Habari za Kitaifa

Raila aitaka serikali ikomeshe ubomoaji unaoendelea Msambweni

January 6th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, ameirai serikali kusimamisha shughuli za kuwahamisha watu kwa nguvu na ubomozi wa makazi yao yaliyo katika ardhi zenye utata nchini.

Kwenye taarifa, Jumamosi, Bw Odinga alisema kuwa ubomozi wa makazi ya watu unaoendelea kwa sasa mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine nchini lazima yakomeshwe mara moja.

Bw Odinga alisema kwamba serikali ya Kenya Kwanza iliwaahidi Wakenya kutowabomolea makazi yao hata kidogo, baada ya kuchukuka uongozi.

“Serikali ilituahidi kuwa, ikiwa ni lazima watu wabomolewe makazi yao, basi wangepewa notisi na muda wa kutosha kujitayarisha na baadaye kulipwa ridhaa kwa haraka. Waathiriwa wa ubomoaji unaoendelea Msambweni, Voi katika Kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine nchini, wanangoja ahadi hiyo kutimizwa,” akasema.

Soma Pia: Ubomoaji wa nyumba za maskwota 3,500 waanza Msambweni

Baadhi ya maeneo ambako makazi ya Wakenya yamebomolewa na serikali kufuatia utata wa ardhi yalikokuwa yamejengwa ni Mavoko katika Kaunti ya Machakos, Thika katika Kaunti ya Kiambu kati ya mengine.

Bw Odinga aliyarai mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kuchukua hatua za haraka kuwasaidia waathiriwa wa ubomoaji wa Voi kwa bidhaa za msingi na kupata haki.

Kiongozi huyo alisema Wakenya wanapitia hali ngumu za kiuchumi, hivyo serikali inafa kujali athari  za vitendo vyake.