Habari Mseto

Raia wa Haiti wahofia dhuluma kutoka kwa polisi wa Kenya

May 28th, 2024 2 min read

NYABOGA KIAGE NA STEVE OTIENO

RAIA wa Haiti wameashiria kutoridhishwa na hatua ya Baraza la Muungano wa Umoja wa Kimataifa Kuhusu Usalama kutuma ikosi vya pamoja vya usalama (MMS) nchini humo, baadaye mwezi huu, ili kusaidia kudumisha amani.

Haiti imekuwa ikishuhudia ghasia na machafuko hasa baada ya Rais wa 43 wa nchi hiyo, Jovenel Moïse, kuuawa mnamo Julai 2021.

Tangu taifa hilo lipate uhuru wa kujitawala kutoka kwa Mfaransa, viongozi wakuu kadhaa wa kisiasa, wakiwemo marais watano wameuawa, suala ambalo limechochea vita vinavyotekelezwa na magaidi sugu.

Kuna historia ya dhuluma na mahangaiko waliyopitia baada ya vikosi vya usalama kutoka nje ya nchi hiyo kutumwa humo kudumisha amani Haiti.

Raia wa nchi hiyo wana wasiwasi endapo mipango ya UN itatimia, hawatakwepa madhila sawa na ya awali. Wanalia hawajui thamani ya amani, huku makovu ya mawimbi ya kisiasa, vita na makundi ya wahuni yakiwahangaisha.

Polisi akikomoa mwandamanaji asiyejihami wakati wa maandamano, Kisumu. Raia wa Haiti wanahofia kukumbwa na hali hii pindi polisi wa Kenya watakapotua nchini mwao kuleta hali ya utulivu. Picha|Maktaba ya NMG

UN imekuwa ikijitolea kutuma vikosi vya maafisa wa kiusalama kutoka nchi wanachama wake, Amerika ikipiga jeki mikakati hiyo.

Historia ya walinda usalama kutumwa Haiti inaonyesha haki za kibinadamu za raia wake zimekiukwa, kuanzia dhuluma, kupigwa kinyama, kuteswa, kubakwa na mazingira kuchafuliwa.

Mwaka 2010, mkurupuko wa Kipindupindu uliripotiwa kufuatia oparesheni iliyoendeshwa na UN watu 30, 000 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.

Isitoshe, visa 820, 000 vya maambukizi viliandikishwa na Februari 2022, Haiti ilitangazwa kuwa huru dhidi ya maradhi hayo hatari, kufikia sasa raia wakiwa wanaendelea kulilia haki ya fidia.

Utafiti uliofanywa na mtaalamu maalum wa afya kutoka Ufaransa, Renaud Piarroux alihoji vikosi vya usalama vilivyohudumu chini ya UN kutoka Nepal, kando na kuharibu mazingira, viliachilia uchafu kutoka kwa kambi walizokuwa wakiishi na kuharibu Mto Artibonite.

UN ilikiri maafisa hao ndio walisababisha mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu, Katibu Mkuu wake wakati huo Ban Ki Moon, akiomba msamaha.

“Tunaomba msamaha kwa raia wa Haiti. Hatukutenda haki kuhakikisha tunasaidia kuzuia msambazao wa Kipindupindu,” Bw Ki Moon akasema.

Visa vya wanawake na wanaume kubakwa na kudhulumiwa viliripotiwa.

Mwaka 2011, video iliyoonyesha mwanamume mwenye umri wa miaka 19 akidhulumiwa na maafisa wa usalama ilifichuka.

Rais wa Haiti wakati huo, Michel Martelly alikashifu vikali kitendo hicho kilichochochea raia kuandamana.

Maafisa wa usalama kutoka Uruguay walihusishwa na kisa hicho, na wahusika walishtakiwa, wakapatikana na hatia na kuishia kurushwa jela miezi kadhaa.

Hata ingawa Kenya inapeleka maafisa wapatao 1, 000 wa polisi Haiti kusaidia kudumisha amani, hatua hiyo imepokea pingamizi kutoka kwa wakosoaji wake.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu Haiti wanalaumu Amerika katika kile wanadai kama taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani kutumia Kenya kuhitilafiana na demokrasia ya nchi hiyo.