Makala

Punda wapungua sana Narok na Bomet, msako wa mabucha waanza

Na KNA, LABAAN SHABAAN September 12th, 2024 2 min read

JUHUDI za kuzuia wizi mkubwa wa punda katika kaunti za Narok na Bomet zimeongezwa kuni baada ya maafisa kutoka kaunti hizo mbili kuazimia kushirikiana kukabili visa hivi.

Makumi ya wakulima wananateta baada ya punda wao kutoweka katika kaunti hizi jirani.

Kuna hofu kuwa nyama zinazouzwa katika mabucha ni ya punda.

Kadhalika, kuna hofu ya kuzuka kwa maradhi na kuathiriwa sana kwa idadi ya wanyama hawa.

Maafisa wa kaunti za Narok na Bomet wameanza msako kudhibiti hali.

Viongozi hao wakiongozwa na makamishna wa kaunti zao Kipkech Lotiatia (Narok) na Dkt Omar Ahmed (Bomet) walikutana katika ukumbi wa kamishna wa Narok kupanga mikakati.

Timu hiyo itajumuisha maafisa kutoka idara ya mifugo, afya ya umma, Huduma ya Kitaifa ya polisi, Maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO) na mfumo wa kilimo Kenya.

Kulinda wanyama

Maafisa hawa watazidi kufanya mikutano ya mara kwa mara kupanga mikakati ya kulinda wanyama wa kufugwa.

Bw Lotiatia alisema timu hiyo ya mashirika mbalimbali itasaidia kusimamia sheria ya ulinzi wa wanyama na kuhakikisha kuwa nyama inayoliwa na wananchi imeidhinishwa na idara ya afya ya umma.

Bw Lotiatia anaitaka timu hiyo kupanga ziara za ghafla katika bucha za kaunti hizo mbili na kuthibitisha ikiwa nyama inayouzwa kwa umma sio nyama ya porini.

“Wale wanaopatikana wakiuza nyama katika maeneo mabovu au nyama ambayo haijaidhinishwa na idara ya afya ya umma wanafaa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka mara moja. Hii ndiyo njia pekee tutakayohakikisha kuwa wananchi wanakula nyama inayofaa,” akasisitiza.

Hatari ya vifo

Aidha amewaonya wakazi dhidi ya kuchinja na kula nyama ya wanyama waliokufa au walio wagonjwa kwani desturi hii inaweza kusababisha magonjwa na vifo.

Dkt Ahmed alikariri haja ya kaunti hizo mbili kufanya kazi kama timu kwa manufaa ya watu wanaoishi katika kaunti za mpakani.

Alitoa changamoto kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojaribu kuchinja mnyama aliyekufa kwa ajili ya kuliwa, ili hatua zichukuliwe mapema.

Kamishna huyo wa kaunti ya Bomet ana imani kuwa timu ya mashirika mengi itasaidia kudhibiti visa vya wizi wa punda katika kaunti hizo mbili.

Samuel Chege, afisa wa programu ya Mfumo wa Kilimo Kenya (FSK) alithibitisha kuna usafirishaji mkubwa wa punda ambao haukuweza kuhesabiwa waziwazi.

Alirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo shirika lake lilinasa punda 68 waliokuwa wakisafirishwa kutoka eneo la Mulot kuelekea mji wa Narok.

Aliongeza kuwa wasafirishaji hao hawakuwa na kibali cha usafiri.

Bw Chege alilalamika kwamba idadi ya punda katika kaunti hiyo inapungua polepole akiongeza ripoti nyingi zilikuwa zikitolewa na wafugaji kuhusu kutoweka kwa wanyama wao.

“Wakati wa sensa ya 2019, idadi ya punda huko Narok ilikuwa takriban 800, 000. Idadi hii imepungua kwa sababu punda wanatoweka,” alisema.

Dkt. Yegon Kibet wa FSK alisema uchinjaji wa wanyama hawa msituni ni hatari kwani huwahatarisha wakaazi kupata magonjwa ya wanyama kama vile kimeta na kichaa cha mbwa.

Dkt Kibet alitoa wito kwa wakazi kuripoti kutoweka na kuchinjwa kwa punda kwa mamlaka husika ili kumlinda mnyama huyo ambaye yuko katika hatari ya kutoweka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Narok Joseph Ole Kireu alipongeza ushirikiano kati ya kaunti hizo mbili akisema utaimarisha ulinzi wa wanyama.