Habari za Kitaifa

Pigo kwa UHC mahakama ikizima Bima ya Afya ya Jamii

Na SAM KIPLAGAT July 12th, 2024 1 min read

MIPANGO ya Rais William Ruto kuzindua huduma ya afya kwa wote imepata pigo baada ya Mahakama Kuu kutangaza Sheria tatu ambazo UHC ingetekelezwa kuwa kinyume na katiba.

Majaji watatu walitangaza Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIA) 2023, Sheria ya Afya ya Msingi, 2023 na Sheria ya Afya ya Kidijitali, 2023, ambayo ilichukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) kuwa batili.

Majaji Alfred Mabeya, Robert Limo na Fredah Mugambi walisitisha utekelezaji wa uamuzi wao kwa siku 120 ili kuruhusu serikali kuanza upya mchakato wa kutunga sheria mpya.

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha alikuwa ametetea Sheria hizo akisema, zilikusudiwa kukuza utekelezaji wa UHC na kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya juu zaidi ya afya.

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha. PICHA| HISANI

Sheria hiyo, alisema, inaanzisha Mamlaka ya Afya ya Jamii, ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia hazina tatu zilizoanzishwa chini yake- Hazina ya Afya ya Msingi, Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii na Hazina  ya Dharura, na Magonjwa Sugu.

Aliongeza kuwa wanachama watachangia asilimia 2.75 ya mapato yao kwenye SHIF na serikali  italipia wananchi ambao hawana uwezo wa kulipa.

Rais Ruto alikuwa ametangaza kuwa uzinduzi huo ungeanza Oktoba 1 na NHIF imekuwa ikiwaarifu Wakenya kujisajili na SHA.