholela.

Kwa sasa nchi tayari inakumbwa na mgomo wa wahadhiri ambao wanataka mshahara zaidi kulingana na makubaliano ya mwaka jana. Je, hali ikiwa hivi watashughulikiwa kweli?.

Jambo la wazi kama mchana wa jua ni kwamba serikali haijaweka mikakati maridhawa ya kupunguza gharama yake na kulitokomeza kabisa donda sugu la ufisadi.

 

Trump akiri Urusi iliingilia uchaguzi wa Amerika 2016

Na AFP

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS Donald Trump, alikiri Jumanne kwamba Urusi na ‘nchi nyingine’ ziliingilia uchaguzi wa urais uliofanywa mwaka 2016 ambao alitangazwa mshindi, lakini akaahidi hilo halitawahi kufanyika tena.

Akizungumza kwenye kikao cha wanahabari ambapo aliandamana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, alidai pia kuwa uingiliaji wa Urusi haukuathiri matokeo katika uchaguzi huo.

“Warusi hawakuathiri kura zetu kwa njia yoyote ile lakini kwa hakika, kulikuwa na uingiliaji na pengine pia kutoka kwa nchi nyingine na watu wengine binafsi,” akasema Trump, ambaye amekuwa akipuuzilia mbali ushawishi wa Urusi kwake na amekuwa akipinga vikali madai kwamba wasimamizi wa kampeni zake walishirikiana na Urusi.

Alipoulizwa kama anahofia kitendo hicho kitashuhudiwa tena, rais huyo alisema, “Tutazuia chochote watakachojaribu kufanya kwa kila njia tuwezavyo. Huwezi kukubali mfumo wa uchaguzi kuvurugwa kwa njia yoyote na hatutaruhusu hilo lifanyike.”

Aliongeza: “Hatujasifiwa na mtu yeyote lakini ukweli ni kwamba tunajitahidi sana kuandaa chaguzi zijazo.”

 

Tisho

Wakati huo huo, rais huyo alikashifu sheria za kibiashara za Muungano wa Ulaya (EU) na kusema muungano huo umefanya iwe vigumu mno kwa kampuni za Amerika kuendeleza biashara zao na akatishia kuongeza ushuru wa bidhaa za mataifa ya EU zinazoingizwa Amerika.

Trump, ambaye ametishia kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa vyuma vinavyoingizwa kutoka nchi za kigeni na asilimia 10 kwa mabati alisema haogopi hata kama kutazuka mgogoro wa kibiashara.

Alionya pia kwamba yuko tayari kuongeza ushuru wa magari ya Ulaya yanayoingizwa Amerika, mengi yakiwa yanatoka nchini Ujerumani.

“Wanafanya iwe vigumu sana kwetu kufanya biashara nao, ilhali wanaleta magari yao na kila kitu kingine Amerika. Wanaweza kufanya chochote kile watakacho lakini wakifanya hivyo, basi tutaweka ushuru mkubwa wa silimia 25 kwa magari yao na mniamini nikisema hawataendelea kwa muda mrefu,” akasema.

Kwa upande wake, Lofven alionya kwamba uhuru na uwazi wa kibiashara ni muhimu sana kwa Sweden na EU.
Aliongeza kuwa ushuru mkubwa utaathiri viwanda vya Ulaya hali wao hutengeneza tu asilimia 10 ya vyuma ulimwenguni huku Uchina ikitengeneza asilimia 50.

“Ninaamini ushuru ukiongezwa tutaumia katika siku zijazo. Hakika, ninaunga mkono juhudi za Uropa kuendeleza biashara chini ya mfumo usiokuwa na vikwazo vingi,” akasema waziri huyo mkuu.

Ndani kwa kunaswa wakiuza vileo Kibera bila leseni

Na BENSON MATHEKA
WATU watatu,  walitozwa faini ya Sh50,000 kila mmoja kwa kupatikana wakiuza pombe bila leseni jijini Nairobi na wengine wawili wakatozwa faini ya Sh40,000 kila mmoja kwa kuuza pombe kabla au baada ya saa zilizowekwa kisheria.

Waliopatikana wakiuza pombe bila leseni watafungwa jela miezi sita wakishindwa kulipa faini hiyo na waliokiuka masharti ya leseni zao watafungwa jela miezi mitano.

Hakimu Mkazi wa Kibera Jane Mutuku aliwapa washtakiwa adhabu hiyo walipokiri mashtaka yaliyowakabili.

Bi Jane Mwende na Catherine Njoki walikiri kwamba walipatikana katika eneo la Ngumo mtaani Kibera wakiuza pombe kinyume na kanuni za leseni zao.

Mahakama iliambiwa kwamba walipatikana wakifungua baa kabla au baada ya muda ambao wanaruhusiwa kufanya hivyo.

Nao Mary Mutheu, Douglas Muthama na Nicholas Muriuki walikiri kwamba walikamatwa eneo la Makina Kibera wakiuza pombe bila leseni.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba washtakiwa walikamatwa kwenye msako uliofanywa na maafisa wa polisi. Kiongozi wa mashtaka Charles Mogaka aliomba washtakiwa wachukuliwe kama wakosaji wa kwanza kwa sababu hakuwa na rekodi zao za uhalifu.

Akiwahukumu, hakimu alisema japo washtakiwa walisema walijuta kwa makosa yao, ni muhimu kufuata sheria zilizowekwa katika biashara yoyote ile.

NYOTA YAKO: MACHI 08, 2018

Na SHEIKH KHABIB 

KONDOO
Machi 21 – Aprili 20: Tafuta mtaalamu akushauri kabla ya kuanza mradi wowote kwa wakati huu. Usipuuze chochote utakachoambiwa ufanye. Naona kuna hatari ya kupoteza pesa nyingi usipokuwa mwangalifu.Usitegemee akili zako kwa jambo hili.

 

NG’OMBE
Aprili 21 – Mei 20: Unataka kufanikiwa lakini haujaweka mikakati inayofaa. Punguza matumizi yako hasa katika anasa kwa sababu naona ukiharibu pesa nyingi. Nia ya kufanikiwa itakupa shida kwa wakati huu.

 

MAPACHA
Mei 21 – Juni 21: Wapigie simu watu unaowadai mara moja ili hali yako ya sasa ibadilike. Naona wanakutafuta lakini hawakupati. Baadhi yao wana habari muhimu zinazoweza kukufanya ubadilishe maisha yako kuanzia sasa.

 

KAA
Juni 22 – Julai 22: Jaribu bahati yako katika biashara. Japo maisha ni magumu, mikono yako inaweza kufanikiwa katika biashara ukiipanga vyema. Uliyozoea kufanya kila siku si muhimu wakati huu kwa sababu hayatakufaa kwa vyovyote.

 

SIMBA
Julai 23 – Agosti 22: Mnunulie mtu aliyekusaidia zawadi. Naona haujafanya lolote kumsaidia ingawa alitumia muda na rasilimali zake kukusaidia ukiwa na shida. Hii imefanya ukose amani na mambo yako kukwama. Zawadi itabadilisha mambo.

 

MASHUKE
Agosti 23 – Septemba 23: Utakuwa na amani hata kama huna pesa. Hii ni kwa sababu mambo mazuri yako njiani. Unashauriwa utumie wakati huu kuandaa miradi ya siku zijazo. Anza mipango mipya sasa.

 

MIZANI
Septemba 24 – Oktoba 23: Mbona huelewani na marafiki zako? Haya mambo unayopuuza kama ya kawaida yanaweza kuharibu uhusiano wako na washirika wako na kuleta majuto. Ikiwa unataka amani na raha kati yenu, jiepushe na mizozo.

 

NGE
Oktoba 24 – Novemba 22: Usirudie penzi la zamani kama unavyopanga. Naona balaa na kilio katika maisha yako kutokana na hatua hii. Mfurahishe mchumba wako wa sasa na utapata raha ya ajabu maishani.

 

MSHALE
Novemba 23 – Desemba 21: Chunga usipoteze pesa zako katika mambo yasiyo na manufaa. Usianzishe mradi wowote mpya wakati huu. Leo ni siku mbaya na usipokuwa mwangalifu utachezwa shere.

 

MBUZI
Desemba 22 – Januari 20: Unachotafuta kiko njiani. Unashauriwa usichoke kamwe. Atafutaye hachoki. Kitakuja na bahati ushangae. Jiandae kwa makuu. Lakini usikubali watu wajue unatarajia mazuri.

 

NDOO
Januari 21 – Februari 19: Utalazimika kutia bidii katika mambo yako il bahati ikuangukie. Kumbuka uzembe hufunga ufanisi. Jambo mbaya lililokufika hivi majuzi lilitokana na uzembe huo. Rekebisha makosa yako, kuteleza sio kuanguka.

 

SAMAKI
Februari 20 – Machi 20: Usishangae kuona mambo yakikwendea kombo wakati huu. Mpango wako wa maisha hautafanikiwa hivi karibuni lakini utafika unapotaka hatimaye. Stahamala ni muhimu.

 

Hakuna pesa serikalini, Rotich aungama

DAVID MWERE na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Rotich asema uhaba wa fedha unaokumba serikali umesababishwa na kipindi kirefu cha uchaguzi pamoja na ukame
  • Hakueleza kwa nini serikali imeshindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri nchini na utumizi mbaya wa pesa za umma
  • Sh302 bilioni zilizopendekezwa kutengewa serikali za kaunti zitapunguzwa kwa kati ya Sh15 bilioni na Sh17 bilioni
  • Imebainika ni Sh134 bilioni pekee kati ya Sh302 bilioni zilizohitajika, zilikuwa zimesambazwa kwa kaunti 47 kufikia Jumatano

SERIKALI imekiri kuwa inakumbwa na upungufu wa fedha na hivyo haiwezi kutimiza mahitaji ya kaunti na ufadhili wa miradi ya maendeleo.

Hii inamaanisha kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara itasimama, vyombo vya habari kupunguziwa matangazo na mgao wa fedha serikali za kaunti kupungua ikilinganishwa na ilivyopangwa awali.

Akifichua hayo Jumatano, Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich alisema uhaba wa fedha unaokumba Serikali umesababishwa na kipindi kirefu cha uchaguzi mwaka uliopita pamoja na ukame, hali ambazo alisema zilifanya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) ishindwe kuafikia malengo yake.

“Tumeishiwa na pesa. Hali ya kisiasa nchini iliathiri vibaya biashara nchini. Hatuwezi kugawa kitu ambacho hatuna,” akasema Bw Rotich, alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti.

Haya yanajiri huku ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Pesa za Umma ikionyesha utumizi mbaya wa fedha za Serikali.  Kwa mfano ripoti ya majuzi zaidi ilifichua kuwa haijulikani jinsi Sh204 bilioni za mkopo wa Eurobond zilivyotumiwa.

Ripoti hiyo pia ilionyesha wabunge walioondoka walilipwa zaidi ya Sh569 milioni za usafiri bila kufuata mwongozo inavyohitajika.

Mbali na hayo, Wizara ya Elimu ilisemekana kutumia Sh231 milioni kununua tarakilishi 3,320 zilizonuiwa kupelekwa katika shule za upili, lakini ni tarakilishi 1,107 pekee ambazo zilifikishwa shuleni.

 

Miradi duni

Serikali za kaunti pia zilitajwa kutumia mamia ya mamilioni ya pesa kwa miradi duni na kwa matumizi ambayo hayaboreshi maisha ya wananchi kwa njia yoyote, kama vile usafiri na burudani.

Bw Rotich hakueleza kamati hiyo kwa nini serikali imeshindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri nchini na utumizi mbaya wa pesa za umma.

Waziri alisema Sh302 bilioni zilizopendekezwa kutengewa serikali za kaunti zitapunguzwa kwa kati ya Sh15 bilioni na Sh17 bilioni ili kuwezesha serikali kufadhili mahitaji mengine.

“Tunahitaji kushauriana nanyi maseneta pamoja na magavana ili tuweke wazi mambo ambayo hayawezekani kufanywa kwa kuzingatia changamoto zinazotukumba,” akasema.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na Maseneta Maalum Rose Nyamunga na Fahriya Ali walipinga pendekezo la kupunguza mgao wa serikali za kaunti.

 

Serikali imepungukiwa

“Tuambie tu kuwa serikali imeishiwa! Kile unachotuambia kuhusu kupunguza mgao kwa serikali za kaunti ni jambo ambalo hatuwezi kukubali. Haiwezekani kufanya hivyo wakati uundaji wa bajeti nyingine tayari unaendelea,” akasema Bw Kilonzo.

Lakini Bw Rotich alishikilia msimamo wake kwamba serikali haiwezi kutumia pesa ambazo haina.

Mabadiliko hayo makubwa katika mgao wa fedha za umma yako kwenye bajeti ya pili ya ziada ambayo inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Taifa wakati wabunge watakaporejelea vikao vyao mapema wiki ijayo watakapokamilisha likizo fupi.

Miongoni mwa sehemu zitakazoathirika ni miradi ya maendeleo, ambayo waziri alisema inaweza kusubiri, na matumizi yasiyo muhimu kama vile usafiri, burudani na matangazo.

Waziri pia alikabiliwa na wakati mgumu katika kikao hicho kwani ilibainika ni Sh134 bilioni pekee kati ya Sh302 bilioni zilizohitajika, zilikuwa zimesambazwa kwa kaunti 47 kufikia Jumatano.

Bw Rotich alisema pesa zilichelewa kusambazwa kwa sababu ya marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya ugavi wa fedha.

Tulitishwa kwa kufuta ushindi wa Rais Kenyatta, Jaji Mwilu afichua

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu ameungama kuwa walipokea vitisho baada ya kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Kulingana na Naibu Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu, vitisho hivyo havikuathiri utendakazi wao katika kesi zingine za aina hizo walizozishughulikia.

“Vitisho hivyo havikuyumbisha kwa njia yoyote maamuzi yangu kuhusu kesi zilizofuatia,” Jaji Mwilu alisema Jumanne alipohutubu katika semina ya wabunge kuhusu yaliyojiri katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Vitisho hivyo, havikuingia rohoni mwangu. Na nashukuru Mungu kwa hilo. Nina hakika kuwa vitisho hivyo havikuathiri maamuzi mengine tuliyotoa,”akasisitiza Jaji Mwilu.

Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Kapenguria Bw Samuel Moroto alimtaka DCJ kueleza ikiwa uamuzi wa kufutiliwa mbali kwa ushindi wa Rais Kenyatta ulichangia yeye na wenzake watatu, kupokea vitisho.

“Tulitishwa, hiyo ni kweli kabisa. Sharti nikubali kwa sababu sijui kuficha ukweli,” akafichua.

 

Dereva kupigwa risasi

Baada uamuzi wa kesi hiyo, iliyowasilishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kutolewa dereva wa DCJ Mwili alipigwa risasi na watu wasiojulikana majambazi katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.

Kisa hicho kilitokea mnamo Jumanne Oktoba , 24 2017 siku mbili kabla ya kuandaliwa kwa marudio ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 26. Matokeo ya uchaguzi huo pia ulipingwa na aliyekuwa Mbunge wa Kilome Harun Mwao pamoja na mwanaharakati Njonjo Mue.

 Baada ya kisa hicho, madai yaliibuliwa kuwa majambazi hao walikuwa wakilenga kumuua Jaji huyo kuhusiana na kubatilishwa kwa ushindi matokeo ya uchaguzi wa urais.

Bi Mwilu ni miongoni mwa Majaji wanne waliounga mkono kufutuliwa kwa ushindi wa Rais Kenyatta. Wengine walikuwa Jaji Mkuu David Maraga na majaji Isaac Lenaola na Smokin Wanjala.

Hata hivyo, majaji Jackton Boma Ojwang’ na Njoki Ndung’u walipinga uamuzi huo na kudumisha ushindi wa Rais Kenyatta.

Wawili hao walisema uchaguzi wa urais uliendeshwa kwa njia huru, haki na iliyozingatia katiba na sheria husika za uchaguzi, kauli ambayo pia iliungwa mkono na waangalizi wa uchaguzi kutoka mataifa ya kigeni.

Mzozo wa kilabu cha Simmers: Mmiliki ataka wakurugenzi wasukumwe jela

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kilabu na mkahawa maarufu cha Simmers kilichobomolewa Ijumaa wiki iliyopita Bw Suleiman Murunga amewashtaki wakurugenzi wa kampuni mbili zinazozozania ploti hiyo.

Katika kesi anayoomba iratibiwe kuwa ya dharura Bw Murunga anaomba wakurugenzi wa kampuni za Nilestar Holdings na Green Valley wafungwe jela kwa kukaidi agizo la mahakama kuu na kubomoa kilabu hicho.

Bw Murunga anaomba mahakama kuu iwasukume jela miezi sita wakurugenzi wa kampuni hizi mbili kwa kuidharau mahakama.

Mbunge huyo wa zamani anasema kubomolewa kwa kilabu hicho ni njia ya kuikejeli korti na anaomba korti “iwasukume jela wakurugenzi wa makampuni hayo ndipo sheria na hadhi ya korti idumishwe.”

Pia anaomba korti iwashurutishe wakurugenzi hao wamlipe gharama na kuamuru atambuliwe kuwa mmiliki wa ardhi hiyo.

Ploti hiyo inadaiwa na Bw Madatali Ebrahim, wanawe  Jalaledin Ebrahim na Jamilleh Ebrahim ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Nilestar pamoja na Bi Margaret Wairimu Magugu ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Green Valley.

Bw Murunga amewashtaki wakurugenzi hao pamoja na MabwKinyanjui Magugu,  Gisbon Muchiri Ndungu  na wakili Leo Masore Nyangau.

Anaomba wote wasukumwe jela kwa kukaidi agizo la mahakama kuu iliyotolewa mnamo Julai 14, 2014 na Desemba 2016 ikiwazuia wasimtatize Bw Murunga kwa njia yoyote ile.

Mabaki ya kilabu cha Simmers karibu na hoteli ya kifahari ya 680 katikati ya jiji la Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Sh9 milioni

Waliobomoa kilabu hicho walidai kodi ya nyumba ya Sh7,560,000, ada ya wakili Sh756,000 na ada ya madalali ya Sh910,860.

Bw Murunga anasema wakurugenzi wanaodai umiliki wa jengo hilo walijua kwamba kuna maagizo ya mahakama ya kuwazuia kudai umiliki wa ardhi ambapo kilabu kimejengwa.

Mbunge huyo wa zamani anaomba mahakama ifutilie mbali maagizo mawili yaliyotolewa dhidi yake.

“Ikiwa mahakama haitaingilia mzozo huu bila shaka walalamishi wataingilia na kuanza kujenga, “anasema mlalamishi.

Wakurugenzi wa makampuni hayo yaliwasilisha kesi ya kumtimua kwenye ploti hiyo Feburuari 20 2018 mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani.

Jaji Elijah Obaga alimwamuru Bw Murunga awakabidhi wakurugenzi wa Green Valley na Nilestar nakala za kesi hiyo aliyoamuru isikizwe Aprili 4, 2018.

“Nimesoma kesi iliyowasilishwa na Bw Murunga na kutambua anaomba maagizo makuu yatolewe ya kumtambua mmiliki wa ardhi iliyojengwa kilabu hicho,” alisema Jaji Ombaga.

 

Miaka 32 iliyopita

Mzozo wa umiliki wa ploti hiyo ulianza miaka 32 iliyopita kati ya Bw Madatali na aliyekuwa Waziri marehemu Arthur Magugu.

Ardhi hiyo ilikuwa imeandikishwa kwa jina la Nilestar na Bw Magugu.

Ushahidi uliopo ni kwamba Bw Magugu alikuwa auziwe ploti hiyo na wenye hisa wa Nilestar kwa bei Sh25 milioni. Alilipa Sh19milioni kisha mzozo ukazuka mpango ulipotibuka.

Bw Magugu aliwasilisha kesi mahakamani mnamo 1989 na mnamo 1996 maagano mapya ya kuuzia kilabu hicho kampubi ya Green Valley na Margaret Magugu kwa $ 1.4 ukatiwa saini.

Bw Murunga hatimaye aliibuka akiwa na hati ya umiliki wa ploti hiyo.

Serikali ikome kuwabagua wabunge wanawake wa NASA – Passaris

Na CHARLES WASONGA

HUKU ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Alhamisi, wabunge wa kike wa upinzani wameilaumu serikali kwa kuibagua katika masuala yanayowahusu wanawake.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Bi Esther Passaris Jumatano alidai serikali imewanyima wabunge wa NASA kibali cha kushiriki katika Kongamano la pili la Tume kuhusu hadhi ya Wanawake (CSW2) linaloanza wiki ijayo jijini New York, Amerika.

“Sio haki kwa serikali kutoa kibali kwa wabunge wa kike wa Jubilee pekee na kuwanyima wenzao wa NASA ambao pia waliteuliwa kusafiri kwa kongamano hilo linaloanza tarehe 12 mwezi huu. Wabunge wanawake hawafai kugawanywa kwa misingi ya kisiasa hasa ikiwa wanaenda kuwakilisha nchi,” akasema Bi Passaris.

Alitoa malalamishi hayo katika hoteli moja jijini Nairobi baada ya kuongozwa uzinduzi wa ripoti kuhusu changamoto zilizowakabiliwa wanawake walioshiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.  Ripoti hiyo kwa jina “The Journey of Women Candidates in the 2017 General Elections” ni zao la uchunguzi uliofadhiliwa na shirika la ActionAid Kenya.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge Wanawake (KEWOPA) Purity Ngirichi alikana madai hayo akisema hana habari kwamba baadhi ya wenzake hawajapata kibali cha kushiriki katika kongamano hilo.

“Ujumbe wa Kenya, haswa sisi kama wanachama wa KEWOPA, haijapokea habari kama hizo. Hata hivyo, nitawasiliana na Wizara ya Mashauri ya Kigeni kwa maelezo zaidi,” akasema Mbunge huyo wa Mwakilishi wa Kaunti ya Kirinyaga.

Baadhi ya masuala yatayojadiliwa katika kongamano hilo ni changamoto na mafanikio katika mchakato mzima wa kuwapiga jeki wanawake na wasichana wa mashambani kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Jumatano, Bi Passaris alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kupigania viti vya kisiasa katika chaguzi zijazo ili waweze kupata nafasi ya kubuni sera ya maongozi ya kuchochea maendeleo nchini.

“Inasikitisha kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita ni asilimia tisa pekee ya wanawake walishinda viti. Hii ni sawa na wanawache 157 pekee, idadi ambayo haitoshi kubisa ikizingatiwa kuwa asilimia 52 ya Wakenya ni wanawake. Kwa hivyo, nawahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kutafuta viti vya uongozi,” akasema Mbunge huyo wa chama cha ODM.

Rais wa China akaangwa kwa nia yake ya kusalia madarakani milele

Na AFP

BEIJING, CHINA

MPANGO wa Rais wa China Xi Jinping kutaka kuwa kiongozi wa maisha umewakera, na kuwashangaza watu wengi nchini humo.

Mmoja wao ni mhariri wa gazeti linalomilikiwa na serikali Bw Li Datong ambaye juzi alitumia maneno makali, ya lugha moja ya kigeni, mbele ya halaiki akilaani njama hiyo ya chama tawala cha Kikomunisti, Communist Party.

Chama hicho kinadai kuwa “umma unaunga mkono” mswada wa sheria unaopania kubatilisha kipengee cha Katiba kinachodhibiti mihula ambayo rais anapaswa kuhudumu.

Bunge la nchini hiyo, linalodhibitiwa na chama hicho tawala, linatarajiwa kupitisha mswada huo Jumapili.

Li ni miongoni mwa raia ambao wamekaidi amri ya serikali na kulalamika hadharani kuhusu mswada huo.

“Nilishangazwa na tangazo hilo. Sikuamini kwamba Rais Xi na chama chake wangechukua hatua hiyo. Inasikitisha zaidi,” Li, 66, ambaye ni mhariri wa gazeti la China Youth Daily alisema kwa lugha ya Kiingereza.

Li alipata umaarufu kimataifa, alipokitaka chama cha National People’s Congresss (NPC), kupinga marekebisho hayo ya katiba.

Kupitia barua ya wazi aliyoiandika wiki jana, mhariri huyo alionya kuwa hatua hiyo “itapanda mbegu ya uhasama ya fujo nchini China.”

“Msipojitokeza wazi wazi na kupinga hatua hii, watadhani kwamba sote twakubaliana nao,” Li akaambia shirika la habari la AFP.

Barua hiyo iliibua msisimko mkubwa miongoni mwa Wachina kwenye mitandao ya kijamii wiki jana, hali iliyopelekea kuzima mjadala kuhusu suala hilo.

Dai kuwa umma unaunga mkono hatua hiyo, kwa kauli moja, liko kwenye taarifa ya marekebisho yaliyopendekeza katika kikao cha ufunguzi wa mkutano wa kila mwaka wa NPC mnamo Jumatatu. Wabunge wote wameelezea imani kwamba watapiga kura ya “ndio” mnamo Jumapili.

Lakini watu wengi nchini China- kuanzia wafanyabiashara, makundi ya akina mama, walimu, viongozi wa kidini na maafisa wastaafu- wamepinga hatua hiyo kupitia mitandao ya kijamii na mahojiano na wanahabari wa kigeni.

SHANGAZI AKUJIBU: Nilifumania mke nikamuacha, wa zamani ananitaka

Na SHANGAZI SIZARINA

Hujambo shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini nikamuacha mke wangu nilipomfumania na mwanaume mpango wake wa kando. Bado sijaoa tena na sasa mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu anataka tuwe na uhusiano wa pembeni ingawa ameolewa. Ananiambia mume wake ni mtu wa shughuli nyingi na huwa anamuachia baridi sana. Bado ninampenda lakini sitaki kuvunja ndoa yake. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Ni muhimu kuheshimu ndoa ya mwanamume mwenzako hata kama mwanamke huyo alikuwa mpenzi wako. Ukweli ni kwamba mkishikana tena kisha mume wake ajue kutakuwa na shida. Ni heri utafute mwanammke ambaye hajaolewa.

 

Nimegundua ana mke baada ya miaka miwili
Salamu kwako shangazi. Nimekuwa na mwanaume mpenzi wangu kwa miaka miwili sasa na nimegundua majuzi tu kuwa ana mke. Jambo hilo limeniudhi sana kwani hajawahi kuniambia lakini nashindwa kumuacha kwa sababu nampenda kwa moyo wangu wote. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Umejua ukweli kwamba mwanaume huyo alikudanganya kwa kutokwambia kuwa ana mke. Na ingawa unasema unampenda sana, huwezi kubadili ukweli kwamba ana mke. Sasa ni juu yako kuamua iwapo utaendelea kuwa mpango wake wa kando ama utamuacha utafute mwingine.

 

Amedokeza anipenda
Shikamoo shangazi? Kuna kijana fulani ambaye amenidokezea kuwa ananipenda nami pia nampenda. Tatizo ni kuwa yeye amemaliza masomo ilhali mimi bado. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Ushauri wangu kwako ni kuwa huu si wakati unaofaa kwako kuanza mahusiano ya kimapenzi kwa sababu bado wewe ni mwanafunzi. Unahitaji kumakinika masomoni ili uweze kufaulu katika mtihani wa mwisho. Mwambie kijana huyo asubiri umalize shule.

 

Nawaona wanaume wote kama shetani
Nina umri wa miaka 24 na niliachana na mume wangu niliyempenda sana baada ya kunitendea unyama. Tangu wakati huo imekuwa vigumu kwangu kuwa na mapenzi ya dhati na mwanaume yeyote kwani kwangu kila mwanaume ni kama shetani. Bahati mbaya ni kwamba bado sijazaa na natamani sana kuwa na mtoto. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Pole mwanangu kwa yaliyokupata ingawa hujaelezea kwa kina. Ni kweli kuna jambo unaloweza kutendwa na mtu umchukie yeye, jamaa zake na binadamu kwa jumla. Lakini nitakukosoa kuwa kitendo au vitendo vya watu fulani wabaya haviwezi kuwafanya watu wote kuwa wabaya. Dunia hii ina wabaya na wazuri pia. Usikate tamaa katika kutafuta mume mwingine kwani naona wewe bado ni mchanga. Kila la heri.

 

Namshuku rafiki
Hujambo shangazi. Ninashangaa kuhusu kinachoendelea kati ya mpenzi wangu na mwanaume rafiki yangu. Sote tunasoma chuo kikuu na siku za hivi majuzi nimewapata mara kadhaa wakipiga gumzo na kucheka. Nimemuuliza mpenzi wangu akasema hakuna chochote kati yao. Tafadhali nishauri.

Inawezekana uhusiano wao ni ule tu wa mwanafunzi kwa mwenzake. Huwezi kukata kauli kuwa wawili hao wana uhusianowa kimapenzi kwa kuwa umewapata wakizungumza. Iwapo unashuku kuna kitu kinachoendelea kati yao, chukua muda wa kutosha uchunguze ili ukweli.

 

Ananiudhi sana
Shikamoo shangazi. Kuna msichana ambaye nimemwambia wazi kuwa ninampenda lakini ananiudhi kwa kunipuuza. Nikimpigia simu ama kumtumia SMS hajibu. Tabia yake hiyo inaniumiza sana moyoni. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Huyo bado si mpenzi wako kwa hivyo sielewi ni kwa nini unaumia moyoni akikosa kujibu simu zako. Hiyo ni kuonyesha kuwa hakujali na kwangu mimi naona unapoteza wakati wako ukimfuata.

 

Nimepata fununu ana mwingine
Vipi shangazi? Nina mpenzi ninayempanda kwa dhati. Hata hivyo nimesikia fununu kuwa ana uhusiano na mwanamke mwingine. Habari hizo zimenitia tumbo joto na sasa nafikiria kumuacha. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Si vyema kuchukua hatua kwa kutegemea uvumi kutoka kwa watu. Inawezekana kwamba watu wanaoeneza habari hizo ni maadui zake na nia yao ni kuvuruga uhusiano wenu. Itakuwa bora ukimuuliza mwenyewe.

 

NYOTA YAKO: MACHI 07, 2018

Na SHEIKH KHABIB

KONDOO
Machi 21 – Aprili 20: Mambo ya kesho yapange leo. Kaa utulie kwako leo. Usioshe sana kwa sababu baridi itaweza dhuru afya yako. Tumia chakula chepesi leo usichafue tumbo.

 

NG’OMBE
Aprili 21 – Mei 20: Ujasiri wako ndio tunu yako kuu. Utapata pesa za ziada leo. Hata hivyo unashauriwa uzitumie vyema. Ikiwezekana weka akiba sehemu ya pesa hizo ikifae siku zijazo.

 

MAPACHA
Mei 21 – Juni 21: Usikutane na rafiki yako leo. Naona mambo si shwari kama zamani. Fanya kazi kwa bidii. Usijali watu wanapokukosoa, hii ni kawaida ya wanadamu. Huwezi kuwaridhisha, jali mambo yako.

 

KAA
Juni 22 – Julai 22: Huenda mambo yasianze utakavyo leo. Hiki kisiwe kizingiti. Songa mbele na miradi yako, kuna faida tele hatimaye. Kumbuka kushukuru wanaokusaidia kwa kila jambo.

 

SIMBA
Julai 23 – Agosti 22: Utawasalimu watu wakubwa kwa mikono yako leo. Toka uende ulikopanga kwenda bila kusita. Epuke kunako watu wengi. Kufaulu kwako kutatengemea imani yako. Songa mbele bila kuangalia nyumba.

 

MASHUKE
Agosti 23 – Septemba 23: Leo ni siku yakufanya uhusiano na mpenzi wako kuwa dhabiti . Si muhali kujumuika na watu wengine lakini kiosha roho wako anakuhitaji zaidi. Mjali anavyokujali .

 

MIZANI
Septemba 24 – Oktoba 23: Ondoa hofu. Utakamilisha mradi ulioanzisha, bora uwe na imani. Wanaokuvunja moyo watashangaa hivi karibuni ukipaa. Hakuna atakayezima bidii yako ya mchwa. Usiungane na watu wengine.

 

NGE
Oktoba 24 – Novemba 22: Wachumba wamekuwa wakikutema na unashangaa ni kwa nini. Unafaa kujiamini kwa sababu naona ukipata mchumba wa kudumu hivi karibuni. Huyu ndiye wako, waliotangulia ni wapita njia.

 

MSHALE
Novemba 23 – Desemba 21: Kupumzika kutakufaa sana wakati huu. Ikiwezekana nenda likizo ya mbali na kazi yako utulie kwa muda. Naona nyota yako imetulia mahali pamoja kwa sasa.

 

MBUZI
Desemba 22 – Januari 20: Naona unajivuta sana kufanya mambo yako na hulka hii imekunyima mengi mazuri. Itakubidi uanze kufanya mazoezi ili upunguze uzito wa mwili unaokutatiza. Anza kufanya hivi mara moja.

 

NDOO
Januari 21 – Februari 19: Unayedhani kaiba pesa zako si yeye. Kuna pepo aliyetumwa na walioiba mkosane naye. Hata hivyo naona walioiba pesa hizo wameanza kukosana wenyewe kwa wenyewe na watarejesha pesa zako.

 

SAMAKI
Februari 20 – Machi 20: Kuna watu wa nia mbaya wanaokuzunguka. Wamekuwa wakijinufaisha na mali yako kwa muda mrefu na hawakutakii mazuri. Na baadaye watakuacha. Waepuke uwe salama.

 

Polo aachilia mkojo ndani ya basi safarini

Na TOBBIE WEKESA

TULIENGE, BUNGOMA

ABIRIA waliokuwa wakisafiria basi moja walipigwa na mshangao baada ya polo kuachilia mkojo ndani ya gari dereva alipokataa kusimamisha gari ili ajisaidie.

Duru zinasema polo alikuwa amelalamika kubanwa na mkojo kwa muda mrefu. Alimuomba utingo amueleze dereva asimamishe gari ili atulize hali. Inadaiwa baada ya kuelezwa na utingo kuhusu ombi la abiria, dereva aliongeza kasi ya gari akimtaka jamaa avumilie hadi mwisho wa safari.

Polo aliamua kumsongea dereva na kumueleza mwenyewe. “Dereva tafadhali simamisha gari kidogo. Nimebanwa sana,” polo alimueleza dereva.

Duru zinasema dereva alimuangalia polo na kuongeza mwendo wa gari. “Ukipanda gari hukujua haina choo. Mimi sisimamishi gari. Jisoti,” dereva alimueleza polo.

Kulingana na mdokezi, polo alirudi kwenye kiti chake na kuachilia mkojo bila wasiwasi wowote ukatapakaa garini.

“Dereva ameniambia yeye hatasimamisha gari kwa hivyo nijisoti,” polo alisema huku mkojo ukiendelea kumtoka.

Utingo alimuamrisha dereva kulisimamisha gari mara moja. Gari lilisimamishwa na polo akaamrishwa atoke nje. “Mbona unasimamisha gari? Shida iko wapi? Mimi nimejisoti ulivyonieleza,” polo alimuambia dereva huku abiria wakiangua vicheko.

Utingo alianza kumzomea polo. “Wewe ni mtu wa aina gani? Huna aibu hata kidogo kutoa kifaa chako na kukojoa hadharani mbele ya umma,” utingo alimzomea polo.

Dereva naye alimuamrisha polo aoshe mkojo garini mara moja. “Sitaki ujinga wenu. Mimi si rika lenu. Nilipowaomba msimamishe gari si mlikataa. Makosa si yangu,” polo naye aliwakemea dereva na utingo na kuungwa mkono na baadhi ya abiria.

 

WANDERI: Falsafa ya Mbaya Wetu inaliponza taifa hili letu

Gavana wa Kericho Paul Chepkwony aliyejitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Bi Lily Koros. Picha/ Maktaba


Na WANDERI KAMAU

HATUA ya viongozi wa Ukanda wa Bonde la Ufa kujitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Bi Lily Koros dhidi ya kutowajibika kwake ni ya kutamausha.

Wakiongozwa na Gavana Paul Chepkwony wa Kericho, viongozi hao wamedai kwamba makosa ambayo yamefanyika katika hospitali hiyo chini ya usimamizi wa Bi Koros ni “njama za mahasidi wake” ili kumwondoa mamlakani.

Kauli hii imeibua tena mtindo wa kawaida ambao umekuwa kama sehemu ya mtindo wetu wa kimaisha, ambapo jamii anakotoka “mkosa” hujitokeza kumtetea kwa vyovyote vile, bila kutathmini kwa kina ikiwa alikosa au la.

Ni mtindo ambao umetaasisika kote barani Afrika, hali ambayo imeathiri uwepo wa uwazi na uwajibikaji.

Katika kesi ya Bi Koros, kilichopo ni kwamba viongozi hao wanamtetea kwani anatoka katika eneo hilo, na pia ni Mkalenjin, sawa na wao.

Hii ni bila kuzingatia maovu yote ambayo yametokea katika hospitali hiyo; kutoka visa vya wizi wa watoto, madai ya kubakwa kwa kina mama waliojifungua na wahudumu wa mochari, visa vya wizi na majuzi kupasuliwa kwa mgongwa asiyefaa.

Kwa hayo yote, msimamo wa viongozi hao ni kwamba Bi Koros “kasingiziwa na mahasidi wake!”

Naam, mantiki ya haya ni kwamba hii ni hadaa ya nafsi. Ni wazi kwamba huu ni mwendelezo wa falsafa mbaya ya ‘Mbaya Wetu.’

Ni mtindo hatari, ambao umeizalia Afrika viongozi mazimwi, ambao wamegeuka kuwa balaa kuu kwa nchi zao.

Mazimwi hao huwanyonya damu wana waliowachagua, kwa kuwadhulumu na kutaasisisha udikteta katika nchi hizo.

 

Mifano

Mifano dhahiri ni viongozi kama marehemu Mobutu Seseseko (DRC Kongo), Idi Amin Dada (Uganda), Meles Zenawi, Haile Mengistu Mariam (Ethiopia), Mohamed Siad Barre (Somalia), Hastings Kamunzu Banda (Malawi), Daniel arap Moi (Kenya) kati ya wengine wengi.

Katika enzi zao, viongozi hao waliziteka nchi zao na kuzigeuza kama makazi yao. Waligeuka kutoka wanadamu hadi miungu wa kidunia, waliosifiwa na kila mmoja.

Cha kushangaza ni kwamba, licha ya dhuluma hizo zote, walibaki kuwa “mashujaa” katika jamii zao! Aidha, jamii hizo ziliwaona kama ‘wakombozi’ wakuu waliotumwa kutoka Kuzimu!

Ujinga na uzumbukuku huo nao umeigeuza Afrika kuwa kama jaa ya utumwa wa nafsi. Bara lililoonyesha dalili za ukombozi liligeuka kuwa mtumwa wa tamaduni hafidhina zisizo na umuhimu wowote.

Mfano halisi wa baadhi ya ujuha huo ni hafla ya kitamaduni ya ‘Umhlanga’ ambayo hufanyika kila mwaka nchini Swaziland, ambapo Mfalme Mswati III huwa anamchagua bibi mpya kila mwaka. Hii ni licha ya taifa hilo kuwa moja ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu sana cha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa ufahamu huo, hatuna jingine kama jamii, ila kupanua mawazo yetu, ili kujikomboa kutoka utumwa huo. Si haki, hata kidogo, kutetea makosa, hata yaliyo dhahiri.

akamau@ke.nationmedia.com

 

TAHARIRI: Watu wasitie siasa zenye ukabila KNH

Na MHARIRI

SHINIKIZO la kumtaka Waziri wa Afya Sicily Kariuki aondoke kwa kumpa afisa mkuu wa Hospitali Kuu ya Kenyatta likizo ya lazima, ni jambo linalostahili kushtumiwa vikali.

Waziri alichukua hatua hiyo ili kutoa nafasi ya uchunguzi kufanywa katika hospitali hiyo, ambayo imegonga vichwa vya habari katika siku za hivi punde.

Huenda kweli kuna njama za kumuondoa afisa mkuu huyo, lakini pia lazima Wakenya wajue ukweli kuhusu yanayojiri katika hospitali hiyo, ndiposa hatua hiyo imechukuliwa.

Kwa hivyo, hatua ya baadhi ya viongozi kujitokeza kudai kusimama pamoja na mtu wa jamii yao, inastahili kushtumiwa. Lazima viongozi wawe wakitoa nafasi ya uchunguzi kufanywa ili ukweli ubainike.

Yafaa watambue kuwa kama afisa mkuu wa hospitali, Bi Koros alikuwa na wajibu wa kufuatilia kinachojiri, hata kama hakuwa mhusika binafsi.

Ni jambo la kushangaza jamii zinapojitokeza kutetea “mtu wao” bila ya kubainisha ukweli ikiwa wana makosa au la.

Kwa taifa hili kukabiliana na ukabila lazima watu waweze kuelewa kuwa hata watu wa jamii zao hufanya makosa, na wanapofanya makosa, lazima wachukuliwe hatua. Wakenya wanastahili kujifunza kutetea haki na sio kabila, kwa nchi hii kuweza kuimarika.

Ingawaje si vyema kukaa kimya mtu anapoona dhuluma, ni muhimu kuhakikisha kuwa unachotetea ni cha haki. Yashangaza kuwaona watu wa jamii fulani wakijitokeza kuwatetea maafisa wakuu serikalini ambao huenda wameshtumiwa kwa ufisadi, ilhali ni pesa za mlipaji kodi ambazo zimefujwa.

Katika suala hili la hospitali ya Kenyatta, tunataka kuona uchunguzi wa kina na Wakenya kuelezewa matokeo yake, bila kuingiza siasa ama dhuluma. Ikiwa afisa mkuu hana makosa yoyote, bila shaka Wakenya wanatarajia kuwa arejeshwe kazini.

Na iwapo ataondolewa, Wakenya pia wafafanuliwe sababu zinazoelekeza kuondolewa kwake.

Hata hivyo, kwa sasa tunatarajia kuwa sawa na jinsi ambavyo malalamishi haya yameshughulikiwa upesi, vile vile huduma katika hospitali hii zitaimarishwa, kuhakikisha mgao wa fedha unaotosha, kuwepo kwa vifaa pamoja na kuwajali wahudumu waliopo.

Serikali ihakikishe kuwa juhudi na hatua inazochukua sio za kuwafumba Wakenya macho kwa muda mfupi, na kesho tunasalia kuzungumzia masuala yale yale.

 

Hatari nchi kugeuzwa jangwa kufuatia ukataji wa miti kiholela

Na BENSON MATHEKA

KENYA inakabiliwa na hatari ya kugeuka jangwa ikiwa ukataji miti kiholela, uchomaji makaa na uzoaji changarawe mitoni utaendelea bila kuthibitiwa.

Wataalamu wa mazingira wanaonya kwamba kasi ambayo Wakenya wanakata miti inaangamiza misitu, kukausha vyanzo vya maji na kuathiri hali ya hewa.

Hofu ya wanamazingira ni kuwa ukataji miti unaendelea bila miti mipya kupandwa jambo ambalo ni hatari kwa mazingira katika nchi ambayo idadi ya watu inaendelea kuongezeka.

Dkt Isaac Kalua, mwanzilishi wa Shirika la Green Africa Foundation asema licha ya hali hiyo, Kenya imepiga hatua katika ukuzaji wa misitu.

“Uchomaji wa makaa ni kwa sababu ya watu kupata riziki. Serikali zinazopiga marufuku ukataji miti zinapaswa kuwapa wakazi njia mbadala za kupata riziki,” alisema.

Anahisi kwamba kuna haja ya nia nzuri kutoka kwa wanasiasa kulinda na kuimarisha misitu kama kubuni jopo kazi la kutafuta jinsi ya kulinda misitu.
Mnamo Jumatatu, naibu rais William Ruto alizindua jopo la watu kumi la kuchunguza jinsi misitu inavyosimamiwa.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, kila nchi inapaswa kuhakikisha ina asilimia 10 ya misitu  jambo ambalo wataalamu wa mazingira wanasema ni ndoto  Kenya.

Misitu mikubwa kote nchini imevamiwa na wafanyabiashara wanaokata miti kiholela kupasua mbao, kuchoma makaa na kupata mashamba bila kujali athari za vitendo vyao kwa mazingira.

 

Marufuku

Ni hali hii iliyofanya serikali ya kitaifa na serikali kadhaa za kaunti kupiga marufuku uchomaji wa makaa, upasuaji wa mbao na uzoaji wa changarawe mitoni.

“Huwezi kutenganisha miti na mito. Ni miti katika misitu inayofanya nchi kuwa na mito yenye maji. Miti ikikatwa, mito huwa inakauka na ikikauka, binadamu na wanyama hukosa maji,” asema mwanamazingira Simion Mutua wa shirika la Trees for Life.

Dkt Isaac Kalua analaumu wanasiasa kwa uharibifu wa misitu.

“Changamoto tulizo nazo ni za kisiasa, tunafaa kufuata mkondo wa sayansi ikiwa tutalinda misitu yetu, lakini matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kuna nia njema kutoka kwa wanasiasa|” ashauri Dkt Kalua aliye mwenyekiti wa shirika la kusimamia vyanzo vya maji Kenya (KWTA).

Ripoti ya hali ya misitu iliyotolewa 2016 na aliyekuwa waziri wa mazingira Judi Wakhungu ilionyesha kuwa misitu Kenya ilipungua kutoka  ekari 4,670,866 mwaka wa 1990 hadi ekari 3,492,358  mwaka wa 2000.

 

Asilimia 7

Kufuatia juhudi za serikali ya Rais Mwai Kibaki, kiwango hicho kilipanda hadi ekari  4,137,701 mwaka wa 2010. Mwaka 2017, serikali ilisema kiwango cha misitu kilikuwa asilimia 7. Bw Kalua anasema mwaka huu Kenya imefikia asilimia 7.2 na ina uwezo wa kufikia asilimia 10.

Kulingana na ripoti hiyo, Kenya hupoteza Sh6 bilioni kwa sababu ya uharibifu wa misitu kila mwaka na kwamba asilimia 70 ya vyanzo vya  maji vinakabiliwa na hatari ya kuangamia.

Baadhi ya misitu mikubwa ambayo imeathiriwa na wakataji wa miti ni Mlima Kenya, Aberdares na Mau,  Mlima Elgon na Cherangani.

Kuna misitu 22 ambayo imesajiliwa na kuchapishwa kama vyanzo vya maji nchini. Hata hivyo, wanamazingira wanasema juhudi za kulinda misitu hutatizwa na maslahi ya kisiasa na ukosefu wa sera madhubuti za kuisimamia.

“Uharibifu wa misitu ili kuwavutia wapigakura unatatiza juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kufikia 2030,” aeleza.

 

Siasa

Afisa mmoja wa shirika la misitu ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa kuhofia kazi yake alisema juhudi za kulinda misitu Kenya zinaingizwa siasa. “Hii inafanya Kenya kualika ghadhabu ya hali ya hewa kama iliyoshuhudiwa kuanzia Desemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu.

Nina hakika tukiendelea kuingiza siasa katika masuala ya mazingira, Kenya itakuwa jangwa katika miaka michache ijayo,” alieleza afisa huyo.

Kufikia 2016, ni asilimia 7 ya Kenya iliyokuwa imepandwa miti. Ripoti  hiyo inafichua uharibifu wa misitu katika Mau, Mlima Kenya na msitu wa Marmanet ambao ulifanya maji katika mito mingi kupungua.

Inaeleza kwamba tisho kuu kwa misitu ni uvamizi,  watu kugawiwa ardhi ya misitu, makao haramu na ukataji miti kinyume cha sheria.
Ripoti iliangazia hali ya misitu katika maeneo ya Kati, Bonde la Ufa, Mashariki na Magharibi.

 

Idara yatabiri kupungua kwa mvua kuanzia Jumatano

Na VALENTINE OBARA

MVUA kubwa ambayo imekuwa ikinyesha tangu mwishoni mwa wiki iliyopita itaanza kupungua Jumatano katika maeneo mengi nchini, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imesema.

Mvua hiyo ambayo kufikia Jumanne ilikuwa imesababisha mafuriko na vifo vya watu na mifugo na pia uharibifu wa mali ilikuwa ni ya muda kabla msimu wa mvua ya masika uanze kati ya mwishoni mwa mwezi huu na mapema Aprili.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa jana ilitoa utabiri wake kuhusu jinsi hali itakavyokuwa kuanzia leo hadi Jumatatu wiki ijayo.

Katika nyanda za juu za maeneo ya Kati ikiwemo Kaunti ya Nairobi, kutakuwa na vipindi vya jua katika kipindi hicho. Maeneo mengine ya sehemu hii ni kaunti za Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi.

Hali tofauti imetabiriwa katika ukanda wa Pwani kwani kutakuwa na mvua katika maeneo machache leo asubuhi hasa Kusini mwa Pwani, lakini vipindi vya jua vinatarajiwa siku nzima kuanzia kesho hadi Jumapili.

Kaunti zinazopakana na Ziwa Victoria, zilizo magharibi mwa nchi na zile za maeneo ya Rift Valley pia zitashuhudia jua asubuhi kuanzia leo hadi Jumatatu ingawa maeneo machache yatapokea mvua leo mchana.

Mvua itakayonyesha mchana leo katika eneo la South Rift, hasa Kaunti ya Narok, itakuwa kubwa kuliko maeneo mengine ya Rift Valley ambapo kutanyesha, kulingana na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini.

Kaunti za Kaskazini Magharibi mwa nchi ambazo ni Turkana, Pokot Magharibi na Samburu zimetabiriwa kuwa na jua isipokuwa katika maeneo machache lao na kesho.

Katika Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos na Taita Taveta zilizo nyanda za chini za Kusini Mashariki mwa nchi, inatarajiwa kutakuwa na mvua asubuhi na mchana leo, ingawa jua litachomoza kesho hadi Jumatatu.

Hali sawa na hii imetabiriwa kuwepo katika Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zilizo Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kundi lamtetea Oparanya kwa kuhudhuria hafla ya Jubilee

Gavana wa Kakamega Bw Wycliffe Oparanya. Picha/ Maktaba

Na SHABAN MAKOKHA

KUNDI la wanasiasa kutoka Kaunti ya Kakamega, limemtetea Gavana Wycliffe Oparanya kutokana na hatua yake ya kuhudhuria sherehe ya kukaribishwa nyumbani ya waziri wa Michezo, Rashid Mohammed Echesa.

Wanasiasa hao walikuwa wakijibu madai yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa chama cha ODM, ambao walimshutumu Bw Oparanya kwenda katika sherehe hiyo, iliyohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto.

Kundi la madiwani wa zamani kutoka maeneo ya Butere na Mumias walisema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna anafaa kufahamu kuwa Bw Oparanya ni miongoni mwa vigogo wakuu wa chama hicho.

Wakiongozwa na Michael Keya, madiwani hao wa zamani walisema Bw Oparanya amewekeza rasilimali nyingi katika chama cha ODM hivyo hafai kudunishwa.

Bw Sifuna na wabunge Samuel Atandi (Alego Usonga) na Caleb Amisi (Saboti) walimshambulia Bw Oparanya huku wakimtaka kuhudumia wakazi wa Kakamega badala ya kujihusisha na siasa za urithi wa kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2022.

Watatu hao walimtaka Bw Oparanya kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Sammy Aina aliyewania kiti cha seneta wa Kakamega katika uchaguzi wa Agosti 8, mwaka jana lakini akapoteza, aliwataka wanasiasa wa NASA kukoma kumshambulia Gavana Oparanya kwa kuhudhuria sherehe za kumkaribisha Bw Echesa.

‘Marehemu alifichua waliomuua kabla ya kufa’

Aliyekuwa diwani wa wadi ya Riruta, Nairobi, Bw Samwel Ndungu. Picha/ Maktaba

Na ERIC WAINAINA

DAKIKA chache kabla ya kufariki, Bi Lucy Njambi, mke wa aliyekuwa diwani wa wadi ya Riruta, Nairobi, aliambia watu wa familia na madaktari kwamba ni mumewe aliyepanga shambulio ambalo alichomwa mwili kwa asidi, Mahakama Kuu ilifahamishwa Jumanne.

Hii ilielezwa kwenye kesi ambapo mumewe marehemu, Samwel Ndung’u, Bi Joyce Njambi, ambaye anadaiwa kuwa mpenzi wake na Bw Wilson Mwangi, wameshtakiwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu kwamba mnamo Januari 24 walishirikiana na watu wengine ambao hawajashtakiwa kumuua Bi Njambi, 24.

Bi Esther Nyambura, ambaye ni shangazi ya marehemu, aliambia mahakama kwamba mnamo Januari 24, baada ya mwathiriwa kupelekwa hospitali ya Kiambu Level Five na Msamaria Mwema aliyempata Kamiti Corner, familia ilipokea simu kutoka hospitali hiyo na wakakimbia huko mara moja.

Akitoa ushahidi, Bi Nyambura alisema alipofika hospitali mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi alimpata marehemu kitandani.

“Nilimuuliza kama alinifahamu na akajibu ndio. Nilimuuliza kilichotendeka na akajibu, ‘haki ni baba Njoro’ , muulize,” Bi Nyambura aliambia mahakama.

Baada ya muda mfupi, Bi Njambi ambaye alisema alikuwa na maumivu mengi, alihamishiwa hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambapo aliandamana na watu wachache wa familia akiwemo Bi Nyambura.

Katika hospitali ya Kenyatta, Bi Nyambura, ambaye mara kwa mara alishindwa kuzuia machozi kortini, alisema alimuuliza kilichotendeka na akarudia kwamba ni mumewe aliyehusika na baadaye alipoulizwa na madaktari alitoa jibu hilo hilo.

Bi Fidelis Muthoni, ambaye pia ni shangazi wa marehemu, aliambia mahakama kwamba kabla ya kisa hicho, Bi Njambi alikuwa amemweleza kwamba alihofia maisha yake kwa sababu Ndun’gu alikuwa akidai alikuwa na uhusiano kimapenzi na wanaume wengine.

Kesi inaendelea.

 

Atoroka baada ya kuua mtu na kunywa damu yake

Na JADSON GICHANA na PETER MBURU

POLISI katika kaunti ya Kisii wanamsaka mwanamume aliyemuua mwenzake kwa kumfuma mkuki kifuani na kunywa damu yake.

Mkuu wa polisi wa Gucha Kusini, Bw Moses Kanyi alisema mshukiwa aliyetambuliwa kama Kennedy Keraka, 45, alitorokea Trans Mara baada ya kumuua Bw Daniel Obara.

Mke wa marehemu, Bi Risper Kwamboka Obara, alisema mumewe alitoka nyumbani jioni na kumweleza kuwa alikuwa akienda kudai pesa zake.

“Mume wangu aliniaga kuwa alikuwa akienda kudai pesa kutoka kwa mtu aliyemuuzia kikapu cha kuchunia majani chai. Baada ya masaa mawili, nikasikia kelele kwa majirani kuwa mume wangu amekufa,” akasema.

Bw Kanyi alisema wananchi waliojawa na hasira baada ya tukio hilo, walizichoma nyumba mbili za mshukiwa na kuharibu mimea iliyokuwa shambani mwake.

Kwingineko mjini Nakuru, mwanamume anayetuhumiwa kumuua shemeji yake wakipigania shati, jJumanne alijitetea kuwa marehemu alikuwa rafikiye mkubwa na kwamba alikufa kwa bahati mbaya.

Joel Mesheti Esho, 31, anatuhumiwa kumuua Bw Joel Mpapa Murumbi ambaye alikuwa mume wa dadake mnamo Mei 15, 2013, ikidaiwa walikuwa wakizozania shati.

Mashahidi awali walikuwa wamemweleza Jaji Maureen Odero kuwa mshtakiwa alimvamia marehemu kwa gongo walipokuwa wakipigana, mshukiwa akitaka kutwaa shati alilokuwa amevalia marehemu. Ndipo mshtakiwa alipompiga kwa gongo hilo kichwani.

Daktari aliyemfanyia marehemu upasuaji alisema kifo cha Mpapa kilitokana na majeraha kisogoni kwa sababu ya kupigwa na kifaa butu, wala si kuangukia jiwe kama alivyojitetea mshukiwa.

Kesi hiyo itaamuliwa Mei 4, mwaka huu.

Wazazi: Vitabu hivi vinawapotosha wanafunzi, viondolewe

Na VALENTINE OBARA

WAZAZI Jumanne waliungana na walimu wa shule za sekondari kushinikiza kuondolewa kwa vitabu vipya vya Kidato cha Kwanza wanavyosema vinapotosha wanafunzi kutokana na makosa mengi.

Lakini kwa upande wao wachapishaji walijitetea vikali wakisema ni jukumu la walimu kurekebisha makosa wanayopata kwenye vitabu hivyo.
Hii inafuatia ufichuzi wa Taifa Leo hapo jana kuhusu vitabu vipya vilivyosambazwa na Serikali kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kuwa na makosa mengi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wazazi (KNAP), Bw Nicholas Maiyo alisema dosari zilizogunduliwa na walimu hazifai kupuuzwa zisije zikapotosha wanafunzi.

“Makosa yaliyomo ni makubwa na tunachukulia jambo hili kwa uzito. Inafaa vitabu hivyo viondolewe na utathmini wa kina ufanywe kwanza,” akasema Bw Maiyo aliongeza kuwa dosari zilizomo zinafanya mpango mzima wa vitabu bila malipo kukosa maana licha ya kugharimu Serikali Sh7.5 bilioni.

Mpango huo uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Januari 5, ulipelekea usambazaji wa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Kemia, Fizikia na Biolojia kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza waliojiunga na shule za upili za umma.

“Inatia wasiwasi sana kama wanafunzi watakuwa wanasoma mambo yenye makosa. Sasa tumeachia wizara iamue kile watakachofanya lakini pendekezo letu ni kuwa vitabu hivyo viondolewe darasani,” akasema.

Alishauri pia walimu wawe wakiripoti mapema wanapotambua kuna makosa kwenye vitabu ili vingine visichapishwe, na hali hiyo itatuliwe mapema.

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi. Picha/Jared Nyataya

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari (KUPPET), Bw Akelo Misori alisema walimu walikuwa wameishauri Serikali ikague kwa kina vitabu hivyo kabla ya kuchapishwa lakini inaonekana ushauri wao ulipuuzwa.

Kulingana naye, asasi husika za serikali ziliharakisha shughuli hiyo iliyolenga zaidi kusaidia watoto wanaotoka katika familia maskini.

 

Jukumu la walimu

Kwa upande wake, Chama cha Wachapishaji Kenya (KPA) kilisema ni jukumu la walimu kufanya marekebisho wakiwa darasani hadi wakati matoleo mapya ya vitabu hivyo yatakapochapishwa baadaye.

Mwenyekiti wa KPA, Bw Lawrence Njagi aliondolea wachapishaji lawama akisema ni kawaida vitabu kuwa na makosa akisema makosa yaliyotajwa ni machache na hayataathiri elimu.

“Hakuna athari kwa mwanafunzi. Hii ndio sababu tuna walimu madarasani. Elimu inahusisha walimu, darasa, wanafunzi na vitabu. Mmoja wao akiondoka, hakuna elimu hapo. Ni jukumu la mwalimu kuelimisha na kufundisha vile inafaa,” akasema.

Kauli yake ilikosolewa na Bw Misori: “Inafaa ikumbukwe kuwa wanafunzi pia hujisomea wenyewe bila walimu kuwepo.

Kama watasoma mambo yenye dosari katika vitabu hivyo bila shaka watachanganyikiwa, na matokeo yao katika elimu yataathirika,” akasema na kuongeza kuwa walimu hawafai kulaumiwa kwa kosa lililotendwa na watu wengine na ambalo lingeepukika.

Mnamo Jumatatu, Mkuu wa Utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, alithibitisha dosari zipo na kusema utathmini unafanyiwa vitabu hivyo na hatua itakayochukuliwa itaamuliwa baadaye.

 

Mafunzo muhimu kuhusu ufugaji wa kuku na ng’ombe

Na FAUSTINE NGILA

FEBRUARI 24, 2018, Akilimali ilijumuika na jarida la kilimo kwa lugha ya Kiingereza Seeds of Gold katika kituo cha utafiti cha Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (Kalro), kilomita moja kutoka mjini Kitale, kaunti ya Trans Nzoia.

Mamia ya wakulima kutoka kaunti za Nairobi, Nyeri, Nakuru, Kakamega, Uasin Gishu, Bungoma, Kisumu na Trans Nzoia walimiminika katika kituo hicho, kila mmoja akitazamia kuelimishwa kuhusu mbinu bora za kilimo na jinsi ya kukabiliana na visiki vya ufugaji na ukuzaji mimea.

Wataalamu wa kilimo, wavumbuzi, kampuni mbalimbali na wapenzi wa kilimo walihudhuria hafla hiyo inayoandaliwa baada ya kila miezi miwili, kwa lengo moja la kuimarisha kilimo nchini.

Kipindi cha maswali na majibu kilianza kuhusu ufugaji wa ndege wa nyumbani, ambapo zaidi ya wafugaji kumi waliuliza maswali mbalimbali ambayo yamekuwa kitendawili kwao kwa muda mrefu.

Mkulima mmoja wa kundi la wafugaji la Shamba la Wanyama kutoka kaunti ya Kakamega aliuliza sababu ya kuku wake wa kienyeji kutoangua asilimia 100 ya mayai wanayolalia, vifaranga kufa ovyoovyo na jinsi ya kutokomeza mazoea ya kuku kula mayai.

Katika jibu lake, mkurugenzi wa kituo cha Kalro cha Kakamega Dkt Luvodicus Okitoi alianza kwa kuwauliza wafugaji mbinu zao za kufuga kuku.

“Ni mayai mangapi kuku wa kawaida anaweza kutaga kabla ya kuyalalia?” aliwauliza. Wakulima walitoa idadi iliyo kati ya 15 na 25, na kukubaliana 18 kama idadi ya wastani.

“Kuku yeyote wa kienyeji anayetaga zaidi  mayai 20 hawezi kuyalalia na yaangue yote. Idadi ya wastani ni mayai 14 na idadi ya vifaranga watakaoanguliwa itakuwa 10 na watakaofikisha umri wa kukomaa ni sita,” wakulima walikubaliana na kauli hiyo.

Mtaalamu huyo alielezea kuwa bei ya kuku mmoja mjini Bungoma ni Sh500, na ikizingatiwa kuwa kuku hawa hutaga mayai mara tatu kwa mwaka, mkulima hupata Sh9,000 kwa mwaka.

Wafugaji wa kuku waliuliza kila aina ya maswali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuongeza mapato
Akielezea jinsi ya kuongeza kiwango hiki cha pesa kutoka kwa kuku mmoja, alisema, “Iwapo kuku atalishwa vizuri, vifo vitapungua. Badala ya kumpa kuku mayai 14, mpe mayai 10 na ataangua yote na vifaranga wote wafikie umri wa kukomaa.”

Mkulima mwingine aliuliza kuhusu kuku kufikia kikomo cha kutaga mayai.

“Unaweza kupyesha uwezo wa kuku kutaga mayai. Mtumbukize kuku ndani ya maji baridi. Baada ya hapo, homoni zake zitabadilika na kuanza kutaga mayai tena.

Kwa kufanya hivi, kuku wako anaweza kutaga mayai mara kumi kwa mwaka, ikilinganishwa na mara tatu bila mbinu hii,” akajibu.

Kwa hilo, wakulima waliduwazwa na mbinu hiyo, na baada ya kupiga hesabu za haraka, waligundua kuwa badala ya Sh9,000 wanazopata kila mwaka, wanaweza kuuza kuku kumi mara kumi kwa mwaka na kutia mfukoni Sh50,000.

Mfugaji auliza swali kwenye kliniki ya Seeds of Gold iliyofanyika katika kituo cha Kalro, Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kuku mlezi
Ili kudumisha ubora wa ndege wanaofuga, wakulima walishauriwa kuvalia njuga ufugaji wa kuteua kuku mmoja ambaye atawalea vifaranga wote.

“Chagua kuku wako bora kwa kulea vifaranga na ataweza kukulelea vifaranga wote 100 walioangaliwa na kuku kumi tofauti,” akashauri mtaalamu huyo.

“Je, hili litawezekanaje?” akauliza mfugaji mmoja aliyeshangazwa na mbinu hiyo.

Daktari huyo alielezea kuwa ingawa kila kuku anajua vifaranga wake kwa harufu, vifaranga wa kuku wengine wanaweza kuletwa kwa kuku mlezi usiku kwa kutumia mikono safi.

Kufikia asubuhi, harufu hiyo itakuwa imeyeyuka na kuku mlezi atawakubali vifaranga wote. Akikataa, basi ujue ulikuwa na marashi kwa mikono yako.

Francis Mathai aonyesha nduma aina ya Dryland aliyopendekezewa na maafisa wa Kalro Mei 2017. Alikuwa amehudhuria kliniki ya mafunzo ya kilimo mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Kugeuza kuku kuwa kiangulio
Mtafiti huyo pia alielezea wakulima jinsi ya kugeuza kuku wao kuwa mashine ya kuangua vifaranga. Aliwashauri kuteua kuku aliye na rekodi nzuri ya kuangua mayai yote.

“Mpe kuku huyo mayai 10 baada ya kila siku 21. Mpe mayai yaliyotagwa na kuku wengine alalie katika siku ya 22. Baada ya kila siku 21, vifaranga 10 walioanguliwa watakuwa na afya njema mpaka waishi mpaka ukomavu. Hivyo, kuku huyu anahitaji chakula na maji ya kutosha.”

Kwa mwaka mmoja, utaangua vifaranga mara 17 watakaolelewa na kuku walezi, na hivyo mfugaji atapata Sh85,000 akiwa mashinani.

Kuhusu utata wa ufugaji wa kuku wa umri tofauti na kuwatibu, Dkt Okoiti alianza kwa kuwakumbusha wafugaji kuwa yai la kwanza kutagwa haliwezi kuangua kuwa kifaranga.

“Pasua yai hilo na ujaze changarawe na ufunike ganda lake. Yai hili feki utaliweka kwa kiota baada ya kuchukua yai lililotagwa. Kuku hupata motisha wa kutaga akiona yai kiotani.”

Aliwataka wafugaji kutia alama mayai yote kuhusu siku yaliyotagwa. Baada ya kati ya siku7-10 tangu kutagwa, mayai yatakuwa tayari kulaliwa na kuangua vifaranga wa umri sawa.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro kaunti ya Kakamega Dkt Ludovicus Okitoi akiwaelimisha wafugaji wa kuku kuhusu mbinu mbalimbali za kuongerza mapato mjini Kitale Februari 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila.

Kupunguza vifo
Ili kukomesha tatizo la vifaranga kufa, aliwashauri kufuga jogoo mmoja kwa kila kuku 10 ambaye hana ukoo na mamake ili kuimarisha uwezo wa mayai kuangua na kuepuka vifaranga kufa.

Kuku wanaokula mayai na kuwala wenzao manyoya, inamaanisha wamesongamana sana na mwangaza huwa mwingi katika kiota ambamo mayai hutagiwa.

Wakigundua ni tamu, hii sasa huwa tabia yao. Kwa hivyo, unafaa kuwakata midomo ukitumia kisu moto ili iwe butu, na watakomesha tabia hiyo kwa muda wa wiki mbili.

Wakiwachanja kuku dhidi ya ugonjwa wa Newcastle, wafugaji walishauriwa kufanya hivyo mwishoni mwa kiangazi au mwishoni mwa msimu wa mvua.

“Je, kuku anaweza kuishi kwa muda gani kwa maisha yake?” mtafiti huyo akatupiwa swali.

“Maisha ya kuku yanategemea mbinu za mfugaji,” alianza.

“Kama nyoka, kuku huondoa magamba yake. Ukiona manyonya yakimtoka, mlazimishe kutoa maganda. Manyoya mengi huashiria ukosefu wa maji na chakula. Mnyime maji na chakula kwa wiki nzima, hawezi kufa. Baada ya hapo atapyesha homoni za kukua na kuanza kutaga mayai upya. Hivyo ndivyo unaongeza maisha yake.”

Wakuzaji wa miche ya matunda, mitishamba na mboga waonyesha ubunifu wao. Picha/ Faustine Ngila

Chakula cha ng’ombe
Maswali sasa yaliegemea ufugaji wa ng’ombe. “Je, ni nafaka zipi bora zaidi kwa kutengeneza chakula cha ng’ombe?” akauliza mfugaji wa kike.

Mkurugenzi wa kituo cha Kalro, Kitale Dkt F Lusweti alijibu kuwa mtama na mahindi ni chaguo bora.

“Kalro inapendekeza mahindi aina ya KH5500-43A kwa kuwa inakomaa haraka na unaweza kukuza alizeti baada ya kuvuna.

Iwapo unataka chakula chenye proteini, basi tumia mahindi mbichi wakati yameanza kuunda maziwa.

Lakini kama unataka chakula kingi kisicho na proteini nyingi, tumia mahindi yakiwa kiwango cha kuchemshwa. Nyasi ya Rhodes pia ni nzuri.”

Swali liliibuka kuhusu nyamakondo (placenta) kukwama ndani ya baadhi ya ng’ombe baada ya kuzaa.

Mtaalamu huyu alisema sababu kuu ni ya kiukoo, jua kali au ndama kuwa mkubwa kupita kiasi. Aliwashauri wafugaji kusaka fahali wanaozalisha ng’ombe ndama wa wastani.

Kampuni ya Simba Corp iliwaelezea wakulima trakta na mashine bora za kilimo na ufugaji inazounda. Picha/ Faustine Ngila

‘Hongo kwa ng’ombe’
Watafiti walionya wafugaji dhidi ya ‘kuwahonga’ ng’ombe kabla ya kumkama, kwa kumlisha chakula cha ng’ombe wa maziwa. Walisisitiza kuwa inafaa ng’ombe watunukiwe kwa kumpa mfugaji maziwa, na si kinyume chake.

Wafugaji pia walionywa dhidi ya kufuga fahali ikiwa wana ng’ombe watano pekee. Gharama ya kumfuga iko juu, hivyo mkulima anafaa kutumia mbinu ya kiteknolojia kuwatunga mimba ng’ombe.

Chuo Kikuu cha Egerton kilitangaza kuwa kimevumbua aina mpya ya mtama inayoweza kutumika kwa uokaji wa mikate. Kilisema kinashirikiana na kampuni za uokaji ili kuitangaza sokoni.

Wote waliohudhuria darasa hilo la elimu ya kilimo walifurahia kupata ujuzi na mbinu mpya za kupunguza gharama, kukabiliana na magonjwa, kuongeza mavuno na kuepuka hasara katika kilimo chao.

 

Baruapepe: fauzagila@gmail.com