Habari za Kitaifa

Raila alivyopasua ODM

Na JUSTUS OCHIENG September 16th, 2024 2 min read

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimejipata katika njiapanda kuhusu iwapo kiegemee serikali au kizingatie wajibu wake wa muda mrefu wa kupigania haki ya Wakenya wa kawaida.

Japo chama hicho kinashikilia kuwa hakina mkataba wowote na utawala wa Rais William Ruto, hatua yake ya kutoa kibali kwa maafisa wake wakuu kuhudumu kama mawaziri inaashiria ushirikiano mzuri na Kenya Kwanza.

Viongozi wakuu wa ODM walioteuliwa serikalini ni waliokuwa manaibu kiongozi wa chama Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti wa kitaifa John Mbadi, aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi, na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi Bi Beatrice Askul.

Hatua hiyo pamoja na kampeni za Rais Ruto za kumpigia debe aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga anayewania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) imewaacha wanachama katika njiapanda.

Wanakabiliwa na kibarua cha kuamua ikiwa waunge serikali mkono au waendelee kutetea raia.

Hali hii imechangia kuibuka kwa makundi ndani ya ODM, viongozi wakuu wakionekana kugawanyika.

Lakini katika majukwaa ya hadhara, wao hutaka waonekane wameungana.

Taifa Dijitali imegundua kuwa kuna makundi ya viongozi wanaounga mkono serikali, kuna wale wanaopinga huku kukiwa na wengine ambao wameamua kutounga upande wowote.

Hii ndiyo maana wiki jana, baadhi ya viongozi wa ODM kutoka Nairobi walisusia mkutano na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi, ishara wanapinga serikali iliyoshirikisha baadhi ya wanachama wao.

Miongoni mwa viongozi wakuu wanaoongoza kundi linaloegemea serikalini ni pamoja na kakake mkubwa Bw Odinga, Oburu Oginga, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, mwenyekiti wa kitaifa Gladys Wanga na naibu kiongozi wa chama Simba Arati.

Wengine ni Mwekahazina wa Kitaifa Timothy Bosire na mwenyekiti wa ODM tawi la Nairobi George Aladwa.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu Edwin Sifuna, dadake Odinga na naibu Katibu Mratibu Ruth Odinga, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi na Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera wanasemekana hawaungi kikamilifu ushirikiano wa ODM na serikali.

Isitoshe, Dkt Oginga na Bw Mohamed wamedokeza kuhusu uwezekano wa ODM kuunga mkono Rais Ruto atakapokuwa akitetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Seneta huyo wa Siaya anasema hamna chochote kitakachowazuia kushirikiana na Dkt Ruto katika uchaguzi huo ikiwa atatimiza ahadi zake, haswa kwa wakazi wa eneo la Nyanza.

Dkt Oginga alisema eneo hilo litakuwa tayari kurudisha mkono hatua ya Dkt Ruto kuunga mkono Odinga 2007, hadi akapata wadhifa wa Waziri Mkuu katika serikali ya muungano iliyoundwa 2008 chini ya uongozi wa Rais Mwai Kibaki.

Naye Bw Mohamed, ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki amemtaka Rais Ruto kuhakikisha kuwa Bw Odinga anashinda kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

“Azma ya Raila ya wadhifa wa AU ni muhimu zaidi kwetu. Tuliona alivyozinduliwa katika hafla ya kufana iliyohudhuriwa na marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tukipata kiti hicho, mambo yatakuwa matatu na mambo hayo matatu tutayatangaza siku nyingine,” akasema Bw Mohamed.

Lakini kwa upande wake Bw Sifuna, ambaye ni Seneta wa Nairobi anashikilia kuwa ODM ingali katika upinzani, ikiongoza mirengo ya wachache katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

“Baadhi ya watu wanaendesha juhudi za kutusukuma ndani ya serikali ilhali tuko katika upinzani na tutaendelea kutekeleza majukumu yetu katika nafasi hiyo. Huu msisimko kuhusu serikali utafifia,” Bw Sifuna anaeleza.