Habari Mseto

Polisi wakataa kuzungumzia mauaji ya mlanguzi wa dawa

March 18th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MLANGUZI wa mihadarati Yusuf Ahmed Swaleh, almaarufu Candy Rain, amekufa katika hali ya kutatanisha huku wakuu wa polisi eneo la Pwani wakisalia kimya.

Mwili wa Swaleh ulipatikana Kilifi siku nne baada ya kuripotiwa kuwa alikamatwa ili kuhojiwa.

Wakili wake, Jared Magolo, akiongea kwa niaba ya familia, alithibitishia Taifa Dijitali kwamba mteja wake aliuawa muda mfupi baada ya kukamatwa na watu wasiojulikana siku tisa zilizopita.

“Ndio. Walimuua. Mwili wake ulipatikana Kilifi. Alishikwa Ijumaa, siku tisa zilizopita,” Bw Magolo akasema kupitia ujumbe mfupi.

Wakati wa kifo chake, Swaleh alikuwa akikabiliwa na mashtaka kadha kuhusiana na ulanguzi wa mihadarati ya thamani ya mamilioni ya pesa.

Maafisa wakuu wa polisi eneo la Pwani hawajasema lolote baada ya mwili wa mwendazake kupatikana, licha ya Taifa Dijitali kuwapigia simu mara kadhaa.

Yeye na mkewe, Asma Abdalla Mohamed, walituhumiwa kushiriki ulanguzi wa mihadarati.

Mwendazake ndiye mshukiwa wa kwanza wa ulanguzi wa mihadarati kuuawa katika utawala wa Kenya Kwanza.

Haya yanajiri licha ya hakikisho kila mara kutoka kwa Rais William Ruto kwamba serikali yake haitaruhusu visa vya mauaji kiholela.

Mauaji ya Swaleh yanatokea mwezi mmoja baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kutangaza operesheni kali dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya Pwani.

Duru zinasema kuwa wakati wa uhai wake, Swaleh alitaka kufuata nyayo za aliyekuwa mlanguzi wa dawa hizo, Ibrahimu Akasha, baada ya wanawe kupelekwa Amerika kujibu mashtaka ya ulanguzi wa dawa haramu.

Baadaye wanawe Akasha, Baktash Akasha na Ibrahim Akasha, walihukumiwa kifungo cha miaka 25 na miaka 23 gerezani, mtawalia.

Swaleh alikuwa amejitokeza kama sura mpya ya ulanguzi wa dawa za kulevya Pwani, hali iliyothibitishwa na kesi nyingi kuhusu biashara hiyo zilizomzingira.

Awali, Swaleh, ambaye alikuwa amefungwa gerezani, aliachiliwa huru kwa njia ya kutatanisha licha ya kupatikana na hatia.

Mnamo Machi 8 mwaka jana, 2023, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kupatikana na kosa la ulanguzi wa pesa.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Shanzu, Joe Omido, alimpata na hatia ya makosa mawili ya ulanguzi wa pesa.

“Bw Swaleh atapigwa faini ya Sh6.2 milioni au akikosa atumikie kifungo cha miaka 10 gerezani,” hakimu huyo akasema.

Hata hivyo, mkewe Swaleh ambaye pia alishtakiwa pamoja naye alipewa kifungo cha miaka mitano kwa kosa lilo hilo.

Bi Mohamed alipewa adhabu nyepesi baada ya mahakama kuambiwa kuwa afya yake ilidhoofika.

Bw Swaleh na Bi Mohamed walipatikana na hatia kwa makosa ambayo walitenda 2017.